Ni vema tukakumbuka tuna wajibu wa kujali na kuheshimu (kuthamini) vyombo vyetu vya Polisi na Mahakama, ambavyo tumeviridhia kusimamia usalama wetu na kutoa haki. Ni vyombo nyeti katika mustakabali wa maisha yetu, uhuru na amani ya taifa letu.

Polisi katika taratibu zake za kazi ni kusimamia usalama wa raia na mali zao. Inafuatilia kuona kila mtu yupo salama na mali zake. Inazuia na kuchunguza uhalifu unaotendwa na jamii. Kama vile wizi, ugomvi na kadhalika.

Kwa upande wa Mahakama ni kutoa haki kwa mtu yeyote bila kujali hadhi yake. Inapokea mashtaka yanayopelekwa na Polisi na kuanza kuendesha na kusikiliza kesi za watuhumiwa na hatimaye kuzifanyia uamuzi.

Yumkini vyombo hivi vinatembea pamoja katika kutoa haki na kukataa batili na kuhakikisha usalama wa watu ni himilivu. Kutokana na mwenendo huu najikuta nikiamini na kutamka kuwa ni vyombo vinavyoshirikiana na kupokezana baadhi ya majukumu vinapokuwa kazini.

Katika nchi huru na yenye kuridhia na kufuata misingi na taratibu za demokrasia ya kweli, Polisi na Mahakama vinapaswa kupata heshima, ushirikiano na uelewano kutoka kwa wananchi, Bunge na Serikali.

 Serikali, Bunge na wananchi ni wajibu wetu kuvitunza vyombo hivi kama mboni mbili za macho yetu. Unyeti wa vyombo hivi katika kudumisha haki na usalama, inatupasa kuweka watendaji kazi waaminifu na waadilifu.

Naamini ni wajibu wetu kuwa na tabia ya malezi bora na kuvijengea miundombinu na kuvipatia vifaa bora vya kufanyia kazi, kuvipatia masilahi mazuri na kuvitamkia lugha tamu. Kwenda kinyume cha haya ni kuvinyanyasa.

Tunahakikisha tunatoa ushirikiano na kujenga uelewano zaidi katika kupokea kazi zao kwa amani na tunazingatia taaluma, weledi na uwezo wao katika kushughulikia mambo ya haki na usalama kwa jamii yetu hii.

Vyombo vyetu hivi kwenda kinyume cha sheria za kazi, kutumia nguvu na madaraka kumwadhibu au kumhukumu mtu bila hatia ni uonevu na ukatili kwa mtendewa na ni dharau na kiburi kwa wananchi walioviweka vyombo hivi.

Polisi ni chombo chenye sifa ya ustaarabu kwa muundo wake. Hivyo kitumie lugha safi kupata taarifa nzuri na mbaya kutoka kwa raia wema. Kisitumie lugha chafu na nguvu nyingi mahali ambapo ni shwari. Nguvu zitumike tu palipo na dalili za uvunjifu wa amani.

Polisi kupokea rushwa kwa dhamira ya kufunika sheria na kupitisha upendeleo au kumwonea mtu fulani kwa sababu tu ya kufurahisha nafsi za watu, ni dhuluma na ni dhambi kwa Mungu.

Mahakama ni chombo cha kiungwana kwa muundo wake. Hivyo hakina budi kuangalia dhana nzima ya kutoa haki na utawala wa sheria katika mfumo wa demokrasia ya kweli, ambayo wengi wapewe na wachache wasikilizwe. Si kusikilizwa tu bali wapewe kile kinachostahili.

Mahakama kupokea hongo kwa nia ya kupindisha sheria ni batili. Kuchelewesha haki kupatikana ni kukiuka maadili ya kazi na kudidimiza haki ya mtu ni dhuluma na ni dhambi kwa Mungu. Haki si ya mahakama ni ya Mungu.

Mahakama na Polisi vinapokiuka maadili ya kazi ni kuhalalisha dhuluma na kupoteza sifa nzuri ya kutoa haki na kusimamia usalama. Ni sawa kama kula tonge la moto na kunywa tone la usaha. Badala ya kula tonge la chakula na kunywa tone la maji.

Wananchi, kwa udi na uvumba tuvijali vyombo vyetu hivi na kuviwezesha kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na tija. Tuache na tujisahihishe kuhusu tabia ya kuvipuuza na kuvibebesha sifa mbaya. Tuvisifu vinapotenda vizuri na tuvionye na kuvishauri vinapofanya vibaya.

269 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!