Ni wiki kadhaa sasa sakata la usajili wa taasisi za dini limekuwa katika vichwa vya habari vya magazeti, huku serikali ikionesha udhaifu uliopo katika baadhi ya taasisi hizo, huku zenyewe zikikiri udhaifu na kuahidi kurekebisha.

Wakati hayo yakiendelea mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba amejitokeza hadharani, kwanza kukana barua iliyosambaa mitandaoni ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi aliyesaini barua hiyo, huku akisema barua hiyo haikuwa na baraka za Serikali.

Kauli ya Waziri, Dk. Nchemba kuwa barua ya msajili wa vyama vya hiari kulitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuufuta Waraka wa Pasaka, ni batili na haina baraka za Serikali imeacha maswali mengi, kubwa likiwa ni mawasiliano ndani ya wizara.

 

Barua iliyosainiwa na mtu anayeitwa M. Komba kwa niaba ya msajili, ilisema chombo kilichotoa waraka huo hakitambuliwi kisheria na kwamba ulizungumzia masuala yaliyo nje ya malengo ya kanisa hilo na kutoa siku 10 kwa KKKT kuufuta.

 

Lakini tangu barua hiyo ilipotolewa hapakuwa na sauti yoyote ya kiongozi wa Serikali, mpaka ilipojibiwa na Katibu Mkuu wa KKKT, Brighton Killewa, ndipo Waziri Nchemba akajiotokeza na kusema aliyoyasema.

Hakuna afya kwa Serikali kuanzisha malumbano na taasisi za dini, maana taasisi hizo wabia wa amani pamoja na maendeleo. Wakati serikali ikiwaita watanzania wananchi kwenye taasisi za dini wanaitwa waumini/waamini. Wote hawa wanategemeana.

Hatari ambayo sisi gazeti la JAMHURI tunaiona ni kuliingiza taifa katika mgogoro wa kidini usiokuwa na tija wala manufaa yoyote. Tunaamini katika mazungumzo ya staha baina ya pande zote mbili, kama Serikali ina jambo inahitaji kuzungumza na taasisi fulani ya dini basi zitumie njia sahihi ambazo hazileti mkanganyiko kama ilivyotokea hivi karibuni.

Kadhia hii ambayo imewakuta Kanisa Katoliki pomoja na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, iwe mwisho wa mambo kama hayo. Maana ni aibu kwa taifa kama Tanzania ambalo limekuwa na utangamano kwa muda mrefu kuanza malumbano ya kidini.

1171 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!