Wamarekani wanaweza kuwa na tofauti zao za ndani, lakini linapokuja suala linalohusu maslahi ya taifa lao huungana na kuwa wamoja. Ndivyo nchi inavyopaswa kuwa.
Waasisi wa taifa letu walitambua thamani ya umoja na mshikamano wa wananchi. Wakautambua umoja kama moja ya tunu adhimu katika kulijenga taifa imara. Awamu ya Kwanza ya uongozi wa Taifa letu ilifanya kazi kubwa sana ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Waasisi walijua kuujenga umoja si kazi nyepesim hivyo ni sharti kuwe na sehemu za ‘jando na unyago’ kitaifa. Ndipo kukaanzishwa vitu kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Lengo kuu la JKT lilikuwa kujenga na kukuza uzalendo miongoni mwa vijana wa Tanzania ili baadaye wawe raia wema wa kulilinda na kulitumikia taifa lao. Kutokana na uzalendo, ndipo mambo mengine ya umoja na mshikamano yanaweza kupatikana.
Pamoja na JKT, kulianzishwa shule za kitaifa. Hapo vijana waliweza kutolewa maeneo walikozaliwa na kusoma elimu ya msingi, na kupelekwa kusoma sekondari na vyuo vilivyo mbali na kwao kwa asili.

Hapo vijana kutoka Musoma walipelekwa kusoma Songea; vijana kutoka Tanga walipelekwa Sumbawanga; vijana kutoka Kagera walipelekwa Mtwara, na kadhalika, na kadhalika. Mwingiliano huo ukawafanya vijana wa Tanzania waweze kuyapokea na kuyakubali mazingira mapya. Hapo udugu na mshikamano miongoni mwa vijana ukaimarika. Wakaoleana, na leo Tanzania ni nchi ya machotara wengi. Kwa vijana wa wakati huo, si ajabu kabisa leo kuwakuta wakipiga soga wakikumbusha maisha ya JKT, sekondari au vyuoni.
Ujenzi wa taifa moja lenye watu wamoja bila kujali tofauti za makabila 126 si jambo dogo. Ni jambo kubwa linalowastajabisha walimwengu wengi. Lakini ni vizuri vijana wa sasa wakatambua kuwa umoja huu haukutokea kama ‘bahati ya Mtende’-bali ni juhudi za makusudi zilizofanywa na waasisi wa Taifa letu.

Nimepata kuandika kuwa waandishi wa habari kuna wakati wanapaswa kuweka kando ‘uandishi wao’ na kuutazama zaidi ‘Utanzania wao’. Uandishi wa habari utakuwa hauna maana kama hakuna “Tanzania ya maana’.
Nikatoa mfano wa namna waandishi wa habari wanavyopaswa kutenda wakati wa vita. Kipindi nchi inapokuwa vitani, ni kipindi pekee muhimu ambacho maadili ya uandishi huendana na hali ya uzalendo ili kulinda maslahi ya nchi.
Wakati wa vita, mwandishi anaruhusiwa kuandika habari za kutia hamasa ya ushindi hata kama anajua nguvu ya adui ni kubwa. Mwandishi hawezi kuandika habari ya kuwakatisha tamaa wananchi wake, na wala hawezi kuandika habari ya kuwabeza adui.
Nayasema haya kwa sababu tayari wapo wanaohoji uhalali wa baadhi ya waandishi wa habari kuamua kuwa ‘upande wa Serikali’ kwenye vita hii ya kiuchumi iliyokwishatangazwa na Rais John Magufuli.
Waandishi, kama raia wazalendo wana kila sababu za kuungana na wananchi na Serikali kwenye mapambano haya. Nayasema haya si kwa kutetea uamuzi mbaya wa kuvifungia vyombo vya habari, bali kwa kuangalia nafasi ya vyombo hivyo katika mapambano haya ya kiuchumi.

Kwa siku za karibuni kumeibuka suala la kuhamasishana woga kwenye mapambano dhidi ya wapora rasilimali zetu za madini. Awali, iliibuliwa hofu kwamba kwa kuyazuia yale makontena 277 ya madini pale bandarini, tungekiona cha mtema kuni. Hilo likapoa. Baada ya kiongozi mkuu wa Barrick kuzungumza na Rais Magufuli, na kuafikiana pande mbili kukutana kwa mazungumzo, kumekuja hoja nyingine. Kwanza, ni madai ya kwamba Barrick hawakusema watalipa.
Mimi si mchumi, lakini kwenye mazungumzo ya kibiashara kunapowekwa maneno ‘win-win’ bila shaka yanalenga kuonyesha kuna namna ya pande zinazokinzana, kuketi na kufanya mazungumzo yenye kuleta tija kwa kila upande. Sasa tija haina maana tusiambulie chochote!

Pili, kunaibuliwa hofu ya kwamba hao Barrick tunaoenda kuzungumza nao ‘si wa mchezo’! Tunaambiwa kuna watu ‘hatari’ na wenye uwezo mkubwa sana! Vigogo hao ni pamoja na mawaziri wakuu, mawaziri wa zamani wa nchi nne tofauti zilizoendelea.
Sawa, wana majina makubwa. Hakuna anayepinga hilo. Lakini ni nani aliyesema Watanzania wote ni mbumbumbu kiasi cha kushindwa kuwapata miongoni mwetu japo watano kwenye idadi yetu inayotajwa kuwa ni watu milioni 52? Miaka zaidi ya 50 ya kuwasomesha Watanzania wote hawa inawezekana vipi tukawa hatuna wa kusimama mbele ya wababe hawa kujenga hoja wakaeleweka?
Watanzania tumekuwa na sifa ya kushiriki mijadala na kushinda! Tuliposhindwa, tulishindwa kibabe, lakini si kwa kukosa wajenga na watetezi wa hoja. Je, tuwaogope Barrick kwa sababu ni wazungu? Ujinga huu wa kuamini kuwa hatuna Watanzania wa kusimama na hawa mabwanyenye kwanini tunaupigia debe?

Kama miaka ya 1960, 1970 na hata 1980 tulikuwa na Watanzania waliotikisa na kuheshimiwa mno kwenye majukwaa ya mijadala ya kimataifa, hili la madini kwanini tujione tu wanyonge sana?
Kanuni kuu ya askari yeyote mzalendo anaponuia kuingia vitani, ni kwenda kushinda vita. Askari wa kweli haendi vitani ‘kujaribu kushinda’. Hakuna kujaribu, ni kwenda kushinda, basi. Hiyo ndiyo kanuni ya vita.
Amiri Jeshi Mkuu wa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipotangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini, alitangaza kwa kujiamini kwa sababu alijua nyuma yake Watanzania walimuunga mkono. Kwa kujiamini huko, Mwalimu akasema: “Uwezo wa kumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo. Na nia ya kupiga tunayo.”
Mwaka 1967 Mwalimu aliyaona haya ambayo leo Rais Magufuli, anajitahidi kuyafanya. Bahati mbaya watu hawasikilizi hotuba wala hawasomi vitabu vya Mwalimu. Huwezi kuwa mzalendo au kiongozi wa nchi kama husomi maandishi ya Mwalimu na wanamapinduzi wengine wa aina yake duniani.

Mwalimu alisema: “Japo jambo ni la manufaa katika nchi yetu wenyewe, ukilifikiria kulitenda unaogopa! Unaogopa wakubwa; kuna mirija yao hapa. ‘Watapenda?’ Tunajiuliza kama watapenda. Japo tunajua lina manufaa kwa nchi yetu wenyewe hatuthubutu kulifanya bila kujiulizauliza, ‘Wakubwa watasemaje, jama? Mirija yao iko hapa; kitendo hiki kitagusa mirija yao?—Huku ni kujitawala? Huko ni kujitawala kwa u-prefect, unyapara! Mnalinda mirija ya waheshimiwa wengine; huko ni kujitawala? Kwamba tunaposema tunataka kujitawala, tujitawale barabara, maana yake ni kulinda mirija ya watu wengine katika nchi yetu, na kuiita zaidi kuja? Hata kidogo!
“Kujitawala ni kujitegemea. Tunataka kuijenga nchi yetu wenyewe. Kazi yetu ni kukata mirija, siyo kuijenga na kuitetea. Kazi yetu ni kujenga, tufike katika hali ya dunia ambapo kila taifa linaishi kwa jasho lake. Tutakuwa na uhusiano wa biashara na mataifa mengine, lakini siyo uhusiano wa mirija na chungu.” Mwisho wa kunukuu.

Tunaambiwa kuna Watanzania wameamua kuungana na mabepari kukwamisha vita hii ya kiuchumi. Maneno haya yamezungumzwa na kiongozi wa nchi. Hatuna sababu ya kuyatilia shaka. Ama, yapo, au yanakuja! Manabii wa mabepari tunao humu humu ndani.
Mwisho, tunapaswa kuwa wakweli. Dhambi hii ya mikataba mibovu imebuniwa, imezaliwa na kulelewa na wabunge wa CCM. Wakati tukijitahidi kutoangalia tulikoangukia, ni vema tukakiri hilo kwanza. CCM kwa kutumia wingi wao bungeni walipitisha mikataba ya aibu. Haya ndiyo matokeo ya ‘ndiyoooo’! Wapinzani waliokuwa na hoja za maana kabisa walipuuzwa kwa sababu tu ni wapinzani. Wengine walifukuzwa na kufungiwa wasihudhurie vikao na mikutano kadhaa. Leo historia inawaweka huru. Mbunge wa CCM wa kweli atakiri haya, hata kama hataomba radhi hadharani. Hili ni funzo. Ndiyoooo za bungeni na ubabe wa maspika na wenyeviti, havifai. Wanaokosoa wapewe fursa ya kusikilizwa. Kitabu kihukumiwe kwa yaliyomo, na si kwa jalada lake. Tunaweza tukawa hatuwapendi wapinzani, lakini hoja zao za zipokewe, zichekechwe na mwishowe zifanyiwe kazi.

Rais Magufuli ndiye Rais wa Taifa letu. Taifa ni kama familia. Familia ya chifu ina watu wengi. Miongoni mwao wamo wenye busara na hekima. Wamo walevi na wasio walevi. Wamo waropokaji na pia kuna wanyenyekevu. Wamo wamwabuduo Mungu na wasiomtambua Mungu. Wamo wafupi na warefu, wanene na wembamba, wenye akili timamu na wenye mtindio wa ubongo. Wamo weusi na weupe. Woooote hao ni wa familia ya chifu! Chifu muungwana huwakubali wanafamilia wake wote, na kuishi nao kulingana na sifa na weledi wa kila mmoja.

Tundu Lissu ana akili, lakini huenda akawa anapungukiwa busara ya uwasilishaji hoja zake. Asipuuzwe. Rais amsikilize, na achukue yaliyo ya maana, yasiyo maana aachane nayo. Hata saa mbovu kuna wakati husema ukweli! Muda hufika pale mshale ulipokwamia na kuonekana kama ni nzima. Naam, kwa Lissu kuna wakati Rais ataambua mawili au matatu ya maana. Asijibizane naye kwa sababu wawili hawa ni wa ngazi tofauti kabisa.
Lakini zaidi ya yote, tutambue nia njema ya Rais Magufuli katika kuwatumikia Watanzania. Hahangaiki na makinikia kwa ajili ya kuneemesha ukoo wake tu. Anawahangaikia Watanzania wote. Tunapomkosoa, tumkosoe kwa staha maana naye ni binadamu. Anapobezwa au kutukanwa kwa lugha za maudhi, anauvua urais na kuuvaa ubinadamu. Anakuwa mkali. Tusimfikishe huko. WOGA NDIYO SILAHA DHAIFU KULIKO ZOTE. Je, tuwaogope wezi kwa sababu ni Wazungu? Hapana. Tumuunge mkono Rais Magufuli katika vita hii halali.

1087 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!