Juni 9, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwasilisha bajeti ya Serikali bungeni kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Bajeti hii imeficha siri nzito yenye mwelekeo wa kuliondoa Taifa letu katika aibu ya kuwa ombaomba.

Ni kweli, bajeti imerejea maeneo yale yale ya kuongeza kodi kwenye soda, vinywaji baridi, bia na vinywaji vikali.

Hata hivyo, kwa maeneo yaliyoongezeka kasi ya ongezeko zamu hii ni ndogo ikilinganishwa na miaka iliyotangulia. Katika maeneo hayo imeongezeka kwa wastani wa asilimia 5, na kama alivyoeleza Waziri Mpango, ongezeko hili iliwalazimu liwepo kuendana na kiwango cha mfumko wa bei.

Tangu wakati wa kampeni na muda mrefu sasa, Rais John Pombe Magufuli amekuwa akieleza nia yake ya kujenga Tanzania ya viwanda. Bajeti iliyosomwa wiki iliyopita ni ya kwanza katika uongozi wake. Bajeti hii, kwa kila hali, haina vyanzo vipya vya mapato. Bajeti hii ni sawa na mkulima unayekuwa na debe la mahidi, hivyo unao uchaguzi mmoja tu, kula hayo mahindi au kuyapanda yakaota.

Sitanii, bajeti hii imeweka maeneo manne ya vipaumbele kama ninavyoinukuu hapa chini. “38. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu ya Hali ya Uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 una maeneo makuu manne (4) ya vipaumbele:- (i) Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; (ii) Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu; (iii) Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji; na (iv) Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango. 

Ili kufikia malengo hayo, mikakati itakayotumika ni pamoja na: kuhamasisha wawekezaji na sekta binafsi kuwekeza katika viwanda na maeneo mbalimbali nchini hususan kupitia mfumo wa ubia baina ya Serikali na sekta binafsi (PPP); kuondoa vikwazo kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.”

Sitanii, maelezo haya ya Waziri yanajenga dira murua na kutia matumaini kuwa ndoto ya nchi hii kuwa nchi ya viwanda iko mbioni kutimia. Ushawishi unaongezeka, kutokana na kifungu cha 39 cha hotuba ya Bajeti ya Waziri Mpango kinachosema: “39. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, kaulimbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni ‘kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira’.

“Katika kufikia azma hii, Serikali imelenga kutekeleza mikakati mbalimbali itakayochochea uwekezaji katika viwanda. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na: kufanya uthamini wa ardhi na mali na kulipa fidia kwa maeneo maalumu ya uwekezaji yaliyotengwa nchini; kugharamia tafiti za viwanda kupitia taasisi za TIRDO, TEMDO, CAMARTEC na COSTECH;

“Kuendeleza miundombinu ya viwanda vidogo kupitia SIDO; kuanzisha kongane za viwanda (industrial clusters); na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rahisi na nafuu kwa ajili ya viwanda. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 50.9 katika fungu 44 na fungu 46 ambazo pamoja na mambo mengine zitagharamia utekelezaji wa maeneo niliyoainisha hapo juu.”

Sitanii, vifungu hivi viwili ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli ya viwanda. Ukiishapima ardhi, ukafanya utafiti na kuweka mazingira wezeshi, basi ni wazi nchi itapiga hatua haraka katika uwekezaji. Miaka yote naweza kusema kuwa eneo hili ndilo ambalo kitambo halikuwapo kwenye bajeti zetu. Hatua hii inawiana na mfano wangu wa debe la mahindi hapo juu; kwa hili naipongeza Serikali kwani imeamua kupanda mbegu, badala ya kuila.

Mambo mazuri si hayo tu, bali yapo pia mambo mengine mengi yaliyotajwa katika bajeti hii. Mfano, zimetengwa Sh bilioni 59 chini ya fungu la 59 la Bajeti ya Hotuba ya Waziri. Fedha hizi ni utekelezaji wa ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji. Utaratibu wa kuanzisha Saccos kwa kila kijiji na kuwapa fursa wananchi kuchukua mikopo na kufanya shughuli zao ni jambo jema mno.

Hata hivyo, napenda kuipa angalizo Serikali kuwa Saccos hizi inapaswa kuzilea na kuweka utaratibu rafiki usio na mawaa katika kusajili Saccos hizi. Nasema hili kutokana na uzoefu kuwa kusajili Saccos katika nchi hii inachukua muda mrefu. Pia, Serikali ipige marufuku ulipaji wa mishahara kwa watumishi watakaosimamia hizo Saccos.

Hizo Sh milioni 50 kwa kila kijiji ikilipa gharama za maafisa ushirika, zikalipa mishahara na posho, napenda kuwahakikishia zitaisha hata kabla ya kukopesha wananchi. Fedha hizi zitumike kwa ajili ya mikopo tu. Viongozi wa kijiji wafanye kazi ya kujitolea na hiyo ndiyo dhamana na gharama ya uongozi. Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kutaka kiongozi alipwe kila kazi anayoifanya hata ambazo ni kwa maslahi ya umma.

Sitanii, hata hivyo, nia hii njema ya kujenga uchumi imetiwa dosari na kifungu cha 47 cha hotuba ya bajeti ya Waziri Mpango. Katika kifungu hiki anasema: “Hatua za Kudhibiti Matumizi. 47. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kupunguza na kudhibiti matumizi bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa na hivyo kuhakikisha uwepo wa ufanisi katika matumizi ya Serikali.

“Baadhi ya hatua hizo zimeainishwa katika Mwongozo wa kutayarisha Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/17 niliouwasilisha hapa bungeni Februari, 2016. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na: (i) Kuhakikisha mikutano yote ikiwa ni pamoja na mikutano ya bodi, mafunzo na semina inatumia kumbi za Serikali na Taasisi za Umma;

“(ii) Kutoa kipaumbele kwa Taasisi za Umma katika kutoa huduma kwa Serikali kama vile bima, usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi, matangazo na usafiri; (iii) Kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara; (iv) Kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa watumishi ili kuepuka malipo yasiyostahili. Aidha, Serikali itaendelea kufanya sensa ya watumishi wote;

“(v) Kudhibiti utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili kuepuka utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasiostahili; (vi) Kuendelea kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja na bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei; (vii) Kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi;

“(viii) Kupunguza na kuondoa matumizi yasiyo na tija katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadhimisho na sherehe za kitaifa, matamasha, machapisho na safari za ndani na nje ya nchi zisizo na tija; (ix) Kuhimiza matumizi ya nakala laini (soft copy) za machapisho mbalimbali hususan yanayozidi kurasa 50 ili kupunguza gharama za uchapishaji na kutunza mazingira; na (x) Kudhibiti matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Umma yasiyowiana na majukumu yao ya msingi na yasiyo na tija.”

Sitanii, nimeamua kuorodhesha maeneo ya kubana matumizi iliyoyataja Serikali kwa nia moja ya msingi. Nataka kuitahadharisha Serikali. Ni kwa upendo mkubwa naitahadharisha Serikali kuwa ikiwa njia za kubana matumizi zote zilizotajwa hapa yatatekelezwa bila kufanyiwa marekebisho Serikali itaua uchumi. Mwelekeo ulio wazi ni kuwa Serikali inarejea katika kufanya biashara.

Wakati katika bajeti hii Serikali inahamasisha Watanzania kuwekeza katika viwanda, inaweka sentensi za hatari katika bajeti yake kuwa “kipaumbele kitolewe kwa taasisi za Serikali katika kufanya ununuzi mbalimbali.” Mfano hai sekta ya hoteli hapa nchini tayari imeanza safari ya kifo. Hoteli nyingi zimefukuza wafanyakazi kutokana na mikutano mingi kufanywa kwenye madarasa ya shule na vyuo.

Kinachotokea ni kwamba hoteli za kisasa zilizokuwa zinaibuka, ikiwa zitafukuza wafanyakazi na zikafunga biashara, watalii waliokuwa wanaliingizia Taifa dola bilioni 2 kwa mwaka, hawa nao idadi yao itashuka kwa kasi kubwa. Bajeti inasema matangazo ya Serikali yaelekezwe kwanza kwenye taasisi za Serikali, hii maana yake ni kwamba agizo hili linafanya maandalizi ya mambo mawili.

Jambo la kwanza, ni kuwa vyombo vya habari binafsi vinaandaliwa kifo cha asili. Hili la kuvinyima matangazo vife, litazaa jambo la pili. Ni vigumu mno kupata fedha za wananchi kwa kuandika habari za kuisifia Serikali. Kutokana na hilo, nauona mkondo wa vyombo vya habari kutafuta upungufu wa Serikali, kisha wananchi wanunue kwa wingi na wao wapate gharama za uchapaji, mishahara na kodi za Serikali.

Yapo makosa hufanywa na Serikali na namuomba Waziri Mpango akasome hotuba ya Waziri wa Fedha ya mwaka 2006 iliyowasilishwa na Zakia Meghji. Bajeti hiyo ilipandisha usajili wa magari, hadi ikashindikana kusajili magari. Leo imeongeza kutoka Sh.150,000 hadi Sh. 250,000. Si kwamba wenye magari wana fedha nyingi, magari mengi tunayoyaona ni mikopo!

Kosa jingine ni kuongeza ada kwa watu wanaotaka kusajili majina yao badala ya namba za magari. Ada hii ingeshushwa hadi Sh 3,000,000 wangepatikana watu wengi wa kusajili na Serikali ikapata kodi nyingi. Kuiongeza kutoka Sh milioni 5 hadi 10 kwa miaka mitatu, hii inaweza kupunguza idadi ya watu wanaosajili magari kwa namba binafsi na Serikali ikakosa mapato.

Sitanii, ukiacha angalizo hilo kwamba Serikali iangalie isijikute inarejea katika mtego wa kufanya biashara yenyewe kwa yenyewe kutokana na msisitizo uliowekwa kwenye bajeti, nimefurahishwa na msisitizo uliowekwa kwenye viwanda. Kikubwa Serikali ifahamu kuwa ndiye mnunuzi mkuu, hivyo hoja ya kubagua sekta binafsi wakati inawahamasisha kufanya uwekezaji, inaweza kuua mwelekeo wa uchumi. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri