Wiki mbili zilizopita nilipata fursa ya kusafiri kwenda Rwanda, Burundi na mkoani Kagera. Sehemu kubwa ya safari hii nilitumia gari. Nimepita nchi kavu kutoka Mwanza, Bukoba Mjini, Biharamulo hadi Ngara. Niliyoyaona yamenikumbusha nchi ilivyokuwa miaka ya nyumba kwenye suala la umeme.

Katika wilaya karibu zote za nchi hii, Serikali imetandaza nguzo za umeme. Chini ya Mpango wa Umeme Vijijini (REA), umeme umefika karibu kila kata ya nchi hii. Wakati unapita njiani, unakutana na nguzo zilizorundikwa kandokando ya barabara hadi unashangaa.

Ikumbukwe kabla ya Maswi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, nguzo ilikuwa ni bidhaa adhimu kwa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO). Maswi alipata kusema kuwa kuna mchezo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wanatoa nguzo Iringa, wanazipeleka Kenya kisha wanazirejesha nchini wakidai zimetoka Afrika Kusini.

Tukumbuke jinsi tulivyokuwa tunawabembeleza TANESCO watuwekee umeme hata fomu (lile karatasi la kijani) zilivyokuwa zinaleta shida kupatikana. Bila fedha ilikuwa huwezi kupata umeme, ila sasa hivi TANESCO wanampigia simu mteja kumwomba radhi kwa kuchelewesha kumuunganishia umeme.

Mimi natokea Kata ya Nyanga, iliyopo Bukoba Mjini. Tangu enzi za mkoloni hii ni kata pakee iliyosalia hadi mwezi huu bila kuwa na umeme. Chini ya REA, nimshukuru Maswi, Mkurugenzi Mkuu wa TENESCO, Felchesmi Mramba, na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela, kufikia Januari 25, kwa maagizo halali ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera umeme utawaka pale Nyanga.

Nimeitaja Kata ya Nyanga kama mfano. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Maeneo mengi ya nchi hii kwa sasa umeme umefika. Tukumbuke Maswi alipoingia rasmi Nishati mwaka 2009 jinsi tulivyokuwa na mgawo wa umeme. Dar es Salaam katikati ya jiji iliko ofisi yangu, ilikuwa kwa wiki tunapata umeme siku mbili tu.

Sitanii, leo katikati ya Jiji la Dar es Salaam umeme ukikatika baada ya Maswi kusimamia mradi wa kujenga laini mpya ya umeme inayounganisha Ilala na City Centre kupitia Kituo Kikuu cha Polisi, tunajiuliza kuna nini. Majenereta mengi yaliyokuwa yanashindanisha sauti katikati ya jiji leo yamedoda.

Wenye wengi wa maduka ya majenereta sasa wamebadili biashara maana hayauziki. Hata sisi tulioyanunua zamani, labda kwa kuwa leo nimesema ndipo umekumbuka kwamba ofisi yenu ina jenereta. Yote haya ameyafanya Maswi kwa uadilifu mkubwa, ila leo eti anachunguzwa kwa suala ambalo wahusika wamejitaja wazi kuhusika la Escrow.

Sitanii, kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, limenishangaza. Jambo la kwanza lililoingia kichwani mwangu ni kwamba, hivi Tanzania tumepataje upofu kutoona aliyotenda Maswi?

Jambo la pili, niliangalia nguzo zilizosambazwa nchi nzima na nikakumbuka kuwa mpango wa REA ulikuwapo siku nyingi na kila tukinunua umeme tunalipia REA, hivyo Maswi kwa kubana fedha hizi zikanunua nguzo kweli, na kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi huenda kuna watu wanataka tuanze tena kununua nguzo kutoka Afrika Kusini wapate fedha. Labda kuna mkono wao.

Nimejiuliza, kabla ya kuandika makala hii, nikakumbuka enzi za TANU tulikuwa na ahadi moja ya mwana-TANU, ambayo ilisema hivi: “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.” Ahadi hii ndiyo iliyonisukuma kuandika makala hii.

Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi kwa sababu ya fedha za Escrow. Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali katika taarifa yake, iliyosomwa na Zitto Kabwe ilieleza jinsi Maswi alivyoandika barua kupinga kutolewa fedha za akaunti ya Escrow akiamini kuwa katika fedha zile kuna fedha za Serikali ndani yake.

“Mheshimiwa Spika, kufuatia madai ya PAP kutaka kulipwa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, tarehe 16 Septemba, 2013 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bwana Eliakim Maswi, alimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali barua Kumb. Na CBD.88/147/29 akimwarifu kuwa PAP imepewa umiliki wa hisa za IPTL kwa uamuzi wa Mahakama wa tarehe 5 Septemba, 2013.

“Hata hivyo alimwarifu pia kuwa Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa capacity charges kati hiyo TANESCO na IPTL na hivyo umiliki wa fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya(o) utabainika baada ya wahusika kukutana na kujadiliana juu ya jambo hili.

“Katibu Mkuu aliomba mwongozo wa kisheria kuhusu masuala hayo na akaambatanisha mapendekezo ya makubaliano ya utolewaji wa fedha kwenye akaunti hiyo yaliyokuwa yameandaliwa na Kampuni ya PAP.

“Mheshimiwa Spika, tarehe hiyo hiyo 16 Septemba, 2013 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alimjibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kwa barua Namba AGCC/E.80/6/58 akikubaliana na maoni ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuwa washirika wa Akaunti ya Tegeta Escrow (TANESCO na IPTL) wakae pamoja kuchambua madai yanayoihusu TANESCO.

“Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza kuwa dhamana ya Serikali kwenye mkataba wa uzalishaji umeme ipitiwe na kujadiliwa upya ili kukidhi mabadiliko yaliyotokea na athari ambazo zingeweza kuipata Serikali,” inasema taarifa ya Kamati.

Sitanii, kama hiyo haitoshi, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonesha katika ukaguzi maalum wa Akaunti ya Escrow, inasema kuwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ndiye aliyemshinikiza Maswi alipe fedha hizo.

Kamati ya akina Zitto inasema Maswi alibadili msimamo na kuruhusu malipo, baada ya awali kuwa amekataa malipo hayo yasitolewe. Kisha inasema: “Mheshimiwa Jaji Frederick Werema kupitia barua Kumb. Na. AGCC/E.80/6/65 ya tarehe 2 Oktoba, 2013 alimwarifu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, kuwa ameipitia ripoti ya wataalamu kuhusu utoaji wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwa maoni yake alisema jambo linaloweza kuleta tatizo katika utoaji wa fedha hizo ni hati fungani zilizowekezwa na Benki Kuu.” Kwa hiyo akaagiza fedha hizo zilipwe kwa PAP.

Hata hivyo, bila kuzunguka mbuyu wasichokisema akina Zitto na hawa waliomsimamisha kazi Maswi kupisha uchunguzi, hawakuigusia taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, iliyoweka wazi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alitoa maagizo PAP walipwe kutokana na ushauri wa Jaji Werema.

“Mnamo tarehe 14 Novemba, 2013, PST (Katibu Mkuu Hazina) aliwasilisha kwa utekelezaji, maagizo ya Mheshimiwa Rais ambaye aliagiza kwamba “Maamuzi ya Mahakama Kuu yatekelezwe kama alivyoshauri AG (Mwanasheria Mkuu)”.  Maagizo ya Mheshimiwa Rais yaliwasilishwa kwa PST kwa barua ya tarehe 13 Novemba, 2013, na ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bwana Prosper Mbena,” inasema sehemu ya taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania.

Kama hiyo haitoshi, Jaji Werema akiwa bungeni alieleza kuwa Maswi alimtaka ushauri wasiwalipe PAP akaukataa. Taarifa zote tatu zinaonesha ushiriki wa wazi wa Werema. Hata Rais anasema bayana amefikia uamuzi wa kuruhusu fedha hizo kwa ushauri wa Werema.

Sitanii, katika hatua hiyo ndipo najiuliza ni uchunguzi upi unaofanywa? Serikalini ni kama jeshini. Kama Rais aliishaagiza malipo yatolewe, unashangaa nini msimamo wa Maswi kubadilika (kama kweli ulibadilika?). Kinachotajwa na Kamati kuwa msimamo ulibadilika ni hatua ya Maswi kuwaandikia PAP hapana shaka baada ya kupokea maelekezo halali kutoka kwa Rais akiwataka wathibitishe umiliki wa hisa za IPTL.

Tunafahamu na iko wazi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano hawezi kushitakiwa mahakamani kwa jambo lolote alilolitenda akiwa madarakani. Ibara ya 46 (3) ya Katiba ya Tanzania (1977) inasema:

“Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ibara ya 46A(10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii.”

Ibara ya 46A, inaeleza utaratibu wa kumshtaki Rais bungeni kwa njia ya azimio la kumwondoa madarakani, ambapo zinahitajika theluthi mbili za wabunge wote kuunga mkono azimio hilo, na hapo mleta mashtaka ataruhusiwa kutoa hoja bungeni, ikiwa Spika ameridhika. Hoja ikitolewa, Spika anaunda Kamati na Rais ikifikia hatua hiyo, anaachia madaraka kupisha uchunguzi unaopaswa kukamilika ndani ya siku 90.

Mashtaka dhidi ya Rais yakithibitika, basi anatakiwa kujiuzulu ndani ya siku tatu au vinginevyo urais wake unaisha kienyeji. Akijiuzulu kwa mujibu wa Ibara ya 46A(10), basi anapoteza haki zake zote ikiwamo malipo ya kustaafu na uzeeni, hivyo huyu sasa anakuwa akiruhusiwa kushtakiwa mahakamani.

Sitanii, wewe msomaji unaijua Tanzania yetu. Je, mlolongo huu chini ya mfumo wa siasa zilizopo unaweza kutekelezwa? Kuna wabunge wa CCM wanaoweza kuungana wakasema Rais kupitia ushauri wa Werema ndiye aliyeidhinisha fedha za Escrow kutolewa hivyo akashitakiwa bungeni?

Taabu ninayopata ni kuona nchi yetu inapoteza hata fedha kidogo tulizobaki nazo baada ya wafadhili ‘kututia kifungoni’ kuchunguza kitu ambacho kiko wazi. Hivi leo unachunguza nini wakati Werema amekwishatamka kuwa ndiye aliyeagiza fedha hizo zilipwe?

Pengine watu wasichojua; Werema kwa sasa si Jaji wa Mahakama Kuu. Amejiuzulu wadhifa wake na wala hakuazimwa kwenda kufanya kazi ya uanasheria mkuu. Alipokubali kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tayari alipoteza kinga ya ujaji. Takukuru wanapaswa kumfikisha mahakamani mara moja aeleze kwa nini amesababisha hii sintofahamu?

Sitanii, kwa uhalisia hata Rais Kikwete katika hili ana kinga ya kisheria. Katibu wake amesema wazi kuwa Rais ameagiza malipo haya yatoke baada ya Werema kumshauri kuwa hukumu ya Jaji Utamwa ilihamishia hadi fedha za Escrow kwa PAP. Anasubiri nini Werema uraiani?

Ametamka mwenyewe bungeni kila mtu amemsikia, leo tunapoteza fedha kufanya uchunguzi. Hicho kiburi chake apelekwe mahakamani akayaeleza huko hayo aliyoyasema bungeni kuwa kwa nini aliidhinisha fedha hizo zitoke kabla ya mgogoro kati ya TANESCO na IPTL kuisha.

Kama nchi hii imewafikisha akina Basil Mramba, Daniel Yona, Nalaila Kiula mahakamani, inamwogopa nini Werema? Labda ninachodhani, ikiwa ameshikilia bomu fulani, ambalo akiliachia uongozi wa juu wa nchi utatikisika, hapo tunaweza kujua kwa nini anaendelea kuwa uraiani.

Sitanii, kumwondoa Maswi Wizara ya Nishati na Madini ni kuwarejesha Watanzania katika mgawo wa umeme, kusimamisha miradhi ya REA na wakati mwingine kuwapa fursa waliokuwa wanapeleka nguzo Nairobi kutoka Iringa wakidai zimenunuliwa Afrika Kusini fursa ya kuigeuza TANESCO shamba la bibi.

Si hilo tu, kwa wanaofahamu na kujua utendaji wa Maswi, ikiwa ataondolewa kwa zengwe madarakani na kumtia aibu, hakika wote watakaopata nafasi kazi pekee watakayofanya itakuwa ni kulinda matumbo na vibarua vyao, hawatakaa milele wasukume maendeleo maana wataogopa yasiwakute ya Maswi. Tufikiri kabla ya kutenda. Tunayo nafasi ya kulinda watumishi waadilifu, tusiipoteze.

By Jamhuri