Ndugu Mhariri,

 

Siasa ni mfumo wa utawala wenye kuleta ustawi wa nchi kimaendeleo, utumikao duniani kote. Mfumo huu umejengeka kwa misingi yake kutokana na kubeba mhimili mkubwa wa nchi au taifa lolote.

 

 

Hii ina maana kwamba mhimili huu ndiyo wenye kupambanua misingi ya usimamizi wa watu, yaani watawaliwa na haki zao kwa ujumla. Taifa lolote duniani lenye viongozi hufuata siasa na kuitumia siasa katika kupata fursa au kuwa na nafasi kwenye serikali ili kujenga ustawi wa nchi husika.

 

 

Mfumo huu pia umepata historia kubwa kwa Taifa letu la Tanzania kabla ya kuwa nchi huru na pia baada ya uhuru. Kabla ya uhuru palikuwepo na siasa iliyosimamiwa na mkoloni na baada ya uhuru nchi yetu ilianza harakati kidogo kidogo katika kujisimamia kama Taifa huru kisiasa.

 

Hapa ndipo ndipo ninapokubaliana na Watanznai wenzangu kwamba siasa ilitumiwa kujenga ustawi wa nchi yetu na viongozi waliopata nafasi mbalimbali serikalini.

 

Tanzania ilijengwa kwa nidhamu na ustadi wa pekee usioweza kusahaulika kirahisi na wananchi kwani viongozi walitumia mamlaka vizuri, akili, uadilifu na kuweka maslahi yao pembeni ili tu kujenga taswira mpya ya nchi yetu.

 

Hata mimi kamwe sitaweza kusahau juhudi za viongozi hao walioongozwa na nuru iliyowajali watu wote bila ubaguzi, yaani nchi ikawa ya haki sawa kwenye huduma za jamii kama elimu, tena siyo tu elimu bali elimu bora, afya bora, pasipo kuweka matabaka ya matajiri na maskini, viongozi na wananchi.

 

Nuru na tunu hii iliyopendwa na Watanzania kwa uzalendo uliojengeka na kulifanya Taifa hili kupendwa na  wananchi wote. Siasa ilikuwa bora kwa watawala kwani waliitumia vyema kufundisha watu, uzalendo ulioheshimu haki, kuitafuta haki na pia kuitumikia haki.

 

Mwalimu Julius Nyerere alifanikiwa kusimamia uzalendo kwenye Taifa hili kwanza kwa kuwafundisha maadili ya siasa ya  utawala viongozi wenzake, pia kuwa mstari wa mbele kupiga vita viongozi walioonekana kufungua  njia au dirisha la mienendo mibaya ya utawala ikiwemo rushwa, ubaguzi, ulaghai na vitendo vingine vilivyoonekana kuhatarisha ustawi wa Taifa.

 

Leo hili suala la uzalendo limegeuka kuwa maneno mepesi yatolewayo na viongozi walioko madarakani si kwa nia njema ya ustawi wa nchi bali kwa nia ya ustawi wa mafisadi, walaji rushwa, viongozi wasiojali maslahi ya Taifa, yaani Watanzania, waandaji na wanaopitisha uwekezaji usiyokuwa na tija kwa Taifa, wenye fikra na mitizimo ya Tanzania ya leo na siyo miaka 100 au 50 ijayo itakayoendeleza ustawi wa nchi au Taifa.

 

Kibaya zaidi Mwalimu Nyerere aliwapatia viongozi hawa elimu bora aliyoisimamia kwa nguvu na kuitetea popote duniani bila kuogopa na hata alipopewa wakati mgumu na Benki  ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), aliendelea kusimamia uzalendo na ustawi wa Tanzania.

 

Maana kubwa aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ni kuandaa wazalendo wenye taaluma mbalimbali kwa elimu bora waliyopewa, tena bila gharama yoyote, ubaguzi wa maskini na tajiri, kiongozi na mwananchi ili kuzidi kuimarisha uzalendo na ustawi wa Tanzania ya baadaye. Badala yake viongozi hao hao wameitumia siasa vibaya, taaluma vibaya kinyume cha matarajio ya wengi na pia walichoandaliwa kukiendeleza kama kizazi cha wazalendo.

 

Yote waliyoyaacha waasisi wetu yamekanwa na kufutika kwenye akili za viongozi wa sasa na kuamua kufanya siasa kama biashara, ndipo wengi wakaamua kuiita mchezo mchafu.

 

Sina pingamizi kwao kwani yawezekana wamechoshwa na ama matumizi ya siasa vibaya inayostawisha ufisadi, haki kudhulumiwa, ruswa, udhalilishaji, ubaguzi, uonevu, utu kutodhaminiwa, ubinafsi kutawala na pia kusahau, au kufunika waliyotendewa.

 

Sina nia mbaya, lakini ukweli utabakia na utasimama, tena bila kuwa na shahidi kwamba hawa ndiyo wasaliti wa Tanzania. Ni jambo la kushangaza kuona viongozi waliopewa taaluma bure, tena taaluma ya kizalendo, yaani fadhila isiyofutika mioyoni mwao, lakini hawana hata huruma wanapowaona Watanzania wanalalamika namna ya kupata suluhu ya mzigo wa matatizo yanayowakabili yakiwamo ya elimu, afya, usafiri na hili wenyewe wanaloliita janga, yaani ukosefu wa ajira.

 

Kimsingi matatizo ya Watanzania yanatatulika iwapo kutakuwa na juhudi za makusudi, fikra pevu, ushirikishwaji na uwekezaji mzuri kwa  vijana, hasa wasomi ili waweze kutengeneza fursa kwa wale wengine ambao hawakupata bahati ya kusoma, na wala hatuhitaji wawekezaji au mataifa mengine kusaidia kutatua matatizo haya ambayo ni dhahiri na ni wazi kupata majibu yake kutokana na hali ya Tanzania yenye rasilimali adhimu kama ardhi, madini, maliasili, gesi, fursa za ujasiriamali na biashara.

 

Ni dhahiri mambo haya yanashindikana kufanyika kutokana na mifumo ya manufaa binafsi na ulevi wa madaraka. Pia natupa jicho kwa Watanzania wa leo ambao wananena wenyewe kuwa wamezoea shida kama kauli za midomoni zinazodhihirisha kukata tamaa na nchi yao huku zikiwaumiza ndani ya mioyo yao.

 

Si vibaya tulipofikia tukaanza upya kwani hata wahenga walisema, “Kuanza upya si ujinga.” Ni vyema tukajiuliza Watanzania kuwa ni lini aliyekusaliti na akaweza kunufaika na usaliti huo kwa kiasi kikubwa, tena kwa njia ambazo siyo halali atarudi nyuma na kukukumbuka? Japo wahenga walisema, “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo,”ni lazima tugange kwa hatua stahiki ili kuibadilisha Tanzania kimaendeleo ambayo tutayakumbuka na kujivunia kama tunavyomkumbuka Mwalimu Nyerere na si jina lake tu bali juhudi, maarifa, utashi wa kupigana na maadui wakubwa ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

 

Kuharakisha siasa na maendeleo kwa Taifa letu yatupasa kubadili nira yetu kwa moyo wa dhati na kwa viongozi wenye dhati na nchi hii pasipo kuogopa, kurubuniwa au kutumiwa ili tukaitazame kivingine nchi yetu ikiwa na taswira tofauti miaka 50 ijayo.

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU LIBARIKI GAZETI JAMHURI.


Narcis Silvester

 

1264 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!