Kwa wiki nzima sasa kuna mjadala unaoendelea hapa nchini juu ya mpango wa kurekebisha viwango vya malipo ya bima ifikapo Machi mosi. Mpango huu unalenga hasa bima kubwa (premiums). Wanalenga kuweka viwango vya kati ya asilimia 3.5 hadi 9 kwa kila gari. Hawakuzungumzia suala la bima ndogo (third part).

Hoja mbili zinatumiwa kutetea mpango wa wamiliki wa mashirika ya bima kupandisha kiwango cha bima. Mosi wanasema ajali zimekuwa nyingi hapa nchini, hivyo wanajikuta wanalipa fedha nyingi na kampuni nyingi za bima kujiendesha kwa hasara, hasa kwenye eneo la magari.


Hoja ya pili ni kwamba Tanzania haina viwango maalum vya bima, hivyo inawawia vigumu wanaoendesha biashara ya bima kupata bima kwa ajili ya mashirika yao (reinsurance) kwani mashirika ya nje yenye kufanya kazi hiyo hayaelewi wanajiendeshaje.


Sisi tunasema hili suala la bima si la kuzomokea. Nchi hii imekuwa na utamaduni wa kugeuzwa shamba la bibi. Wenye makampuni wanachuma tu. Kila mwenye mradi wake katika nchi hii anauelekeza kwenye magari. Magari tayari yameongezewa 30,000 ya zima moto kimyakimya.


Madai kwamba wanapata hasara kwenye biashara ya bima tunayapinga. Kama biashara haizai unafunga na kuanzisha nyingine, lakini hawa wamiliki wa bima wamo tu. Waseme tu, kwamba wanataka kuongeza wigo wa faida lakini si kweli kuwa wanapata hasara.


Kwa upande mwingine, tunakubaliana na wamiliki wa mashirika ya bima kuwa ajali zimeongezeka. Ajali zimeongezeka kutokana na ujio wa magari ya automatic. Watu wananunua magari na kuanza kuendesha kabla ya kufundishwa udereva na wengi wanapata ajali wakiwa wamelewa.


Nchini Uingereza walikuwa na tatizo sawa na letu. Ufumbuzi waliupata kwa kuanzisha utaratibu wa kufuta bima za magari. Walifuta bima za magari na kuweka bima za madereva. Kila dereva analipa bima yake kulinga na uzoefu, historia yake kuhusiana na ajali, kiwango cha mafunzo ya udereva alichopewa na uadilifu wake.


Kwa mantiki hiyo ukitaka kumkabidhi mtu gari aendeshe, unajihakikishia iwapo ana bima hai. Hii itaondoa mwelekeo wa kuwaadhibu madereva wasiopata ajali za kijinga, na itaongeza pato kwani hata kama kila dereva atalipa Sh 70,000 kwa mwaka fedha zitakazokusanywa ni nyingi kuliko hali ya sasa. Bima za magari zisipandishwe, bali zifutwe.


By Jamhuri