Uchaguzi Mkuu bado mbichi

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 umekwisha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuibuka kidedea. Hata hivyo, katika hali halisi ngoma inaelekea kuwa bado ni mbichi.

Katika  kuitolea ufafanuzi  hoja hiyo, sina budi nielezee, japo kwa muhtasari, historia ya kibwagizo kilichozoeleka hapa nchini kwetu cha ‘Mapinduzi daima’.

Wakati wa uhai wake, mwasisi wa mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa akielezea mara kwa mara ya kwamba Wazanzibari hawana imani na mfumo wa kupata uongozi wa nchi kupitia uchaguzi kwa sababu wakati Mwingereza anaachia ngazi ya utawala wa visiwa hivyo, aliendesha uchaguzi uliokipora ushindi chama cha ASP na kuweka madarakani vyama ambavyo kwa maoni yake vilikuwa haviwakilishi matakwa ya wananchi.

Kwa maoni yake ni hali hiyo iliyosababisha ASP kuamua  kuchukua madaraka  kwa nguvu katika mapinduzi ya mwaka 1964. Inavyoelekea tangu hapo, waasisi wa mapinduzi hayo walikura na nadhiri ya kwamba madaraka waliyoyapata kwa mtutu wa bunduki kamwe hawatakubali kuyaachia kwa kile walichokiita vipande vya karatasi, wakiwa na maana ya kura.

Katika kuhakikisha nadhiri yao hiyo inaendelea kuheshimiwa vizazi na vizazi, liliundwa Baraza la Mapinduzi chini ya uenyekiti wa Raisi wa Zanzibar na kupewa jukumu hilo la kudumisha dhana ya ‘Mapinduzi Daima’.

Ni katika mazingira hayo, ambayo inaaminika kwamba tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi katika Tanzania, Maalim Seif Shariff Hamad mara zote palipofanyika uchaguzi mkuu amekuwa akiibuka mshindi wa kiti cha rais wa Zanzibar, lakini mara zote amekuwa akiporwa ushindi huo na wana-CCM kwa dhana hiyo ya mapinduzi daima.

Kwa maoni ya wadadisi wa siasa hapa nchini, kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti wa ZEC ni mwendelezo wa kumpora ushindi wake Maalim Seif. Hata hivyo,  safari hii wanasema uporaji huo wa ushindi kwa Maalim Seif utagonga mwamba, wanatoa sababu mbili zitakazosababisha kushindikana kwa jambo hilo.

Sababu ya kwanza ni mabadiliko yaliyofanyika kwenye taratibu za kuhesabu kura za urais. Hapo zamani, kura za urais hazikutangazwa kwenye vituo vya kupigia kura, bali zilikuwa zikipelekwa bila ya kuwekwa bayana kwa ZEC ambayo ndiyo pekee iliyokuwa ikichambua kura hizo na kuzijumlisha, na baadaye kutangaza matokeo.

Utaratibu huo ulitoa mwanya mdogo wa kukosoa ZEC kutokana na takwimu za kura inazotangaza. Safari hii, kura za rais zimebandikwa ubaoni kabla ya kupelekwa kwenye Tume.

Hivyo, yeyote ana fursa ya kunukuu matokeo ya kura za urais kwenye kila kituo cha kupigia kura na kuzijumlisha yeye mwenyewe na kuona nani  ni mshindi.

Hali hiyo inampa nguvu Maalim Seif si tu kudai ushindi wake anapobaini pasipo shaka kwamba umeporwa, bali pia inatoa fursa kwake kuweka uporaji huo bayana kwa kila mtu kuona. Hali hiyo inaiondolea CCM uhalali wa kuendelea kung’ang’ania  madaraka.

Sababu ya pili itayofanya uporaji wa ushindi dhidi ya Maalim Seif kugonga mwamba, ni uungwaji mkono alionao kwa karibu Wazanzibari wote bila kujali itikadi yao ya vyama, juu ya suala la Zanzibar kuwa nchi inayotambulika kimataifa.

Kwa Wazanzibari wengi, mfumo wa sasa wa Muungano wanauona kama ni ukoloni mamboleo, na hivyo wanataka mfumo wa serikali tatu.

Na Maalim Seif amepania kutekeleza jambo hilo akiingia madarakani. Na ndiyo maana uporaji wa ushindi wake ukiendelea huenda kukawapo uasi mkubwa kwa Serikali ya CCM itakayokuwa madarakani.

Baada ya ufafanuzi huo, sasa nizungumzie kidogo ni jinsi gani hali hiyo inaathiri siasa za Tanzania Bara. Kama nilivyoelezea hapo awali ushindi wa Maalim Seif kwenye kiti cha urais wa Zanzibar haukwepeki. Na kama alivyoahidi mara tu baada ya kushika hatamu za uongozi kutaitishwa kura ya maoni ya kuamua iwapo Zanzibar iwe nchi kamili au iendelee kuwa sehemu ya Muungano wa Tanzania.

Kwa maoni ya wengi, Wazanzibari wataamua Zanzibar iwe nchi kamili kura ya maoni hayo ikifanyika. Katika hali hiyo, pande mbili zote za Muungano zitalazimika kuunda Katiba mpya ya serikali tatu.

Jambo litakalosababisha kufanyika kwa uchaguzi mpya kabla ya kumaliza kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kwa jina la Leopold L. Rweyemamu anayepatikana kwa anwani za SLP 1995 au barua pepe: [email protected]