Misitu inavyokinufaisha Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ (1)

Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi ni mojawapo za wilaya chache Tanzania Bara zilizobahatika kuwa na misitu ya asili ya kutosha ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Pamoja na kuwa na rsilimali misitu ya kutosha yenye aina za miti ya thamani sana mfano, mipingo (Dulbergia melanoxylon), Kilwa ni kati ya wilaya maskini nchini.

Unaweza ukajiuliza nini viashiria vya umaskini katika wilaya kama hii au katika Mkoa wa Lindi kwa jumla. Kama ilivyo katika maeneo mengi vijijini ambako Watanzania wengi wanaishi maisha yao ni ya kiwango cha chini sana kwa sababu hawana kipato cha kutosheleza maisha yao ya kila siku.

 

Wengi hawana shughuli za kila siku za kuwapatia kipato au fedha ili wazitumie kufanya mambo mengine ya kuwaletea maendeleo kama vile kujenga nyumba nzuri, au kununua vyombo vya usafiri, mathalani baiskeli au pikipiki.

 

Pamoja na kutegemea kilimo kama shughuli yao muhimu, bado wakulima wengi vijijini wanatumia nyenzo duni, hususani jembe la mkono na hawafuati kanuni za kitaalamu ipasavyo katika kupanda na kutunza mazao.

 

Isitoshe, bado wanafyeka misitu na kuchoma moto miti na uoto mwingine wa asili, kama njia rahisi ya kusafisha mashamba au sehemu wanazotaka kulima wakati wa mvua za vuli au masika. Kwa maneno mengine, bado ni kilimo cha kuhamahama kwa mantiki kwamba mkulima anafyeka eneo lenye msitu kama hekta moja au mbili kulingana na uwezo wa nguvukazi aliyonayo na kulichoma moto.

 

Eneo hilo hutumika kwa kipindi kifupi cha miaka miwili au mitatu na hatimaye kuhamia eneo jingine kwa mwendelezo huo huo wa kufyeka misitu. Hali hiyo huendelea hivyo hadi msitu unakwisha. Kilimo cha aina hii hakitoi tija ya kutosha na kumwezesha mkulima kupata mazao mengi na ya kutosha, badala yake tunashuhudia uharibifu mkubwa wa rasilimali misitu na mazingira; kitu ambacho kinaashiria kuwapo kwa hali ya umasikini katika kijiji husika.

 

Hali katika vijiji vingi wilayani Kilwa si nzuri, maana mazingira ambayo wananchi wanaishi si mazuri kutokana na kukithiri kwa ufukara. Kaya nyingi nyumba zao ni za miti, udongo na kuezekwa kwa nyasi.

 

Nyumba zilizojengwa kwa matofali yawe ni ya kuchoma au ya simenti na kuezekwa na mabati au vigae ni chache mno; na sehemu kubwa ni nyumba za kutolea huduma kwa jamii kama shule, zahanati, ofisi za vijiji au masoko. Ni wananchi wachache sana wenye nyumba za kuishi za aina hiyo.

 

Vilevile, ni kaya chache au watu binafsi wenye baiskeli au pikipiki; ila simu za mikononi zinaonekana kuenea kwa kasi hasa katika maeneo ya vijijini ambayo yanapata huduma ya mitandao ya simu kama Vodacom, Airtel, Tigo na TTCL.

Kwa hali hiyo kipato vijijini si kizuri na hivyo kuashiria maisha ya kila siku kuwa magumu kutokana na umasikini uliokithiri sana. Hata hivyo, hali au kiwango cha umasikini kinaweza kubadilika iwapo rasilimali ardhi na misitu vitatumika kwa umakini na uangalifu mkubwa na katika misingi endelevu.

 

Mnamo Mei 22-24, 2013 nilipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ ikiwa ni mojawapo ya vijiji 12 vinavyotekeleza mpango wa kutunza misitu ya asili kwa kusaidiwa na asasi isiyo ya serikali (NGO) ya Mpingo Development and Conservation Initiative (MCDI). Asasi hiyo inajitahidi kwa uwezo iliyonao kuvisaidia vijiji kwa kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu ya asili, hasa iliyopo katika ardhi ya vijiji ili viweze kunufaika na kuwapo kwa rasilimali misitu ndani ya ardhi ya vijiji.

Wanafanya hivyo ili wanavijiji kushuhudia rasilimali walizonazo zikiwanufaisha wao badala ya watu wengine kutoka nje ya mipaka ya vijiji na ndani na nje ya Wilaya ya Kilwa. Hadi Juni 2013, MCDI ilikuwa ikishughulikia uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali miti aina ya mpingo pamoja na aina nyingine za miti kama vile mininga, mitondoro, mipangapanga, mikongo na misenjele katika vijiji vitano ambavyo hadi sasa vimeanza kunufaika na mpango huo wa kuwezesha vijiji kusimamia na kutumia vizuri rasilimali misitu kwa manufaa ya wakazi wa kijiji husika.

 

Vijiji ambavyo vimeanza kunufaika ni Nanjilinji “A”, Kikole, Kisangi, Nainokwe na Liwiti. Hata hivyo, vipo vijiji vingine saba vinavyotarajia kunufaika katika siku chache zijazo ambavyo ni pamoja na Ngea, Likawage, Mchakama, Mandawa na Mitole vikiwa wilayani Kilwa, Lindi; na Tawi na Nyamwage vikiwa katika Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.

 

Nikiwa Mwenyekiti wa Bodi ya MCDI nilipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ kujionea mwenyewe hali halisi na kupata maelezo kutoka kwa wanufaika wenyewe. Katika ziara hiyo nilifuatana na wajumbe wawili wa Bodi ya MCDI ambao ni  A. Muro kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kitengo cha Ujenzi wa Barabara ya Morogoro sehemu ya Mabasi ya Kasi; na Paul Nyitti, kutoka Taasisi ya Kuhifadhi Viumbe Hai nchini Tanzania (Wildlife Conservation Society of Tanzania-WCST).

 

Kwa upande mwingine, MCDI imekuwa ikipata misaada ya fedha na ushauri wa kitaalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Viumbe Hai na Mimea: Ofisi za Denmark na Tanzania (World-Wide Fund for Nature-WWF in Denmark na Tanzania), na mashirika mengine ya nchini Uingereza (United Kingdom).

By Jamhuri