Nachukua fursa hii kumpongeza Padre Vedasto Ngowi kwa makala zake mbili zilizopita katika gazeti la Raia Mwema. Makala ya kwanza ilikuwa inasema, ‘Ngozi nyeusi, Kinyago cheupe’.
Makala ya pili ilikuwa inasema; Historia yetu inahitaji kuponywa? Rejea gazeti la Raia Mwema, Toleo Na. 500, Machi 8-Machi 14, 2017. Katika mfululizo wa makala hizi, Padre Vedasto amejaribu kuchimbua fikra za Mwafrika zilivyochangia kukwamisha maendeleo katika bara lake.
Anasema; Afrika inajibu changamoto zake kwa kutumia fikra za Kizungu. Katika hilo nakubaliana na Padre Vedasto Ngowi. Kwa ndani Waafrika wanaishi Uafrika uliopitwa na wakati, kwa nje wanaishi Uzungu usio na mizizi katika historia ya Afrika.

Nilivyomwelewa Padre Vedasto katika makala zake hizi ni kwamba amezungumzia vitu viwili kwa wakati mmoja. Mosi, amezungumzia utamaduni wa Mwafrika akimaanisha kwamba Mwafrika ameusaliti utamaduni wake. Pili, amezungumzia mkwamo wa maendeleo wa Mwafrika. Makala yangu itajikita zaidi kuwatazama viongozi wa Afrika wanaoliongoza bara la Afrika.
Makala yangu inauliza: Tuwatundike Viongozi wa Afrika msalabani? Kama utaguswa na makala hii unakaribishwa kutoa maoni yako. Maoni yako kwa kiasi kikubwa yanaweza kusaidia kutatua tatizo linalolikabili bara la Afrika.
Maendeleo katika bara la Afrika bado ni kitendawili ambacho hakijapata jibu lake. Binafsi ninaamini kabisa kwamba viongozi wa Afrika ndiyo wamechangia kwa kiasi kikubwa mkwamo wa maendeleo katika Bara la Afrika.
Pamoja na kwamba Mwafrika kwa maana ya mtu mmoja mmoja amechangia udumavu wa maendeleo katika taifa lake, lakini pia kuna mkono wa nyuma. Huu mkono wa nyuma ni viongozi wa Afrika waliopewa dhamana na Waafrika wenzao kuwaongoza.

Tabia sugu waliyonayo viongozi wa Kiafrika ni kwamba wanalewa madaraka waliokabidhiwa na wananchi wao. Madaraka hulevya na madaraka makubwa hulevya zaidi. Viongozi hawa wamewasaliti wananchi wao.
Ninaungana na Prof. Patrick Lumumba aliyewahi kukosoa kwamba; Viongozi wetu wa Afrika wanamiliki Ipad ambazo hawajui hata kuzitumia na wakati huo mabinti wetu wanakosa hata pesa ya kununulia pamba za kike (pedi). Wanajenga majumba ya kifahari kila kona ya dunia wasiyoweza kuishimo.
Wananunua vyakula vya kila aina na wakati hawana hamu ya kuvila. Wananunua vitanda vya dhahabu wasivyoweza kuvilalia. Hii ndiyo sura halisi waliyonayo viongozi wa Afrika. Kila kukicha viongozi wa bara la Afrika wanabadili katiba za mataifa yao, ili waendelee kutawala.

Hawataki kuondoka madarakani kwa amani. Wanataka watawale milele. Watawala hawa wamejigeuza kuwa miungu-watu katika mataifa yao. Kwa Afrika ‘Rais ni mungu mdogo’. Rais Afrika hakosolewi. Anakumbushwa. Nimekuwa nikijiuliza swali hili: Ikulu za Afrika kuna nini?
Askofu Dag Heward Mills katika kitabu chake cha Viongozi na uaminifu anasema; Tatizo la Afrika ni uongozi. Afrika inatatizwa na viongozi wabaya, kuwa na viongozi wabaya ni sawa na kumkaribisha shetani kuwa rafiki yako.
Nchi nyingi za Afrika zinapata viongozi ambao wanaiba rasirimali za mataifa yao. Viongozi wa nchi za Afrika wana utajiri binafsi kuliko wa nchi wanazoziongoza. Tabia ya viongozi wa Afrika kujilimbikizia mali za umma imekuwa kama jadi.

Kila kiongozi anayebahatika kuwa rais wa taifa lolote la hapa Afrika anajilimbikizia mali za umma. Tabia hii ni lazima isakamwe na kila raia wa bara la Afrika ili ikome. Bara la Afrika limesimama kwa sababu ya viongozi kujilimbikizia mali za umma.
Bara la Afrika limezama kwa sababu ya viongozi kujilimbikizia mali za umma. Bara la Afrika limedumaa kwa sababu ya viongozi kujilimbikizia mali za umma. Bara la Afrika limezimia kwa sababu ya viongozi kujilimbikizia mali za umma.

Akihubiri katika Mkesha wa Krismasi wa Mwaka 2014, Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcius Ngalekumtwa, alisema; “Leo tunao viongozi wanaojilimbikizia mali, kuliko hata wanavyoweza kuzitumia, mtu unakuwa na mamilioni ya fedha ambayo unaweza ukafa hata hujayatumia. Huu si uongozi, hata simba hajilimbikizii nyama ya ziada kuliko anayoihitaji.” Hii ni aibu.
Afrika ni yetu. Wa kuijenga ni sisi na wa kuibomoa ni sisi. Bara la Afrika utawala umetushinda. Tumeshindwa kujitawala. Tatizo ni nini? Rais Dolnad Trump wakati wa kuwania kiti cha urais katika taifa la Marekani alinukuliwa na vyombo vya habari vya ulimwengu akisema, “Afrika inahitaji kutawaliwa upya.”
Swali; Kwa nini Afrika ndiyo itawaliwe upya na mabara mengine yasitawaliwe? Kauli hii niliipokea kwa mshituko. Nisingependa kumshambulia kwa matusi Rais Trump ninaamini kuna kitu alikiona barani Afrika ambacho kilimshawishi kutamka kauli hiyo. Uongozi wa Kiafrika ni wa kitoto-kitoto.

Haukui. Kwa maneno ya mwanahabari Jererali Ulimwenguni ni kwamba, “Jamii ikishindwa kuonesha dalili za kukomaa na ikabakia kuwa jamii ya “kitoto” ambayo bado inahitaji baba mkali wa kuicharaza bakora, jamiii hiyo inakuwa imevia, imedumaa, imekwama mahali fulani katika mchakato wa kukua. Inakuwa jamii ya kunyonya dole gumba daima.” Bara la Afrika bado linanyonya dole gumba. Aibu kwetu.
Mwanafalsafa George Wilhem friedrich Hegel (1770-1883) alipokuwa akizungumzia tabia ya Waafrika alisema, “Waafrika ni mazimwi” (Africans are monsters). Hili ni tusi kubwa sana. Ingawa hoja alizotumia Hegel kumfikisha kwenye hitimisha hilo juu ya Waafrika zinaweza kupingwa na wengi.
Wanafalsafa wengi wa Kiafrika walipoisoma kauli ya Hegel walimchukia. Walimwambia kuwa yeye hajui Afrika na haelewi lolote kuhusu Afrika. Mwanafalsafa wa Kiafrika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa upande  wake alipenda mawazo ya Hegel, sina uhakika sana kama Nyerere angekuwa hai mpaka leo hii kama angeshindwa kuwafananisha Waafrika  na viongozi wao kama mazimwi.
Mpaka Mwafrika kufikia kiwango cha kufananishwa na zimwi ama kuitwa zimwi ni kwamba katika bara la Afrika kuna mambo mengi hayaendi sawa. Pale unapokosea njia, ukaambiwa umekosea njia bado ukawa king’ang’anizi kupita ile njia ulioambiwa kwamba umekosea lazima utaitwa zimwi.

Waafrika njia tumeikosea lazima tuitwe ‘mazimwi’ tu. Mawazo ya Hegel yameungwa mkono na wasomi kadhaa wa Kiafrika. Prof. Ali Mazrui katika andiko lake la ‘The Liberal Revival Privatization and Market; Africa Cultural Contradiction’’, anatoa mtazamo wake namna Mwafrika asivyoweza kuumiliki uchumi wake anasema, “Mwafrika hawezi kuongoza na kuendeleza uchumi wake, yeye hutawaliwa na ufahari na majigambo badala ya kiu ya kupata faida. Tatizo la Mwafrika siyo jinsi ya kubinafsisha uchumi na kuchochea uchu wa kupata, bali tatizo ni jinsi ya kudhibiti na kupiga vita jeuri ya ufahari, majivuno na majigambo ya kiuzawa katika kutawala uchumi’’.
Mtazamo wa Prof. Mazrui haupo mbali sana na kejeli ambayo ilipata kutolewa na Rais wa kwanza wa Senegali, Leopold Sedar Senghor, kupitia kitabu chake cha ‘La Negritude’ yaani Uafrika. Anasema, “Mtu mweusi siku zote hatumii akili yake ili aweze kuendesha maisha yake yeye mwenyewe. Mwafrika anatumia sana mdomo, tumbo, macho, pua, ulimi na sehemu zingine za mwili ili kuweza kutatua matatizo yake”.
Kauli za wasomi hawa ni za kuudhalilisha Uafrika. Siungani na wasomi hawa. Lakini kwa yale yanayotendwa na baadhi ya viongozi wa Kiafrika kauli hizi zinaweza kuwa na ukweli ndani yake. Lakini kwa kile kinachoendelea barani Afrika kauli ya Hegel itakuwa kweli kama Waafrika hawatakuwa tayari kuvaa viatu vya kuutafuta uhuru wa ufahamu katika bara lao.

Haiba iliyojengwa na wapigania uhuru wa bara la Afrika imepotea. Imepotea kwa sababu Afrika sasa inapata viongozi wenye uroho wa madaraka na wasio na mbinu za kuyainua mataifa yao kiuchumi, kielimu na kisiasa. Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Nelson Mandela na wengine wengi, hawa walikuwa ni wazalishaji wa mawazo katika bara la Afrika.
Ni hakika kwamba baada ya umauti wa viongozi hawa bara la Afrika limepoteza uwezo wa kuwafikirisha watu wao. Waafrika wamekuwa masikini wa mawazo, lakini matajiri wa starehe za matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali za umma. Binafsi ninaamini kabisa kwamba, viongozi wa Afrika ndio kikwazo kikubwa cha mkwamo wa maendeleo katika bara la Afrika.
Viongozi hawa wa Waafrika wamewekeza zaidi katika wizi wa mali za umma na ubabe wa kimadaraka kuliko kuwekeza kwenye fikra za watu wake. Leo hii Afrika nzima inateseka, ina mahangaiko, manyanyaso, vifo vya watoto, vifo vya akina mama, vita, ujinga na maradhi kwa sababu tu, ya hawa watawala wasio na maono kwa watu wao. Ni hakika bara la Afrika haliko salama! Haliko salama kielimu. Haliko salama kisiasa. Haliko salama kimaendeleo.
Haliko salama kiuchumi. Machafuko yanayotokea barani Afrika ni sura halisi iliyopo barani Afrika kwa sasa.

Mwanamuziki Bob Dylan siku moja aliulizwa swali na mtoto wake.  Mtoto wake alimuuliza hivi, “Baba unapenda sana kuimba, je, siku ukilewa na sifa za watu halafu ukawa unaimba vibaya vibaya utafanyaje? Baba yake alimjibu hivi, “Nitaacha kuimba”. Ninawaomba viongozi wa Kiafrika wasio na maono wakae pembeni. Mwandishi wa kizazi kipya aliyezaliwa huko Marekani, shakti Louisa Gawain, alipata kuandika haya “Matatizo ni ujumbe’’. Matatizo yanayolisubu bara la Afrika ni ujumbe kwa Wafrika na watawala wa Waafrika.
Waafrika tunaishi yale maisha ambayo hayakukusudiwa tuyaishi na ndiyo sababu maendeleo katika bara letu yanaenda mwendo wa chatu aliyeshiba. Mwandishi  Haroub Othman katika kitabu chake  kinachoitwa, Reflection on Leadership in Africa; Forty years after Independence; Essay in Honour of Mwalimu Nyerere on the occasion of his 75th birthday amemnukuu Mwalimu Nyerere akisema; ‘Siku inakuja ambapo watu wanyonge na wanaonyanyaswa watachagua kifo kuliko fedheha, na ole wao watakaiona siku hiyo’.

Na ole wao wale watakayoifanya siku hiyo isiepukike. Natumaini na kusali kwa Mwenyezi Mungu kuwa siku hiyo kamwe haitofika.”  Nachelea kusema kama viongozi hawatabadilika ipo siku uvumilivu utawashinda Waafrika. Watapaza sauti zao. Dunia itaona hisia zao na Mungu atasikiliza kilio chao.
Na hapo wataupokea uhuru wa kutumia rasilimali zao kwa usawa. Mama Afrika Mungu akubariki. Mama Afrika Mungu awabariki watoto wako. Mama Afrika ninapowaona watoto wako wanavyoteseka machozi yanatiririka. Usikate tamaa Mama Afrika kesho njema inakuja.

By Jamhuri