Yah: Acha nizikumbuke enzi zetu, labda kwa hali hii zitashabihiana

Nakumbuka Lango la Chuma Mabibo bia ikiuzwa Sh. 18 yaani hii Sh. 100 ya sasa hivi unakunywa bia tano na chenji inarudi, maisha mazuri kwa mtumishi wa kila mahali, iwe serikalini au kwa mtu binafsi. Mshahara wa kima cha chini Sh 420 ulitosha kufanya kufuru zote pamoja na kuweka amana benki.

Hii ndiyo Tanzania ambayo ujana wangu nimeitumia, Tanzania ya asali na maziwa, Tanzania ya burudani baada ya kazi, Tanzania ya kudharau biashara na siasa na kutukuza ufanyaji kazi na kuleta maendeleo ya kweli, ni kama ndoto lakini huo ndiyo ukweli, naona kama ujana wa Taifa letu ni maji moto.

Ni juzi tu kama miaka kadhaa kila kitu kimebadilika, tulikuwa hatuagizi bidhaa kutoka nje ya nchi, kila kitu kilikuwa kinapatikana hapa hapa nchini, ni juzi tu tulikuwa tukiuza bidhaa na malighafi kwa wingi nje ya nchi, ulikuwa ukienda bandarini unakutana na mizigo mizito ya pamba, kahawa, katani, chai, mahindi, maharage, korosho, mtama  na kadhalika vikipelekwa nje.

Sisi tulikuwa tukiuza nje na kutumia ndani, ni juzi tu nchi hii ilikuwa na viwanda vikubwa sana na vingine vikubwa barani Afrika, lakini leo ni hadithi pekee tunazoweza kusimulia na mtu akatuelewa na kumuonesha magofu yetu, hiyo ndiyo fahari pekee ya Mtanzania.

Nakumbuka Kiwanda cha Karatasi Mgololo kama kiwanda kikubwa sana Afrika, kikitengeneza karatasi na kuziuza nje baada ya kutosheleza mahitaji ya ndani, nakumbuka viwanda vya nguo vilivyotapakaa nchi nzima kama ishara ya kujitosheleza katika mavazi, hatukuwa na shida ya mbeleko au khaki ya rangi yoyote ya shule.

Nakumbuka viwanda vya sukari na mashamba ya chumvi, nakumbuka zana za kilimo. Ujana wa Taifa hili maji moto umepoa.

 

Nakumbuka Kiwanda cha Bora kilichokuwa kikizalisha viatu vizuri sana kwa matumizi ya ndani na mahitaji yetu, wasambazaji wetu RTC waliweza kufikisha katika kila wilaya viatu bora vilivyotokana na ngozi yetu iliyotengenezwa katika kiwanda cha ndani.

Nayakumbuka makaa ya mawe Kiwira na Kiwanda cha Almasi Iringa japokuwa ilikuwa ikichimbwa Mwadui, hii ndiyo Tanzania, nayakumbuka mashamba makubwa ya chakula ambayo yalikuwa yakimilikiwa na majeshi yetu ya JKT kama Dunia, Shamba la Mungu, sitasahau Kiwanda cha Nyumbu kwa kutengeneza magari, lakini pia TAMCO kwa kuunganisha magari hapa nchini.

Zamani kulikuwa na maisha na kwa kweli huwa sielewi yaliishia wapi, tulikuwa tukienda hospitali hatuulizwi kadi na wala chanjo haikuwa jambo la kitaifa, watoto walifuatwa walipo na kupewa chanjo zote muhimu kwa afya zao, tulipata chanjo za kichaa cha mbwa, pepopunda, polio, kifua kikuu, tetekuwanga na vidonge vya minyoo. 

 

Naikumbuka UDA na Ikarusi yetu, yakiuzwa nusu milioni, tunakatiwa tikiti ya Sh. 45 na kupanda miezi mitatu au siku 90 popote uendapo hata ukipanda mara mia kwa siku, kweli maisha yanabadilika, lakini leo ni ‘mwendokasi’ na bado hayakidhi mahaitaji – watu ni wengi kuliko magari.

Nakumbuka benki zetu za nchi hii kwa wingi wake, sitaki kuzitaja napata maradhi ya kipanda uso, nakumbuka maduka ya ushirika, vyama vya ushirika, nawakumbuka Ugawaji na kufikisha bidhaa hadi vijijini,  nakumbuka mashirika makubwa kama ya Ndege, Bima na yale ya manispaa za leo.

Kukumbuka asali na maziwa, na ndiyo maana namuelewa sana mkuu wa kaya anaposema anataka nchi ya viwanda, nahisi anakumbuka Tanzania ya kweli, Tanzania ya kujitegemea kwa bidhaa, Tanzania ya kupigiwa mfano na nchi nyingi za Afrika, Tanzania ya uzalendo wa kweli.

Yapo mengi ya kukumbuka, lakini uwekezaji unafuta historia ya kweli, uwekezaji unaondoa utamaduni wa kujitegemea kwa Mtanzania, ubinafsi na ufisadi unaliangamiza Taifa, umwinyi na uvivu unatufanya tutawaliwe na wachapakazi kutoka nje, Umagharibi unatutoa katika historia ya kweli ya asali na maziwa.

Naona kama ndoto, siamini kama nauli ya sasa ni mara elfu moja kutoka katika nauli ile ya Relwe, siamini kama sasa kila kitu nalipa shuleni na hospitali, siamini kuwa sasa hatuna umeme na kwamba hata vichokonoleo vya meno vinatoka China.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu 

Kipatimo