Na Nizar K Visram

Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Cape Town (Afrika Kusini) alipofariki dunia Desemba 26, 2021 akiwa na umri wa miaka 90, ulimwengu ulimlilia. 

Wengi wakakumbuka jinsi alivyokuwa mwanaharakati aliyepambana na ubaguzi wa rangi (ukaburu) nchini mwake. Wakakumbuka jinsi alivyopambana na udhalimu na ukandamizaji duniani kote.  

Ni nadra kukuta kiongozi wa dini akitumia jukwaa lake kuhubiri theolojia ya ukombozi,  Tutu alikuwa mtu wa aina hiyo. Hakutaka makuu na ndiyo maana aliagiza mazishi yake yawe ya kawaida. Mwili wake ukachomwa na majivu kuzikwa katika kanisa lake alimokuwa akihubiri.

Mwamko wake wa kisiasa ulikomaa mnamo miaka ya sabini wakati mapambano dhidi ya ukaburu ulipopamba moto chini ya Chama cha ANC kilichopigwa marufuku. Viongozi wa ANC kina Nelson Mandela wakatiwa gerezani na wengine kama Oliver Tambo wakakimbilia nje na kuanzisha harakati za kimataifa. 

Tutu alipingana na utawala wa Makaburu. Wakamkamata kwa shutuma ya kushiriki katika maandamano “yasiyoruhusiwa”. Akatozwa faini na pasipoti yake ikazuiliwa. Baada ya muda akarudishiwa ndipo akasafiri kwenda kuonana na Papa. Kwa mara nyingine Makaburu wakamnyang’anya pasipoti. 

Hata hivyo akadharau amri ya serikali kwa kusafiri hadi Zambia ambako alikutana na viongozi wa ANC. Urafiki wake na chama hicho cha ukombozi ulidhihirika pale Mandela alipotoka jela alilala katika nyumba rasmi ya Askofu Tutu. 

Wakati wananchi wa Afrika Kusini walikuwa wakipambana na ukaburu, nchi za Magharibi zilikuwa zikiunga mkono utawala huo wa Wazungu wachache. 

Mwaka 1984 Tutu aliliambia bunge la Marekani kuwa ukaburu ni dhambi mbele ya Mungu, kwa hiyo serikali ya Rais Reagan ilikuwa ikitenda dhambi kwa kuunga mkono ukaburu. 

Mwaka 2001 mjini Durban (Afrika Kusini) ulifanyika mkutano wa kimataifa kupinga ubaguzi wa rangi. Ikaamuliwa kufanya kampeni nchini Marekani ili kuishawishi serikali ya Reagan iache kuunga mkono ukaburu. Tutu aliuambia mkutano:

“Tumejaribu kumshawishi Reagan aiwekee Afrika Kusini vikwazo lakini amekataa katukatu. Tukazungumza na wananchi wa Marekani nao wakatuunga mkono. Maandamano yakafanyika kote Marekani. Matokeo yake bunge likalazimika kupitisha sheria dhidi ya ukaburu licha ya upinzani wa Reagan.”

Tutu akatembelea Denmark ambako aliikosoa nchi hiyo kwa kununua makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini. Aliporudi nyumbani Tutu akaitwa na mawaziri wawili ambao walimtaka aombe radhi la sivyo angechukuliwa hatua.  Tutu akakataa. 

Kimsingi Tutu alikubaliana na sera ya ANC kama chama cha ukombozi ingawa yeye hakuwa mwanachama. Ndiyo maana alikuwa na uhuru wa kutoa mawazo yake pale alipotofautiana na uongozi wa ANC. Tofauti hii ilionekana zaidi baada ya Afrika Kusini kujikomboa na ANC kuwa chama tawala. Kitu ambacho kilimkera zaidi ni pale viongozi wapya wa nchi walipojitumbukiza katika ufisadi na kujilimbikizia mali.

Kwa mfano Aprili 2017 aliyekuwa rais Jacob Zuma alimuengua waziri wa fedha Pravin Gordhan baada ya waziri huyo kufichua ufisadi. Wananchi waliamua kuandamana wakilaani kuenguliwa kwa waziri Gordhan. Askofu Tutu aliamua kuungana nao. 

Alisema serikali inapoteza uhalali iwapo imeshindwa kuwatumikia vema wananchi walioichagua. Akamwambia Zuma: “Wewe na serikali yako hainiwakilishi mimi, bali mnawakilisha masilahi yenu. Hivyo nawaonya kama nilivyowaonya makaburu. Siku moja tutafanya maombezi ili serikali ya ANC ianguke.”

Hapa tunaona Tutu wa aina mbili.  Wa kwanza ni mwanaharakati aliyepigania ukombozi wa Afrika Kusini. Tutu wa pili ni yule aliyepigania ujenzi wa taifa jipya la Afrika Kusini ili kutimiza ndoto ya wananchi. Harakati hii haikuwa rahisi na ndiyo maana mara nyingi watawala wa ANC walimuona kama mchochezi. 

Ndipo akasema: “Wakati tunapigania ukombozi tulikuwa na ndoto ya kuunda jamii inayowajali wananchi, si jamii ya watu wanaolala njaa, si jamii ya wanafunzi wanaojifunza chini ya miti.” 

Matokeo yake watawala hawakumualika katika mazishi ya rafiki yake mpendwa Nelson Mandela. Huyu ni Mandela ambaye alilala nyumbani kwa Tutu alipotoka gerezani. Sasa katika mazishi yake watu 5,000 walialikwa lakini Tutu aliachwa. Wananchi wakapiga makelele mpaka ikabidi Tutu atumiwe mwaliko wa dharura dakika za mwisho. Mpasuko kati yake na wakuu wa ANC ulionekana waziwazi.

Tutu wa kwanza aliyepigana na ukaburu alituzwa zawadi ya Nobel kwa shangwe na matarumbeta. Tutu wa pili aliyepigana na ufisadi alipata tuzo kubwa zaidi, nayo ni mapenzi ya wananchi. Ndipo wakati wa mazishi yake ilibidi mwili wake uwekwe siku mbili ili maelfu ya wananchi wapate fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Tofauti yake na ANC haimaanishi kuwa Tutu alikanusha yote yaliyofanywa na ANC, hasa chini ya uongozi wa Mandela. Alikubali kuwa wananchi vijijini walianza kupata maji safi na salama, kupata umeme pamoja na ruzuku. Pale chama kilipostahili sifa Tutu alikisifu, lakini pale kilipostahili kukosolewa alikuwa wa kwanza kukosoa.

Hii ilidhihirika wakati alipoteuliwa na Mandela kuwa mwenyekiti wa tume ya ukweli na maridhiano (TRC). Tume hiyo ilisikiliza shuhuda za wananchi walioteswa na kudhalilishwa na makaburu ambao wengi wao waliomba msamaha. Tume pia ilisikiliza malalamiko ya wananchi dhidi ya ANC.

Ripoti ya TRC ilipotoka ililaani dhambi za makaburu lakini pia ilifichua makosa ya ANC. Chama kilitaka ripoti isisambazwe lakini rais Mandela akapinga. 

Chama kikaomba mahakama izuie lakini mahakama ikakataa kutoa zuio. Ndipo Tutu akasema: “Maisha yangu yote nimepigana na dhuluma. Sikuwa na maana kuondoa dhuluma moja na kuleta dhuluma mbadala.”

Mwaka 2013 akatangaza kuwa hatapigia tena kura ANC kwa sababu ya rushwa, umaskini, matabaka  na kushindwa kuzuia ubaguzi dhidi ya Waafrika wanaoishi Afrika Kusini (xenophobia). Akasema: “Haikuwa rahisi kwangu kuchukua uamuzi huu. Sina nia ya kuisaliti serikali bali nimeamua kumtii Mungu.”

Mbali na kuwa mwanaharakati wa Afrika Kusini, Tutu alikuwa pia mpiganaji dhidi ya udhalimu na ukandamizaji kote ulimwenguni. 

Hii ndiyo taswira yake nyingine ambayo ilimfanya afananishe hali ya Palestina na hali ya Afrika Kusini chini ya ukaburu. Akasema: “Ukaburu wetu angalau ulikuwa afadhali kidogo, kwani hatukuona ndege za F-16 zikishambulia nyumba zetu na kuwaua mamia ya watoto kama inavyofanyika leo katika Palestina.” 

Haya alisema duniani kote. Mwaka 2008 wanafunzi walimualika kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha St. Thomas mjini Minnesota (Marekani). 

Chuo kikampiga marufuku. Lakini kutokana na upinzani mkubwa uliojitokeza ikabidi chuo kibadili uamuzi wake na Tutu akaruhusiwa kuzungumza chuoni.

Tutu alipinga vikali pia mashambulizi ya Iraq yaliyoongozwa na Marekani mwaka 2003. Alitaka George Bush, aliyekuwa rais wa Marekani na Tony Blair, aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza wafikishwe katika mahakama ya kimataifa kwa makosa ya kuishambulia Iraq kinyume cha sheria ya kimataifa na kwa kuudanganya ulimwengu. Katika mkutano mmoja uliofanyika Afrika Kusini, Tutu alialikwa lakini alikataa kwa sababu hakutaka kukaa meza moja na Blair.

Huyu ndiye Askofu Mkuu Tutu ambaye baada ya kufariki dunia kwake amemwagiwa heshima na sifa kemkemu kama vile kuitwa “dira ya maadili”.

Miongoni mwa waliomsifu ni wakuu wa Marekani na Ulaya, nchi ambazo zilikataa wito wake wa kuwawekea vikwazo makaburu wa Afrika Kusini na wavamizi wa Palestina. 

Waziri mkuu wa Uingereza na waziri wake wa mambo ya nje walimsifu Tutu. Naye kiongozi wa Chama cha Labour nchini Uingereza alisema Tutu siku zote alikuwa “upande wa wanyonge.”

Katika mtandao wengi wakamkumbusha kuwa kama Tutu angekuwa mwanachama wa Labour, angemvua uanachama kwa sababu ya kuwaunga mkono Wapalestina.

Tony Blair, aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza alisema: “Amesikitishwa sana” na kifo cha Tutu. Wengi wakakumbuka maneno ya Tutu kuwa ni unafiki kusema kuwa Robert Mugabe afikishwe mahakama ya kimataifa wakati watu kama George Bush na Tony Blair wanatamba ulimwenguni licha ya kuivamia Iraq na kuwaua wananchi wake.

nizar1941@gmail.com

0693-555373 

330 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!