Makala ya leo yenye anuani ‘Tuwatakie ndugu zetu Wakristo heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2022’ inaangazia suala lenye mitazamo miwili inayopingana katika jamii ya Kiislamu kutokana na kutofautiana rai za wanazuoni wa Kiislamu kuhusu suala hili. 

Mtazamo mmoja ni ule wa wanazuoni wanaopinga kuwatakia ndugu zetu Wakristo heri ya Krismasi na Mwaka Mpya na kwamba jambo hilo ni haramu (anayeliacha anapata thawabu na anayelifanya anapata dhambi).

Ufuatao ndio msimamo wa kundi hili:

“Mwanazuoni mkubwa wa kundi hili, Shaykh al-Islaam (Sheikh wa Uislamu)  bin Taymiyah (Allaah Amrehemu) alisema kwenye ufafanuzi wake wa Ayah ya 72 ya Sura ya 25 (Surat Al-Frqaan) katika Qur’an tukufu isemayo Na wale ambao hawashuhudii uongo, (az-zuur) kuwa: 

 “Ama kuhusu sherehe za mushrikiyn  wanakusanya pamoja mambo yenye kutia wasiwasi, mahitaji ya mwili na uongo, hakuna chochote ndani yake ambacho kina faida ya kidini, na mwisho wa kutosheleza hizo shahawa, ni maumivu. Hivyo, vitendo vyao ni vya uongo, na kuvishuhudia kunamaanisha kuvifanya. Hii Aayah peke yake inawapandisha daraja na kuwapa moyo (wale ambao hawashuhudii uongo), ambayo ina maana ya kuwahimiza watu kuachana na kushiriki kwenye sherehe zao mushrikuun (watu wanaomshirikisha Mwenyeezi Mungu) na aina nyinginezo za uongo. 

Tunafahamu kwamba ni vibaya kushiriki kwenye sherehe zao kwa sababu wanaitwa az-zuur (waongo). Inamaanisha kwamba ni haraam kufanya hivi kwa sababu zilizo nyingi, kwa sababu Allaah Ameiita ni az-zuur.

Anas bin Maalik (Allaah Amrehemu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja (Madiynah) na walikuta siku mbili ambazo kipindi cha Jaahiliyyah watacheza (na kujipumzisha).” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Allaah Amekupeni kilicho bora zaidi kuliko mambo hayo: Yawm adh-Dhuhaa (‘Iyd al-adh haa) na Yawm al-Fitr (‘Iyd al-Fitr).” (Imesimuliwa na Abuu Daawuud).

Hii inaonyesha wazi kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila ya shaka alizuia Ummah wake kusherehekea sherehe za kikafiri, na alihakikisha kuziondosha kwa njia zozote zinazowezekana. 

Ukweli wa kwamba dini ya Watu wa Kitabu inakubaliwa, haina maana kwamba sherehe zao zinakubalika au ziendelezwe na Ummah, kama yalivyo matendo yao mengine ya kikafiri yasivyokubalika, na dhambi zao pia hazikubaliki. Hakika, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifikia hadi kuamrisha Ummah wake kujitofautisha nao kwenye mambo mengi ambayo ni mubaah (yanaruhusiwa) na kwa taratibu nyingi za ibada, kwa sababu tu; kwamba vinasababisha kuwa sawa nao kwenye mambo mengine pia. 

Hii kuweka tofauti; ni kuonyesha kizuizi katika nyanja zote, kwa sababu namna utakavyokuwa tofauti na watu wa Motoni, ndivyo utakavyokuwa mchache wa kutenda matendo ya watu wa Motoni.

Kuwatakia kheri ya Krismasi makafiri na hata sikukuu nyingine za dini tofauti ni haraam kwa mujibu wa makubaliano ya wengi, kama Ibn al-Qayyim (Allaah Amrehemu) alisema kwenye Ahkaam Ahl adh-Dhimmah. (Chanzo: https://www.alhidaaya.com/sw/node/6043).

Akijibu swali kuwa: “Je, inafaa kwa Muislamu kusherehekea Krismasi? Mwanazuoni wa Kiislamu nchini Tanzania, Sheikh Daktari Abdulqadir Shareef, (Msomi wa Sharia na Sheria aliyepata Shahada ya Awali na Shahada ya Umahiri ya Sharia nchini Saudi Arabia na Shahada ya Uzamivu nchini Uingereza) amefafanua ifuatavyo:

“Hakuna uharamu kusherehekea mazazi au tukio jema lolote lile, ilimradi si kwa vitu au mambo ya haramu yaliyokatazwa kuyatenda, wala si kwa matambiko ya kishirikina. Huo ndio msingi wa amali yoyote ile njema katika Dini ya Uislamu.

Na Uislamu unatutaka tuamini mitume wote wa Mwenyezi Mungu, tokea mitume wa kawaida waliotajwa ndani ya Qur’ani, hadi mitume waliotumwa kwa watu wao mahususi, yaani wajumbe wa  Mwenyezi Mungu,  ambao pia wametajwa ndani ya Qur’ani na kutajiwa vilevile na mtume wetu, pasi na kutofautisha katika kuamini utume wao. 

Mwenyezi Mungu amewaelezea waumini kuwa ni wale wenye kuamini mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kama anavyoamini Mtume Muhammad (Swalla Llaahu Alayhi wa Sallam). 

{Tunasaoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat l-Baqarah), Aya ya 285 kuwa}: “Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na waumini nao vilevile. 

Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na malaika wake, na vitabu vyake, na mitume wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika mitume wake. Na waumini husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghafira Mola wetu, na marejeo ni kwako.”

Hivyo, Waislamu wote wanaamini Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, na kamwe hawatofautishi baina ya mmoja dhidi ya mwingine, na wanafurahi kwa siku za mazazi yao na kwa matukio yao mema, na pale wanapo fanya hivyo huwa wanamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewaleta mitume hao na kuwapa mafanikio katika mahubiri yao na amali zao za kuwaongoza watu wao, kwani wao ni  miangaza kwa watu wao kutoka kwa Mola wao. Hivyo, kuletwa kwao ni Rehema, Nuru na Mwangaza kwa umma wao, na kwa wasio  kuwa wao. 

Na wote wameletwa kwa ujumbe mmoja mkubwa nao ni kumuabudu Allah, Mmoja, pasi na kumshirikisha na  chochote. Huo ndio ujumbe wa kila Mtume wa Mwenyezi Mungu. 

Kwa maana hiyo, mazazi yao ni neema kwa umma wote, na ni miongoni mwa neema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa watu wote.  

Nabii Isa (Wakristo wanamuita Yesu) ni miongoni mwa mitume hiyo, hatumtofautishi na mitume wengine wa Mwenyezi Mungu, wala hatumtengi na mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. 

Na Mwenyezi Mungu ameelezea mitume kadhaa kuwa ujio wao ni Amani na Usalama, katika aya mbalimbali, ikiwa pamoja na Amani na Usalama katika siku za kuzaliwa kwao. 

Hivyo, mazazi na ujio wa mitume wote ni Rehema na Amani kwa viumbe vyote.  Na kwa maana hiyo kuonesha furaha au kusherehekea ni kuonesha shukrani kwa Aliye waleta Mitume hao, na hivyo ni jambo halali, halina mushkeli wowote, ilimradi linaadhimishwa na kusherehekewa kwa njia halali pasi na kumshirikisha Mwenyezi Mungu wala kutenda yaliyo haramu. Hakuna junaha. 

Mtume(Swalla Laahu Alayhi wa Sallam)  aliwakuta Mayahudi wa Madina wanafunga  Ashura, akauliza wanafunga kwa sababu gani? 

Wakamjibu kuwa wanafunga kuadhimisha siku ya kuokolewa kwao kutoka kwenye makucha ya Firauni, kupitia kwenye mikono ya Nabii Musa. Hivyo wanafunga kama alivyokuwa akifunga Musa kutoa shukrani kwa Mola wake. 

Mtume akasema: “Mimi nina haki zaidi kwa Musa kuliko wao,” yaani ana haki zaidi ya kuisherehekea siku hiyo kuliko wao. Akafunga na kuamrisha Waislamu wafunge vilevile, na waongezee tarehe 9 ili kujitofautisha na Mayahudi. 

Hivyo, kufunga Waislamu siku ya Ashura hakujazingatiwa wala hakuwezi kuzingatiwa kuwa ni haramu kwa dai kuwa tunaigiza swaumu ya Mayahudi, wala haimaanishi kuwa funga yao ni sawa na funga yetu sisi Waislamu, au kuwa tukifunga basi tumeigiza itikadi na imani ya Mayahudi.

Hivyo, hakuna ubaya wala dhambi za kusherehekea matukio mema ya mitume wa Mwenyezi Mungu, ilimradi si kwa matambiko ya kishirikina. 

Lakini mambo yoyote yale mengine ambayo ni halali kuyafanya, basi hakuna ubaya kuyafanya kwa kusherehekea matukio mema hayo. 

Ni kwa msingi huo huo, hakuna junaha kwa Waislamu kusherehekea na kuadhimisha mazazi ya Sayyidinaa Isa (Amani iwe juu yake) siku yoyote ile, mwezi wowote ule, na kadhalika; maana kufanya hivyo, kwa atakaye, ni kuonyesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu. 

MtumeMuhammad (Swalla Llaahu Alayhi wa Sallama) amesema kuhusu Nabii Isa (Amani iwe juu yake): “Mimi ndiye mwenye haki zaidi kumhusu Isa mwana wa  Maryam, Duniani na Akhera; hakuna baina yangu na baina yake mtume yeyote.” Yaani mini ndiye ninayefuata kwa utume baada ya Nabii Isa (Amani iwe juu yake).

Asiye taka asifanye. Ila asiwakufurishe wenye kufanya; anajifanya mungu-mtu. 

Na kwa msingi huo huo, hakuna junaha (dhambi) kuwatakia Wakristo,  au Mayahudi, bali watu wowote wale, kuwatakia vilevile, kheri na baraka kutoka kwa  Mwenyezi Mungu katika siku yoyote ya maadhimisho ya matuko yao mema, iwe ni maadhimisho ya sikukuu yao, au ni maadhimisho yenye kuhusiana na mitume wao. Hakuna junaha. Haikatazwi kumuombea mema mwanadamu yeyote aliye hai, awe Mwislamu au si Mwislamu, Muumini au Si Muumini sahihi wa Mwenyezi Mungu Mmoja. Ilimradi unayemuomba ni Allah si mwingine. Na kuomba, kama ninavyosema siku zote, ni kuabudu. 

Hivyo, ukimuomba Mwenyezi Mungu umemuabudu, na kumuabudu ndiyo kazi kuu uliyoumbiwa, hivyo unapata thawabu; hauna unachopoteza wala kula khasara. 

Na ukiomba unaabudu. Kukubaliwa au kutokukubaliwa mwachie Mwenyezi Mungu; si kazi yako, wala si jukumu lako!

Zaidi, ni kwamba ikiwa huyo unayemtakia wema katika mnasaba  wa jambo jema, ni jirani yako, basi kumuombea dua ni sehemu ya wajibu wako juu yake, ikiwa sehemu ya ujirani mwema katika Uislamu. 

Vivyo hivyo, iwapo mtu huyo ni mfanyakazi mwenzako, muajiriwa mwenzako, au ndiye aliyekuajiri katika kazi halali, au una fungamanisho njema naye, fungamanisho za utu na ubinaadamu, basi hakuna junaha, hata kidogo, kumtakia kheri katika sikukuu  yake.  

Wala hakuna junaha kumtakia siku njema, siku yoyote ile. Kama ilivyo ni wajibu wako kujibu dua njema kutoka kwao katika minasaba mema yako wewe. Mwenyezi Mungu amesema: “Mkiamkiwa basi jibuni maamkuzi vema zaidi, au kama mlivyoamkiwa.”  

Kufanya hivyo hakumaanishi, hata kidogo, kwamba sasa na wewe  unaamini wanachoamini wao, wala kuwa wao wanaamini unachoamini wewe: Kila mmoja anasalia na dini yake, na anayemuamini. Lakini utu na ubinadamu ni mmoja. (itaendelea wiki ijayo In-Shaa-Allaah).

Haya tukutane Jumanne ijayo!

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.

Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri