Sehemu ya pili ya makala hii, mwanishi alisema huko Ulaya kuna kasoro chungu nzima. Nchi zao katika Umoja wa Ulaya (EU) bado kuna mitazamo tofauti na ya kibinafsi na ndiyo sababu Uingereza imefanya kura ya maoni ya kujitoa katika Umoja huo. Mwandishi anapinga dhana ya kuamini kila linalofanywa au kuamuriwa na Wazungu, ni sharti lifuatwe na Waafrika. ENDELEA…

 

Tujiulize ujumbe huo unapokuwadia matakwa ya vyama fulani fulani, udalali huo ni kwa manufaa ya nani? Waafrika huru au ukoloni mamboleo? Kama wanawaonea huruma wale wa upinzani kwa vipi Wazungu hawa hawa wanawaua wakimbizi Waafrika katika Bahari ya Mediterranean? Hebu tufikirie hilo. Mwafrika ni Mwafrika tu, huwezi ukamsulubu yule kule pwani ya Mediterranean na kumhurumia huyu wa Tanzania. Huo ndiyo unafiki wa Magharibi katika utawala wa haki za binadamu na wa kidemokrasia.

Ningali nina mtazamo wa kutokuwaamini Wazungu! Bado nakumbuka maneno ya Gavana Edward Twining alipotukejeli Watanganyika mwaka 1959. Alitumia maneno haya, namnukuu: “Those who had money were not thrift, and Africans in general were very backwards, they regarded a Makerere Certificate as a passport to heaven. They were impatient…I have always refused to appoint an African simply because he was an African” (East Africa and Rhodesia Journal la tarehe 20 Nov. 1958 uk. 358).

Hapo Mwafrika unaona msimamo wa Mzungu. Kwanza anatuona sisi, “impatient and backwards” maana yake hatuko wavumilivu na hatujaendelea. Kwa mtazamo huo, Mzungu haamini kama tunaweza kufanya yale wao wanayafanya. Basi, hata utawala wa kidemokrasia kwetu hatuwezi sharti Mzungu aje ausimamie ndipo mambo yatakuwa sawa! Tunayakubali mawazo hayo mpaka leo? Kama hatuyakubali vipi ujumbe wa EU uthaminiwe hivi hata kama wajumbe wake ni watoto wadogo kiumri kuliko Wenyeviti wa Tume zetu za uchaguzi? Kinachoogopwa hapa ni ile rangi nyeupe ya uzungu wao na fedha zao wala si hekima na busara za uzoefu wa utawala bora.

Mzee Nelson Mandela katika uzee wake aliwahi kutamka haya, “…moja ya faida ya umri mkubwa ni kwamba watu wanakuheshimu kwa vile una mvi kichwani na wanakutakia mema mengi bila kujali wewe ni nani? (Rais Mandela tarehe 19/07/1998). Katika Biblia, Kitabu cha Methali 20:29 tunasoma maneno haya: “Fahari ya vijana ni nguvu zao; na UZURI wa WAZEE ni KICHWA CHENYE MVI”.

Vijana katika vyama vya upinzani watumie elimu yao kwa nguvu zote wakati wazee watulize jazba kusitokee machafuko.

Ndiyo sababu mimi nasema ule ujumbe wa EU unawezaje huku kwetu Afrika kuaminiwa zaidi kuliko matamshi ya wazee wetu Wenyeviti wa Tume zetu za Uchaguzi? Ni kasumba ya kuogopa Wazungu tu wala si suala la demokrasia hapa. Jamani, mimi ni muono wangu huo. Si kila kisemwacho na Mzungu ni kizuri na kikumbatiwe! Sisi tujione tuko huru kabisa kujiamlia mambo yetu wenyewe – (we are physically and mentally liberated). Kwenda Magharibi kuomba huruma (sympathy) ya Wazungu ni kuthibitisha unyonge wetu wa kimawazo. Kwani lazima tuongozwe na fikra za wenye demokrasia na wenye fedha wa Magharibi? Hapo ndipo penye udhaifu wa mtu mweusi (Typical African inferiority complex).

Kabla ya Uhuru Katiba zetu – ile ya Tanganyika na ile ya Zanzibar -zote zilitungwa Lancaster House, Uingereza. Tuliziacha zote baada ya kujipatia Uhuru wetu na tukajitungia Katiba zetu za Jamhuri za nchi zetu. Sheria za kikoloni tuliziacha sasa tunatunga sheria zetu. Iweje EU wanakuja na mawazo ya kubadili sheria na Katiba zetu ili mradi zitie vipengele wanavyovitaka?

Hapo lazima tujiulize vipi ile Katiba waliyotutungia kule Lancaster House kwanini hawakuliweka wazo hili? Hakuna hata mahali wameelezea juu ya uchaguzi na haki za mtu binafsi kugombea. Hii ina maana kwamba wanapodai Katiba ya nchi zetu lazima iwe na kipengele cha mgombea binafsi wanalitoa wapi wazo hilo? Eti hata katika ripoti ya waangalizi wametaja hili. Wamelitoa katika Katiba ipi mbona ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 halimo wala hii ya Muungano ya mwaka 1977; halimo sasa kwa nini walizue jambo ambalo sisi wananchi hatuna kikatiba?

Haya yanakuwa ni matarajio yao Wazungu wa EU Community (aspirations which are mere WISHFUL THINKING). Sielewi inakuwaje viongozi wetu huku Afrika pamoja na usomi wao vyuo vikuu bado wanaamini demokrasia ya nchi za Magharibi ndiyo yenyewe na lazima tuikumbatie. Hapo hatujakubali tu kuwa Mwafrika bado yu “Le Grande Enfante?”

Mimi bado nasema Watanzania tunayo demokrasia safi na asilia yaani “original” kwa Wabantu. Nchi gani ulimwenguni kiongozi wa nchi anakabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine, lakini mwenye kukabidhi madaraka yale akitaka tena anarudishiwa? Si mnakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya Mzee Rashid Kawawa?

Mwalimu akiongea na wanajeshi pale ukumbi wa Msasani Beach Club wakati anawaaga aking’atuka alikuwa na haya ya kusema: “Nilifanya vizuri sana kumwachia Rashid. Na wala Rashid alikuwa hatazamii kuwa Waziri Mkuu. Walikuwepo wenyewe waliotazamia! Rashid alikuwa siku hiyo tunamtuma kwenda Nigeria. Sikumbuki tulikuwa tunamtuma kwenda kufanya nini. Lakini nilimrudisha alipokuwa katika kiwanja cha ndege. Alirudi, akaambiwa huondoki, utakuwa Waziri Mkuu. Nasema ilikuwa vizuri sana nilimkabidhi Rashid. Sababu Rashid si msomi kama mimi. Hana woga wa kisomi. Kwa hiyo katika miezi tisa ile alibadili sana nchi”. (Mwl. JK Nyerere akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM Jeshini; Agosti 2, 1985 uk. 25 ibara ya 1).

Sote tunajua utamu wa kutawala na hulka ya Waafrika kung’ang’ania madaraka. Basi, tungetazamia kwa hali ya kawaida kama Mzee Kawawa asingekuwa muungwana angeweza kabisa kuendelea kutawala na kumzuia Mwalimu Nyerere asiweze kutawala nchi hii tena. Kumbe demoksasia ya Kitanzania siyo kuwa na ubinafsi.

Mzee John Magoti, Mkuu wa Chuo cha Kivukoni cha Mwalimu Nyerere ameandika hivi: “Kawawa ambaye kabla ya Tanganyika kuwa Jamhuri, kwa unyenyekevu mkubwa na bashasha alimkabidhi Mwalimu madaraka ya kuongoza Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1962 baada tu ya Uchaguzi (Taz. Rashid Mfaume Kawawa by John MJ Magotti uk. 42 ibara ya kwanza).

Haya yote ni historia vijana wetu wa vyama vya siasa waijue na wajifunze na kuthamini demokrasia ya Tanzania. Hakuna haja kung’ang’ania demokrasia ya Wazungu ambayo haieleweki, ni ya kujipendelea wao na ya kinyonyaji.

Hakuna Mzungu atasifia utawala wa Mwafrika kwa sababu Mwafrika huyo ndiye aliyemnyang’anya tonge la ulaji wake kiuchumi pale alipodai Uhuru wake wa kujitawala – Mwalimu anasema: “…we are waging our anti – imperialism war. Colonialism is an intolerable humiliation to us. We shall wage a relently determined battle against it until we are free. We shall use no violence” (Nyerere: Uhuru na Umoja sura 8 uk. 59).

Hakuna sababu ya kutumia mitulinga (violence) katika kudai haki. Hizi ni busara na hekima za kuzaliwa kwa uongozi huo wa upinzani kwa dola enzi za ukoloni. Je, hatuhitaji uongozi wa hekima na busara za namna ile wakati huu wa sasa? Viongozi wetu wa upinzani hawaoni ubora wa kutumia non – violent methods?

By Jamhuri