Wiki iliyopita tulipata kusoma katika maandiko ya mwalimu  “Maendeleo ni Kazi” jinsi chama kilivyotoa maagizo mawili ambayo ni siasa ni kilimo na agizo juu ya viwanda vidogo vidogo kama njia ya kutekeleza masharti ya uongozi. Sehemu inayofuata ni mwendelezo wa tulipoishia wiki iliyopita. Endelea…

 

Udumishaji wa udugu na Nchi za Kirafiki na Misaada kwa Wapigania Uhuru:

Mkutano Mkuu wa 15 ulitutaka tuimarishe uhusiano, ushirikiano na kuunga vyama vya Ukombozi wa Afrika. Ulitutaka tujenge pia uhusiano wa vyama vya ukombozi vya Asia na vya Marekani ya Kusini. Kadhalika ulitutaka tujenge uhusiano wa kindugu na kimapinduzi na raia wa Amerika wanaopigania haki za usawa wa Binadamu.

Uhusiano wetu na vyama vya ukombozi wa Afrika umekuwa mzuri kwa muda mrefu na unaendelea kuwa hivyo. Chama kimeunda Kamati ndogo inayoshughulikia  suala la ukombozi, Makamu wa Rais ni Mwenyekiti wake. Kwa ujumla wananchi wote wako nyuma ya vyama hivyo vya Ukombozi na wameonyesha kwa njia mbali mbali kama vile michango ya kusaidia vyama vya ukombozi wanayotoa mara kwa mara. Kadhalika uamuzi umefanywa na Halmashauri Kuu ya kuufanya mwaka 1974 uwe mwaka wa Ukombozi wa Afrika na michango yote itakayotolewa itapokelewa na Rais wa Chama 7/7/74 kutoka mikoa yote ikiwasilishwa na wenyeviti wa Mikoa.

Katika miaka miwili Chama kimepeleka ujumbe katika nchi zifuatazo:- Rumania, Bulgaria, Urusi, Guyana, Amerika, Ufaransa, Sudani, Yemen, Ujerumani, Somalia, Zaire, India, Algeria, Zambia, Guinea (kuhudhuria mazishi ya Mheshimiwa Amilcar Cabral)

Pia chama kilipita wajumbe kutoka Bulgaria, Ufaransa na ndugu zetu raia wa Amerika wanaopigania haki na usawa wa Binadamu watokao Amerika.

Uchumi:

Mkutano Mkuu wa 15 ulitoa maagizo yafuatayo kuhusu uchumi: kuongeza juhudi ya kuwashirikisha wananchi katika shughuli zote za maendeleo; kufikiria kwanza mahitaji muhimu ya ulinzi na usalama, maji, shule na afya wakati matumizi yanapofikiriwa na kwa vile mpango wa pili wa Maendeleo haukufanya hivyo, basi urekebishwe; kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika utayarishaji wa mipango ya maendeleo, kufanya jitihada ya kukomesha matumizi ya fahari na anasa ili fedha tuliyo nayo iweze kuhudumia watu wengi zaidi; kuchukua hatua za kuipa Mikoa na Wilaya mamlaka na uwezo wa kutekeleza maendeleo ya sehemu zao; kutumia mali zetu za asili kama vile madini, maji, samaki, misitu, n.k. ili kupanua uchumi wa Taifa letu na kuchukua hatua za kustawisha uchumi wa ndani.

Utekelezaji mkubwa wa maagizo hayo uko mikononi mwa vyombo vyetu yaani Serikali na Mashirika. Serikali imechukua hatua kadhaa za kuwashirikisha watu katika shughuli mbali mbali za nchi. Mpango mpya wa madaraka mikoani umewashirikisha wananchi na umeanza kuonyesha matunda. Tume ya mipango imeundwa ambako viongozi wengi na watu wameshirikishwa. Si hivyo tu operesheni nyingi zimewashirikisha wananchi.

Kuhusu matumizi ya ziada, Chama kimetoa maagizo baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati maalum iliyochaguliwa na chama kuhusu utoaji wa Bonasi. Chama kimetamka kwamba wafanyakazi watalipwa bonasi wakati tu watazalisha mazao zaidi kuliko lengo  lao lililokubaliwa. Kwa vyovyote utumizi wa fedha za ziada katika mashirika ya umma umewekwa na chama chini ya usimamizi wa serikali kama ilivyoagizwa.

Utamaduni:

Kuhusu utamaduni Mkutano Mkuu ulitilia mkazo umuhimu wa kuelewa utamaduni kama vile ni kielelezo cha utashi na uhai wa Taifa, katika maisha ya kila siku ya watu wake, na ukaagiza chama kuhusika  na shughuli zote za utamaduni.

Chama kimeshughulika sana kutekeleza agizo hilo. Kwanza kabisa chama kimeshughulika kupanua ufahamu kwa wananchi juu ya utamaduni. Utamaduni kwa wengi wetu ni mila za kienyeji, ngoma na michezo. Ile maana kubwa ya utamaduni, shabaha na manufaa yake, havijaeleweka vema kwa wengi wetu. Utamaduni ni utushi na uhai wa Taifa katika maisha ya kila siku ya watu: yaani ni tabia na jumla ya vitendo vyote vinavyofnywa na mtu  akaonekana na kutambulikana kama ni wa Taifa Fulani – ni Mwafrika, ni Mhindi, ni         Mzungu, ni Mwarabu.

Unaunga mila na desturi kama vile malezi, heshima na adabu, ndoa na harusi, kanuni za kuzikana, vyakula na vinywaji na kanuni zake; imani na dini; elimu, sheria, utawala, ulinzi, silaha, mavazi, mapambo, ngoma na nyimbo, na namna zake;  michezo mbali mbali ya akina mama, wasichana, wavulana, wazee, ya mchanganyiko, kazi mbali mbali na taratibu zake, na inaungana sana yaani ufundi wa namna mbali mbali kama vile ufinyanzi, usukaji, ufumaji, uchoraji, uchongaji, ufuaji na uhunzi, uandishi na kadhalika.

Chama kimeanzisha Kamati ya Utamaduni Mikoani na Wilayani, kadhalika Watumishi wa Chama kutoka Makao Makuu wametembelea sehemu nyingi kueleza na kusaidia kuufufua kwa njia mbali mbali. Ofisi Kuu imetoa maagizo mikoa na wilaya kufanya mambo kadha wa kadha ili kuimarisha utamaduni. Baadhi ya mambo hayo ni kupendekeza mila na desturi nzuri zinazofaa kufanywa za Taifa na zilizo mbaya kuachwa, kuhifadhi magofu ya zamani kama vile Kilwa; kuhifadhi michoro na vitu vyovyote vilivyo mapangoni, kupendekeza nyimbo na ngoma zinazofaa kufanywa za Taifa. Mpaka hivi sasa Bendi ya jeshi la usalama imeweza kutaifisha nyimbo 27 kutoka Mikoa 17 ya Tanzania Bara. Kadhalika kikundi cha ngoma cha Taifa kimetaifisha ngoma 68 kutoka Mikoa kumi na sita (16). Kadhalika maagizo yamepelekwa mikoani na wilayani kuhimiza ufinyanzi wa vyombo vya nyumbani vya kiasili kwa kutumia udongo wetu.

Mambo mengine yaliyoshughulikiwa ni kuhusu Filamu za sinema, sasa bodi mpya imekwisha undwa ili kuhakikisha kuwa filamu zisizofaa hazionyeshwi.

Kwa upande wa lugha ya Taifa; Chuo cha Uchunguzi wa lugha ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Baraza la Kiswahili vinaendelea kuimarisha na kukuza lugha ya Kiswahili. Na kwa mara ya kwanza mwaka jana, 1972 Chuo kilitoa shahada za somo la Kiswahili kwa wanafunzi waliofuzu. Kadhalika shughuli moja kubwa ya hivi sasa ni kutayarisha na kusanifu Kamusi za Kiswahili kwa Kiingereza na Kiingereza kwa Kiswahili.

Kuhusu Ustawi wa Jamii: Chama kinashirikiana na Serikali katika kuwahudumia wasiojiweza. Kamati ndogo ya utamaduni na Ustawi wa Jamii ya Kamati Kuu imetembelea vituo vingi vya wasiojiweza pamoja na kambi za wakoma. Jukumu la Chama hasa kwa upande huu limekuwa ni kuelimisha wananchi umuhimu wa kuwasaidia wasiojiweza huko huko vijijini kwao ili wasikimbilie na kuanza kutanga tanga mijini. Pili kuwaelimisha wasiojiweza wakubali kuishi kwenye Makambi yanayojengwa kwa ajili yao badala ya kutanga tanga mijini.

Mpaka sasa hivi kwa upande wa Tanzania Bara Makambi 47 ya wasiojiweza  yenye wakazi 4,500 yakiendeshwa na Serikali na madhehebu mbali mbali ya dini.

 

By Jamhuri