Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanataka mabadiliko kwenye kanuni za uchaguzi ndani ya chama hicho ili kuruhusu kiongozi kuwa na kofia ya uongozi zaidi ya moja.

Hata hivyo, wajumbe wameambiwa wanaotaka nafasi nje ya CCM wako huru kufanya hivyo, lakini wawe tayari kupoteza nafasi walizonazo sasa, na endapo huko wanakotaka kugombea watashindwa, hawataruhusiwa kurejea kwenye nafasi walizoshika awali.

Kanuni ya kuzuia kofia zaidi ya moja ilipitishwa na NEC kwenye kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Desemba 13, 2016. Mabadiliko hayo yalitangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa wakati huo, Nape Nnauye.

Nape alisema muundo wa chama umebadilika na mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi wa CCM, Toleo la 2012, Kifungu cha 22 na 23.

Nafasi hizo ni mwenyekiti wa tawi, kijiji au mtaa, kata/wadi, jimbo, wilaya na mkoa. Wengine ni makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zote, mbunge, mwakilishi na diwani.

Kwenye kikao cha NEC kilichoketi jijini Mwanza hivi karibuni, baadhi ya wajumbe walionyesha shauku ya kutenguliwa kwa kanuni hiyo ili kuwapa fursa ya kuwania uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2020. Pamoja na urais, nafasi nyingine zitakazowaniwa ni ubunge, uwakilishi, masheha na udiwani.

Wazo la kuwapo kwa mabadiliko hayo liliibuliwa kwenye kikao cha NEC. Baadhi ya wajumbe wa NEC waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wamelithibitishia JAMHURI kuwa suala hilo liliibua mjadala.

“Kulianza minong’ono ya chini chini, lakini baadaye ikaonekana hili suala si la kuachwa bila kujadiliwa. Baadhi ya wajumbe kama mzee (Sephen) Wassira walijenga hoja kuwa kuwazuia wanachama kuwania nafasi nyingine kwenye serikali ni kuwakosesha haki yao ya msingi.

“Wapo waliotoa hata mfano wa Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wengine kuwa wana nafasi zaidi ya moja na bado wanafanya kazi zao vizuri,” kimesema chanzo chetu.

Baada ya msimamo huo wa wajumbe, JAMHURI limeambiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, alizungumza na akaonekana kuunga mkono, lakini akisimama zaidi kwenye kanuni zilizopo.

Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, ameulizwa na JAMHURI kuhusu kiu hiyo ya mabadiliko iliyoonyeshwa na baadhi ya wajumbe wa NEC, na kusema kanuni ya kuzuia kofia zaidi ya moja haijatenguliwa.

“Kanuni ya kofia moja iko pale pale, haijatenguliwa na sidhani kama itatenguliwa kwa sasa. Msimamo ni mtu mmoja, nafasi moja. Ni marufuku kwa kiongozi wa CCM kushika kofia mbili.

“Lakini tumeweka bayana kabisa kwamba anayetaka kuwania nafasi nyingine nje ya CCM, aache nafasi aliyonayo, aende agombee. Akishinda, anabaki na hiyo aliyoshinda. Akishindwa, anakuwa amepoteza nafasi zote – ile aliyokuwa nayo, na ile aliyoshindwa. Akipoteza anapoteza zote. Hatumzuii mwanachama ambaye ni kiongozi kwenda kugombea, lakini ajue akipata anapoteza ile aliyoacha na akikosa hiyo anayokwenda kuwania, ajue harudi tena kwa ile ya mwanzo – anakuwa amepoteza zote. Hatujamzuia mwanachama, lakini ajue kanuni ndivyo zilivyo,” anasema.

Kuhusu Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Polepole anasema: “Kila kwenye general rule (kanuni kuu) kuna exception (kinga). Hapa kwenye uenyekiti wa chama na urais kuna exception, ndiyo utaratibu wetu,” anasema. 

Oktoba, 2017, Polepole alisema chama hicho kimewataka watumishi wa umma wenye nafasi mbili kutumia hekima na busara kujitathmini kama bado wanaweza kutumikia nafasi zao ndani ya utumishi wa umma, ilhali wana nafasi nyingine za uongozi ndani ya CCM.

Kauli hiyo ilikuwa ni msimamo wa CCM ambao ni sehemu ya mabadiliko ya kimuundo na uongozi, unaolenga kuwafanya watumishi wa umma kuwa karibu zaidi na wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma.

Kwenye kipindi cha TUAMBIE kinachorushwa na Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1), Polepole akasema Katiba ya nchi na ya CCM zimejieleza vizuri kuhusu jambo hilo.

“Katiba na Kanuni za Chama zimejifafanua vizuri, lakini tunaongozwa na hekima, kwa sababu hakuna kanuni zilizotungwa zikaweza kutuongoza moja kwa moja.

“Msingi ulikuwa CCM ni chama kinachoongoza nchi. Kama sisi ndio serikali na serikali inasema utii wa sheria bila shuruti, CCM tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuishi maisha yanayoakisi usemi huo,” alisema.

Alirejea waraka namba moja kwa watumishi wa umma uliotolewa mwaka 2015 unaoeleza utaratibu wa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini.

“Waraka huo umeeleza bayana kwenye kifungu cha 3.1.6, kinachoeleza kuwa endapo mtumishi wa umma kama akiamua kugombea nafasi yoyote ndani ya chama cha siasa, analazimika kuacha kazi au kuomba likizo isiyokuwa na malipo. Likizo hiyo itaanza siku ya kupokea majina ya wagombea wa nafasi za uongozi kwa mujibu wa taratibu za chama husika.

“…Endapo mtumishi atashindwa kwenye uchaguzi na akataka kurejea kwenye utumishi wa umma, hana budi kuomba ajira upya kwa mamlaka husika. Na atakayekwenda kinyume cha waraka huu, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“CCM tunawapenda wanachama wetu ambao wana dhamana mbalimbali kwa mujibu wa sheria ndani ya serikali. Wana-CCM ambao ni watumishi wa umma, milango iko wazi kuendelea kukiunga mkono chama. Wasije wakaingia kwenye uongozi wakapata matatizo ya ajira zao,” alisema Polepole.

Kwa upande wa wakuu wa mikoa na wilaya, Polepole alisema suala lao linapaswa kuongozwa na hekima.

“Wengi wao waligombea nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, ambapo kanuni ya uchaguzi ndani ya CCM imeweka katazo kwa baadhi ya watu wenye nafasi moja kushiriki kugombea nafasi nyingine.

“Kwenye kanuni ya uchaguzi ya CCM, toleo la mwaka huu [2017], inasema nafasi ya uongozi yenye kazi za muda wote, mkutano mkuu wa taifa haujatajwa.

“Lakini mkuu wa wilaya ni kiongozi wa serikali na kiongozi wa chama na kamisaa wa chama kwenye serikali, ambaye pia ni ofisa wa umma anayefanya kazi zote ndani ya CCM. Hekima ituongoze kama mtu una dhamana zote hizo, kwanini mkutano mkuu usimwachie mwanachama mwingine?” alihoji.

Wakurugenzi wa miji, manispaa na majiji wanabanwa na Waraka Na. 1 wa Watumishi wa Umma wa mwaka 2015.

“Wakurugenzi ni watumishi wa umma na viongozi, hivyo kama wameomba nafasi hizo, itakuwa mtihani. Upande mmoja ni Katiba, kanuni na maelekezo ya serikali, ambayo CCM inapaswa kuyaheshimu. Upande wa pili ni hekima ya kuwa na kiasi, kwamba kwa nafasi nyingine, tumwachie mwingine asiyekuwa na nafasi.

“Lingine linakwenda na maelekezo ya CCM, yanayosema mtu mmoja, kofia moja. Ukiwa kiongozi, una dhamana, nafasi nyingine waachie wengine nao waweke mawazo yao,” alisema.

Polepole alisema kwa wakati huo kuwa mabadiliko ya CCM kwenye Awamu ya Tano ya serikali yanayohusu mifumo ya uongozi, muundo na utendaji, yataleta ufanisi mkubwa kwa lengo la kurudi kwenye asili ya CCM, ambayo pamoja na mingine ni haki, watu na uongozi wa kiutumishi.

“Uongozi wa Awamu ya Tano, falsafa yake na mtindo wa kiuongozi – ni uongozi wa kiutumishi. Kwamba, sisi ni viongozi, lakini ni watumishi wa Watanzania, hivyo tueleweke kwamba sisi wanachama tunazungumza lugha moja na mwenyekiti wetu. Mageuzi ndani ya CCM yapo kwenye uongozi, muundo na kiutendaji, ambapo lengo la mageuzi ya kiuongozi ni kutaka kuwapatia wananchi viongozi waaminifu, waadilifu, wanaochukia rushwa na wapole, lakini wakali kwenye mambo ya ovyo,” alisema Polepole.

1942 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!