Watu waungwana hawashangilii binadamu anapofikwa na mabaya, lakini huwa hawajizuii kufurahi wanapoona haki imetendeka.

Naam! Wapo wanaoshangilia si kwa kuwa Lengai Sabaya amefungwa, bali kwa kuona haki imetendeka. Ni jambo la huzuni kwa kijana mdogo kuhukumiwa kifungo kikali kiasi hicho, lakini hakuna namna.

Yeyote anaweza kujikuta yuko jela, ama kwa haki, au kwa kuonewa. Kwa hili la Sabaya lililosindikizwa na teknolojia ya CCTV, na kama mwenyewe alivyokiri, limetushawishi tuseme mkono wa serikali uende mbali zaidi kwa wengine.

Wakati akijitetea, alisema yote aliyokuwa akifanya, aliyafanya kwa baraka za wakubwa wake serikalini. Miongoni mwa aliowataja ni Rais wa wakati huo. Haya ni madai mazito. Fikiria, rais anamtuma mkuu wa wilaya kwenda kupora kwa mtutu wa bunduki! Haya ni madai mazito sana. Japo ni magumu kukubarika kichwani, bado ujasiri wa Sabaya unaashiria jambo kwenye madai yake, maana kama wakubwa walikuwa hawakubaliani na uhuni na ufedhuli wake, kwanini walikaa kimya? Huo ukimya uliashiria nini kama si kubariki uhalifu huo? Haya ni madai mazito.

Sabaya ni tone dogo sana katika bahari ya uonevu. Amejulikana kwa sababu alitumia njia iliyotuwezesha tuone anayofanya. Tukitaka kufukua tutaona mengi, makubwa, mazito na machafu kuliko haya. ‘Wahuni’ waliotumia madaraka kuumiza watu wasio na hatia ni wengi kweli kweli.

Bado tunakumbuka namna Mkoa wa Arusha ulivyogubikwa na matukio ya uchomaji moto shule nyingi. Taarifa zilizopo ni kuwa uchomaji moto huo ulikuwa mkakati wa viongozi wapenda madaaraka kuonyesha waliokuwa na madaraka hayo wamefeli kuongoza. Ilikuwa vita ya kuwania ukubwa. Hilo walifanikiwa.

Tunajua mkuu wa mkoa aliyewatesa wafanyabiashara na matajiri wengine kwa kuwaundia kesi kwa husuda baada ya kunyimwa fedha na mali alizoomba. Akawatumia Takukuru kuunda kesi zisizo na ushahidi akidai ni maelekezo kutoka Ikulu.

Watu wamewekwa mahabusu kwa miaka miwili hadi mitatu kwa uonevu wa waziwazi, na wametoka rumande baada ya kulipa fedha za dhuluma. 

Mkuu wa mkoa akafikia hatua ya kuzuia watu kwenda kusalimia wapendwa wao mahabusu. Akaagiza wanyimwe huduma muhimu. Watu wameumizwa mno kana kwamba hawakuwa katika nchi yao.

Watu wanapomshangilia Rais Samia Suluhu Hassan wanafanya hivyo kwa maana halisi ya kujawa furaha. Amefuta dhuluma. Watu hawakuwa na amani. Simu zilikuwa za WhatsApp kwa hofu ya kudukuliwa simu za kawaida. Watu walijawa hofu na wakaishi kwa shaka kuu kama waishivyo digidigi ndani ya pori lenye simba na fisi.

Hao hao viongozi miungu-watu walikuwa wakiwatukana viongozi wengine wakijiona wao ndio alfa na omega katika ulimwengu huu. 

Tanzania ikawa yao. Waliimba mapambio ya kila aina alimradi tu kumpumbaza mtawala aamini anakwenda vizuri.

Tulikuwa naye mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa wakati huo ambaye nchi ya Marekani yenye vyombo vya uchunguzi kuliko nchi yoyote katika sayari hii imethibitisha pasi na shaka uhusika wake mkubwa kwenye genge la utesaji na mauaji ya binadamu. Akapigwa marufuku asithubutu kuzuru Marekani kwa sababu ni muuaji.

Kukawapo tuhuma za viongozi kujipatia fedha na mali kutoka kwa waliotuhumiwa kujihusisha na biashara haramu, lakini hakuna aliyehangaika kuwachunguza au kuwafikisha mbele ya sheria. Bado Watanzania wanakumbuka tambo zao za ulaji maisha usiokaribiwa na wanadamu wengine hapa nchini.

Mtu huyu ambaye Marekani imesema ni mtesaji na muuaji, hakuna dalili za kuhojiwa wala kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Aliongoza magenge yenye silaha kuvamia vituo vya televisheni na redio akijiona ana mamlaka ya ki-mungu.

Bado Watanzania walioumizwa wanayakumbuka magenge ya kiharamia yaliyowatisha kwa silaha mchana kweupe watu kama Nape Nnauye. 

Bado wanawakumbuka wahuni waliojipachika usemaji wa nchi – wakitukana kila waliyedhani ni tishio la ulaji wao wa maisha. Wakajipendekeza kwa kila hali hata wakawatukana wazee mashuhuri waliolitumikia taifa letu kwa moyo na uadilifu wa hali ya juu sana. Wakawafanya wazee wasiwe na thamani katika nchi waliyoihangaikia.

Walihakikisha wanajipendekeza kwa watawala na wakawa viwanda vya kuunda majungu na uongo alimradi tu wawe wazuri na wengine wanonekane hawafai mbele ya watawala.

Magenge haya ya kihalifu yaliyojipenyeza kwenye mfumo wa utawala yakawa na ukwasi usiokuwa na maelezo. 

Wakati wengine tukihangaika na kulia ugumu wa maisha, wao wakawa wanaajiri hadi walinzi binafsi alimradi tu waonekane ndio wenye nchi.

Tunapoendelea kujadili kifungo cha Sabaya tusisahau madhila yaliyotendwa na magenge haya ya kihalifu na kihuni yaliyojipa uhalali ndani ya mfumo wa utawala wa nchi.

Magenge haya haya mengine yalikuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yakiwa yameshika nyadhifa kubwa. Machoni yakahubiri mapambano dhidi ya rushwa hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. 

Matokeo yake wakawa manabii wa rushwa na kugeuza kura za maoni ndani ya CCM kuwa biashara kubwa na mbaya kuwahi kutokea katika historia ya chama.

Kundi hili hili lililovuruga haki ndani ya chama na kuendekeza ubabe, leo linahubiri uongozi bora na linataka Watanzania wawe wafuasi wao! Bado wako kwenye lepe la ulevi wa madaraka. Wameuvaa ujasiri wa kumpinga rais na mwenyekiti. Wanasema ni haki yao kutoa maoni, lakini haki hizo za kikatiba na kisheria hawakuziona wakati wa kutamba kwao madarakani. Zama zao waliwadhibiti wote waliompinga mwenyekiti hata kama zilikuwa hisia tu.

Lililo dhahiri ni kuwa kama kuna siku magenge haya ya utesaji yatafikishwa mbele ya sheria, Sabaya akaonekana malaika. Wapo waliofanya mambo ya hovyo na mabaya zaidi. Wapo waliosababisha watu wapoteze maisha kwa msongo wa mawazo. Wapo waliosababisha watu wakimbie familia zao kwa kuhofu kuteswa.

Muhimu katika yote haya ni ukweli kwamba machozi na damu ya mwanadamu huwa haipotei bure. Imeandikwa katika Mithali 21:13 “Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.”

Naam! Sasa ni zamu ya walioziba masikio kulia. Tumuunge mkono Rais Samia katika mkakati huu wa kutenda haki kwa Watanzania wote.

572 Total Views 7 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!