Utafiti uliofanywa na wataalamu kadhaa umebaini hali ya kushangaza katika Bonde la Mto Nile. 

Wataalamu hao wanasema ubashiri unaonyesha kuwa kiwango cha mvua katika eneo la bonde hilo kitaongezeka lakini kiasi cha maji yanayotiririka katika mto huo mrefu kuliko yote duniani, Afrika kutapungua.

Mto Nile unapita katika nchi 11 barani Afrika, ikiaminika kuwa chanzo chake kipo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi. Mto huo pia hutambaa katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda kabla ya kuingia katika nchi za Ethiopia, Eritrea Sudan Kusini, Sudan na Misri.

Bonde la Mto Nile lina ukubwa wa kilometa za mraba zipatazo milioni tatu, ikiwa ni asilimia 10 ya eneo lote la Afrika. Zaidi ya watu milioni 250 barani Afrika wanautegemea Mto Nile kuendesha shughuli zao za kimaisha. Kwa kiasi kikubwa, wananchi wengi wa Ethiopia, Uganda, Sudan Kusini, Sudan na Misri.

Mvua ambazo zinaingiza maji mengi katika mto huo katika matawi yake yote mawili, Blue Nile na White Nile, zinanyesha katika ukanda wa juu hasa katika nchi za Sudan Kusini, magharibi mwa Ethiopia na Uganda. 

Ukanda wa chini wa Mto Nile, unaojumuisha nchi za Sudan na Misri, zinapata mvua kidogo sana lakini ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea maji ya mto huo kwa ajili ya shughuli zake za kijamii na kiuchumi.

Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa karne hii, kiwango cha mvua katika ukanda wa juu wa Nile kitaongezeka hadi kwa asilimia 20. Hata hivyo, licha ya kuongezeka kwa kiwango cha mvua, pia kutakuwapo hali ya hewa ya joto na ukame katika maeneo mengi ya ukanda wa juu wa Bonde la Mto Nile.

Hali hiyo itatokea kwa wakati mmoja na ongezeko la kasi la idadi ya watu, inayokadiriwa kukua maradufu itakapofika katikati ya karne hii. Hivyo, hali hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya maji na kufanya ongezeko hilo la mvua lisisababishe mto huo kuwa na kiasi kikubwa cha maji.

Kwa wakati huu, asilimia 10 ya watu wote wanaoishi katika bonde hilo wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji kutokana na hali ya ukame ambayo inatokana na ukame katika misimu ya mvua, pia mgawanyo wa maji usio na usawa. 

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2040, kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya watu watakaokabiliwa na upungufu wa maji itafikia asilimia 35 ya wakazi wote wa bonde hilo. Idadi hiyo ni zaidi ya watu milioni 80 ambao hawatakuwa na kiasi cha kutosha cha maji kuendesha maisha na shughuli zao.

Joto kali na ukame vitafanya hali kuwa mbaya sana. Hali hiyo itasababisha mazao kutostawi mashambani, kiasi cha umeme unaozalishwa kutokana na nguvu ya maji kupungua, kiasi cha maji kwa ajili ya shughuli za uchumi na kijamii nacho kitapungua sana na kuathiri mgawanyo wa maji kutoka katika mto huo. 

Hadi kufikia mwaka 2040, joto na ukame vinaweza kusababisha asilimia 45 ya watu katika bonde hilo, sawasawa na watu milioni 110, kukabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Watafiti hao wamebaini pia kuwa licha ya sababu hizo, ongezeko la idadi ya watu kutaongeza upungufu wa maji, hasa katika maeneo ya ukanda wa juu. Lakini kupungua kwa kiwango cha maji yanayoingia katika mto huo kutoka ukanda wa chini nako kutasababisha hali kuwa mbaya zaidi. Hiyo itawafanya watu wengine kati ya asilimia tano na 15 katika ukanda wa juu wa Bonde la Mto Nile kukabiliwa na upungufu mkubwa wa maji.

Hali hiyo ya hewa na ongezeko la watu kutaliingiza eneo hilo katika hali mbaya zaidi kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Tayari hali hiyo imeshaanza kujitokeza kupitia mgogoro wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme kwa njia ya maji nchini Ethiopia, jambo ambalo linapingwa sana na Misri kwa maelezo kuwa mradi huo utatumia maji mengi kutoka Mto Nile na kusababisha athari kwa nchi hiyo.

Hivi sasa kuna migogoro mikubwa miongoni mwa nchi 11 zinazopitiwa na mto huo kuhusiana na matumizi ya maji ya mto huo. 

Nchi zilizo katika ukanda wa juu zinajitahidi kuzidhibiti nchi zilizo katika ukanda wa chini kuhusu kiwango cha maji ambacho wanakitumia katika shughuli zao. 

Hii inalenga kuhakikisha kuwa nchi hizo za ukanda wa juu nazo zinapata kiasi cha kutosha cha maji katika shughuli zao.

Ukichanganya na utegemezi mkubwa wa maji ya mto huo kwa ajili ya kilimo cha kujikimu na hali ya kisiasa, eneo hilo linaingia katika hatari ya kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Takwimu za joto na ukame

Utafiti huo unaonyesha kuwa watafiti walikuwa wanahitaji kujua ni kwa kiasi gani hali ya joto na ukame inajitokeza katika eneo hilo, licha ya ongezeko dogo la kiasi cha mvua. 

Ili kubaini hilo, watafiti hao waliangalia historia ya hali ya hewa katika eneo la ukanda wa juu wa Bonde la Mto Nile wakitumia takwimu kutoka vituo vinane vilivyokusanya takwimu. 

Vituo hivyo vilirekodi takwimu katika ukanda wa juu wa Bonde la Mto Nile kuanzia mwaka 1961 hadi 2005. Pia walitumia modeli za hali ya hewa kukadiria jinsi joto na mvua zitakavyobadilika katika kipindi kilichosalia cha karne hii.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa hali ya joto kali na ukame imekuwa ni ya kawaida katika eneo hilo katika kipindi cha miongo mine, hasa katika ukanda wa juu wa Bonde la Mto Nile na kuwa hali hiyo itaendelea. Hali hiyo ya joto na ukame itakuwa kama ile hali ya hewa ambayo imeshawahi kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula, hivyo kusababisha majanga ya kibinadamu katika eneo hilo katika miongo kadhaa iliyopita.

Hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 21, matukio haya ya joto na ukame yatakuwa yameongezeka, utafiti huo ulibaini. Awali, mzunguko wa miaka ya joto na ukame mkali ulitokea kila baada ya miaka 20, lakini ongezeko la matukio hayo linabainisha kuwa mzunguko huo unaweza kujirudia kila baada ya miaka sita au kumi, na kuyafanya kuwa jambo la kawaida katika eneo hilo.

Pamoja na matukio hayo kujirudiarudia mara kwa mara, pia yatakuwa makali zaidi. Katika kipindi cha joto kali, joto linaweza kuongezeka kwa kati ya nyuzi mbili na sita,  hivyo kuathiri binadamu, wanyama na mimea kuliko ilivyo leo hii. 

Watafiti walikadiria kuwa idadi kubwa ya watu watakakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji kwa kulinganisha na utiririkaji wa maji katika mto na vijito vinavyolisha mto mkubwa, maji ambayo yanaweza kutumika kwa matumizi ya binadamu, kwa kulinganisha na kiasi cha maji ambacho mtu anakihitaji kwa ajili ya matumizi yake muhimu. 

Unapofanya ulinganisho huo, inaonekana kuwa ongezeko la idadi ya watu huku kukiwa na matukio ya mara kwa mara ya joto kali na ukame, ongezeko la mvua halitaweza kusaidia kuuwezesha mto kuhimili mahitaji ya maji kwa ajili ya watu, wanyama na mazao.

Nini kinasababisha?

Kama ilivyo kwa maeneo mengine duniani, joto katika eneo la Bonde la Mto Nile limekuwa likiongezeka kutokana na ongezeko la joto duniani kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa hewa ukaa. 

Kwa kuwa kiwango cha mvua kinatarajiwa kuongezeka katika eneo hilo, mzunguko wa miaka ya ukame hautarajiwi kupungua sana. Hata hivyo, kuongezeka kwa joto kunamaanisha kuwa ukame utakapotokea, utaandamana na hali ya joto kali.

Kwa upande mwingine, ongezeko hilo la joto litasababisha mabadiliko ya mifumo ya mvua, jambo ambalo linaweza kusababishwa pia na matukio ya El Nino na La Nina. Hiyo itaongeza mzunguko wa misimu ya mvua nyingi na ukame kuwa karibu karibu zaidi.

Nini kifanyike?

Jambo moja kubwa na muhimu ni kuhakikisha mgawanyo wa chakula na maji unakuwa na usawa kwa wote. Licha ya kuwepo kwa chakula na maji ya kutosha, watu wengi wanaweza wasiwe na uwezo wa kuvipata vitu hivyo iwapo mgawanyo wake usipokuwa wa haki. Hali hii inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.

Hatua muhimu ya kwanza ni kwa nchi wanakopitiwa na Bonde la Mto Nile kutengeneza mfumo wa matumizi na mgawanyo wa maji ambao si tu kuwa utaondoa mifumo ya “haki za kikoloni” za matumizi ya maji hayo – kama vile ambavyo Misri imekuwa ikidai muda wote kuwa theluthi mbili ya maji yanayotiririka katika mto huo yanapaswa kuwa haki yake – bali pia mfumo utakaozingatia mahitaji ya nchi zilizo katika ukanda wa juu kama vile Sudan Kusini na Ethiopia, ambazo zinahitaji maji kwa ajili ya kuendeleza uchumi wao.

Ushirikiano katika matumizi ya maji katika eneo la Bonde ni jambo muhimu ili kuepuka migongano na misuguano baina ya nchi. Mathalani, Ethiopia hivi sasa inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme ambalo litatumia maji kutoka Mto Nile. 

Kwa kuwa hakuna taasisi zenye nguvu za kikanda zinazotoa miongozo ya kisiasa na kisheria kuhusu matumizi ya maji katika Mto Nile, ujenzi wa bwawa hilo tayari umeshaishtua Misri ambayo imelalamika kuwa kiwango cha maji kitakachotiririka hadi katika nchi hiyo kitapungua sana na kuathiri kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuathiri kilimo nchini humo.

Kila wakati, maji yatatajwa kama chanzo kikubwa cha migogoro, lakini kama ilivyo kwa Israel na Jordan, maji yanaweza kuwa jambo linalowaunganisha watu na nchi. Jinsi dunia inavyokabiliwa na hali ya ongezeko la idadi ya watu na kupungua kwa kiasi cha maji miaka ya usoni, nchi katika Bonde la Mto Nile zitapaswa kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa rasilimali katika eneo hilo zinatumika kwa umakini. Ipo haja ya nchi hizo kufikiria namna ya kuhifadhi rasilimali, hasa maji. 

Mathalani, inabidi kuwe na miradi ya kuhifadhi maji ya mvua, kudhibiti mafuriko yanapotokea na kuwa na mifumo mizuri ya mgawanyo wa rasilimali maji hasa wakati wa ukame.

Vita ya maji

Iwapo nchi zitashindwa kufanya hivi, kuna uwezekano mkubwa wa migogoro ambayo inaonekana kuwa midogo katika kipindi hiki, inaweza kugeuka na kuwa vita kubwa baina ya nchi hizo. 

Ni rahisi kwa nchi hizo kuingia katika mapigano kutokana na rasilimali maji kwa sababu kila mtu anafahamu kuwa maji ni uhai. Hivyo, kubana matumizi ya maji kunaweza kuonekana kama njia ya kuondoa uhai kwa baadhi ya nchi.

Haya si mambo ya kufikirika. Miaka kadhaa iliyopita, tulishuhudia mgogoro (ambao bado haujafa) kati ya Tanzania na Misiri, pale Tanzania ilipoamua kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika mikoa kadhaa. 

Misri ilipinga mradi huo kwa maelezo kuwa utapunguza kiasi cha maji kinachoingia kwenye Mto Nile, hivyo kupunguza kiasi cha maji kinachoifikia nchi hiyo.

Huo unaweza kuwa mgogoro wa zamani kidogo. Mwaka juzi BBC iliripoti uwezekano wa vita kuu ya tatu ya dunia kusababishwa na migogoro inayotokana na matumizi ya maji na kutoa mfano wa migongano inayotokea baina ya nchi zilizo katika Bonde la Mto Nile. 

Mradi wa ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme nchini Ethiopia unatajwa kama moja ya mambo yanayoweza kukuza migogoro na kusababisha mapigano. Wakati Misri na Ethiopia zikibishana kuhusiana na mradi huo, Sudan inajikuta ikiwa katikati yao na italazimika kuhimili mbinyo wa kisiasa na kijiografia.

Mradi huu ulizungumzwa kwa miaka mingi na ukaanza kujengwa katika kipindi ambacho Misri ilikuwa inahangaika kuzima vurugu za kisiasa zilizojulikana kama Arab Spring.

Mafarao wa Misri wanaamini na wamewaaminisha Wamisri wenzao kuwa Mto Nile ulitolewa na Mungu kama zawadi kwa nchi yao. Hivyo, Arab Spring ilipokwisha, Misri ikaigeukia Ethiopia na kuanza kuhoji kuhusu mradi huo.

Kutokana na sababu za kihistoria, Misiri ndiyo ilikuwa na kauli kuhusiana na matumizi ya maji ya Mto Nile, hivyo suala la Ethiopia kujenga mradi mkubwa kama huo bila kuihusisha nchi hiyo likaonekana kuwa jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho na Misri. 

Lakini kwa upande mwingine, Ethiopia haikutaka kabisa kusitisha mradi huo ikiamini kuwa kwanza, bwawa hilo halitapunguza kiasi cha maji yanayotiririka kwenda Misri na pia yenyewe inahitaji sana umeme kwa ajili ya maendeleo yake ya kiuchumi kutokana na kukua na kupanuka kwa shughuli hizo katika miaka ya hivi karibuni.

Ethiopia inaamini kuwa mradi huo ndio suluhisho la muda mrefu kwa mahitaji yake ya nishati ya umeme. Mradi huo ndio unaonekana kuwa roho ya uchumi wa Ethiopia na nchi hiyo haipo tayari kusikiliza jambo lolote linalolenga kusitishwa kwa mradi huo.

Lakini, sababu hizo za Ethiopia hazikuiridhisha Misri ambayo inaendelea kuamini kuwa kwa kuwa asilimia 85 ya maji yanayopaswa kuingia kwenye bwawa hili yanatokea katika miinuko ambayo ndiyo hiyohiyo ambayo inatiririsha maji kwenye Blue Nile ambayo inaungana na White Nile na kufikisha maji nchini humo, bwawa hilo litameza maji hayo yote na kusababisha kupungua kwa maji yanayoingia mtoni na kuifikia Misri. 

Lakini kwa upande mwingine, Ethiopia haiangalii suala hilo, ikiamini kuwa suala hapa si mtiririko wa maji bali ni uchumi wa nchi hiyo.

Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa nchi hiyo, Seleshi Bekele, aliwahi kunukuliwa na BBC akisema: “Huu ni moja ya miradi kielelezo ya Ethiopia. Suala si kudhibiti utiririkaji wa maji katika mto, bali ni kutoa fursa kwetu kujiendeleza kupitia maendeleo ya nishati. Pia mradi huu utakuwa na faida sana kwa nchi nyingine zinazopitiwa na Mto Nile.”

Katika hatua ya kushangaza, Sudan ikakubaliana na Ethiopia. Sudan ilikubaliana na mradi kwa sababu utakapoanza kufanya kazi, maji katika mto huo yataweza kutiririka kwa mwaka mzima bila matatizo. 

Sudan inafurahia hali hiyo kwa sababu itakuwa na uhakika wa maji kwa ajili ya miradi yake ya umwagiliaji mwaka mzima. Hivi sasa kina cha maji katika mto kinapungua hadi kuwa meta nane, lakini inaaminika kuwa mradi huo utakapoanza kufanya kazi, kina kitapungua kwa meta mbili tu na maji hayo yatakuwepo kwa kipindi chote cha mwaka.

Sudan inaamini kuwa kuwepo kwa maji kwa kipindi chote cha mwaka na upatiakanaji wa umeme mwingi wa bei nafuu, ni jambo ambalo linapaswa kumfurahisha kila mmoja katika eneo hilo. 

Kama anavyoeleza Osama Daoud Abdellatif, mmiliki wa Dal Group, inayoendesha kilimo cha umwagiliaji nchini humo: “Kwa Sudan hili ni jambo zuri sana. Ni jambo zuri ambalo halijawahi kutokea katika miaka mingi na ninaamini kuwa kuwepo kwa umeme wa uhakika na wa bei nafuu na maji ya kutosha ni baraka kwetu.”

Hata hivyo, Abdellatif anafahamu kuwa mradi huo ni tishio kwa Misri, hasa ikizingatiwa kuwa Mto Nile ndio maisha kwa nchi hiyo.

Misri inaamini kuwa kuchezea maji ya Mto Nile ni kuchezea uhuru wake. Umoja wa Mataifa tayari umeshatabiri kuwa kuna uwezekano wa kupungua kwa mvua nchini Misri katika miaka ya hivi karibuni. 

Jambo hilo limeitisha Misri ambayo inaamini kuwa sasa ‘uhai’ wake kwa kiasi kikubwa utategemea Mto Nile.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya kimataifa.

207 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!