Tangu ilipoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, Serikali ya Rais John Magufuli imefanya uamuzi mgumu unaohusu kurejesha mali za umma zinazodaiwa kuhujumiwa pasipo kujali maslahi mapana ya nchi.

Ipo orodha ndefu ya matukio yanayodhihirisha kufikiwa kwa hatua hiyo, ingawa kwa upande mwingine pamekuwapo wakosoaji wa mbinu na njia zinazotumika katika utekelezaji wake.

Pamoja na changamoto zinazosababisha kuibuka kwa hoja za wakosoaji wa mchakato kurejesha mali za umma kutoka kwa ‘waporaji’, ukweli unabaki kuwa hitaji la kuzitetea na kuzilinda rasilimali hizo lipo kwa kizazi cha sasa na baadaye.

Kama ilivyoelezwa awali, matukio yanayohusiana na kurejeshwa rasilimali za umma kutoka mikononi mwa wachache waliozihodhi kwa maslahi binafsi yapo mengi.

Lakini la hivi karibuni ni kuhusu umiliki wa hisa za kampuni ya simu za kiganjani ya Airtel, uliowahi kuibua utata miaka kadhaa iliyopita na sasa Rais Magufuli ametangaza kuutafutia ufumbuzi wa kudumu.

Tamko la Rais Magufuli limeungwa mkono na Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ya simu (TTCL) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Omary Nundu, kueleza kuwa Airtel inapaswa kurejeshwa serikalini na si vinginevyo.

Desemba 20, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, kufuatilia utata uliopo kwenye umiliki wa Airtel akisema ni mali ya Serikali.

Tamko hilo limeibua hoja tofauti ikiwamo kutoka kwa kampuni ya Bharti yenye hisa nyingi katika Airtel, ilipotoa tamko kwamba uwekezaji wake ulifuata taratibu na kupata baraka za Serikali.

Ni dhahiri kwamba tayari Tanzania imeingia katika ‘mzozo’ unaohusu uwekezaji kwenye kampuni hiyo. Sasa kila upande yaani Serikali na mwekezaji mwenye hisa nyingi yaani Bharti wanatofautiana kwa hoja.

Kutokana na hali hiyo, na kwa vile azma hii inatarajiwa kutekelezwa katika maeneo mengine hasa ya uwekezaji nchini, ipo haja ya kuiunga mkono Serikali, lakini pia kuishauri kwamba hatua zinazochukuliwa zisitoe mwanya wa kuibua migogoro ya kibiashara na uwekezaji.

Migogoro ukiwamo wa biashara na uwekezaji ni jambo lisiloepukika katika jamii, lakini inapoyagusa maeneo hayo pasipo mhusika mkuu (Serikali) kuwa makini, inaweza kuleta matokeo hasi. Hilo ni jambo la kuliepuka kwa kiasi kikubwa.

Tunatambua kwamba Tanzania inayoongozwa na sera, sheria, miongozi na maagizo ya mamlaka za utawala katika kufanikisha uwekezaji nchini.
Maeneo hayo na mengine yanayohusika katika ujenzi wa mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na wawekezaji wa ndani na nje, yanapaswa ‘kupembuliwa’ kwa kina kila inapotokea sitofahamu ama mianya ya uporaji wa rasilimali za umma.

Tunaamini kwamba mchakato wa aina hiyo, utaisaidia nchi kupata taarifa sahihi zenye mapendekezo yatakayoongoza kufanya uamuzi ulio sahihi na usiokuwa na athari hasa kwa nchi.

Tunasema hivyo kwa sababu, kile ambacho Rais Magufuli anakiita ‘mambo ya hovyo yamefanyika hapa nchini kwa muda mrefu’, kina asili na vyanzo vyake vinavyoweza kufananishwa na mizizi ya miti.

Vyanzo hivyo ndivyo vinavyopaswa kujulikana na kushughulikiwa haraka, ikibidi kupitia uamuzi na hatua nyingine zinazochukuliwa ikiwamo ya kurejesha rasilimali za nchi mikononi mwa umma.

1026 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!