Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi wananchi wanavyojitetea kwa kupigana lakini wanakwamishwa na ukosefu wa silaha za kisasa na ukosefu wa umoja miongoni mwao wenyewe. Hali hiyo inaelezwa kutokea baada ya mkoloni kuvamia nchi mpya na kujitwalia madaraka ya siasa na kuubadili utaratibu. Leo ni mwendelezo wa pale tulipoishia wiki iliyopita…

Yaani rasilimali inayoajiri vibarua kwa kuzalisha mali. Kwa hiyo, kuwa msingi wa ukabaila ni Ardhi na ule wa ubepari ni Mtaji, kiini cha shughuli za uchumi kilitoka mashambani kwenda mijini, kutoka kwenye ardhi kwenda katika mtaji, fedha, mabenki, biashara, uchukuzi, viwanda nk. vyote vikawa mijini. Mabadiliko haya yaliitwa mapinduzi ya viwanda (Industrial Revolution). 

Ubepari una tabia ya kujipanua. Viwanda viliongezeka, vikakua na kadri viwanda vilivyokua ndivyo kadiri mahitaji ya viwanda pia yalivyopanuka. Na mahitaji ya viwanda ni rasilimali ya asili (raw materials) vibarua wa ujira mdogo (cheap labour) na masoko ya kuuzia bidhaa za viwanda (markets).

Hatimaye mahitaji ya viwanda yaliyotajwa juu yanashindwa kutoshelezwa ndani ya mipaka ya nchi inayohusika. Hayana budi yatafutwe nje ya mipaka ya nchi ile. Ubepari unabadilika kuwa ubeberu. Mabepari huenda katika nchi za kigeni kutafuta uhondo wa watumwa, makoloni, masoko, n.k.

Na katika pilikapilika hizo za kujipatia makoloni kunatokea mashindano ambayo yanasababisha vita baina ya nchi za kibeberu ambazo zinakumba hata wale wasiohusika. 

Katika Ulaya na Amerika uchumi wao ulifika kiwango ambacho kilihitaji mtindo mpya wa utumwa – utumwa wa kikoloni.

Ukoloni ni aina mpya ya utumwa uliolingana na mahitaji ya uchumi wa nchi za kibeberu wakati wake. Na kulikuwa na njia mbili za kuvamia koloni. Kwanza, walitumia mikataba ya udanganyifu, na pili walitumia majeshi. 

Ingawa wananchi hujitetea kwa kupigana, lakini hushindwa kwa sababu ya ukosefu wa silaha za kisasa na ukosefu wa umoja miongoni mwao wenyewe. 

Baada ya mkoloni kuvamia nchi mpya, hujitwalia madaraka ya siasa na kubadili utaratibu. 

1. Utawala kulingana na mahitaji yake. 

2. Uchumi kuwa wa kikoloni. 

3. Anafanyisha wenyeji kazi kwa viboko, kisha kwa kukodi. (silabu) kufungua mashamba ya walowezi na njia za reli, barabara n.k. 

4. Usalama unahakikishwa na majeshi yake, zaidi akitumia wenyeji wenyewe. Kwa maneno mengine anajenga utaratibu unaolingana na mahitaji yake. Mkoloni anahakikisha umilikaji wa vyombo vyote vya kufikia watu. 

1. Kwa kutumia njia mbalimbali za habari na wakati mwingine hata dini. Mkoloni alitumia elimu hasa ya mashuleni kwa kupigia kasumba ya kudumu kwa mpango wa utaratibu maalumu ili kumkatisha tamaa mtawaliwa kwa: Kuua imani, binafsi, kuua utamaduni wake, awe nusu mnyama. 

2. Kujenga utamaduni wa mtawala katika moyo wa unyonge wa mtawaliwa ili kujenga na kudumisha ngome ya ukoloni wa fikra. Hadi ukafikia wakati mtawala anabebwa katika machela kama sisi tumekuwa farasi au punda.

VYAMA VYA SIASA

Kujitawala kwa Tanganyika kusingekamilika iwapo nchi zingine za Afrika zilikuwa bado chini ya watawala wa kigeni. 

Muda uliopita wananchi walitambua kwamba Chama cha TAA kilikwisha kuzeeka kulingana na mazingira ya kilimwengu ya wakati ule na msisimko wa siasa katika Bara la Afrika.

Ndipo Chama cha TAA kikabadili katiba yake na Chama cha TANU kikazaliwa hapa Tanganyika mwaka 1954.

Sasa ndiyo mapambano ya kulilia Uhuru yakadhihirika. 

UHURU 

Hatuna haja ya kurudia historia ya mapambano kwani kila mmoja wetu au alishiriki au aliona mapambano yalivyoendeshwa. Lakini hatimaye uhuru wa kisiasa ukapatikana. 

Kama mkoloni amefaulu kuwagawa wapigania uhuru na kuweza kuficha Chama cha Wananchi halisi, basi Uhuru hutolewa kwa wenye busara, yaani watoto wazuri wa mkoloni.

Uhuru wa siasa kwa waheshimiwa hawa ndio mwisho wa mapambano, kilichobaki sasa ni kula uhondo wa mabaki ya unyonyaji. 

Hao waheshimiwa Wazungu weusi hujiunga na weupe kutetea unyonyaji. Serikali na vyombo vyake hutumika kulinda wanyonyaji na mirija yao.

Wananchi wanapolalamika juu ya maisha yao wanakumbushwa kwamba waheshimiwa walioshika madaraka ndio waliokuwa katika mstari wa mbele wakati wa kupigania uhuru.

Wanapoonekana kuonyesha kichwa ngumu majeshi yanatumika kukomesha jeuri yao. Mambo hubaki vilevile kama zamani. Kilichobadilika ni gavana na bendera. Waheshimiwa mabepari wa ndani ndio wanatumiwa na wale wa nje kuendeleza na kupanua unyonyaji. Hali hii ndiyo huitwa Ukoloni Mamboleo. 

Ikiwa mkoloni hakufaulu katika jitihada zake, kugawa wapigania uhuru kama ilivyokuwa hapa kwetu, na kama madaraka ya kisiasa yatapatikana katika hali ya umoja na kwa wananchi halisi, basi kupata uhuru wa siasa ni hatua ya kwanza tu, ingawa ni muhimu sana.

Kwa wananchi mapambano bado yanaendelea. Kwani uhuru kamili hauna budi ukamilishe hatua nne: 

(i) Uhuru wa Siasa au Uhuru wa Bendera. (ii) Uhuru wa Uchumi, yaani uwe wa kitaifa. (iii) Uhuru wa fikra. 

(iv) Uhuru wa utamaduni. 

Hatua zote nne ni muhimu kwa uhuru kamili, ambao unatupa mtu mpya — Mtanzania huru ambaye ni lazima kwa mapinduzi ya kijamaa. 

Kupata mtu huyu mpya, hatuna budi tutumie njia zote alizotumia mkoloni kupigia kasumba kwa kupigia msasa. 

Kwa kujenga nchi ya kijamaa; na jitihada ya kujenga ujamaa ni kitu kimoja na jitihada ya kujitoa katika hali ya kutoendelea katika nchi zetu za dunia ya tatu, ni budi ikamilishwe,  Hii ndiyo sababu Mwongozo unatuelezea kuwa ni lazima tupigane na unyonyaji wa aina yoyote ile pia kuachilia mbali fikra za kikoloni na kuzipiga vita.

Tukiweza tu kufanya hivyo ndipo tutakapoweza kupiga hatua ya kujikomboa kikweli kweli kutokana na kuonewa, kunyonywa na kupuuzwa. 

Kwa kifupi, ni budi tuelewe kuwa Mwongozo huu ni:

“Tamshi rasmi la chama linalotilia mkazo katika kuimarisha utekelezaji wa Azimio la Arusha kufuatana na mambo yalivyo sasa nchini mwetu na katika Afrika.

Tumefikia tamati ya kitabu hiki cha UAMUZI WA BUSARA, kilichoandikwa na Ofisi Kuu chini ya Katibu Mtendaji wa Chama cha TANU, lengo likiwa ni kuelezea historia ya uongozi wa Mwalimu kabla nchi haijapata uhuru na baada ya kupata uhuru.

Kumalizika kwa maandiko yaliyomo katika kitabu hiki ni mwanzo wa kitabu kingine. Gazeti la JAMHURI linawakaribisha wasomaji wa ukurasa huu wa ‘Maandiko ya Mwalimu’ katika maandiko ya kitabu kingine wiki Ijayo.

By Jamhuri