DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Safari itakayowafikisha Watanzania kuanza kupata faida kubwa zitokanazo na uchumi wa gesi bado inazidi kuwa ndefu kutokana na vikwazo kadhaa vinavyoibuka kila wakati.
Wakati wa kilele cha vuguvugu la mgogoro wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, wananchi, hasa kutoka mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara, waliaminishwa kuwa ujenzi wa bomba hilo utaleta manufaa makubwa si tu kwa mikoa hiyo, bali kwa nchi nzima.
Lakini ukiwauliza leo hii, wale waliopewa ahadi wanabaki wakiwalaumu viongozi kwa kuwaongopea kwa sababu manufaa waliyoahidiwa hayajaonekana wazi wazi na kwa kiwango walichoelezwa huku viongozi wakitaja mlolongo wa sababu kwa nini uchumi wa gesi bado haujaanza kuinufaisha nchi na watu wake.
Na katika kile kinachoonyesha kuwa hali haiwezi kutengemaa katika siku za hivi karibuni, JAMHURI lina taarifa za uhakika kuwa shughuli za utafiti wa gesi asilia zimesimama nchini kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo uamuzi wa serikali kupitia Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSA), iliyokuwa imesainiana na kampuni binafsi.
Viongozi wa kampuni mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za gesi nchini wameliambia JAMHURI katika nyakati tofauti kuwa wamelazimika kusitisha uwekezaji kwenye eneo la utafiti mpaka hapo watakapokuwa na uhakika wa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji katika eneo hilo.
Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limekiri kusimama kwa uwekezaji katika eneo la utafiti wa gesi na kubainisha kuwa hilo limetokana na sababu ambazo zipo juu ya mamlaka na uwezo wa shirika hilo.
Wachumi waliozungumza na gazeti hili wameishauri serikali kuhakikisha kuwa inafanya haraka kuandaa mazingira ambayo yatawafanya wawekezaji kuendelea na shughuli za kuiendeleza sekta hiyo.
Shughuli za uzalishaji gesi zinafanyika chini ya mikataba miwili tu kati ya PSA 11 ambazo zimesainiwa. Gesi inayozalishwa ni kama asilimia 13 tu ya kiasi cha gesi iliyogunduliwa na kuipatia nchi mapato ya Sh bilioni 348 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za TPDC za mwaka 2018.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wa gesi wanasema Tanzania ingenufaika zaidi na gesi iwapo mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi ungeanza lakini mazungumzo kuhusiana na mradi huo nayo yamekwama.
Kukwama kwa mazungumzo hayo kumesababisha kusimamishwa kwa shughuli na baadhi ya kampuni zinazojihusisha na masuala ya gesi. Mathalani, Kampuni ya Shell Tanzania, ambayo imegundua kiasi kikubwa cha gesi katika vitalu namba moja na nne, imesema haiwezi kuendelea kutafuta gesi nyingine wakati wameshagundua gesi nyingi ambayo walipanga kuiendeleza kupitia Kiwanda cha LNG.
Kampuni hiyo inaeleza kuwa haiwezi kuendelea kutafuta gesi zaidi wakati tayari wana kiwango kikubwa cha gesi walichokigundua ambacho kinaweza kuendelezwa kwa muda wa zaidi ya miaka 30.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Panafrican Energy Tanzania (PAET), Mwinshehe Said, ameliambia JAMHURI kuwa kampuni nyingi zinazojihusisha na masuala ya gesi hazina taarifa rasmi ya nini kinaendelea katika sekta hiyo baada ya serikali pia kutangaza kuipitia upya mikataba yote ya PSAs kwenye sekta ya mafuta na gesi nchini.
“Serikali haijatuambia nini kinafanyika lakini hiyo si mbaya sana, ni vizuri wakatoa taarifa baada ya kuwa wamekamilisha kila kitu. Hilo litatusaidia sisi kujipanga vizuri kuhusu tufanye nini katika mazingira ambayo serikali itataka tufanye kazi,” anasema.
Hata hivyo, anakiri kuwa sintofahamu katika sekta hiyo hivi sasa imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kampuni nyingi kwa sababu biashara huhitaji kuwa na uhakika wa mazingira ya kufanyia kazi zao.
“Uwekezaji unaofanyika sasa hivi si wa kutosha, kwani hii uncertainty (hali ya kutotabirika) iliyopo inafanya watu wajishauri mara mbili mbili ku-commit resources (kuweka rasilimali) kwa kiasi kikubwa,” anabainisha.
Anasema kampuni yake hivi karibuni imewekeza takriban dola 8.5 milioni za Marekani kununua mtambo wa kusaidia kuzalisha gesi katika visima vilivyopo Kisiwa cha Songo Songo ambako wanaendesha mitambo ya kuchakata gesi.
Mtambo huo ni aina ya kipozeo cha gesi inayochimbwa na ufungaji wa mtambo huo ulikamilika Juni mwaka huu na kuanza kutumika rasmi kwenye robo ya tatu ya mwaka.
“Tulilazimika kuwekeza hivyo ili tuweze kukidhi mahitaji ya wateja ambao tunao hivi sasa,” anafafanua.
Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, mmoja wa viongozi wa juu wa Songas ambaye hakupenda kutajwa gazetini, alisema ukweli ni kuwa gesi nyingi iliyogunduliwa ndani ya bahari itaendelezwa pale tu makubaliano ya ujenzi wa Kiwanda cha LNG yatakapofikiwa.
Anasema si jambo la busara kibiashara kuendelea kutafuta gesi nyingine wakati umeshagundua kiasi kikubwa cha gesi lakini hakuna mpango unaoeleweka wa kuiendeleza.
 
Utabiri

Kusuasua kwa shughuli za gesi nchini kulitabiriwa mwaka 2017 na taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Natural Resource Governance Institute (NRGI) iliyosema kuwa kuanzishwa kwa kiwanda cha kuchakata gesi ndio msingi wa kuendelea kwa uwekezaji katika sekta hiyo.
“Kampuni zimeonyesha kuwa uwekezaji katika gesi waliyoigundua utafanyika na kuendeleza visima hivyo pale tu kiwanda cha kuchakata gesi kitakapoanza kujengwa na kufanya kazi. Hakuna mahitaji makubwa ya gesi nchini hivi sasa ambayo yatafanya uwekezaji katika visima hivyo ulete faida kibiashara,” inasema taasisi hiyo.
Akiandika katika kitabu kuhusu mustakabali wa sekta ya petroli kiitwacho Governing Petroleum Resources; Prospects and Challenges for Tanzania, Mkurugenzi wa Repoa, Prof. Donald Mmari, anasema kuwa kampuni nyingi za kimataifa za mafuta na gesi hufanya uamuzi wa kuwekeza mahali fulani kulingana na mfumo wake wa kisheria katika eneo hilo.
“Ni kweli kuwa tuna rasilimali lakini kwa bahati mbaya sana tunakosa mtaji na teknolojia ya kuendeleza rasilimali hiyo. Hapo ndipo linapokuja suala la kukaa chini na kampuni hizi ambazo zina fedha na teknolojia na kuona ni jinsi gani mtakuwa na makubaliano ambayo yanazinufaisha pande zote,” anasema Prof. Mmari.
Kwa upande mwingine, mtaalamu nguli wa uchumi nchini, Prof. Samwel Wangwe, aliliambia JAMHURI kuwa kuna haja kwa serikali kuharakisha mazungumzo yatakayowezesha kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi.
“Kwa jinsi hali ilivyo, kiwanda hicho ndicho pekee ambacho kitaisaidia Tanzania kupata uwekezaji zaidi na kuhakikisha inanufaika na gesi, la sivyo tutabaki na rasilimali yetu,” anasema.
Hata hivyo ameonyesha kuelewa kuchelewa kwa serikali kufikia makubaliano na kampuni za kigeni ni kwa kuwa bado eneo la gesi ni jipya hapa nchini, hivyo linahitaji uangalifu mkubwa kulitekeleza.
“Katika mazingira kama hayo ni vema serikali ikatumia wataalamu wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa inaingia katika makubaliano ambayo yatainufaisha nchi,” anashauri.
Katika andiko lake la mwaka 2017, NRGI inaonya kuwa kuendelea kuchelewa kwa uamuzi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kunaweza kuiumiza Tanzania, kwani uzalishaji wa gesi unaongezeka duniani, jambo ambalo linashusha bei ya gesi duniani.
NRGI inasema kuwa bei ya gesi ndiyo msingi mkubwa unaotumiwa na kampuni kubwa wanapotaka kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa kiwanda cha kuchakata gesi.

642 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!