Katika orodha ya uvumbuzi muhimu katika karne ya ishirini hakuna ubishi kuwa mtandao wa Intaneti utakuwa miongoni mwa uvumbuzi muhimu zaidi kwenye orodha hiyo.

Kupitia matumizi ya mtandao, binadamu wameweza kuharakisha kasi ya maendeleo kwa kiasi kikubwa si tu kwa sababu ya kuongeza ufanisi katika shuguli zao, lakini wakati huo huo matumizi ya mtandao yamewezesha pia kupunguza gharama za shughuli mbalimbali za kiuchumi za kujiongezea kipato.

Kupitia mtandao na teknolojia mpya za habari na mawasiliano leo hii inawezekana umati wa watu ukakusanyika kijijini Butiama kushiriki kwa njia ‘mubashar’ kwenye mkutano unaohutubiwa kwenye nchi yoyote ulimwenguni. 

Sizungumzii ule uwezo wa kuangalia mechi ya mpira inayochezwa Uingereza sasa hivi. Nazungumzia mimi kushiriki mkutano kama mjumbe nikiwa chumbani kwangu kama vile nipo kwenye ukumbi unaohutubiwa huko ughaibuni na nikachangia mawazo yangu kikamilifu.

Ilipolazimu mtu kusafiri kwenda kuhudhuria mkutano, sasa haja hiyo inakuwa muhimu kwa aina chache sana ya mikutano ambako bado upo umuhimu wa wajumbe kuonana ana kwa ana. Kama isingekuwa kwamba ipo tofauti kubwa kati ya nia ya kutumbua wajumbe wanaofunga safari kuhudhuria vikao bila ulazima, na tofauti iliyopo kati ya uwezo wa watu kukubali nia hiyo basi gharama za kusimamia maendeleo ya nchi zingeweza kupungua kwa kiasi kikubwa sana. Huu ni mfano mmoja wa maeneo yanayoweza kumnufaisha mwanadamu kwa matumizi ya mtandao.

Inahitaji makala nyingi kama hii kuorodhesha faida zote zinazoletwa na matumizi ya mtandao. Lakini faida mojawapo muhimu sana ni ile hazina ya taarifa mbalimbali ambazo zimetapakaa kwenye mtandao ambazo zinatunufaisha.

Mwenye nia ya kutumia mtandao kujiendeleza anaweza kufanya hivyo kwa ufanisi mkubwa. Na akifanikiwa kufanya hivyo anaweza hata kudhaniwa kuwa ni mwanataaluma katika taaluma mojawapo. Vyuo mbalimbali sasa vinatumia mtandao kufundisha baadhi ya masomo. Ni baadhi tu ya masomo kwa sababu wanazuoni wameamua kuwa na elimu ambayo haipatikani bila kuingia darasani. Daktari hawezi kusomeshwa kwa kutumia mtandao pekee. Lakini yapo mafunzo ya ufundi wa kila aina, au mafunzo ya kujiongezea uwezo wa kufanya tunayofanya kwenye shughuli zetu za kila siku. 

Si hayo tu, kupitia taarifa zilizopo kwenye mtandao watu wengi zaidi kuliko ambavyo imetokea tangu enzi za Adamu na Hawa sasa wanaweza kujiongezea elimu na ufahamu wa kila aina ya mada, hata zile ambazo hazihusiani na kazi zao.

Walioimba ‘barabara ndefu haikosi kona’ na ‘mwanamke mzuri hakosi kasoro’ wanatukumbusha kuwa hakuna kizuri kisicho na kasoro. Mtandao ni kokoro, unabeba yenye kufaa na yasiyofaa, mema na maovu, ya kujenga na ya kubomoa. Hali kadhalika, mtandao unao wenye elimu, na wajinga.

Napenda kukumbusha tu kwamba neno ujinga kwa maana yake ya kawaida siyo tusi. Wote tumezaliwa wajinga ila ni mabadiliko yetu kutoka utoto na kuelekea kwenye utu uzima ndiyo hutupa uwezo wa kupata elimu inayotuwezesha kupunguza ujinga wetu. Tunazo fursa na uwezo unaotofautiana wa kupunguza ujinga wetu kwa hiyo ni kosa kubwa kumlaumu mtu kwa nini anabaki mjinga. Hata hivyo siyo vizuri kumuonea haya mjinga mwenye uwezo wa kuondokana na ujinga wake lakini ambaye kila kukicha yeye anaendekeza ujinga tu.

Katika mjadala wa hivi karibuni juu ya ndege mpya za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imezuka hoja kwamba hizo ndege hazifai hata kidogo. Ukisoma ukosoaji mwingi juu ya ndege hizo uliopo kwenye baadhi ya mitandao ya jamii utagundua ni hoja zisizo za msingi. Tunaambiwa ni ndege za kizamani kwa sababu eti ni ndege za pangaboi. Kwa bahati nzuri siyo hoja zinazotolewa na marubani au na wataalamU wa usafiri wa anga.

Kwanza kuna mashirika mengi ulimwenguni ya usafiri wa anga ambayo yamenunua ndege za kampuni ya Bombardier Aerospace. Tunaweza kukubali kuamini kuwa uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuagiza ndege hizi umefanywa kwa misingi ya ujinga, lakini itakuwa vigumu kukubali na kuamini kuwa hicho kirusi cha ujinga kimeathiri pia karibia mashirika mengine ishirini.

Kampuni ya Bombardier Aerospace ilijenga uzoefu kwenye ndege yake aina ya Dash 7 iliyokuwa na uwezo wa kupaa na kutua kwenye viwanja vifupi. Hata hivyo, mashirika mengi kwenye miaka hiyo ya 1980 yalitaka kununua ndege zilizokuwa na gharama ndogo za uendeshaji. Kwa hiyo shirika hilo likajikita zaidi kwenye uundaji wa ndege zenye gharama ndogo ya uendeshaji, sifa ambayo ilitajwa na Rais Magufuli alipozindua matumizi ya ndege hizi mpya.

Hizi taarifa za sifa za ndege hizi zinapatikana kwenye mtandao na haihitaji elimu kubwa sana kuzipata. Tatizo letu kubwa ni mtu anaweza kuibuka tu na bila msingi wowote kuibua ukosoaji ambao hauna msingi wowote. Baadhi ya wale wasiojua nao, badala ya kutafuta taarifa za uhakika, wanafuata mkumbo tu.

Tunakubali kuwa kwenye siasa, ukweli siyo kigezo muhimu sana cha kuzingatia katika kujenga hoja. Lakini wajanja wanaozusha uongo ambao unakubaliwa na wale ambao hawana uwezo wa kubaini ya kweli na ya uongo hawasaidii jamii kujifunza. Uongo huo huo unaowapa faida wao unaweza kuwaletea hasara pia.

Hakuna mtu duniani mwenye elimu ya kila kitu. Wajinga hawataisha kamwe. Kwa bahati mbaya mtandao hausaidii kusambaza elimu wakati wote, lakini huharakisha kasi ya kusambaza ujinga.

By Jamhuri