Siku ya Jumamosi iliyopita imekuwa nzuri kwa wafuatiliaji siasa na sera. Rais John Magufuli ametoa mwelekeo wa mabadiliko ya sera kubwa mbili, moja ikiwa ni Sera ya Mambo ya Nje, na ya pili ikiwa ni ya elimu ya juu.

Vyuo vikuu sasa vimeruhusiwa kudahili wanafunzi kulingana na sifa stahiki, tofauti na awali ambapo ilikuwa vyuo vinapatiwa wanafunzi na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Rais Magufuli amesema uamuzi wa kuwapa fursa wanafunzi kuchagua vyuo wavitakavyo, mbali na kuondoa rushwa katika upangaji wa idadi ya wanafunzi kwa vyuo, utawapa wanafunzi fursa ya kusoma kozi waitakayo. Sisi tunasema huu ni uamuzi mwafaka.

Lengo letu si kuzungumzia mabadiliko katika sekta ya Elimu ya Juu, bali kuzungumzia mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje. Kiitifaki Rais wa nchi ndiye mwanadiplomasia namba moja katika taifa. Hivyo, Rais John Magufuli ndiye kioo cha diplomasia yetu huko nje.

Rais Magufuli, ameitangazia dunia azma ya Tanzania kutojiingiza kwenye migogoro ambayo nchi haina tija nayo, huku akisisitiza kwamba Tanzania imeshiriki siasa hizo wakati wa ukombozi wa baadhi ya nchi za Bara la Afrika kwa kiasi cha kutosha.

Amekwenda mbali zaidi na kukumbusha kwamba Tanzania itaendelea na msimamo wake wa kuwa na marafiki wa aina zote, bila kujali marafiki hao wana migogoro ya namna gani.

Maneno hayo ya Rais Magufuli, yamelenga kuionesha dunia urafiki mpya kati ya Tanzania na Israel na Tanzania na Morocco. Tanzania imekuwa na msimamo usioyumba kuhusu kuzitetea Palestina na Polisalio.

Tanzania chini ya awamu zote nne zilizopita, imesimama pamoja na wanyonge hao. Msimamo huo ulianzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ni wazi kwa msimamo huu wa Rais Magufuli msimamo huu umewekwa kando.

Inawezekana Rais Magufuli ameamua kutanua wigo wa Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote, ambayo pia ni moja ya Sera inazozitekeleza Tanzania kimataifa, ila kiuhalisa tunaamini sababu na misingi iliyotusukuma kusimama na Polisalio na Palestina, hazijaisha na si vyema nchi yetu kuzipa kisogo.

Tunafahamu gharama tunayoingia kama nchi kwa kushikilia msimamo huo, na tunashuhudia ugeni wa viongozi wakubwa kutoka Israel na Morocco baada ya nchi yetu kubadili msimamo, ila tusipozitetea sauti za wanyonge ilihali tunazo fursa, ni wazi zitatulilia hata tukienda mbinguni. Tuendelee kubeba wanyonge bila kuwachoka, kwani ipo siku tutahitaji msaada wapo pia. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri