Ligi kuu ya sokaTanzania Bara inaendelea katika viwanja mbalimbali hapa nchini. Hii ndiyo ligi kubwa hapa nchini ambayo imekuwa ikifuatiliwa na wapenzi pamoja na wadau mbalimbali wa soka nje na ndani ya nchi.

Kuna mengi ya kusema juu ya ligi hii likiwemo lile la ushindani mkubwa uliopo tofauti na miaka iliyopita. Wachambuzi wa masuala mbalimbali ya soka wanasema kuwa hali hii ya ushindani huenda imechangiwa na ongezeko la udhamini kutokana na kuongezeka kwa wadhamini kwa mwaka huu.

 

Kiungo kikubwa katika kufanikisha soka katika nchi yoyote ile ni kuwa na viwanja vizuri vya kuchezea. Kwa hali inavyokwenda hapa Tanzania kuna wakati viwanja vya kuchezea vitakuwa kama viwanja vya ndege au seheme ya bararabani magari yanakopita kila siku.


Kumekuwa na gumzo la ubovu wa viwanja hapa nchini, kitu ambacho inaonekana hakijapatiwa njia mbadaya ya kuweza kutatua tatizo hilo. Kuna baadhi ya wadau ambao wanaonekana kulitupia lawama Shirikisho la soka hapa nchini (TFF) kuwa limeshindwa kutatua tatizo hilo.

 

Wadau hawa wa soka huenda wakawa sahihi au hawako sahihi. Matatizo ya ubovu wa viwanja vya soka hapa nchini yanahangiwa na vitu vingi likiwemo lile la mfumo mbovu wa umiliki wa viwanja.


Kuna wakati TFF walijitetea wakasema kuwa hawahusiki na fujo ambazo zinatokea uwanjani kwasababau wao siyo wamiliki wa viwanja. Hili nalo lina ukweli ndani yake kwasababi viwanja vingi vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi.


Viwanja vingi vya soka hapa nchini viko nchini ya viwango. Lakini pia historia inaonyesha kwamba viwanja hivyo vimekuwa vikitumika katika michezo mbalimbali ya ligi kuu kwa muda mrefu. Si kwamba vinatumika bure bali vimekuwa vikiigiza mapato kila vinapotumika.


Kinachoonekana hapa ni kwamba wamiliki wa viwanja hivi wameshindwa kuvitunza japokuwa vimekuwa vikiingiza mapato kila mara. Ni dhahiri kuwa utunzaji wa viwanja vya soka ni gharama lakini ni muda mrefu sasa ambapo wamiliki waviwanja wameshindwa kuonyesha jitihada zozote za kufanya ukarabati japo kwa mbali. Kila kukicha viwanja vinachakaa, wakati vinaendelea kutumika na kuingiza kipato.


Umefika wakati wa kutatua tatizo kabla viwanja havijafikia hatua ya kukimbiwa na timu kutokana na uchakavu. Kuna umuhimu wa TFF na wadau wengine wanaodhamini ligi za ndani kufahamu kuwa ligi kuu ndiyo ligi pekee ambayo inaushindani hapa nchini. Kutokana na sababu hiyo kuna haja ya ligi hiyo kuchezwa katika viwanja vyenye ubora unaokubalika.


Sasa hivi viwanja vinatumika bila utaratibu, Kwa mfano leo kuna mkesha wa tamasha kubwa la burudani ambalo linakusanya umati mkubwa, kesho mchana inachezwa mechi ya ligi kuu. Je kwa stahili kutakuwa na usalama? Hata kama kutakuwa na utaratibu wa kuwafanyia ukaguzi watazanaji kanbla ya kuingia uwanjani, bila ya kuwa na viwanja bora, bado kuna safari ndefu kufikia mafanikio. Kuimarisha ulinzi katika viwanja vibovu ni sawa na kazi bure.


Hali ilivyo kwa sasa kuna viwanja havina uzio, vingine vina kuta fupi, vingine havina majukwaa. Haya ni baadhi ya matatizo yalitoko katika baadhi ya viwanja vinavyotumika kwa sasa.


Kuna kero nyingi ambazo zimekuwa zikitokana na ubovu wa viwanja hivi, wachezaji kuumia wakiwa uwanjani, timu kucheza chini ya viwango na wakati mwingine kuchangia kukosa ushindi. Halikadhalika kumekuwa na fujo za hapa na pale kwa watazamaji kuwashabulia wachezaji wakiwa uwanjani kutokana na baadhi ya viwanja kutokuwa na miundo mbinu imara.


Ifike wakati TFF ikae na wamiliki wa viwanja ili kuweka mikakati ya pamoja ambayo itahakikisha kuwa viwanja hivi vinafanyiwa marekebisho. Kwa mfano njia mojawapo ambayo inaweza ikasaidia uboreshaji wa viwanja ni pamoja na wamiliki kubinafsha viwanja hivyo kwa TFF.


Hii inaweza kuwa njia mojawapo kutokana na hali inayoonekana kwa sasa kuwa wamiliki wa viwanja wameshindwa kabisa kuboresha viwanja na badala yake ni kukusanya mapato tu, hali ambayo inasababisha soka la bongo kuchezwa katika mazingira magumu.


Katika hili wamiliki wa viwanja hawatakiwi kulaumiwa sana, ila TFF wachukue jukumu la kukaa nao na kuwapa wazo hilo ambalo hatimaye linaweza kufanikiwa na hata kwa nguvu ya wafadhili. Sina uhakika kama wafadhili wa ligi kuu wanajisikia vizuri kuona ligi wanayoidhamini inachezewa katika viwanja vibovu. Hii ni kazi ya TFF kuhakikiska kuwa inabinafsisha viwanja na hatimaye kumshirikisha mfadhili ili kuwa na bajeti ya kukarabati viwanja ili view na viwango vya kisasa.

1708 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!