Si kwamba ninapingana na vitabu vitakatifu, la hasha! Lakini nina uhakika mimi na wewe wote hatuna ushahidi wa kile ambacho kinatendeka huko mbinguni ambako hata mimi nina ahadi nako kwa kuishi maisha yenye raha sana iwapo nitatekeleza zile amri kumi za Musa.

Kuishi kwingi ni kuona mengi, kama unabisha basi jua kuwa una miaka michache hapa duniani. Omba Mungu akujalie miaka mingi zaidi upate cha kusimulia. Nina mambo mengi ya kusimulia lakini kwa kuwa kizazi hiki ni cha jana, wengi hawatanielewa, wenzangu wametangulia makao mapya, sina watu wa kuzungumza nao historia ya kweli.

Leo ninaandika waraka huu kwa sababu nyingi, lakini kubwa zaidi ni kwa wale ambao wanafanya dhambi mbaya zaidi duniani wakiamini wao wataishi vizuri. Kwa uzoefu wangu hakuna aliyewahi kuishi vizuri kwa sababu ya matokeo ya ubaya na akamaliza maisha yake vizuri hapa duniani.

Kuna wakati ninakumbuka mambo yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu juu ya mapigo saba ya adhabu ya Mwenyezi Mungu. Pia katika maandiko hayo  ninaikumbuka mvua ya moto iliyoshuka huko Sodoma na Gomora. Ninakumbuka matendo ya waadhibiwa na nyakati tunazopitia. Najipa faraja ya kutojifunza kuogelea kwa sababu ya Agano la Mwenyezi Mungu kutorudisha gharika kwa awamu nyingine.

Sisi binadamu, naamini, tunapenda maendeleo na maendeleo yakizidi tunaanza kufuru. Wapo waliofikiria kubadilisha jinsi zao kwa sababu tu wamechoka kuwa na jinsi walizopewa na Muumba. Wapo ambao wanadhani ni bora kuoana na wenye jinsi moja na wenzao kwa kuwa hawataki tena amri iliyowekwa na Muumba kuja kuzaliana na kuijaza dunia. Hiki ndicho kiburi cha mwanadamu akiwa na ziada ya utajiri.

Tumeachana na maelekezo ya vitabu vitakatifu katika kuonya watoto wetu, kuwa na subira ya kuoa, kutoadhibu binadamu wenzetu, kuwa na muda wa kumshukuru Muumba na mengi ambayo yamo katika vitabu vitakatifu vyote duniani, ukiachilia mbali zile amri ambazo tulipewa kupitia mitume.

Sisi binadamu tumekuwa na kiburi sana sasa hivi, tunajiona ni miungu katika maisha yetu, tunataka kunyenyekewa kuliko aliyetuumba, tunafanya miadi kama vile ndio wamiliki wa roho zetu. Hiki ni kiburi cha kusahau baada ya ulemevu wa mali au madaraka.

Badala ya kuchinja kondoo sasa hivi binadamu tunachinjana mchana kweupe wenyewe kwa wenyewe, bila hofu ya Mungu wala kuogopa kutoa roho ya binadamu mwenzetu. Leo tunapeana uongo wa dhahiri kana kwamba katika amri zile hakuna mahali tulipoonywa juu ya kusema uongo.

Leo tunatumia gharama kubwa sana kutengeneza silaha za kivita, hatuendi sayari nyingine kupigana bali tunajiandaa kupigana wenyewe kwa wenyewe. Ninajua sitakuwa Mungu, lakini pia ninajua mwenyewe ana huruma sana na sisi na bado anatutazama kwa kujiuliza, hawa binadamu wanaelekea wapi? Anatupa muda wa kutubu lakini sisi muda huo tunatafuta ugomvi wa kuanzisha vita.

Nawakumbuka watu wengi sana ambao wameua na wao wakafa pia. Ninawakumbuka waliokufa kwa mateso makali sana kutokana na mambo ambayo waliyafanya hapa duniani. Ninawajua watu wachache ambao wamepoteza maisha yao na tulio hai tukasikitika kwa mapengo yao.

Ninajua kuna tamaa ambazo zinatufanya tutoe utu wetu kama binadamu, ninajua kuna watu ambao hawajui katika maisha yao kama kuna msamiati uitwao kifo, ninajua wako watu wenye fedha na mali lakini hawana uwezo wa kununua uhai. Kwa lugha nyepesi mali na fedha  si kitu katika maisha tuyaishiyo.

Tukubali kuwa mali na fedha ni matokeo ya majaliwa ya duniani, ambayo hayana thamani katika ulimwengu wa roho safi mbele ya Muumba. Kila mtu afikirie anafanya nini ili kumfurahisha binadamu mwenzake na matokeo yake yatakuwa kamfurahisha aliyemuumba.

Wosia wangu kwenu wenye maisha marefu ni kwamba ili muweze kuepuka mapigo ya corona, BP, vita, mafuriko, vimbunga na mengineyo kama hayo, basi kumbukeni kuacha mambo ya Sodoma na Gomora, kumbukeni kuacha kufanya mambo yasiyomfurahisha binadamu mwenzio na ndipo muumba atatupa baraka zake na kutuepusha na majanga yote ya hatari.

Ipo siku ambayo tutaiona dunia kuwa jehanamu kamili kwa matendo yetu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri