NA ANGELA KIWIA
Ni wiki moja sasa tangu nchi yetu ikumbwe na kilio cha kumpoteza
mpendwa ndugu yetu, Akwilina Akwilini. Sitaki kabisa kukumbuka tukio
hilo lililojaa simanzi na taharuki katika bongo zetu.
Maisha ya Mtanzania sasa yanaanza kuogofya. Tunaishi kwenye nchi
ya amani iliyoanza kumea vilio vya kukosekana na kutoweka kwa
amani.
Tunamzika binti yetu huku Mtanzania mwingine akiuawa kwa kupigwa
mapanga akiwa nyumbani kwake Morogoro.
Godfrey Luema, ambaye ni diwani, ameuliwa kikatili. Ameuliwa kikatili
kwa mwili wake kukatwakatwa na mapanga. Hii si nchi yangu Tanzania
ninayoifahamu hata!
Tumeshuhudia shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, IGP Simon Sirro na Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa,
kutokana na kifo cha Akwilina.
Pamoja na shinikizo hilo, ni vyema viongozi wetu wakajifunza
kuwajibika pale inapobidi. Madai haya ni kutokana na kudumisha
utawala bora wenye kuzingatia sheria.
Nchi yetu kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu, kipindi ambacho siyo
cha kujivunia wala cha kunyamazia. Watanzania wanauawa na kuuliwa
katika mazingira tatanishi.
Pamoja na kwamba dunia ni uwanja wa fujo, hizi fujo zinazotokea nchini
kwetu kwa kila mwenye uwezo wa kumuua mbaya wake anaua bila
kujali. Ni vyema tukajiuliza ni wapi tumekosea kiasi cha kufika hapa
tulipofika.
Ni wakati wa viongozi wetu kutafakari kwa kina nini kimetufikisha hapa
na nini kifanyike kutokomeza hali hii isiendelee kuota mizizi kwa vizazi
vyetu. Tusipoziba ufa, utajenga ukuta.
Tanzania ni yetu sote. Itakuwa busara iwapo majukwaa ya amani
yakishirikishwa, na watu wakatoa maoni yao tuweze kumzika huyu

mdudu wa kumwaga damu za ndugu zetu wasio na hatia, aliyehamia
nchini kwetu.
Nchi yetu ipo kwenye hatari ya kuingia kwenye machafuko iwapo
tahadhari za mapema hazitachukuliwa.
Nawaomba viongozi wetu wastaafu washirikishwe katika kutafuta
ufumbuzi kuliko kuendelea kunyamaza huku chuki ikiendelea
kupandikizwa kwa Watanzania.
Tanzania ni yetu sote, hivyo ni jukumu letu kuamua kwa ajili ya nchi
yetu. Ni vyema tukasema sasa imetosha. Hatutaki kuona mauaji
yakiendelea na kuishi kwa hofu.
Watanzania tuna sifa ya upendo. Sifa hii imeanza kupotea huku
tukinyemelewa na chuki na visasi. Watanzania ni wakimya, ukimya
sasa umeanza kutoweka huku tukinyatiwa na ukatili.
Tanzania sasa inaanza kupoteza nuru yake ya nchi ya utulivu na amani.
Tunachafuka kwa kuonekana kuwa tumepoteza nuru yetu huku
tukionekana kuwa binadamu wa ajabu kwa kushindwa kuilinda amani
inayoliliwa na kuombwa na nchi zote duniani.
Dunia ni tambara bovu halishoni nguo, ukilishika lazima likuchanikie.
Tusipokuwa makini basi litachanika na nchi yetu itaparaganyika.
Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Tumekiuka miiko ya uongozi
iliyowekwa na waasisi wa Taifa letu, tumejikuta tunaishi maisha ya pata
potea. Ni vyema tukazingatia ya kuwa ulinzi na usalama wa nchi yetu
upo mikononi mwetu, hivyo ni jukumu letu sote kuilinda tunu hii.
Tanzania nchi yangu, nakupenda kwa moyo wote.
Mwisho

By Jamhuri