Awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua ambayo tumefikia katika kupambana na ujangili nchini Tanzania. Hakika ujangili umeshamiri sana katika taifa letu siyo tu kwa meno ya tembo peke yake bali hata kwa nyara nyingine za Serikali. Kwa muda mrefu sana Tanzania imegubikwa na tatizo kubwa la ujangili katika Mapori ya Akiba (Game Reserves) pamoja na Hifadhi za Taifa (National Parks). Vilevile, tumekuwa tukisikia kupitia vyombo vya habari: vikituhabarisha kwamba meno ya tembo yamekamatwa huko Hon-Kong; Vietnam; Thailand; Indonesia; Philippines na sehemu nyinginezo na yanapokamatwa taarifa hutolewa kwamba yanatoka Barani Africa hususani nchini Tanzania. 

Inapodhihirika kwamba meno ya tembo yamekamatiwa nje ya nchi yetu, ni nadra sana kutosikia kwamba hayatoki Tanzania. Nchi yetu hutajwa mara kwa mara kwanza, kutokana na ukweli kwamba ndani ya Tanzania kuna mbuga nyingi za wanyama kuliko mataifa mengine Barani Africa. Kutokana na ukweli huo inawezekana wanaokamata meno ya tembo nje ya nchi wakaamini ni mali ya Tanzania. Pili, inawezekana kwa kutumia Bandari zetu za Dar-es-Salaam, Mtwara na Tanga meno haramu ya tembo kutoka nchini nyingine yakawa yamepitishwa kwetu bila kuyagundua lakini yanapofika huko na yakakamatwa yataonekana yanatoka Tanzania kumbe Tembo waliokufa ni kutoka nchi nyingine. Kwa kusema hivyo simaanishi kwamba hapa kwetu tatizo la ujangili ni dogo hapana; tatizo lipo kubwa na kwa ujumla hali inatisha sana. 

Kwa mathani, katikati ya mwezi Novemba, 2016 kupitia vyombo vya habari tulihabarishwa kuwa huko mkoani Simiyu Askari Polisi (kupitia taarifa za raia wema) walikamata meno ya tembo mawili (uzito 32kg) eneo la Ipililo Wilayani Maswa yakiwa yamefichwa chini ya kitanda nyumbani kwa anayetuhumiwa kuwa jangili au mshirika katika mtandao wa ujangili. Hii ni dalili kwamba tembo wengi bado wanauawa na majangili. Vilevile, juhudi zinazoendelea za kupambana na ujangili nchini zinaashiria kuwa tatizo lililopo ni kubwa kiasi kwamba hata Mheshimia Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameona ni heri yeye binafsi akaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ujangili nchini. Juhudi hizi ni za kupongezwa sana na mwenye nia njema ya kuwaona tembo wakiwa na meno yao wanaendelea kuishi. 

Tembo tunawapenda sana ni sehemu ya urithi wetu kama taifa pia wanayo haki ya kuishi wakiwa na meno au kama hawana wawe wamezaliwa hivyo. Kukatisha maisha yao kwa uroho wa kupata utajiri kutokana na biashara haramu ya meno ya tembo ni kuliangamiza taifa. Tanzania tusipokuwa na tembo wa kutosha biashara ya utalii nchini itadorora sana. Tembo ni kati ya wanyama muhimu katika hifadhi zetu wajulikanao kama “the big five” ambao pamoja na mambo mengine kama Mlima Kilimanjaro huwa ni vivutio vikubwa kwa biashara ya utalii nchini. Wengine aina ni Simba, Nyati, Chui na Faru. Vilevile, wanyama kama Faru maisha yao pia yako hatarini kutokana na kushamiri ujangili kwa sababu ya meno waliyonayo. Faru pia anatafutwa sana na majangili kutokana na biashara haramu ya jino lake. Majangili bila woga yanadiriki kuingia katika maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa lengo la kuua tembo na faru pamoja na wanyamapori wengine kwa faida zao binafsi. Majangili ni watu hatari sana siyo tu kwa tembo na faru bali pia kwa askari wanyamapori na kwa kuwa majangili hutumia silaha nzito askari wanaweza wakapoteza maisha. Ikitokea kwamba majangili yameua askari itakuwa hasara mara mbili: taifa kupoteza askari wanyamapori lakini pia na tembo kuuawa. Hali kama hiyo ikitokea siyo nzuri hata kidogo hivyo inabidi tupambane kwelikweli tena bila ya kuwaonea huruma majangili.

Nathubutu kusema kwamba hatua aliyoichukua Mkuu wa nchi tarehe 29 Oktoba 2016 (siku ya Jumamosi) kwenda gafla kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni jambo lenye kutia moyo. Naamini Kikosi maalum cha Wizara chenye jukumu la kupambana na ujangili pamoja na viongozi wa Wizara watakuwa wamefarijika sana na ujio huo wa Mheshimiwa Rais (hata kama ulikuwa wa kushutukiza). Nia ya Rais wa Serikali ya awamu ya tano, kwa kufanya hivyo, ilikuwa njema sana badala ya yeye kukaa Ikulu akisubiri kuletewa taarifa. Aliona ni vyema akafika na kushuhudia mwenyewe nini kimefanyika ikiwa ni pamoja na kuyaona meno ya tembo pamoja na majangili waliohusika kuua Tembo kwa sababu ya tamaa zao binafsi. 

Kwa muda mrefu sana tumekuwa na jitihada za kupambana na ujangili nchini lakini mafanikio yamekuwa siyo ya kuridhisha. Kwa mfano, operesheni kadhaa za kupambana na ujangili bila kuwa na mafanikio mazuri zimekuwa zikifanyika. Mara ya mwisho ilifanyika operesheni iliyojulikana kama TOKOMEZA Ujangili. Operesheni hii ilikuwa ya aina yake na kubwa kuliko zote. Utekelezaji kwa operesheni hiyo ulifanyika kijeshi lakini haikutufikisha kwenye matokeo yaliyotarajiwa yaani kuutokomeza ujangili. Pamoja na ukweli kwamba opereshi tokomeza iliandaliwa vizuri na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikisha Wizara nyingine na vyombo kadhaa vya kitaifa ikiwemo Mambo ya Ndani; Usalama wa Taifa; Jeshi (JWTZ); Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; iliingia dosari baada ya kuona kumekuwepo na kelele na malalamiko mengi na kwamba watu wasio na hatia wanaonewa. 

Inawezekana ikawa ni kweli watu walionewa na kwa kuwa malalamiko yalikuwa mengi hadi kufikia Mawaziri waliokuwa wakiongoza Wizara zilizoshiriki katika operesheni hiyo, wakalazimika kujiuzuru nyazifa zao. Hili halikuwa jambo dogo na ni operesheni iliyogusa sana hisia za watu wengi ikiwemo wafanyabiashara wakubwa, baadhi ya  viongozi wakubwa Serikalini (vigogo) na wanasiasa. Kumekuwepo na malalamiko pia kwamba biashara ya meno ya tembo inahusisha baadhi ya viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa. Pengine katika kutekeleza operesheni “tokomeza ujangili”; yawezekana baadhi ya watu waliona sasa ni hatari na huenda wakakumbwa na dhoruba ya tokomeza. Hivyo ikabidi waanzishe mtarafuku kwamba operesheni haifai kuendelea na kwa nguvu zote kushinikiza isitishwe na kwamba viongozi husika wawajibishwe ili iwe salama kwao na wakati huohuo tembo wanaendelea kuuawa. 

Kusema kweli tulichosahau ni kwamba operesheni hiyo iliendeshwa kijeshi na kwa maana hiyo ilikuwa ni “vita dhidi ya ujangili” (war against poachers). Ilikuwa ni dhamira ya taifa kwamba tuutokomeze ujangili ambao ulionekana kuwa ni tishio kubwa kwa maisha ya tembo na faru: hasa kwa majangili kutumia silaha kali za kivita kuwaua wanyama hao.  Kwa hali hiyo, majangili yakawa na nguvu sana kuliko kikosi cha kuzuia ujangili kilichopo Wizarani. Hivyo msaada wa kijeshi ulihitajika sana kuweza kuutokomeza ujangili katika Mapori ya akiba, Hifadhi za Taifa na Misitu iliyohifadhiwa kisheria. Kama tunavojua vita ni vita na siyo “lelemama”: ni mapigano makali kwa nia ya kumshinda adui. Zaidi ya hapo tukumbe kwamba kwenye uwanja au maeneo ya vita, kwa bahati mbaya (bila kukusudia), huwa wanakumbwa hata watu wengine ambao siyo walengwa au wasiokusudiwa. Ndiyo maana huwa tunasema: “vita haina macho”. Ndivyo tunavyoshuhudia sehemu wanakopigana vita mfano, Syria, Sudani Kusini, DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) au Iraq. Inapotokea kosa kidogo katika uwanja wa mapigano wanaathirika pia wasiohusika kama kupigwa mabomu hispitali, shule na makazi ya jamii na hizo ndizo athari za vita. 

Tangu mwanzo wa kutekeleza operesheni “tokomeza” wananchi walifahamishwa kuwa ni vita dhidi ya majangili hivyo walitakiwa wachukue tahadhari kwa kujisalimisha iwapo mtu alikuwa na aina zozote za nyara za Serikali au bunduki au silaha ya aina yoyote. Nia ilikuwa ni kuepuka madhara ambayo yangeweza kujitokeza mara vita dhidi ya ujangili itakapoanza. Kwa kuwa binadamu anayo asili ya kukaidi na inavyotokea mhusika akanaswa akiwa na silaha au nyara za Serikali atalalamika kwamba ameonewa. Hata hivyo mhusika akikamatwa na nyara akiwa katika eneo la uhifadhi huyo ni jangili. Vilevile, mtuhumiwa mwingine hata kama yuko nje ya eneo la uhifadhali, lakini akakutwa anayo meno ya tembo au nyara nyingine za Serikali kwa vyoyote vile atatiwa matatani kama ni jangili na haijarishi ni wa jinsia gani.

Kwa kuwa sasa msako wa majangili unafanywa na kikosi maalum na mwelekeo wake siyo wa kijeshi, naamini shughuli wanayoifanya itakuwa ya mafanikio makubwa kwa taifa letu. Pamoja na kutofanyika kijeshi ni vema watu wakaelewa kwamba atakayekutwa na meno ya tembo, faru au nyara nyingine za Serikali na yuko ndani ya eneo la hifadhi au karibu na hapo atatiwa matatani. Tayari dalili za mafanikio tumeanza kuziona kama alivyodhibitisha Mheshimiwa Rais, tarehe 29 Oktoba 2016 kwenye eneo la Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya kikosi hicho kukamata meno ya tembo 50 pamoja na majangili husika. Vilevile, ilielezwa kwamba kazi ya kuwakama majangili hao haikuwa rahisi maana kikozi hicho kimekumbana na changamoto na vikwazo vingi. Wanzania wanaopenda kuwaona tembo wakiishi kwenye Mapori ya Akiba na Hifadhi za Taifa, tuunge mkono juhudiu hizi zinzofanywa na Maliasili kwa kushirikiana na wadau wengine. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais kwamba ifike mahali majangili watakapokuwa wakiona tembo badala ya kuwaua wao (majangili) wakimbie kwa kuhofia kuwa hata kama watawaua hawatafika mbali bila ya kushughulikiwa ipasavyo. Vilevile, majangri waone kuwa biashara hiyo haina faida tena hivyo waachane nayo na kutafuta riziki kwa njia iliyo rafiki kwa tembo na wanyamapori wengine. Tukifikia hali kama hiyo taifa litakuwa limetimiza wajibu wake wa kusimamia, kutunza na kuwalinda wanyamapori kwa nguvu zake zote na kwa faida ya watu wake. 

Nini kifanyike ili kuifikia hali hiyo? Kwanza, taifa liongeze nguvu kupambana na majangili kwa kukiimarisha kikosi maalum ili kiwe na vitendea kazi vya kutosha. Pili, Askari Wanyamapori pia waongezwe na wapewe motisha pamoja na kuwajengea uwezo (capacity) ili waweze kuyasimamia mapori ya akiba na hifadhai za taifa ipasavyo. Tatu, kuwepo na mkakati wa makusudi wa kushirikisha vyombo vingine hususani wananchi wanaoshi katika vijiji au vitongoji vilivyo karibu au kupakana na Mapori ya Akiba au Hifadhi za Taifa ili waweze kutoa taarifa za majangili katika maeneo wanayoishi. Hii ni pamoja na kuwapatia motisha mara wanapofanikisha kukamatwa kwa majangili. Jamii ihamasishwe na iweze kuchukua hatua katika vita dhidi ya majangili. 

Uhamasishaji unaweza kupitia mikutano vijijini au hata kupitia michezo kama wanavyofanya katika Hifadhi ya Ruaha kwa kupitia mradi wa kuboresha uhifadhi chini ya msaada wa GEF kupitia UNDP. Kupitia mradi huo, hifadhi inaendesha mashindano ya “SPANEST CUP” kwa kushirikisha vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Ruaha mkoani Iringa. Lengo kuu ni kutaka jamii iunge mkono vita dhidi ya ujangili katika hifahi hiyo iliyokubwa kuliko zote nchini. Kupitia mradi huo Uongozi unahamasisha wananchi kwa njia ya michezo na kwa kushindanisha vijiji vinavyozunguka hifadhi. Wachezaji wanatoka vijijini wanasaidiwa vifaa kama jezi, viatu pamoja na mipira na timu zitakazoshinda zinapatia zawadi. Kauli mbiu kupitia michezo ni “PIGA VITA Ujangili, OKOA TEMBO”. Michezo inapokwisha sehemu kubwa ya jamii inakuwa imeelimishwa vya kutosha kuweza kuchukua hatua dhidi ya ujangili kwa kushirikiana na Uongozi wa hifadhi na vyombo vingine kama Polisi na Kikosi cha kuzuia ujangili.  

Inawezekana hali ikajitokeza kama ilivyokuwa wakati wa “operesheni tokomeza” kwa baadhi yetu kuanza kupiga kelele kwamba wananchi wanaonewa na kadhalika. Uwezekano huo wa hali kama hiyo kujirudia unatokana na kuwepo mtandao mkubwa wa ujangili ndani na nje ya nchi yetu wenye lengo kwa baadhi yetu kutaka kujitajirisha haraka.  Iwapo mtandao wa uhalifu huo ni mkubwa na kuhusisha “vigogo” kibiashara, kiserikali na kisiasa kuna hatari ya kikosi maalum cha kuzuia ujangili kikadhoofishwa kwa kukatishwa tamaa, kutishiwa au kutopewa ushirikiano mzuri hivyo kukosa motisha na morali mzuri wa kufanya kazi ipasavyo. Kwa suala hili ni kikosi kuwa na moyo thabiti wa kupambana na ujangili bila kujali vitendo vyovyote vya kuwakatisha tama. Wanakikosi jipeni udhabiti na muwe na moyo mkuu katika kulitekeleza jambo hili muhimu. Na kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonyesha dhamira njema katika mapambano haya ya vita dhidi ya ujangili hakuna litakaloshindikana.  Sasa ni kusonga mbele mkielewa kwamba mapambano yenu ni kwa maslahi ya Watanzania wote na kwa kufanya hivyo naamini Mwenyezi Mungu atawaongoza katika kufanikisha ushindi juu ya vita hii ngumu. HAKUNA LISILOWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO: MWENYEZI MUNGU AIBARIKI TANZANIA PAMOJA NA WATU WAKE. 

By Jamhuri