Naamini pasi na mashaka ukweli hauna mahaba na baba, mama, ndugu au rafiki wala hauna hiyana na adui. Ni neno linalojipambanua ni pekee katika mazungumzo na vitendo. Ukweli una tabia ya kulipa na kutoficha uongo, uovu, wema au uadilifu. 

Sheria inapotafuta haki juu ya jambo lolote hushirikisha ukweli ambao una uhakika na uaminifu katika kuweka kanuni zitakazosimamia utaratibu utaofuatwa na watu au nchi katika kutoa haki sawa kwa wote. Tunasema sheria ni kanuni. Ni msumeno unaokata mbele na nyuma.

Katiba inapotaka kuwezesha serikali itawale au chama au kampuni iendeshe shughuli zake, inaweka kanuni zitakazosimamia utaratibu wa kupata na kutenda haki sawa kwa wote. Tunasema Katiba ni sheria mama. Inapochakarishwa na watu hutimua vumbi mbele na nyuma.

Katika hisabati za aljebra tunasema, iwapo thamani ya X ni sawa na thamani ya Y, na thamani ya Y ni sawa na thamani ya Z , kwa hiyo thamani ya X ni sawa na thamani ya Z. Kwa nadharia hiyo naweza kusema sheria ni ukweli; katiba ni sheria na katiba ni ukweli. (kanuni, uhakika na uaminifu).

Kama inavyofahamika, ukweli hauna rafiki wala adui. Hauna hiyana kwa mkubwa wala upendeleo kwa mdogo. Hauna huruma kwa mnyonge wala uonevu kwa mbabe. Mwenendo huu wa ukweli ndiyo mwenendo huo huo wa katiba ndani ya serikali, ndani ya kampuni na ndani ya chama. 

Tangu Taifa la Tanzania liasisiwe Aprili 26, 1964, Watanzania wanazungumzia Katiba ya nchi yao, vyama vyao na vikundi vyao kama sheria mama za kufuatwa na kuzingatiwa ndani ya mustakabali wa kuendesha na kusimamia demokrasia ya ukweli.

Mara kadhaa katiba hizo zimetekelezwa, zimesimamiwa na zi

merekebishwa ziweze kwenda na hali halisi ya watu ndani ya serikali yao na ndani ya vyama vyao vya siasa na vyama vyao vya michezo, burudani na vikundi vya ujasiliamali.

Waandaaji wa Katiba hizo ni wao wenyewe katika maendeleo yao. Wamefanya hivyo kwa nia njema ya kuweka utawala au uongozi bora kwa faida na maendeleo yao katika milango ya haki, uongozi na heshima, na kusukuma mbali unafiki. Hiyo ndiyo katiba.

Tumeshuhudia migogoro kati ya Serikali na baadhi ya vyama vya siasa kuhusu demokrasia ya ukweli. Ukweli ni katiba inayolalamikiwa kutumika kombo. Baadhi ya viongozi wanapindisha ukweli na baadhi ya viongozi wananyoosha ukweli. Ni katiba.

Ni mashuhuda katika mivutano ndani ya vyama vya siasa, baadhi ya wanachama wakitaka kutekeleza ukweli na kuwa viongozi. Walio viongozi hawataki kufuata ukweli na kuachia uongozi. Wanafiki wametokea eti kusema ukweli kwa kuweka uongo kuwa kweli. Ni katiba.

Mgogoro wa muungano wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar wenye maelezo ya kutoweka ukweli wa makubaliano ya muundo wa Muungano huo. Baadhi ya watu wanaona hakuna ukweli na baadhi ya watu wanaona upo ukweli. Ni katiba.

Leo ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) kuna mgogoro unaohusu ukweli Profesa Ibrahim Lipumba ni mwenyekiti au la. Wapo wanaotetea ni mwenyekiti halali na wapo wanaosema si mwenyekiti halali. Hii ina maana ya kupinda au kunyoosha misingi ya katiba iliyoko. Ni katiba.

Tayari mgogoro huo umeshakumba wapambe na visalata mtaa ndani na nje ya chama na kuweka chama katika mapande mawili ya uongozi ya katibu mkuu na mwenyekiti wa chama. Tusishangae kuona na kusikia baadhi ya Watanzania wanafurahia na wengine wanakereheka na yanayotokea CUF.

Dawa si wapambe na wanafiki kushabikia na kulalama kuhusu mgogoro huu kwenye majukwaa na vyombo vya habari. Tiba ni pande mbili hizo kukaa pamoja mezani kuchambua mbivu na mbichi kuukabili ukweli ambao ni katiba.

Ama sivyo waelekee huko walikosemea kwenye vyombo vya haki ambako sheria, ukweli na katiba zitaangaliwa na kutolewa tafsiri sahihi ya kanuni za wanaCUF walizojiwekea. 

Namaliza kwa kusema si hoja kumlaumu mlezi. Vipi mlezi awe na wajibu wa kulea na asiwe na wajibu wa kusema ukweli? Nini basi, maana ya mlezi kumpa mwana kulea? 

By Jamhuri