Rais Jakaya Kikwete ametoa baraka za ugawaji Mkoa wa Mbeya ili ipatikane mikoa miwili.

Tayari ameshafanikisha uanzishaji mikoa minne ya Simiyu, Njombe, Katavi na Geita. Pamoja na mikoa hiyo, ameanzisha wilaya nyingi mpya.

Tunambua na kuheshimu madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba ya uanzishaji maeneo mapya ya utawala hasa kwenye wilaya na mikoa.

 

Kumekuwapo sababu kadhaa za kufanya hivyo lakini zilizo muhimu ni za wingi wa watu, kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi, na pia kurahisha utawala kwenye maeneo hayo.

 

Hata hivyo, ugawaji wilaya, mikoa na hata majimbo ya uchaguzi ni mambo yanayohitaji umakini wa hali ya juu sana.

 

Waasisi wa Taifa hili walipoondoa majimbo na badala yake wakaweka mikoa, walikuwa na sababu nyingi. Sababi hizo kwa wakati huo zingeweza kuwa hazina umuhimu sana ikilinganishwa na leo, hasa ikingatiwa kwamba teknolojia ya mawasiliano na ujenzi wa miundombinu kama barabara, imeyafanya maeneo mengi yasifike kirahisi.

 

Miaka ya 1960 au mwanzoni mwa miaka ya 1970 kungeweza kuwapo madai ya msingi ya kuifanya Tukuyu kuwa mkoa ili wananchi wa karibu na maeneo hayo, wakiwamo wa Kyela wasisafiri kwa shida kwenda kupata huduma katika Makao Makuu ya Mkoa mjini Mbeya ambako ni mbali. Lakini leo kutoka Kyela au Tukuyu kwenda Mbeya, ni jambo jepesi linalowezekana ndani ya muda mfupi.

 

Tunapenda kutoa tahadhari kwa mamlaka zinazohusika kuwa makini na ugawaji huu ili tusife mahali pa kukuta nchi inagawanywa kwa misingi ya ukabila. Mjadala unaoendelea sasa mkoani Mbeya una vimelea vya kuyafanya makabila makuu yawe na pande zake. Endapo jambo hilo litatekelezwa, kunaweza kuibuka dhana ya ukabila katika mikoa na wilaya zetu.

 

Aidha, Wilaya ya Butiama sasa kuna mikakati mizito mno ya kuigawa. Tayari baraka zimeanza za kuifanya wilaya hiyo iwe na halmashauri mbili. Lakini kinachoonekana ni kwamba ugawaji huo utalenga zaidi kwenye ukabila kwa sababu upande wa mashariki kuna watu wenye asili moja au inayokaribiana mno, na upande wa kaskazini ina wengine wa aina hiyo. Hatari yake ni kwamba kuna wakati tunaweza kuwa na halmashauri au wilaya ya Wazanaki ambao ni sawa na Wakurya, na nyingine ya Wajita ambao ni jamii hiyo hiyo na Wakwaya na Waruri.

 

Lakini pia ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika na ugawaji huu kutumia busara zaidi kuona kama kweli kuna umuhimu wa “kuwafurahisha” watu kwa kuwapa wilaya na mikoa, wakati huo huo Serikali ikawa haina uwezo wa kujenga miundombinu na huduma muhimu za kijamii.

 

Ni ukweli ulio wazi kwamba unapoanzishwa mkoa au wilaya, ukubwa wa Serikali unaongezeka kutokana na idadi ya watumishi. Hali hiyo inaweza kuzifanya wilaya na mikoa kuwa chanzo gharama kubwa kwa walipakodi, na hivyo kuufanya uamuzi mzima wa kuianzisha usiwe na tija.

 

Muhimu zaidi tunaomba mamlaka husika zigawe wilaya au mikoa au majimbo ya uchaguzi kwa kukwepa zaidi vigezo vya ukabila. Watanzania ni lazima waendelee kuwa wamoja. Kutaka kumfurahisha kila mtu kunaweza kuligawa Taifa letu.

 

By Jamhuri