Katu ushoga haukubaliki Tanzania

Hivi karibuni, chombo kimoja cha habari nchini kimemnukuu Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe, akisema kuwa Serikali haihitaji ushauri wala ushawishi wa chombo  chochote cha ndani ama nje ya nchi, kuhusu masuala ya ushoga na ndoa za jinsia moja.

Chombo hicho maarufu hutoa habari zake kila wiki mara moja (siyo JAMHURI) kimenukuu maneno hayo na kueleza zaidi; “Nakubaliana na maafisa wangu kuyakataa mambo hayo, mwelekeo wa asasi hiyo iliyo ada kwa asasi nyingi za nje ni ushawishi kwa nchi yetu kuyachukulia masuala ya ushoga kama ya haki za binadamu,” mwisho nukuu.

Binafsi nakubaliana na maneno ya waziri, maafisa wake na msimamo wa Serikali kuhusu masuala hayo. 

“Ni batili kisheria, kiimani na hata kiutamaduni. Masuala hayo ni ya jinai na yamechelewa. Hayajadiliki mpaka pale Bunge litakapoamua vinginevyo,” Maneno ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwakyembe.  

Kauli hizo zilitolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 16, mwaka huu kati ya Dkt. Mwakyembe na mwakilishi wa Ukanda wa Afrika wa Asasi ya UPR Info (Universal Periodic Review), Gilbert Onyango, zinastahili kukubaliwa na Watanzania.

Watanzania wenzangu, mimi naamini kwamba watu wenye kuamini masuala ya dini, wanaofuata sheria za nchi na wanaoheshimu utamaduni wa Watanzania, kamwe hawawezi kutoa nafasi kwa masuala batili ya ushoga na ndoa ya jinsia moja kutamalaki nchini mwetu.

“Kama lengo ni kushawishi Tanzania itambue ushoga na ndoa za jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu kama ilivyo katika baadhi ya nchi Ulaya na Marekani, atakuwa anapoteza muda wake bure,” alisema Dkt. Mwakyembe kumwambia Onyango.

Nasema ni sawa. Kauli na msimamo wa Serikali tumeusikia. Je, Watanzania wenzangu tumepokea uamuzi huo kwa nia moja? Nazungumza hivi kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni kuanzia kwa miaka ya 2000, ujio na ushamiri wa utandawazi nchini, vitendo hivi vinapewa nafasi.

Kila uchao vyombo vya habari vinafichua, vinaripoti na vinahabarisha, na kadhalika huko mitaani na majumbani simulizi kuhusu watoto kubakwa na kulawitiwa, baadhi ya vijana na watu wazima (wake na waume) wanalawiti na wanalawitiwa kweupe kwa madai na maelezo mbalimbali.

Wapo wanaoeleza sababu ni haki za binadamu, hali ngumu za maisha, mmomonyoko wa maadili, dunia inafikia mwisho (kiama) na kadhalika. Inawezekana ikawa ni hivyo. Kwangu lililo kuu ni imani ya kumcha Mwenyezi Mungu na kutokwenda kinyume na matumizi ya maumbile ya miili yetu.

Kama vikundi, jumuiya, vyombo vya mawasiliano na umma na viongozi mbalimbali mnaweza na kuthubutu kukemea, kuhubiri, kuhamasisha na kukampeni  mambo mema na mazuri, vipi mshindwe kufanya hivyo kwa mambo mabaya na machungu kwa jamii hii?

Au mnaogopa michuzi kuchachuka? Kama ndiyo, kwa faida ya nani? Iwapo siyo, ni hasara kwa nani? Wenye dhamana nawasihi msije kuwa kama mung’unya kuharibikia ukubwani. Nina maana ya nyinyi kuruhusu uchafu huo kuwa ni sehemu ya maisha. Mnakataa mnaruhusu. Ni undumilakuwili.

Na kwetu Watanzania haifai kusifu na kupongeza tu juhudi za Serikali za kukataa ushoga na ndoa za jinsia moja, wakati pembeni mwazima taa. Tukumbuke kwenye nuru kuna mema na kwenye giza kuna mabaya. Tusikaribishe majuto kuwa mjukuu wetu. Tukaribishe hadhari kuwa mtoto wetu.

Ikumbukwe pia ibiliisi ana nguvu za ushawishi na vitu vizuri kwa nje lakini ana moto kwa ndani. Mungu ana uwezo mkubwa na vitu vichungu kwa nje lakini ndani ana pepo. Mashehe, maaskofu na viongozi mnatambua hilo. Lipi linawakwaza kuisema na kuihukumu jamii kinagaubaga?

Naona wakati ni huu kusimama imara pamoja kutoa elimu, nasaha na matangazo, kukataa matendo hayo machafu yaliyo kinyume na dini, sheria na utamaduni wa nchi yetu. Bila kufanya hivyo Serikali, viongozi na Watanzania ‘itakula kwetu’ na asasi ya UPR Info italamba dume na vicheko katika pumzi zao.

Namalizia kusema mara kadhaa nagusia na kuzungumzia suala la mila na desturi, utamaduni na maadili. Sijaona kasi ya msukumo, hadhari wala hukumu dhidi ya vitendo hivyo kutolewa na mamlaka husika. Tusisubiri matokeo ya matukio ndipo tuanze kushughulika.