Wiki iliyopita wajasiriamali wawili marafiki zangu wa muda mrefu walinitembelea ofisini, mtaa wa Uhuru, mjini Iringa na tukapata wasaa wa kuzungumza kwa kirefu kuhusu mienendo ya biashara katika mazingira ya sasa.

Ninafahamiana na wajasiriamali hawa wote wawili vizuri sana. Wamekuwa wajasiriamali kwa miaka mingi. Mmoja ni mfanyabiashara wa mazao na mwingine anajishughulisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi na benki za simu (mobile banking).

Katika mazungumzo yetu tulitumia muda mwingi kutafakari kwa kina changamoto kubwa zinazozikabili biashara kwa sasa, na mustakabali wa ujasiriamali tulionao kwa siku za baadaye. Rafiki yangu anaejishughulisha na mazao alieleza kwa kina namna biashara za mazao zilivyopungua faida sambamba na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa husika. Kwa upande wa ndugu yangu wa vifaa vya ujenzi, alieleza kilio chake kuhusu mfumo wa kodi na ushindani mkali uliopo sokoni.

Kimsingi, tangu kutokea kwa mapinduzi na kuendelea kukua kwa kasi kwa teknolojia ya mawasiliano, kumeleta enzi mpya za ufanyaji biashara hasa kwa wajasiriamali wadogo na wale wa kati. Kwa mujibu wa huyu rafiki yangu mwenye biashara ya vifaa vya ujenzi (ambaye ni mzee kiumri); ni kwamba hapo zamani ilikuwa rahisi sana kwa mfanyabiashara kuchukua bidhaa Dar es Salaam kwa Sh 1,000 na kwenda kuiuza Iringa kwa Sh 3,000.

 

Hii ilikuwa ni kawaida kwa bidhaa takriban zote. Asilimia kubwa ya wafanyabiashara walikuwa wanapata faida si chini ya mara mbili, au zaidi kwa bidhaa nyingi walizokuwa wakiziuza.

Kwa siku za nyuma ilikuwa ni rahsi sana kwa mjasiriamali kupata haraka haraka kimtaji na kutajirika. Faida zilikuwa ni mara mbili au zaidi kwa bidhaa nyingi; ikiwa mjasiriamali angeanza na mtaji wa Sh milioni moja ndani ya mwaka mmoja lilikuwa jambo la kawaida kumkuta ana mtaji mara tatu hadi nne ya alioanza nao.

Kadiri siku zilivyosogea hadi sasa, suala la kupata faida kubwa za kupindukia katika bidhaa nyingi linatokea mara moja moja na tena ni kwa baadhi tu ya bidhaa ambazo nazo ni chache mno. Jambo hili limechagizwa na mambo takriban matatu; teknolojia ya mawasiliano, kuongezeka kwa ushindani na kuongezeka kwa uelewa wa watumiaji.

Nikianza na hili suala la mageuzi ya teknolojia ya mawasiliano ni kwamba mteja wa sasa ana nafasi nzuri mno ya kutafuta taarifa tofauti na ilivyokuwa zamani. Wateja wa sasa wamekuwa ni wajanja sana, wanauliza na kupeleleza kabla ya kununua.

Rafiki yangu huyu mwenye duka la vifaa vya ujenzi alieleza hili kwa namna hii; “Unapokuwa na bidhaa mpya dukani kwako hapa Iringa, labda tuseme ni nguo mpya; wateja walio wengi kwa siku hizi kabla ya kukurupuka kununua atajaribu kupiga simu mjini kwa mtu anayemfahamu kuuliza bei ya kule.

“Mteja huyu akiona bei yako inapishana pakubwa kati ya unayouzia wewe na ya kule mjini, hatanunua. Atakachofanya ni kuwa atamtumia pesa kwa simu nduguye wa huko mjini atamnunulia na kumuagizia kwa mabasi.”

Katika habari hii ya wateja kuwa wadadisi mno kumerahisishwa kutokana na mawasiliano ya simu yaliyoenea kila sehemu. Rafiki yangu anayejishughulisha na biashara ya mazao anaeleza kwa hisia kali suala hili kwa jinsi hii; “Zamani tulipokuwa tukienda vijijini kununua mazao tulikuwa sisi wanunuzi ndiyo tunaopanga bei. Siku hizi mkulima akishavuna anapiga simu mjini kujua zinazotembea sokoni.

“Wewe ukienda unakuta ameshapanga bei ambayo unapoyafikisha mazao yale sokoni unajikuta ama inakukata au unapata faida ndogo mno. Zamani ungeweza kununua gunia la mpunga kule kijijini kwa shilingi elfu thelathini na ukaja mjini kuliuza kwa laki moja, lakini kwa siku hizi faida kama hizi ni nadra sana kutokea kwa sababu watu wamekuwa wajanja na waelewa mno kutokana na kukua kwa mawasiliano.”

Kukua kwa miundombinu ya usafirishaji kumefanya ununuzi na usafirishaji wa bidhaa kutoka na kwenda maeneo mbalimbali kuwa rahisi. Kwa sasa mtu aliyepo Mwanza anaweza hata kununua pea moja ya kiatu kutoka Dar es Salaam na akaipata baada ya saa chache.

Hii ina maana wauzaji wa rejareja katika maeneo husika wanatakiwa kushindana vilivyo linapokuja suala la upangaji wa bei. Kwa sasa ukizoea kuwa na bei za juu katika bidhaa ama huduma unazotoa ni rahisi sana si tu kupoteza wateja lakini pia unakuwa katika hatari ya kutopata wateja kabisa.

Hivyo, utabaini kuwa zile zama za kale za kupigilia bei kubwa na kupata faida mara mbili au zaidi, zimetoweka katika ulimwengu wa biashara na tumeingia katika zama za msawazo wa bei, yaani ni zama ambazo moyo wa mteja unafurahi pale anapoona kuwa bei ya bidhaa ni ile ile kule Kigoma kama ilivyo Dar es Salaam.

Inapotokea kuna utofauti basi mteja atafurahi kuona kuwa tofauti hiyo inafidia gharama na usumbufu wa kuisafirisha. Nini maana yake? Ni hivi: Mathalani ikiwa seti ya televisheni inauzwa Sh 250,000 Dar es Salaam na ikwa inauzwa Sh 300,000 kule Manyara, kitu cha kwanza ambacho mteja atajiuliza ni hiki: Je, gharama ya kusafirisha seti hii kutoka Dar hadi Manyara ni shilingi ngapi?

Kama gharama ya kusafirisha ni Sh 50,000 mteja ataridhika kununua seti hiyo kule kule Manyara. Lakini ikiwa kule Manyara seti hiyo inauzwa Sh 400,000 mteja atabaini kuwa kama akiiagiza kutoka Dar na kuisafirisha hadi Manyara bado atabakiwa na Sh 100,000; atakachofanya ni kuinunulia kutoka Dar. Kwa hakika suala la upangaji wa bei ni moja ya maarifa ambayo wajasiriamali tunatakiwa kuwa nayo makini katika zama hizi.

Ukiacha hilo la urahisi wa mawasiliano, pia kumetokea ushindani mkubwa baina ya wazalishaji wa bidhaa na huduma kwa nyakati za sasa. Kimsingi, wazalishaji wengi wamekuwa wakiwategemea watu wa kati (wasambazaji, wauzaji wa jumla na wauzaji wa rejareja) kufikisha bidhaa zao kwa walaji.

Mfano, kiwanda cha sabuni kikizalisha sabuni kinampa msambazaji, ambaye anampa muuzaji wa jumla, ambaye anampa muuzaji wa rejareja, ambaye hatimaye anazifikisha sabuni hizo kwa mlaji. Mchakato huu wa bidhaa kupita katika mlolongo wa watu wengi umekuwa ukiongeza gharama za bidhaa hadi kumfikia mlaji.

Kutokana na wingi wa wazalishaji na ushindani uliopo sokoni, wazalishaji wengi wamekuwa wakihaha usiku na mchana kutafuta namna ya kufikisha bidhaa kwa mlaji wa mwisho kwa bei ndogo kadiri iwezekanavyo. Harakati hizi za wazalishaji zimewafanya wauze bidhaa moja kwa moja kutoka viwandani hadi kwa walaji.

Siku hizi ni kawaida kuona magari ya viwanda na kampuni mbalimbali zikiwa mtaani zikiuza bidhaa kwa rejareja kwa walaji wa mwisho. Wazalishaji wa bidhaa na huduma kuuza bidhaa moja kwa moja kwa walaji kunaleta changamoto kubwa mno kwa wafanyabiashara wenye maduka ya jumla na rejareja.

Fikiria kuwa kampuni imekujumlishia bidhaa inazozizalisha halafu wakati huo huo inazunguka kuuza kwa rejareja mitaani; wewe utamuuzia nani tena? Si hivyo tu, isipokuwa kampuni nyingi (ambazo ni wazalishaji) zimekuwa na kawaida ya kuuza bei sawasawa kwa wateja wa rejareja na wa jumla. Kwa wewe mwenye duka unayenunua bidhaa kwa jumla, ni vigumu sana kushindana na mzalishaji sokoni ambaye naye anahangaika kumtafuta mlaji wa mwisho huko mitaani!

Kufanya ujasiriamali katika nyakati hizi kunahitaji akili zilizochajiwa sana. Wajasiriamali kwa sasa tunahitaji kuwa na akili zenye ubunifu mkubwa na zinazoona mbali zaidi na zaidi. Kinyume na hapo ni vigumu sana kuona mtaji wako ukikua na kupanuka kwa sababu licha ya ushindani mkali na kunyang’anyana wateja, lakini vile vile faida zinazopatikana katika bidhaa na huduma tunazoziuza ni ndogo mno. Na ikiwa utazembea ni rahisi sana ama kujikuta mtaji unashuka, au unapoteza kabisa mtaji.

Zama hizi ni vema mjasiriamali yeyote akafikiria ujasiriamali wa mnyororo. Ujasiriamali wa aina hii si mgeni sana kwa wengi lakini namna ya kuufanya ndiyo tunatakiwa kuuzoea. Katika ujasiriamali wa mnyororo ni ule uwezo wa mjasiriamali kuanzisha biashara zaidi ya moja zinazotegemeana ama zisizotegemeana, ili kupambana na mabadiliko yaliyopo ama yanayoweza kutokea katika ulimwengu wa biashara.

Katika ufanyaji huu wa biashara, unatakiwa kuiweka akili yako standby kuwahi fursa yeyote inayoweza kujitokeza katika zile sekta ambazo umejipanga nazo. Kama leo biashara inayolipa ni kuuza viatu unaifanya hiyo kiufahasa, na unapoona uuzaji wa viatu unaingiliwa basi unakuwa ‘fasta’ kuhamia kwenye biashara nyingine labda tuseme ya kuuza vyombo. Pia si lazima ufunge kabisa biashara ya viatu, bali unaweza kuanzisha biashara ya kuuza vyombo wakati ile ya viatu ikiendelea.

Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia ninapoitambulisha dhana hii ya ujasiriamali wa mnyororo. Mosi, ni kwamba mjasiriamali hutakiwi kuogopa mabadiliko ya kibiashara yanayojitokeza katika biashara yako.


Ni lazima utambue kuwa mabadiliko ni jambo la kawaida na kamwe kulalamika na kulialia havitakusaidia kurudisha mtaji ama faida iliyopungua. Hali na mazingira ya biashara vinapobadilika unatakiwa kubadilika pia.

Siku hizi tofauti na zamani, kwa sababu zamani ilikuwa rahisi mtu kudumu na biashara ya aina moja katika mazingira yaleyale, kwa mfumo ule ule na kwa staili ile ile hata kwa miaka kumi; akiendelea kuzalisha faida na kukua. Siku hizi mambo ni tofauti, ukianzisha biashara hapa, watu wanaanza kukusoma na kufuatilia faida unayopata.

Unaweza kufanya hiyo biashara hata kwa mwezi mmoja halafu ukashangaa kuona biashara za aina hiyohiyo zimeshaanzishwa na kutapakaa kila kona, tena mara nyingine zikiwa bora kushinda hata ya kwako. Kinachofuatia? Ni wateja kupungua kwako. Ule wakati unapoona biashara yako inazalisha faida ndiyo wakati unaotakiwa kuumiza kichwa kwa kubuni biashara nyingine kwa sababu ndiyo wakati ambao utaingiliwa na wengine.

Pili, ni kuwa mjasiriamali huna sababu ya kufunga ndoa ya kudumu na biashara ya aina moja miaka nenda rudi. Kama unauza dagaa usije ukasema huwezi kuiacha biashara hiyo eti kwa sababu umeizoea hata kama imeshaingiwa na mdudu. Ukifanya hivyo utafilisika na litabaki jina tu!

Tatu, ni kuwa mjasiriamali wa zama hizi unatakiwa kuwa na maarifa na taarifa nyingi, ili uendelee kuboresha biashara yako na kujiboresha wewe mwenyewe.

Yale mazoea ya wajasiriamali kuendesha mambo yao kimyakimya na kisirisiri bila kubadilishana mawazo na wenzao, hayatakupeleka mbali kibiashara katika dunia ya sasa ya kiteknolojia.

Wajasiriamali tunahitaji ushindi katikati ya changamoto kali.

[email protected]

+255 766 719 127 901


By Jamhuri