Kwa sisi tuliozaliwa na kukulia vijijini miezi ya Agosti, Septemba, Oktoba, Novemba na Desemba huwa ni miezi ya sherehe, harusi, ngoma za kila aina na hata ndugu kukumbukana (okuzilima). Miezi hii huwa watu wana furaha. Kingazi cha Julai kinakuwa kimekwisha na hata mavuno waliyopata mwezi Machi, inawabidi washindane kuyamaliza ghalani maana Septemba na Oktoba ni miezi ya mavuno.
Mahindi kwa mikoa mingi hapa nchini yanakomaa kati ya Novemba na Desemba, kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa huu huwa msimu wa senene na wakati mwingine kunakuwapo majani ya kunde, maharage (omushokolo) na mbogamboga nyingi ikiwamo ile maarufu mkoani Kagera – eibota. Hakika katika kipindi hiki huwezi kusikia ugomvi katika familia.
Miezi hii ni ya kutakiana heri. Kimbembe kinakuwa katika miezi ya Januari, Februari, Juni na Julai. Kwa wapangaji mijini Januari tunakoelekea ni mwezi wa balaa. Wenye nyumba wanataka kupeleka watoto shule, na sasa hivi watoto wa mjini wanasema vyuma vimekaza, ingawa bosi wetu anasema vikikaza wekeni grisi, watoto wanadai nguo za siku kuu na wazazi nyumbani wanaita watoto waende kusalimia.
Sitanii, hakika katika miezi kama hiyo kauli za mifarakano katika familia ni jambo la kawaida. Nafahamu kuwa nchi yetu inapitia wakati mgumu. Kipindi tulichomo katika uchumi wa mtu mmoja mmoja ni sawa na miezi ya Februari, Machi, Juni na Julai. Watanzania walio wengi hawakuwa na biashara halali. Hawajui kufanya biashara.
Siku za nyuma tumepata Watanzania wengi waliokimbia kazi zao na kuingia kwenye siasa. Tunao madaktari, maprofesa, mainjinia na wengine wengi ambao ilibidi wawe kwenye shughuli za uzalishaji, lakini sasa wameingia kwenye siasa. Kwa bahati mbaya katika siasa hakukuwapo uzalishaji wa aina yoyote zaidi ya kukusanya posho kutoka mashirika ya umma.
Tunao madaktari wengi katika siasa ambao ukiwauliza, tena wengine ni mawaziri kuwa anasimamia nini, hakuna jibu analoweza kukupatia. Wengine wanaletewa mezani fursa kama za kuuza muhogo nchini China, ukiwauliza sababu za msingi kwa nini hadi leo nchi yetu haijapiga hatua yoyote kuuza muhogo China hakuna majibu ya msingi utakayopewa. Sana sana nimshukuru Katibu Mkuu wa Kilimo, maana angalau ameonyesha kuwa kuna jambo anafanya.
Sitanii, sasa katika mazingira haya ya kutokuwa na ujuzi au biashara yoyote ya maana, hawa walio wengi wanaanza debe la hatari. Wanaanza kumshawishi Rais aliyepo madarakani kuongeza muda kutoka miaka mitano hadi 7. Hii haijaanza leo. Hata wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi lipo kundi lililoomba aongezewe muda. Rais Benjamin Mkapa nilikuwa naripoti Bunge wakati huo, wengine walitaka kupeleka hoja binafsi kuomba ongezewe muda.
Hata wakati wa Rais Jakaya Kikwete, wapo walioanza kampeni za chini chini wakitaka aongezewe muda. Tena wengine walitumia hoja kuwa hajamalizia mchakato wa Katiba Mpya. Hili lilielekea kushika kasi, ila Kikwete mwenyewe kama alivyosema Mkapa, akakataa. Rais Magufuli amekwishakataa, ila sasa baada ya kadhia hii iliyokuwa imeanzishwa na Juma Nkamia, sasa imeibukia Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amechukua maneno ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wachache wenye uroho wa madaraka akasema suala la kuongeza muda kuwa miaka 7 linazungumzika. Napata wakati mgumu. Nchi yetu shida yake si wingi wa miaka ya kiongozi kuwa madarakani, bali mfumo unaofanya kazi.
Mfano mzuri ni taifa la Marekani kwa sasa. Nchi hiyo inaye Rais Donald Trump anayeshinda kwenye mtandao wa twitter, ila hujasikia sarafu ya Marekani imeshuka thamani. Tujenge mfumo badala ya kutegemea watu kuongoza mataifa yetu. Nchi haipaswi kuongozwa kwa matukio, bali sheria, kanuni na Katiba imara isiyochezewa.
Sitanii, naomba kuhitimisha makala yangu kwa kusema hivi: Nchi yetu inahitaji kuwekeza katika uchumi wa viwanda. Kuongeza miaka ya uongozi haitasaidia kumaliza matatizo ya nchi hii bali kujenga misingi ya watu kufanya kazi kwa kutumia mashine. Tusipoteze muda kuleta vurugu za kisiasa kwa kuchezea Katiba.  Alijaribu Komandoo Dk. Salmin Amour miaka ya 2000 hakuweza. Tusipoteze muda. Tuwekeze kwenye viwanda badala ya siasa. Hatuna la kuiga kutoka Rwanda!

By Jamhuri