Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limesema litajitosa kufanya utafiti wa gesi baharini kuanzia mwakani kama njia ya kuifufua sekta hiyo ambayo shughuli zake zimesimama kwa sasa.





Wataalamu kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakionyesha gari ambalo limefungwa mfumo wa kuliwezesha kutumia gesi asilia kama nishati ya kuendeshea.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake hivi karibuni, Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Kelvin Komba, alithibitisha kuwa shirika hilo litaanza kufanya utafiti huo kwenye eneo la bahari mkoani Mtwara.

Hata hivyo, kutokana na uwezo wa kifedha kuwa mdogo, TPDC haitafanya utafiti kwenye maeneo ya kina kirefu cha bahari.

“Tutakwenda maeneo ya karibu, kama meta 800 hivi kutoka ufukweni, kwani kwenda kwenye kina kirefu kuna ghamara kubwa sana ambazo kwa sasa hivi hatutaweza kuzimudu,” anasema Komba.

TPDC imechukua uamuzi huo baada ya shughuli katika sekta ya gesi kusimama. Kampuni nyingi zinazojihusisha na masuala ya utafutaji na uchimbaji wa gesi nchini zimesimamisha uwekezaji kutokana na sababu kadhaa. 

Sababu kubwa zinazotajwa ni mbili, ikiwemo uamuzi wa serikali kupitia mikataba ya Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSA), pia kusuasua kwa utekeleaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi.

Komba ameliambia JAMHURI kuwa wao kama wasimamizi wa rasilimali hiyo hapa nchini hawana uwezo wa kukabiliana na sababu hizo, kwani zipo nje ya mamlaka yao.

“Serikali yenyewe, kwa maana ya wizara ndiyo imeamua kupitia hii mikataba ambayo sisi haituhusu kwani sisi tupo kwenye eneo la utekelezaji tu. Serikali ikishakubaliana na kampuni kuhusu mambo hayo ndipo sisi huingia kuona utekelezaji wa makubaliano hayo,” anabainisha.

Aidha, Komba anasema kuwa ingawa TPDC pia inahusika kwa kiasi fulani, lakini suala la ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi bado lipo serikalini ambako linajadiliwa kwa umakini mkubwa.

Ingawa wapo baadhi ya watu wanailaumu serikali kwa kuchelewesha kufikia makubaliano, lakini wengine wanaipongeza kwa kuchukua tahadhari.

Wanaoiunga mkono serikali wanabainisha kuwa umakini unahitajika katika mazungumzo hayo ili kuhakikisha kuwa nchi inanufaika ipasavyo na rasilimali gesi.

Wanatoa mifano ya rasilimali madini ilivyotumiwa na kampuni za kimataifa kutajirika wakati Tanzania ikiachiwa mashimo na faida kidogo sana.

Utafiti wa gesi na mafuta

Kuhusu utafiti wa kutafuta gesi ambao utafanyika Mtwara mwakani, Komba anasema TPDC imeamua kufanya hivyo ili kuipa uhai sekta hiyo ambayo kwa sasa ni kama imesimama.

Anasema upo uwezekano mkubwa wa kuvumbua gesi nyingine katika maeneo hayo, kwani si maeneo yote yameshafanyiwa utafiti wa kina.

Anasema utafiti kama huo utafanyika pia kwenye maeneo mpakani na Msumbiji. Eneo hilo limechaguliwa kwa sababu taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Msumbiji imegundua kiasi kikubwa cha gesi katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Tanzania.

“Huo ni ukanda mmoja, hivyo kuna uwezekano kuwa hata huku upande wetu pia kuna rasilimali gesi,” anasema.

Aidha, pamoja na utafiti huo unaopangwa kufanyika Mtwara, TPDC pia imeshaanza kufanya utafiti wa kutafuta mafuta katika Bonde la Wembere, katika mikoa ya katikati ya nchi.

Akifafanua, Komba anasema kuwa walishapiga picha za anga katika eneo husika kwa kutumia ndege.

Anasema hivi sasa wanakusanya data za mitetemo kutoka katika maeneo hayo na mwakani watazifanyia uchambuzi.

“Kutokana na uchambuzi huo ndipo tutajua iwapo eneo hilo lina rasilimali ya mafuta au la. Iwapo tutagundua kuwa kuna rasilimali, baada ya hapo tutakusanya data nyingine ambazo zitatusaidia kujua kiasi cha rasilimali kilichopo kama kinatosha kuchimbwa kwa faida au la, hapo ndipo tutakuwa tumekamilisha utafiti, kwani tutakuwa na majibu yote. Hili litachukua muda,” anafafanua Komba.

Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, utafiti wa gesi na mafuta umefanyika katika maeneo kadhaa ya nchi na kufanikiwa kugundua kiasi kikubwa cha gesi ingawa mafuta bado hayajagunduliwa hadi hivi sasa.

Kiasi kikubwa cha gesi kimegunduliwa katika maeneo ya Songo Songo wilayani Kilwa, mkoani Lindi, pia Mnazi Bay, na ukanda wa Ruvuma katika Mkoa wa Mtwara. Kampuni kadhaa za kimataifa za masuala ya gesi na mafuta zimehusika katika utafutaji wa rasilimali hiyo kwa vipindi tofauti, kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya TPDC.

Zaidi ya visima 50 vya utafiti vimechimbwa katika kipindi hicho katika eneo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 100,000 zikijumuisha kilometa 70,000 baharini na kilometa 30,000 nchi kavu.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi hivi sasa, TPDC ikishirikiana na kampuni nyingine ilifanya utafiti katika kina kirefu cha bahari na kufanikiwa kugundua dalili za uwepo wa kiasi kikubwa cha gesi. 

Maeneo hayo yalitolewa leseni kuanzia mwaka 2002 hadi 2007 kwa kampuni za Petrobras (kitalu namba 5 – 2004), Ophir (kitalu namba 1 – 2005), Ophir (vitalu namba 3 na 4 – 2006), Statoil (kitalu namba 2 – 2007), Dominion (kitalu namba 7) na Petrobras (kitalu namba 8 – 2012).

Kampuni hizo zikachoronga visima vya utafiti zikiwemo BG (vitalu namba 1, 2 na 3), Statoil (kitalu namba 2) na Petrobras (kitalu namba 5), na kufanikisha ugunduzi wa gesi katika vitalu namba 1, 2, 3 na 4.

Kwa mujibu wa TPDC, kipindi kati ya mwaka 1992 na 1999 hakikuwa na harakati nyingi za utafiti wa gesi na mafuta isipokuwa kazi ndogo ndogo na mazungumzo ya mkataba katika eneo la Songo Songo ambako gesi ilishagunduliwa.

Hata hivyo, kuanzia mwaka 2005 kampuni kadhaa za kimataifa zilipewa leseni za utafiti katika maeneo ya pwani. Kampuni ya Tanganyika Oil Company ilichimba visima viwili vya utafiti mwaka 1996/97 katika eneo la bonde la Mandawa.

Kusambaza gesi majumbani

JAMHURI linafahamu pia kuwa pamoja na utafiti wa gesi utakaofanyika Mtwara, TPDC pia itaendelea na zoezi lake la kusambaza gesi asilia majumbani.

Tayari mfumo wa usambazaji wa gesi asilia umefanikiwa kuzifikia nyumba kadhaa jijini Dar es Salaam. Pia kituo cha kujaza gesi kwenye magari kimeshajengwa na baadhi ya magari yameanza kutumia nishati hiyo. Tayari zaidi ya magari 200 yamekwisha kubadilishiwa mfumo na kuanza kutumia gesi asilia kama nishati, kazi inayofanywa na Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Septemba mwaka huu TPDC ilikaribisha kampuni ambazo zina uwezo wa kufanya tathmini ya athari za mazingira kwa mradi wa kujenga bomba la gesi kwenda Bagamoyo kujitokeza.

Hiyo ina maana kuwa TPDC imeamua kupanua mtandao wa gesi asilia hadi mkoani Pwani.

By Jamhuri