Wiki iliyopita alifariki dunia mmoja wa watu niliowapenda na kuwaheshimu mno. Utendaji kazi wake uliniaminisha kuwa pengine hakuna haja ya kuwa na mfumo huu wa sasa wa Serikali za Mitaa katika miji, manispaa na majiji. 

Charles Keenja, alifanya kazi kubwa katika Jiji la Dar es Salaam – akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji hilo kuanzia mwaka 1996-2000 akiwa na makamishna kadhaa.

Tume ilituthibitishia kuwa tunaweza kupata maendeleo makubwa na kwa haraka bila kuwa na mlolongo wa uongozi wa madiwani na wengine wa aina yao. Alama iliyoachwa na Mzee Keenja na timu yake itaishi kwa miaka mingi katika Jiji la Dar es Salaam. Kuna siku mahususi nitaandika kuhusu maisha ya uongozi wa Mzee Keenja. Apumzike kwa amani.

Keenja amefariki dunia bila shaka akiwa na kitu kinachomuumiza mno moyoni. Ameondoka Dar es Salaam ikiwa miongoni mwa majiji machafu si tu Afrika, bali duniani. 

Ameondoka akiiacha Dar es Salaam ikinuka kila mahali. Amefunga ukurasa wa maisha yake duniani akiiacha Dar es Salaam na miji mingine ya Tanzania ikiwa ndiyo mashamba darasa ya miji michafu.

Punde tu baada ya Komredi Amos Makalla kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, miongoni mwa matamko yake ya awali ukiacha la ujambazi, lilikuwa la usafi. 

Alianza kupita huku na kule kujionea hali ilivyo, na mara moja akatoa mwongozo. Kwenye mkutano wake na watendaji akaweka hadhari kwa wananchi na viongozi kwamba operesheni ya kulipanga jiji hilo kwa usafi ingeanza mara moja.

Wapenda mazingira wakawa wanasubiri kuona mabadiliko makubwa ya kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kioo cha nchi kweli.

Tukiwa kwenye subira hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia vijana mkoani Mwanza, akatengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya, na Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya ya Morogoro. Rais alisema anawaondoa kwa sababu hakufurahishwa na namna mgambo walivyowaondoa wachuuzi katika maeneo waliyokuwa wakiendesha biashara zao mjini Morogoro.

Kuanzia hapo, si Makalla, wala kiongozi mwingine amethubutu kutamka neno kuhusu wachuuzi waliovamia mitaa jijini Dar es Salaam na katika miji yote nchini. 

Ukimya huu haumaanishi wameridhika na hali iliyopo katika miji yetu, la hasha! Ni woga wa kulinda ajira zao. Mioyoni wananung’unika sana. Walidhani baada ya Rais Magufuli, basi Rais Samia angewapa meno ya kurekebisha hali hii ya aibu.

Haki za binadamu ni kuwatendea wanayostahili wanadamu. Hakuna binadamu timamu anayependa au anayeshabikia binadamu wengine wanyanyaswe. Lakini pia ni haki kwa binadamu kupata kile anachostahili kwa mujibu wa kanuni au sheria. Kama hivyo ndivyo, basi waenda kwa miguu nao wana haki ya kuachiwa maeneo yao ili wapite bila bughudha za wachuuzi.

Miji yetu ni michafu mno. Inatia aibu. Inatia kinyaa. Wageni wanatushangaa. Mara kadhaa tumezungumza nao. Wanatusifu kwa mengi, hasa ukarimu wetu. Wanasifu mandhari zetu asilia. Wanasifu mipango ya maendeleo. Lakini linapokuja suala la ustaarabu, wanatunanga.

Uchafu na mwonekano mbovu wa Jiji la Dar es Salaam ni matokeo ya siasa. Tumekubali tuendeshwe na siasa zaidi kuliko utaalamu na wataalamu. Kinadharia tunazo Serikali za Mitaa, lakini kwa uhalisia, hazipo. Haishangazi kuona watendaji wa Serikali za Mitaa wakiamua mambo kisha yanapingwa au yakafutwa kwa nguvu za kimamlaka kutoka juu.

Dar es Salaam ni chafu kwa sababu kiongozi wa nchi aliamuru watu waachwe wafanye wanavyotaka. Hakutaka kushirikisha Serikali za Mitaa katika kuandaa mipango ya kukabiliana na uzito wa ruhusa yake. Tulipaswa kabla ya kuruhusu uhuria huu, Serikali za Mitaa ziketi na kupendekeza maeneo mahususi ya kuwaweka wachuuzi. Duniani kote kuna wachuuzi, tofauti pekee ni namna ya kuwaandalia mazingira.

Badala ya kuzishirikisha Serikali za Mitaa, amri ikatolewa waachwe wafanye kazi zao bila kuulizwa. Matokeo yake ndiyo haya tunayoshuhudia sasa. Miji haitamaniki. Hapa kuna muuza mihogo, pale kuna mkaanga samaki. 

Yule anakamua miwa bila hata kuwa na hakika ya afya yake. Pembeni kuna fundi bodaboda – anamwaga oili hapo hapo alipo. Pembeni anapita muuza mishikaki na jiko la mkaa likiwaka -hatujui mishikaki ni ya mbwa au paka!

Mama ntilie anauza chakula, lakini hana sehemu ya kumwaga maji machafu. Wateja wake wakibanwa haja wanajibanza kwenye uchochoro au ukuta ulio kando. Hakuna wa kuhoji maana Rais amesema ‘waachwe’.

Maeneo kama CBE na IFM kote kumepangwa mabanda mabovu ambamo wanakula wasomi tunaotarajia wakiwa wamefuzu watusaidie kuishi kisasa – kuishi kisomi – kwa kuzingatia kanuni za afya. Kama haya ndiyo mazingira wanamokulia wasomi wetu, nini kitawafanya wawe na mpangilio wa maisha huko baadaye wakihitimu?

Mbele ya jengo la Wizara ya Afya ambamo tunatarajia wawemo waangalizi wa afya zetu kumepangwa matunda yaliyokwisha kumenywa – nzi wakitua na kutoka kama maonyesho, huku moshi wa bodaboda ukitua kama vile kunamiminwa viungo vya kutia ladha kwenye chakula. Wanunuzi nao wanabofya mihogo na matunda kuona ubora wake. Haujui alikotoka ameshika wapi au ameshika nini?

Vituo vya daladala kuna aina zote za pombe. Hakuna leseni, wala hakuna wa kuhoji. Tumezuia viroba, lakini sasa pombe zinauzwa kwa kupimwa. 

Viwanda hivi vya maradhi vinazidi kuzalisha maradhi huku serikali ikitamba kila mwaka kuongeza bajeti ya dawa za kuwatibu Watanzania! Kwa maneno mengine tumeandaa mazingira ya kuugua sana ili tununue dawa nyingi zaidi. Hii vita hatuishindi.

Mapendekezo, waziri mwenye dhamana aketi na viongozi wa Serikali za Mitaa. Waainishe maeneo (si viwanja vya michezo na ya wazi) kwa ajili ya kuwaweka wachuuzi. 

Mfano, pale Mnzese kunaweza kutengwa bilioni kadhaa wakafidiwa watu, kukapatikana uwanja mkubwa utakaosheheni majengo kwa ajili ya wachuuzi na huduma nyingine za kijamii. Hapo kodi pia itakusanywa. Majengo yawe ya ghorofa. Cairo wamefanya hivyo, twende tukajifunze.

Pili, maeneo kama CBE au IFM mamlaka za manispaa na majiji zijenge vibanda vyenye muonekano wa kisasa ili kuwaweka hao wachuuzi. Tuondoe makaratasi haya ambayo ni uchafu. Hayo yafanywe kote kunakowezekana. Pia vyoo vya umma, hasa vinavyotembea viwepo vingi.

Ndugu zangu, tunachekwa. Uwezo wa kuondokana na aibu hii tunao. Rais awape ruhusa watendaji wa Serikali za Mitaa wafanye kazi, alimradi wasionee watu. 

Tuidhibiti hali hii kabla haijapevuka. Tukichelewa hili ‘jeshi la uchafu’ halitakubali kupangwa ki-mfumo. Tukiendelea hivi kuna siku watatundika bidhaa kwenye ukuta wa Ikulu na hawatakubali kuondolewa.

Dunia ya wastaarabu huishi kistaarabu. Niliwahi kusema huko nyuma kwamba mgeni anapozuru nyumbani kwa mtu, katika mazingira ya Kiafrika, akakuta nguo za ndani zimeanikwa sebuleni, si tu atashangaa, bali atatilia shaka afya ya akili ya mwenyeji wake. 

Kila kitu kina utaratibu wake. Maisha ni utaratibu. Ukiuvunja unaoneka kituko. Leo hii sisi mbele ya macho ya walimwengu tunaonekana hatuko sawa mahali fulani kwenye viungo vyetu, maana tunayofanya si ya kufanywa na binadamu wa ulimwengu wa karne ya 21. Wachuuzi watengewe maeneo yao. Tunatia aibu, tunachekwa.

By Jamhuri