Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi Mwalimu Julius Nyerere anavyowaondoa wasiwasi watu juu ya jina la Muungano, na kwamba vifungu vya Katiba vinaweza kubadilika ikiwa theluthi mbili ya wajumbe wakiamua kufanya hivyo. Endelea…

Kutokana na hayo maelezo, tunaona wazi kwamba Katiba yetu imechukua kwanza mambo ya lazima, halafu kadiri

tunavyoendelea tutaweza kuongeza au kupunguza baadhi ya yale yaliyomo katika Katiba yenyewe.

Ingefaa tujue kwa kifupi mambo ya Muungano wetu ambayo kwa sasa ndiyo yanayoendesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mambo yenyewe ni:-

1. Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

2. Mambo ya nchi za Nje.

3. Ulinzi.

4. Polisi.

5. Uwezo wa Hali ya Hatari.

6. Biashara ya nchi za nje na ukopaji.

7. Uraia.

8. Kazi za Serikali za Jamhuri ya Muungano.

9. Kodi ya mapato, kodi ya kampuni na ushuru wa bidhaa.

10. Forodha, usafiri wa ndege, posta na simu.

Mambo hayo yote ni baadhi tu ya hatua kubwa sana ya mwanzo iliyochukuliwa na serikali zote hizi mbili katika MUUNGANO. Ni wazi kabisa kuwa mabeberu wanajitahidi kila siku, usiku na mchana ili kuutenganisha

umoja wetu.

Historia hii ambayo tumefaulu kuifanya Unguja na Tanganyika ni hatua kubwa ya kujenga UMOJA WA AFRIKA. Ni wazi kwamba mfano huu ni fundisho kwa wenzetu wa sehemu za bara hili. Tunaomba Muungano uzidi kudumu milele.

TANU kukubali kupitisha Azimio la Arusha

Si siku nyingi tangu Azimio la Arusha kupitishwa na kutangazwa hadharani. Uamuzi wa kulipitisha Azimio hili

ulifanywa baada ya kikao maalumu cha TANU kijulikanacho kama Halmashauri Kuu, kilipoketi huko Arusha tangu 26/1/1967 hadi 29/1/1967 kikifanya mikutano usiku na mchana hadi kufikia uamuzi wa kulikubali Azimio hilo.

Rais wa TANU Mwalimu Julius Nyerere alitangaza hadharani tarehe 5/2/1967 baada ya kukubaliwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa TANU uliofanyika mjini Dar es Salaam.

Haikuwa rahisi kulipitisha Azimio hili, maana viongozi wengi wa TANU na Serikali walikuwa wameanza kuona

uzuri wa kuwanyonya wananchi. Majadiliano makali yaliendeshwa katika mkutano huo. Mwanzoni wengi walikuwa hawaelewi kwanini TANU ilikuwa imependekeza Azimio kama hilo.

Lakini baadaye kama tutakavyoona sababu zilizolifanya Azimio hili lipitishwe, ndipo wajumbe wakaona kwa

uwazi ukweli wa mambo kama yalivyo.

Kwanza ingefaa tuelezee kwa kifupi nini maana ya Azimio la Arusha. Kwa maelezo machache tunaweza kusema kuwa Azimio la Arusha ni tamshi rasmi la Chama cha TANU linaloelezea jinsi nchi yetu itakavyoendelezwa kwa kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Msingi wake mkubwa ni Imani katika haki na Usawa kwa Binadamu wote.

Azimio hili linaitwa la Arusha kwa sababu Arusha ndipo majadiliano yote hadi kufikia uamuzi, yalipofanyika.

Hivyo jina la Arusha linatumika kwa ukumbusho tu wa mahali lilipopitishwa. Azimio hili ni kwa wananchi wote wa Tanzania Bara.

Lakini, ili tuweze kuelewa sababu maalumu zilizofanya chama kitoe uamuzi wa Busara na kulikubali Azimio la Arusha, ingefaa tuone chanzo chake kwanza.

Tukianza na msingi wa chanzo chake, tutaona kuwa: Azimio la Arusha…limepitishwa ili kukazia kwa dhati zaidi yale yaliyomo katika Katiba yetu ambayo kwa sababu mbali mbali ambazo tutazitaja hapo baadaye hayakutiliwa mkazo sana.

Linaeleza kwa uwazi zaidi juu ya usawa wa binadamu kama ulivyoelezwa katika Katiba yetu. Ni kwa nia ya kuleta usawa huo ndiyo maana TANU ilizaliwa. Chini ya serikali ya mkoloni, hapakuwa na usawa barabara kwani palikuwepo na makundi kadhaa ya watu kwa kufuata ubora wa mtu kama walivyoamini wao kwa faida zao.

Mzungu, kwa sababu ya rangi yake, alikuwa bora zaidi kuliko Mhindi au Mwasia yeyote na Mwafrika. Vivyo hivyo, Mwafrika kwa kuwa alikuwa mweusi hakuwa na thamani kama Mwasia au mwingine yeyote.

Mwafrika kila wakati alikuwa mtu wa mwisho. Vita hii ilipiganwa na TANU kwani ndugu zetu hawa walisahau kuwa sote ni binadamu na kwamba sote twahitaji chakula, malazi na mavazi.

Ndugu hao pia walisahau kuwa sote tukiwa ni binadamu tunazaliwa na kulelewa kabla hatujakuwa watu wazima na wenye akili timamu. Vita hii ya TANU tuliishinda mwaka 1961 tarehe 9, Desemba; tukawa huru. Ingawaje Uhuru ulikuwa wa bendera tu.

Katiba hiyo hiyo ya TANU inatueleza kuwa kila binadamu anastahili heshima. TANU ilipingana na mkoloni ili kurudisha heshima yetu. Hakuna heshima ya kweli kwa taifa lolote linalotawaliwa na taifa jingine.

Azimio la Arusha limekuja kuweka heshima ya kweli kwa Mwafrika.

Iwapo kabaila na bepari anamfanya fulani chombo chake cha kutumia ili aishi, je, nani ataheshimiwa? Kwa kuzuia unyonyaji wa aina yoyote, Azimio la Arusha linakuja kuweka sawa heshima ile ambayo chini ya mkoloni na vibaraka wake ilikuwa inapotea.

Azimio la Arusha katika ukurasa wake wa 5 linasema: “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kuupuzwa.”

Ni wazi kwamba Azimio la Arusha halikuja kufanya mageni ila kututoa kutokana na hali ya unyonge; kunyonywa na kupuuzwa. Ndiyo maana Azimio la Arusha linapingana na aina yoyote ya dhuluma na uonevu.

Katika sehemu (i) ya Imani ya TANU, maelezo yake ni wazi kabisa: “Ni wajibu wa serikali ambayo ni watu wenyewe kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi wa taifa ili kuhakikisha ustawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa.”

Azimio la Arusha limetuma serikali kuingilia kati katika shughuli za uchumi wa taifa kwani ilionekana wazi wazi na bado ni wazi kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa nchi yetu umo mikononi mwa watu wachache na hali hii ina kuwa mbaya zaidi wakati watu wachache hao wanawatumia walio wengi ili wawachumie mali.

Huu ni unyonyaji na utaendelea kupingwa kwa kila njia. Siasa yetu ni ya watu wote kuwa sawa. Tutakuwaje sawa

iwapo watu wengi wanataabika na njaa, pia hawana mahali safi pa kulala wala nguo ya kuvaa?

Katiba ya TANU ilisema na iko wazi tangu TANU izaliwe kuwa raia wa taifa hili kwa pamoja tutamiliki 

utajiri wa asili wa nchi yetu. Tutamiliki ili uwe kama ni dhamana kwa vizazi vyetu vijavyo.

158 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!