Pg 2Wiki iliyopita sikuandika kwenye safu hii. Sikupata wasaa huo kutokana na ukweli kwamba nilikuwa kwenye harakati za uchaguzi. Naomba kuwashukuru wahariri wenzangu walionichagua kwa kishindo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF). Pamoja nami, walichaguliwa Mwenyekiti, Theophil Makunga, Katibu Neville Meena, Naibu Katibu, Nengida Johannes; wajumbe Jesse Kwayu, Bakari Machumu, Mzee Salim Said Salim, Lilian Timbuka na Joyce Shebe.

Wakati tunafanya kampeni, nilieleza nia ya kuhakikisha TEF inaimarisha weledi wa sekta ya habari na mpango wa kuliwezesha Jukwaa kusimama kwa miguu yake kiuchumi kwa kufanya uwekezaji, hali itakayokuwa nguzo katika kuongeza weledi.

Mawili hayo yataiwezesha tasnia ya habari kuheshimika zaidi kwa kukusanya, kuchakata na kuchapisha taarifa zisizoacha maswali au kuwakatisha tamaa wasomaji na wasikilizaji wetu. Kimsingi Jukwaa linalenga kushirikiana na wadau wengine kuwekeza katika Habari za Uchunguzi.

Nampongezi kipekee Mwenyekiti wa TEF aliyemaliza muda, Absalom Kibanda. Kibanda amekuwa kiunganishi cha ncha zaidi ya mbili za Jukwaa kwa kuwaleta pamoja wahariri wote nchini, na hivyo kuimarisha kazi njema aliyoianzisha Sakina Datoo, ya kuanzisha Jukwaa hili mwaka 2008.

Naamini chini ya uongozi wa Mzee Makunga kwa busara na umri wake tutalisogeza mbele zaidi Jukwaa kwa kutimiza malengo ya kuimarisha weledi wa kitaaluma na kuboresha uwezo wake kiuchumi likaweza kufadhili mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa wanahabari. Tutakuja kwenu na mawazo haya, tutaomba mtuunge mkono tuisaidie nchi hii.

Sitanii, leo nimeamua kuandika mada hii baada ya kusikia, kuona na kushiriki vikao vilivyodhihirisha kuwa TEF na tasnia ya habari kwa ujumla nchini tunaweza kuisaidia Serikali, vyama vya siasa na wadau wa maendeleo ya Taifa letu kufikia dhima ya kuondoa umasikini katika nchi yetu na kujenga Taifa lililostaarabika.

Baada ya kuchaguliwa Januari 30, 2016, Bodi ya Wakurugenzi TEF iliteua wajumbe watatu; Deodatus Balile (Makamu Mwenyekiti na kiongozi wa msafara), Neville Meena (Katibu) na Jesse Kwayu (Mjumbe) kwenda Dodoma kuzungumza na uongozi wa Bunge juu ya sintofahamu iliyoibuka juu ya wanahabari kuzuiwa kufanya kazi kwa uhuru na baadhi ya maofisa wa Bunge.

Kikao cha kwanza tulikutana na Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Nape Nnauye. Hakika Waziri huyu anastahili pongezi za pekee kwa jinsi alivyoshirikiana na Kamati hii. Alitusikiliza, akashauri na kuweka msukumo ilipohitajika kuwaona viongozi wa kitaifa. Kwa jinsi tulivyofanya kazi na Nape mjini Dodoma, kama hatabadilika, naomba kusema kwa mara ya kwanza Wizara ya Habari imepata Waziri.

Sitanii, si nia yangu kufukua makaburi, lakini niseme wazi kuwa mawaziri waliotangulia katika wizara hii, muda wote walijipanga kupambana na waandishi, na nafikiri hata nyie wasomaji mnalifahamu hili. Mtangulizi wa Nape, Fenella Mukangara, alifika mahala akapendekeza sheria iliyolenga kuua kabisa uhuru wa vyombo vya habari. Nape ukizungumza naye na kwa anayofanya, napata faraja kusema hata sheria ya habari Mungu akipenda tutapata sheria nzuri.

Najua mtahoji itakuwaje awe Waziri mzuri wakati hivi karibuni amelifuta gazeti la ‘Mawio’. Nasema bayana, kuwa sikubaliani na uamuzi alioufanya Nape kulifuta gazeti la ‘Mawio’, tumezungumza naye kwa kina suala hili, ameonesha kusikitika kutokana na mazingira na sheria iliyopo vilivyomsukuma kufikia uamuzi huo, lakini naamini inawezekana kuwa na “Baniani mbaya, kiatu chake kikawa dawa.”

Narudia, Nape asipobadilika, akaendelea na moyo wa kupenda kuona sheria mbaya zinafutwa kama alivyotamka mara kadhaa katika mikutano na wanahabari, na akaendelea kupambana na wahafidhina ndani ya wizara wenye kutamani magazeti yote binafsi yafungiwe yabaki Habarileo, Daily News na Uhuru, basi nchi hii itafaidi matunda ya tasnia ya habari.

Februari  mosi tulikutana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah. Itakumbukwa na kulikuwapo mvutano mkubwa kati ya waandishi na maafisa wa Bunge. Pia wiki hiyo, Televisheni ya Taifa (TBC1) ilitangazwa kusitisha kurusha matangazo ya Bunge ‘live’ kutokana na gharama ya Sh bilioni 4.1 kwa mwaka!

Mazungumzo yalimhusisha na Naibu Katibu wa Bunge, Said Yakub, ambao kwa pamoja walieleza kusikitishwa na mzozo uliotokea bungeni dhidi ya waandishi na wakaumaliza kwa Katibu wa Bunge, Dk. Kashilillah, kumtaka Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya, kuwaomba radhi wanahabari kwa kuwabughudhi wakati wanafanya kazi halali.

Kikao pia kilimaliza mgogoro wa mwandishi Elias Msuya aliyerejeshewa kitambulisho na kuruhusiwa kuendelea na shughuli za Bunge. Katika kikao na Spika wa Bunge, Job Ndugai, yeye alifurahia ujio wa viongozi wa TEF na akashauri uhusiano huo kukuzwa zaidi kwa kufufua Chama cha Waandishi wa Habari za Bunge.

Ndugai na Kashilillah waliahidi uhuru mpana zaidi kwa waandishi wa habari na kusema Bunge halijazuia chombo chochote kurusha matangazo ya Bunge ‘live’, na wameeleza utayari wao wa kukutana na wanahabari wakati wowote itakapohitajika kufanya hivyo.

Kikao cha mwisho, Kamati yetu ilikutana na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa. Aliahidi kusaidia kupatikana sheria nzuri isiyokwaza waandishi wa habari, vyombo vya habari, Serikali na jamii. Pia alizungumza jambo lililonisukuma kuandika makala hii leo. Waziri Mkuu Majaliwa alisema yeye na Rais John Magufuli wana imani kubwa na vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari ni chanzo cha taarifa muhimu zinazoisaidia Serikali kutambua wapi mambo yanakwenda vyema na wapi yanakwenda vibaya. Hata hili la makontena bandarini, nilichukua hatua baada ya kusoma habari hizi gazetini [gazeti la JAMHURI ndilo lililoandika kwa kina habari za Bandari]. Niliviagiza vyombo vya dola kufuatilia habari hizi, tukakuta ni za kweli,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Hakuishia hapo tu, alisema: “Kila wakati napitia magazeti, na nikiona headline (kichwa cha habari) inayohusu wizara fulani, nampigia waziri mwenye dhamana na wizara hiyo na kumwambia asome gazeti, afanye uchunguzi na kuniletea ripoti haraka,” anasema Majaliwa.

Sitanii, ametwambia hata Rais Magufuli anasoma magazeti na wote wana imani magazeti yanazo taarifa sahihi zinazoweza kukomboa uchumi wa nchi hivyo akaomba waandishi waendelee kuandika, na wao watasoma na kuyafanyia kazi yote yanayoandikwa. Ni katika nukta hii nasema, kwa kuthamini vyombo vya habari, Magufuli na Majaliwa wamechukua mkondo sahihi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa Serikali haiwezi kuwa na polisi kila kona – iwe hospitalini, bandarini, mahakamani, viwandani na kwingine, lakini wanahabari wanaweza kupenya kila kona na kufikisha taarifa sahihi. Msimamo wa kuviamini vyombo vya habari ukiendelea, nchi itapata taarifa sahihi kwa wakati.

Sitanii, ikizifanyia kazi tofauti na uongozi uliopita ulioviita vyombo vya habari ‘kelele za mlango’ itaongeza makusanyo ya kodi maradufu, nchi itakuwa na uchumi imara na huduma za jamii zitaimarika. Mungu ibariki Tanzania.

1891 Total Views 2 Views Today
||||| 4 I Like It! |||||
Sambaza!