Na Waandishi Wetu, Lindi na Dodoma

 

Familia ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ilifuata taratibu zote halali katika kununua Shule ya Sekondari ya Nyangao, iliyopo mkoani Lindi, JAMHURI limefahamishwa.

Meneja wa Shule ya Nyangao, Mathias Mkali ameliambia JAMHURI kuwa licha ya taratibu zote kufuatwa aliyenunua shule si Waziri Mkuu Majaliwa, bali aliyenunua ni mkewe Mary Benjamin Mbawala kwa bei halali iliyokubalika. Hakutaka kueleza shule hiyo ilinunuliwa kiasi gani kwa maelezo kuwa suala hilo ni taarifa za ndani.

Wiki iliyopita, Gazeti la JAMHURI limeandika habari kuwa Waziri Mkuu Majaliwa ameshiriki kununua mali za CCM katika njia zenye utata, hivyo yuko matatani. Baada ya habari hizo kuchapishwa wamejitokeza wajumbe wa NEC wanaosema taarifa lilizochapisha gazeti hili waliozitoa walitia chumvi na kuacha kueleza ukweli wote. Mmoja ameliambia JAMHURI; “Ripoti ilikuwa inamtetea Waziri Mkuu na ikampongeza kwa kufuata taratibu yeye na mkewe katika kununua shule ya Nyangao, sasa iweje atokwe jasho. Loooo!, waliowambia wana lao jambo.”

Mjumbe mwingine amesema wapo waliokuwa viongozi ndani ya Jumuiya ya Wazazi ambao maji yako shingoni “kutokana na madudu waliyoyafanya, hivyo wanadhani wakimhusisha Waziri Mkuu itawasaidia, kumbe nyaraka zipo na wao watapaswa kulipa uovu walioufanya si Mhe. Majaliwa. Yeye na familia yake walifuata taratibu. Nimeona nami niseme kidogo, japo sivujishi siri za vikao kwa kusema haya.

“Nakumbuka Katibu Mkuu, Dk. Bashiru alisema, ‘awali walidhani Waziri Mkuu Majaliwa naye amejichukulia mali ya chama kienyeji na hivyo walitaka kumwambia achague kati ya kubaki na shule au kurejesha Uwaziri Mkuu. Lakini walipochunguza na kupata nyaraka, wakakuta Waziri Mkuu alifuata taratibu zote kwa usahihi.’ Sasa hapo ndipo wachomekeaji walipopitilizia kusema Waziri Mkuu amejiuzia shule, wakati hata Dk. Bashiru alitamka bayana kuwa shule aliuziwa Mama Mary Majaliwa kuinusuru ilikuwa na hali mbaya,” amesema mjumbe huyo wa NEC.

JAMHURI limemtafuta Waziri Mkuu Majaliwa jijini Dodoma mwishoni mwa wiki kumtaka ajibu maswali ya alinunua shule hiyo shilingi ngapi, fedha alizipata wapi, ameikarabati kwa shilingi ngapi na fedha hizo alizipata wapi na iwapo zinalingana na mshahara anaoupata au kama ana miradi mingine. Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Mimi sina la kusema. Kila kitu kinafahamika kwa uwazi. Hakuna kilichofanyika kwa siri. Mtafuteni meneja wa shule ya Nyangao anayo majibu,” amesema Majaliwa.

Taarifa lilizozipata Gazeti la JAMHURI zinaonyesha kuwa shule hii ilianzishwa na ‘Mabruda’ wa Parokia ya Nyangao wilayani Lindi, mwaka 1982/83 kama shule ndogo ya ufundi (workshop) kwa ajili ya kufundisha vijana ufundi wa kutengeneza magari. ‘Bruda’ aliyeianzisha muda mfupi baadaye alifariki kwa ajali ya pikipiki wakati anatoka Mtama kwenda Nyangao.

Baada ya kifo chake shughuli za shule hii zilisimama. Wananchi walifanya harambee wakajenga vyumba vya madarasa na wakaamua kuisajili wilayani Lindi. Mtu aliyewasaidia kuisajili aliisajili kama Shule ya Wazazi Nyangao. Baadaye Jumuiya ya Wazazi ya CCM Lindi, iliitambua shule ya Wazazi na baada ya hapo mwaka 1984 ikachukuliwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM ikaanzisha kidato cha kwanza wakaendelea hadi kidato cha nne.

Shule hii ilijiendesha hadi mwaka 2000 ilipoanza kupoteza mwelekeo kutokana na kushindwa gharama za uendeshaji. Kuanzia wakati huo walimu walianza kufundisha kwa kusuasua, wanafunzi wakawa hawapati chakula na mishahara ya walimu na watumishi wengine ikawa kitendawili.

Mwaka 2012 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Abdallah Chikawe, alimwendea Majaliwa wakati huo akiwa mbunge wa Jimbo la Ruangwa na kumwomba awasaidie wazazi wa Nyangao kutafuta mwekezaji kuifufua shule hiyo.

“Hadi mwaka 2012 shule tayari ilikuwa msituni, kuta zilikuwa zimechakaa, lipu imeachana na ukuta ikadondoka, tofali nyingi zilikuwa za udongo mbichi, hivyo ikawa shule imechakaa kweli. Chini vyumba havikuwa vimesakafiwa, nyavu za madirishani zilikuwa zimechakaa, shimo la gereji lilikuwa limejaa takataka, hakukuwapo na vyoo wala jiko, madirisha yote yalikuwa yamechakaa, yaani kimsingi huyu baba (Majaliwa) mimi sijui alikabidhiwa nini, ila naweza kusema yalikuwa magofu,” mmoja wa wananchi wa Nyangao ameliambia JAMHURI.

Nyaraka ambazo JAMHURI limeziona, zinaonyesha kuwa Shule ya Sekondari Nyangao ilifungwa rasmi Desemba 30, 2013 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, wakati huo Ludovick Mwananzila kwa barua yenye Kumb. Na. EA. 144/249/07/48 iliyotumwa kwa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM akimweleza sababu za kuifunga kuwa ni shule kuchakaa, wanafunzi kukosa chakula, walimu na watumishi wengine kukosa mishahara.

 

Nini kilifuata baada ya kuifunga

 

Baada ya shule hiyo kufungwa, Mwenyekiti Chikawe alimwendea Mbunge Kassim Majaliwa na kumweleza kilichotokea na kuhoji wafanye nini. Majaliwa alishauri Jumuiya ya Wazazi ishirikiane naye kufikia uamuzi. Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mkurugenzi wa Elimu wa Jumuiya na viongozi wengine waliitembelea shule ya Nyangao na kubaini kuwa imechakaa kwa kiwango cha kutisha.

“Mwaka wa 2013 shule hii ilikuwa vichakani kabisa. Baada ya uongozi wa Jumuiya kuitembelea, ulimwambia Mbunge Majaliwa kuwa ni Mwalimu kwa taaluma, hivyo ni vyema akafanya kila awezalo kunusuru shule hiyo. Yule baba alikuwa na Sh milioni 20 akaziweka hapa shuleni. Walikarabati majengo yote yaliyokuwa yamechakaa, wakapiga ‘chupingi’, wakaisakafu na Jumuiya ikamwambia kuwa eneo la shule ni jumla ya ekari 120.

“Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa sasa Ndugu Gratias Luoga ndiye aliyekuwa Mwanasheria wa Jumuiya. Alishauri Mbunge na Jumuiya waingie ubia wa kuendesha shule ya Nyangao. Hii iko wazi. Mbona aliyewambia hakulisema hili? Alifanya haya bila kificho,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limeuona mkataba wa ubia ulioingiwa kati Mbunge Majaliwa na Bodi ya Wadhamini ya Umoja wa Wazazi Tanzania, ambapo Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Charles Tizeba alisaini kwa niaba ya Jumuiya Novemba 1, 2014. Mbunge alipewa jukumu la kuendesha shule hiyo kwa maana ya kuikarabati, kulipa mishahara ya walimu na kuendeleza taaluma. Majaliwa wakati huo akiwa mbunge aliitangaza shule hiyo ikakosa soko. Ilifanikiwa kupata wanafunzi 16 tu pamoja na kuikarabati.

Hata hivyo, kutokana na pilikapilika za uchaguzi wa mwaka 2015 na kwamba shule hii ilikuwa na wanafunzi 16 tu, huduma zilidhoofika na Jumuiya ikaamua kutekeleza pendekezo la Mwenyekiti wa CCM, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete la kuuza shule zilizoshindwa kujiendesha alilolitoa mwaka 2013.

JAMHURI limeuona Muhtasari wa Kikao cha Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Tanzania kilichofanyika kwa siku 2 Novemba 24 na 25, mwaka 2015 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, kilichohudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Dk. Charles John Tizeba, Katibu wa Baraza, Seif Shaaban Mohamed na wajumbe, Haji Juma Haji, Balozi Job M. Lusinde, Yasmini Y. Alloo, Dk. Didas Masaburi, Haidary Haji Abdallah na Diana Chilolo.

Kikao hicho pia kilikuwa na waalikwa watatu, ambao ni Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Abdallah M. Bulembo, Mhasibu Philemon Aroko Agola na Katibu wa Elimu, Yusufu Bwire. Katika kikao hicho walijadili Waraka Maalum wa Agizo la Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete wa Septemba 3, 2015. Pamoja na mambo mengine walijadili kuwa majengo ya Shule ya Sekondari ya Nyangao yamechakaa, hivyo wakapendekeza:

“Mwekezaji aliyeko Nyangao sekondari aelekezwe kufidia gharama za majengo na eneo la shule badala ya mkataba uliopo sasa ambao unasomeka ni ubia. Uongozi wa Umoja wa Wazazi ufanye mazungumzo ya pamoja juu ya fidia hiyo kama ilivyoelekezwa kwneye Kikao cha Baraza Kuu la tarehe 26/8/2013.”

Baada ya kikao hicho, Jumuiya ya Wazazi ilithamanisha majengo. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Aprili 16, 2016 Mary Benjamin Mbawala ambaye mi mke wa Waziri Mkuu, aliandika kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi akiomba kufikiriwa kuuziwa shule hiyo aweze kuibomoa na kujenga majengo yenye hadhi kuinua elimu mkoani Lindi.

Ombi hilo la Mama Mary Majaliwa lilijibiwa kwa barua yenye Kumb. Na. TA/BWJ/C/794/271 ya Mei 9, 2016 na Katibu Mkuu wa Jumuiya, Seif Shaaban Mohamed, aliyesema: “Itakumbukwa kwamba wewe umekuwa mdau wetu wa shule ya Nyangao kwa muda mrefu. Baada ya kuthaminisha mali zote zilizopo hapo shuleni ikiwa ni pamoja namajengo ulioyojenga wewe mwenyewe wakati ukifanya maandalizi ya kuingia ubia na Umoja wa Wazazi Tanzania, tumefikia uamuziwa kulipwa Tshs. 200,000,000 (milioni mia mbili tu) kama fidia ya majengo na mali zilizopo.

“Fedha hizo zilipwe kwenye A/c No. 3301162398 (KCB). Umoja wa Wazazi Tanzania. Baada ya kuingizwa kwa fedha hizo kwenye A/c uliyoelekezwa, utaratibu wa makadbidhiano utafuata. Eneo hilo halina hati ya kumiliki hivyo baada ya kukamilisha taratibu za fidia unaruhusiwa kuandaa hati ya kumiliki ardhi,” ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo nakala tumeiona katika Ofisi za Jumuiya ya Wazazi, Dar es Salaam.

Mmoja wa watu walio karibu na Waziri Mkuu Majaliwa, ameliambia JAMHURI kuwa baada ya mkewe kukubaliwa kununua shule hiyo, Majaliwa alichukua mkopo wa Sh milioni 200 kutoka Benki ya NMB kwa kutumia dhamana ya Mfuko wa Bunge kama wanavyofanya wabunge wengine na fedha hizo akazilipa kwa Jumuiya ya Wazazi mara moja. JAMHURI limepata nakala ya Sitakabadhi ya Umoja wa Wazazi ya Juni 6, 2016 inayodhihirisha kuwa Mama Mary alilipa fedha zote alizochukua mumewe kama mkopo kutoka NMB ikiwa gharama ya kununua shule ya Nyangao.

“Huwezi kuamini wakati wanafanya makadirio, walimwambia Mheshimiwa Majaliwa kuwa eneo la shule lina ekari 120. Amekwenda kupima eneo baada ya kulipa gharama hizo akakuta lina ekari 11 na nusu. Hapo alipo ana maumivu. Eneo jingine lote lilikwishachukuliwa na wananchi, akasema hataki kugombana na wenyeji wake. Akawaacha, akabaki na ekari hizo 11 na nusu,” amesema mtu aliye karibu na Majaliwa.

Mbunge mwingine ameliambia JAMHURI kuwa Lindi imeachwa nyuma kielimu hivyo hatua anazochukua Majaliwa kukarabati shule ya Nyangao zinasaidia kuvutia watumishi wa mashirika binafsi na wa umma ambao wangependa wototo wao wasome katika shule za michepuo ya Kiingereza.

“Kwa mfano amejenga Academy pale Ruangwa kwa kutumia mkopo kutoka NMB. Mimi namfahamu huyu Mheshimiwa. Ameweka dhamana nyumba yake ya Tuangoma Dar es Salaam kufanikisha ujenzi wa hiyo academy. Wanafunzi wanalipa ada Benki inakata fedha zake. Kuna wanafunzi zaidi ya 100 sasa wa wazazi ambo zamani walikuwa wanakataa kufanya kazi Lindi kwa watoto wao kukosa shule wanazozitaka.

“Shule ya Nyangao sasa ina kidato cha tano. Ameikarabati inavutia. Imetoka wanafunzi 16 wa mwaka 2014 kwa sasa ina wanafunzi zaidi ya 300. Unaona Lindi inaibuka katika elimu kwa sasa. Tusimkatishe tamaa Mheshimiwa Majaliwa tumuunge mkono,” amesema.

Awali, Meneja wa Shule ya Nyangao, Mathias Mkali ameliambia JAMHURI kuwa Mhe. Majaliwa baada ya kuwa amekabidhiwa majengo ya shule hiyo mwaka 2014 wananchi walipata mradi wa TASAF wakaomba wajengewe maabara shuleni hapo. “Jengo la maabara lilijengwa na lipo hadi leo wanalitumia kama ofisi ya kijiji. Ingawa Mama Mary Majaliwa ameinunua hii shule, jengo linaendelea kuwa mali ya wananchi na yeye amekuwa akisema atajadiliana na wanakijiji kama ni kulinunua au waendelee kulitumia ndani ya shule, ingawa tayari wameishajenga ofisi ya kijiji nyingine,” amesema Mkali.

Mkali ameongeza kuwa alisikia kuwa Tume ya Dk. Bashiru ilihojiana na Waziri Mkuu Majaliwa, lakini aliwapa vielelezo wakaridhika, hivyo watu wanaosema amerudisha shule wanachosema si sahihi.

JAMHURI limefanya mahojiano na Dk. Charles Tizeba kuhusiana na uuzwaji wa mali za Jumuiya ya Wazazi amesema mali hizo ziliuzwa na Jumuiya ya Wazazi na si mtu binafsi.

“Kwa hivyo CCM ilipogawa Chimwaga ni Anna Abdallah amegawa Chimwaga? Tafsiri hiyo inatoka wapi? Kwanini usiseme Jumuiya imeuza shule zake? Ukisema wewe litakuwa ni jambo la binafsi.”

“Tuanze tuelewane kwanza, Jumuiya ndiyo iliyouza shule, sio Tizeba, Bulembo au Katibu au nani, umenielewa lakini?” amesema Tizeba.

Alipoulizwa ni utaratibu upi ulitumika kuuza shule hizo na ziliuzwa kiasi gani amesema kwamba afuatwe aliyesema hayo maneno ndiye anaweza kuzungumzia suala hilo.

“Mimi sijaenda hadharani kuzungumzia hilo suala, sasa wewe mtafute aliyesema hivyo yeye atakueleza utaratibu uliotumika kuuza hizo shule. Au wasemaji wa Jumuiya wapo mimi sio Msemaji wa Jumuiya, yupo Msemaji wa Jumuiya sio mimi. Siwezi kuzungumzia hilo suala,” amesema Tizeba.

Alipoulizwa kuhusiana na ripoti ya Bunge iliyobainisha kuwa alitoa kibali cha kuondoa ushuru wa kuvua samaki katika baharini katika Bahari Kuu (deep sea fishing) na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni, amesema kuwa hawazi kujibu ripoti ambayo hajaisoma.

“Sasa unataka nianze kujibizana na taarifa ya Kamati? Wewe andika hivyo hivyo kwamba alipoulizwa alicheka, na kusema kwamba hayuko tayari kwa sasa kuzungumzia hayo mambo,” amesema.

Kuhusu kulia bungeni, Tizeba amesema kwamba, alishangazwa kuona Spika akifanya utani katika jambo ambalo halikupaswa kufanyiwa utani.

“Nilisikia wakisema kwamba nililia kwenye Kamati, nchi nzima kweli wanatarajia kujua kwamba nililia bungeni. Nililia kwenye Kamati nalilia bajeti kwani mimi ni yangu? Spika alikuwa anafanya utani katika jambo ambalo halitakiwi utani. Nilizungumza naye akanambia kuwa alikuwa anafanya utani,” amesema Tizeba.

Mei 24, mwaka huu Spika wa Bunge Job Ndugai alisema kwamba Waziri Tizeba alipofika kwenye Kamati ya bajeti alilia kama mtoto mdogo.

Spika Ndugai alitoa kauli hiyo bungeni, Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuwa wakati mwingine mawaziri wanashindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yao katika wizara kutokana na serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kutotoa fedha.

“Haya mambo yanasikitisha sana. Mara ya mwisho waziri wetu wa kilimo alipokwenda kwenye Kamati ya bajeti, ilibidi atoe machozi. Amelia kama mtoto mdogo,” alisema Ndugai.

Kwa upande wake, Abdallah Bulembo, yeye ametoa taarifa ndefu akitafuta mchawi juu ya nani ametoa taarifa za yeye kushiriki kuuza shule za Jumuiya na badala yake akaanza kuvuta watu wengine kwenye mgogoro huo.

Please follow and like us:
Pin Share