Sylvester AmbokileIkiwa zimepita wiki mbili tangu Rais Dk. John Magufuli awasimamishe kazi Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile, na Kamishna wa Fedha na Utawala, Piniel Mgonja, mambo mapya yameanza kuibuka.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya idara hiyo vinasema Serikali imefanya ukaguzi maalumu na kugundua ubadhirifu wa fedha, jambo ambalo limeanza kuzua taharuki.

Ukaguzi huo unafanywa huku kukiibuliwa taarifa za makamishna kujikopesha kiasi kikubwa cha fedha kutoka idarani na kuwapo kwa mishahara hewa kutokana na baadhi ya watumishi kufukuzwa kazi bila kuifahamisha Idara ya Utumishi.

Kadhalika, kumekuwa na upotevu wa fedha za madai ya wafanyakazi zilizolimbikizwa kwa muda mrefu ambako wakaguzi wameelezwa zilipitishwa, lakini wahusika (wafanyakazi) hawakulipwa.

“Kuna pesa za malimbikizo ambazo tunaidai idara, lakini jambo la kustaajabisha tumegundua ya kuwa zilishatoka muda mrefu na watu wametumia tu, pia kuna pesa za likizo ambazo nazo pia zilishatoka,” anasema mmoja wa watumishi waandamizi wa idara hiyo.

Makamishna hao wanadaiwa kujikopesha kiasi kikubwa cha fedha za idara ambazo hazijarejeshwa mpaka sasa. Walijikopesha katika vipindi tofauti, na idadi yake haijafungwa na taarifa zinasema si chini ya Sh milioni 500.

Pia kuwapo kwa mtandao mkubwa wa wafanyabiashara ya binadamu ambao uliivuruga idara hiyo na kutengeneza mtandao wake ndani ya idara hiyo.

Hata hivyo, JAMHURI  imedokezwa kuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa barani Afrika alilipa idara kiasi cha dola 900,000 za Marekani kwa makubaliano yenye utata. Jina la mfanyabiashara tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu tulikosa ushirikiano kutoka ofisi yake Dares Salaam.

“Huyu tajiri aliingia makubaliano na wakubwa, akaingiza kiasi hicho cha fedha kwa maelezo kuwa akileta watu wake asipate usumbufu wa malipo, kama kuna malipo yanahitajika basi watakata kwenye kiasi hicho cha fedha ambacho amekiweka kwenye akaunti,” anasema mtoa taarifa.

Anasema kuwa pamoja na kuelezwa kuweka kiasi hicho cha fedha, bado Idara ya Uhamiaji imeshindwa kuelewa sababu za kuwapo kwa makubaliano hayo ambayo ni kinyume cha taratibu za utendaji wa Serikali.

Vyanzo hivyo vya habari vya uhakika vimeidokeza JAMHURI kuwa mtandao huo uliwateka baadhi ya wakubwa katika Idara hiyo ya Uhamiaji na kuweka mizizi yake.

Mtandao huo mkubwa umekuwa ukiongozwa na raia kutoka nchi za Pakistan na Nigeria ambao umekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya makamishna katika idara hiyo nyeti nchini na kuafikiana katika utendaji kazi wa pamoja.

Inaelezwa kuwa baadhi ya makamishna katika idara hiyo wamekuwa wakiwasiliana na kukutana na kuwasiliana na wanamtandao hao jijini Dar es Salaam pamoja na waliopo nje ya nchi.

Mtandao huo hatari uliivuruga idara hiyo mwaka 2014 kwa kuhakikisha unashughulikia watumishi wanaokwenda kinyume cha mipango katika idara hiyo kwa kuwahamisha vituo vya kazi. Mipango ilikamilika mwaka 2015.

Uhamiaji ilifanya uhamisho wa watendaji nchi nzima huku ukiigharimu Serikali kiasi cha bilioni 2.6 ambazo mpaka sasa hazijalipwa kwa maafisa hao.

Tuhuma zote zinamwangukia Ambokile ambaye alipozungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, anasema kuwa hawezi kuzungumzia mambo asiyoyajua hivyo atafutwe mtu aliyetoa taarifa hizo ndiye aweze kuongea.

“Sina ufahamu katika hayo unayoyasema, watafute waliokwambia wakupe data vizuri siyo mimi niliyekwambia. Kama ni masuala ya mikataba siyo mimi ni watu wa Mipango, hivyo siwezi kukwambia lolote,” anasema Ambokile.

Kadhalika, Ambokile alizungumzia utata wa kiwanja cha ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya askari wa idara hiyo kilichonunuliwa mkoani Mbeya, ambacho kinaelezwa kugharimu kiasi cha Sh milioni 400 katika eneo lisilofaa kujengwa taasisi hiyo nyeti.

Inaelezwa kuwa kiwanja hicho chenye ukubwa wa hekari 25 kipo katika mteremko, jambo ambalo limezua maswali mengi.

Hata hivyo, wakati Uhamiaji wakinunua kiwanja hicho kati ya mwaka 2007 na mwaka 2009, Serikali ya Mkoa wa Tanga iliwahi kutoa kiwanja katika Wilaya Mpya ya Mkinga. Kiwanja hicho kinaelezwa kuwa na zaidi ya ekari 300 ambacho kilitolewa kwa lengo la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji nchini.

Kiwanja hicho kilichopo ufukweni mwa bahari katika vijiji vya Manza na Vuo, hapo awali kilikuwa ni shamba la mkonge huku baadhi ya maeneo yakiwa mashamba ya wanakijiji wa vijiji hivyo ambao walilipwa fidia na Serikali ili kupisha ujenzi wa chuo hicho.

Hata hivyo, pamoja na kutengwa kwa shamba hilo kubwa kwa ajili ya ujenzi huo, viongozi wa Uhamiaji Makao Makuu waliamua kununua eneo jingine, jambo ambalo limesababisha mtafaruku ndani ya idara hiyo.

Kumekuwa na madai ya Ambokile kujimilikisha shamba hilo lililostawi mkonge kinyume cha taratibu, lakini hata hivyo, katika mazungumzo na JAMHURI amekanusha akiziita, “Ni uzushi.”

“Hatujaamua kujenga chuo Mbeya, tunatafuta bado eneo, nia yetu ni kuwa na chuo chetu wenyewe, ila Tanga tunalo eneo lakini siyo lazima lijengwe chuo,” anasema Ambokile.

Alipoulizwa kuhusiana na  kuwapo kwa eneo lililotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa chuo mkoani Tanga, anasema kuwa hana kumbukumbu kama lililotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa chuo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuwapo kwa taarifa za yeye binafsi kujimilikisha eneo hilo, anasema kuwa eneo hilo lilitafutwa na watangulizi wake, kwanini alichukue wakati hana mpango wa kuwa mkulima? “Kwanza sina interest ya shamba, kwani sina uwezo wa kutafuta eneo langu binafsi? Kwanini ufuatilie mambo ya kufikirika?” Anahoji Ambokile.

Hata hivyo, alipoulizwa ni kwanini idara hiyo ihangaike kutafuta eneo jingine la kujenga chuo wakati eneo hilo lipo, anasema kuwa siyo lazima chuo kijengwe mkoani Tanga na kuwa idara inatakiwa kuwa na maeneo zaidi ya moja.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, alimuagiza Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani kupeleka wakaguzi katika Idara ya Uhamiaji ili kuweza kuondoa utata na kujua malipo yanayofanyika kwa njia ya benki ikiwa ni pamoja na matumizi ya idara hiyo.

Pamoja na kukanusha taarifa hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu ililazimika kuanza kusaka taarifa za ununuzi wa eneo hilo unaoelezwa kuwa na utata huku ukiomba kupatiwa taarifa za kina.

“Tayari Waziri Mkuu amemtaka (jina linahifadhiwa) kumpatia taarifa zote kuhusiana na kiwanja cha Tanga, ambacho ni kama kimetaifishwa na tayari amekwishapelekewa ripoti nzima ikiwa ni pamoja na ile ya ununuzi wa kiwanja cha mkoani Mbeya” anasema mtoa taarifa.

Kadhalika JAMHURI imezungumza na Kamishina wa Operesheni na Mipaka, Abdullah Abdullah, kuhusiana na shamba hilo na kusema alihusika kutafuta eneo hilo baada ya aliyekuwa Kamishna wakati huo, Kihomano, kutoridhishwa na mafunzo wanayopata mkoani Kilimanjaro.

“Kamishna alitaka tuweze kuwa na chuo chetu wenyewe kitakachokuwa kikitoa mafunzo ya Uhamiaji tu, siyo kama ilivyo sasa. Chuo hiki kitaweza kuwapika ipasavyo maafisa wetu katika utekelezaji wa majukumu yao, akaniagiza kutafuta eneo, nikapata mkoani Tanga. Lakini kwa sasa sijui nini kinaendelea na mimi si msemaji wake,” anasema Abdallah.

Aidha, inaelezwa kuwa chuo hicho kilikuwa mahususi kwa ajili ya mafunzo yote ya kijeshi yanayohusiana na ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya majini kutokana na kuwapo ufukweni, hivyo kuwawezesha askari hao kumudu mafunzo ya aina zote.

1762 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!