Mafanikio katika akili yangu (21)

Katika toleo liliopita tuliishia katika aya isemayo: “Lakini mume wangu nina safari ya kwenda Afrika,’’ alisema mama yake Meninda. “Afrika unakwenda kufanya nini mke wangu?’’ aliuliza profesa kutaka kujua. “Ni safari ya kikazi nchini Tanzania,” alisema. Sasa endelea… 

Profesa akaona kama ni muujiza. Kisha akamwambia mke wake: “Nina mgeni hapa nyumbani ni kijana kutoka nchini Tanzania amenitembelea,’’ alisema profesa akimwambia mke wake. 

“Aisee ninaomba unipe nimuulize baadhi ya vitu,’’ alisema Mama Meninda akiwa anapata shauku zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida.

Profesa akatoka hadi sebuleni akamkuta Noel na Meninda wakiwa wamekaa. Profesa akafika na kumuwekea Noel simu sikioni. Noel akasikia sauti ya kike katika simu. “Haloo, haujambo?’’ Noel akaitika: “Sijambo!’’ Mke wa profesa akamuuliza: “Eti umetokea Tanzania?’’ Noel akajibu: “Ndiyo nimetokea Tanzania.’’ Aliongea Noel akiwa hajiamini kutokana na kutojua kilichokuwa kikiendelea.  “Sawa, huko kuna mbuga za wanyama?’’ aliuliza. 

Noel akajibu kwa kukubali, kisha profesa akachukua simu na kuongea na mke wake. “Naam! Mke wangu,’’ aliongea profesa kwa upendo. Noel alikuwa makini kuangalia maisha ya profesa. Aligundua alikuwa na upendo hadi kwa mke wake. “Yaani huyo kijana natamani kumuona,’’ alisema mama yake Meninda katika simu. “Utamuona tu siku moja lakini pia ni mwandishi mzuri.’’ 

Mke wake akakumbuka walikuwa wakimtafuta mtu wa kuandika vitu kuhusu haki za binadamu. Alipolikumbuka hilo akamwambia mume wake: “Halafu ngoja niulize hapa ofisini tulikuwa tunahitaji mtu anayeweza kuandika vizuri machapicho ya haki za binadamu.’’ 

Profesa baada ya kusikia hivyo akamwambia: “Tena huyu kijana anaweza, ana kipaji kikubwa.’’ Noel na Meninda wao walikuwa kimya kusikia alichokuwa akiongea profesa na mke wake. “Sawa ngoja niulize kesho nitakupa jibu,’’ alisema mke wa profesa kisha wakamalizia maongezi yao na kukata simu.

Noel na Meninda walikuwa wakimsikiliza profesa lakini wakati huo pia walikuwa bize na kuangalia barua pepe ya Noel. Meninda alikuwa amepanga kila alilokuwa analikusudia kwa Noel hataweza kulisema mpaka litakapokuwa limekamilika.

Nia yake ilikuwa ni kuhakikisha Noel anasonga mbele. “Noel wewe tulia usiwe na pupa, nina mambo ninayaweka sawa huko, yakienda vizuri hautajuta kuja Moscow hata kama ukiwa unasoma utasoma bila msongo wa mawazo,’’ alisema. 

Noel aliposikia vile na akizingatia pia Meninda alikuwa akifanya kazi katika shirika kubwa, alijua atakuwa huenda akimwandalia nafasi nzuri ya kuonyesha uwezo wake mkubwa alio nao katika uandishi. Noel alifanya kila aliloweza katika kompyuta ya Meninda, ghafla usingizi ukaanza kumpata. 

“Dada Meninda tukalale kesho nitaendelea kuandika kitabu changu,’’ alisema Noel huku akiwa anasimama kujiandaa kuelekea chumbani kwake kulala.

Penteratha naye akiwa ameandika kiasi cha kufikia mwisho, akakumbuka: “Juma linalofuata ni juma la maadhimisho ya vitabu katika mji wa Moscow.” Alikumbuka Penteratha kisha akatoa simu yake na kumpigia profesa mmoja aliyekuwa idara ya uchapishaji katika Kitivo cha Fasihi ili ampatie utaratibu wa kupata meza au eneo la kuuzia riwaya zake. Alipopiga simu ya profesa huyo ilikuwa bize ikitumika, akaamua kuacha kwanza na kuendela na mambo mengine. 

***

Nchini Tanzania katika Jiji la Mwanza, yule mkurugenzi wa redio aliyokuwa akifanya kazi Noel pasipo malipo yoyote alipewa namba za Zawadi, dada yake Noel, akaamua kumpigia simu usiku huo bila kupoteza muda. 

Zawadi akiwa anaagana na mchungaji huku akiwa na mama yake, mara simu yake ikaita. Zawadi akaangalia simu yake akagundua ilikuwa ni namba ngeni. Akaagana na mchungaji kwa haraka na kwenda ndani, kisha akaipokea hiyo simu.

“Haloo!’’ aliongea kwa sauti ya chini Zawadi. “Habari yako, mimi ni Mkurugenzi wa redio…” Alijitambulisha mkurugenzi kisha akaenda moja kwa moja katika dhumuni lake. 

“Naomba namba ya kaka yako Noel.’’ Zawadi hakusita kumwambia ukweli. “Noel hayupo Tanzania, alikwenda kusoma nchini Urusi,’’ alisema Zawadi pasipo kupindisha maneno. Mkurugenzi wa redio akaishiwa shauku, akakata simu kisha akatoka ofisini mwake akiwa mwenye mawazo mengi. “Dah! Sasa tutafanya nini?’’ alikuwa akijiuliza na akashindwa kupata jibu kwa wakati huo.

Mchungaji akatoka nyumbani kwao Noel akiwa mwenye furaha na amani moyoni. Kabla hajaondoka, walifunga mazungumzo yao kwa maombi na mama yake Noel. Sasa alikuwa ndani ya gari lake akielekea nyumbani kwake alikokuwa akiishi. Nyumbani alipokuwa akiishi palikuwa nje kidogo ya mji.

Mama Noel aliingia ndani huku akiwa anaongea: “Kumbe mwanangu Noel atafika mbali, nilifikiri amekwenda kuwa mtu wa ajabu huko Urusi,’’ alisema Mama Noel akiwa anaweka pesa mezani alizokuwa ameachiwa na Mchungaji. Zawadi alitoka kule alikokuwa anaongea kwa njia ya simu na mkurugenzi wa redio amemaliza kuongea na simu kisha akamjibu mama yake.

“Si nilikwambia mama, Noel watu mpaka sasa wanamkumbuka, nimetoka kuongea na mkurugenzi wa redio anamuulizia.’’ Mama yake akasimama na kuanza kumsikiliza Zawadi. “Heee! Si alimfukuza?’’ alishangaa Mama Noel. Tumaini lilikuwa limemjia mama yake Noel baada ya kuongea na mchungaji na kupewa mustakabali wa mipango vizuri. Mama Noel akajikuta kuhamasika Noel kwenda nchini Urusi kusoma.