“Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa huru na wa haki.” Ni maneno thabiti na kuntu yaliyotamkwa na Rais Dk. John Magufuli akiutangazia ulimwengu na wananchi.

Kauli hii inatia mihemko na imani katika mioyo na vichwa vya Watanzania, pia wale wote wapenda haki na amani katika mwenendo wa maisha yao. Wote wanasubiri kushiriki katika uchaguzi kwa furaha amani na utulivu.

Neno huru ndiyo mashiko ya fasihi hii leo. Watanzania hivi sasa wamo katika mazungumzo na mijadala binafsi kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasema sawa. Kwa sababu nchi yetu ni taifa huru na lenye sifa na uwezo wa kujiamulia mambo yake lenyewe.

Hitaji la Tume Huru ya uchaguzi si geni kwa Watanzania. Limeanza kutinga ndani ya fikra na mawazo yao tangu mwaka 1991, katika iliyokuwa Tume ya kuangalia mfumo bora wa siasa nchini (vyama vingi vya siasa) iliyokuwa chini ya Jaji Mkuu Francis Nyalali.

Likapata makazi katika Tume ya Kuratibu Maoni kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1999 chini ya Jaji Robert Kisanga. Na kufahamika pasi na shaka mwaka 2013 katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2014, chini ya Jaji Joseph Warioba.

Bunge la Katiba, asasi za jamii, asasi za serikali, taasisi za dini na umma nchini zimepokea na kuridhia hitaji la kuweko Tume Huru ya Uchaguzi. Kongole kwa marais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete kuunda na kuridhia tume hizo.

Rais Dk. John Magufuli kukubali na kutamka kuwako uchaguzi huru na wa haki, ni kuridhia maoni na matakwa ya wananchi. Hapana shaka kauli hii itatoa mshindo kwa sababu Rais Magufuli ni kiongozi mwadilifu, mchapakazi na akisema anatenda.

Huru ni neno rahisi kutamkwa na jepesi kuhitajika na mtu yeyote apendae. Lakini ni gumu kueleweka na zito kutumika, kutokana na asili na maana ya neno. Sina uhakika iwapo wewe mwenzangu unaelewa maana ya huru. Sikia. Huru ni kama vazi koti, joho n.k. linahitaji umakini katika kulivaa mwilini.

Huru ni vazi la moyo na nafsi ya mtu. Sakafu ya moyo na nafsi lazima ziwe huru kupinga dhuluma zote na kutii ukweli wakati wote. Huru ina sifa zake mbili, wajibu na haki. Unapotimiza wajibu utapata haki, na usipotimiza utakosa haki. Sifa hizi kila siku zinawasumbua wanadamu katika mambo yao.

Mtu au kiongozi mwelevu hawezi kudai haki bila kwanza kutimiza wajibu. Kuwa na tume huru ni jambo moja na kuwa na watendaji huru ni jambo jingine. Ukweli ni kwamba unapokuwa na watu huru ndiyo kunapokuwa na tume huru. Je, watu hao ni huru?

Huru ya mtu si umbile, sura nzuri, au usemaji wa itikadi na lugha safi. Ingekuwa hivyo ndivyo tusingepata viongozi uchwara, wazembe, wezi, wasaliti na wengine wa aina hiyo. Ili uwe kiongozi huru moyo wako na nafsi yako ziwe zimejaa ukweli na haki.

Watanzania tunapodai tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi maana yake tuwe na viongozi na watendaji huru katika sakafu ya mioyo na nafsi zetu. Kauli na matendo ya watu hao yaonyeshe uhuru wa mioyo na nafsi.

Tunapotamka uchaguzi utakuwa huru na wa haki, ina maana waandaaji, watendaji na wasimamizi wa Tume Huru ni watu huru watakaofanya kazi kwa amani na salama. Tume Huru haianzii kwa viongozi wa tume, inaanzia kwa wananchi wenyewe. Sisi tunaotaka Tume Huru tupo huru?

Tume Huru ya Uchaguzi ni chombo kama vile ilivyo Mahakama, kusimamia na kupatikana haki baada ya wajibu kutekelezwa ipasavyo. Tume Huru ya Uchaguzi si dude au chombo cha kuwekwa kufurahisha watu kama ufanyavyo mshumaa.

Zipo sifa nyingi zinazomwezesha mtu kuwa kiongozi au mjumbe wa tume. Sifa kuu mbili kupita zote, awe ni mwaminifu, mwadilifu na mwenye mwenendo usiotiliwa shaka na jamii. Pili, awe ni mtu ambaye hajawahi kushika nafasi ya madaraka katika chama cha siasa.

By Jamhuri