ManyerereSauti nyororo ya mwana mama inapokea simu, na kabla sijasema lolote, nakaribishwa kwa maneno: “Precision Air, Can I Help You?” Baada ya kujua nazungumza Kiswahili, ananiuliza: “Nikusaidie…” Namjibu: “Naam, naomba kununua tiketi ya kwenda Musoma Jumanne tarehe 19, 2016…”

Baada ya maswali mafupi na kwa sauti iliyojaa ukarimu, naambiwa naweza kulipa tiketi kwa kutumia njia ya M-Pesa au tIGO Pesa. Sipotezi muda, nafanya hivyo haraka kwa sababu muda niliopewa kabla ya booking yangu kufutwa, si rafiki.

Leo ni Jumanne, Januari 19. Muda ni mchana, nipo katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Ndege inaondoka saa 7, lakini nimewahi saa 5 kama yalivyo maelekezo ya Shirika hili la usafiri.

Hapa uwanjani watu ni wengi. Wapo wanaosafiri, na wengine ni wasindikizaji. Kwa umuhimu wa safari hii, naenda moja kwa moja katika mlango wa kuingia kwenye ukaguzi. Hapo nakumbana na ‘adha’ ile ile ya siku zote-ya kuvua koti, viatu, mkanda, saa na kila kinachodhaniwa kinaweza kutunza vitu vya hatari. Hatimaye nafanikiwa kuvuka kizingiti cha kwanza.

Sasa nakwenda moja kwa moja kwenye meza yenye kibao chenye maandishi: “Precision Air, Musoma”. Hapa natakiwa nitoe kitambulisho. Nakabidhi mizigo miwili, lakini hii mingine miwili-mmoja wenye nguo zisizozidi nne na mwingine wenye laptop, naruhusiwa niingie nao sehemu ya abiria ndani ya ndege. Ni mizigo midogo na inakidhi sheria zote za usalama katika usafiri wa anga.

Muda umewadia wa kuingia katika ndege. Tunaambiwa safari yetu inadumu kwa saa 1 na dakika 50 kutoka hapa Dar es Salaam hadi Musoma. Tofauti na lile shirika jingine la ndege, hawa Precision walau wana uungwana. Tunapewa sandwich, maji, soda na sharbati. Wale waliozoea kupata vinywaji nje ya hivyo, siku hizi hakuna!

Muda wa safari yetu umeshatimia na sasa tunatua katika ‘kiwanja’ kinachoitwa Uwanja wa Ndege wa Musoma! Ni uwanja usio wa lami. Mashimo yamezibwa hapa na pale na ndiyo maana Precision wamerejesha safari zao hapa. Mmoja wa abiria ambaye yaelekea ni mara yake ya kwanza kutua hapa anauliza: “Hapa ndipo Musoma? Huku ndiko kwa Nyerere?”

Nashindwa kumjibu kwa sababu najua maswali yake yanaelekea wapi!

Huu ndiyo uwanja katika mkoa uliotoa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Kambarage Nyerere. Uwanja huu unaweza kuwa kielelezo halisi cha namna mwasisi huyu ambavyo hakuwa mbinafsi.

Haya nayaweka pembeni nikijisemea moyoni kuwa kama Mzee Mwinyi alishindwa, Mzee Mkapa alishindwa, Dk. Profesa Kikwete kashindwa, huyu mtaalamu wa kemia bila shaka katika mengi ya kumuenzi Mwalimu, hili litakuwa miongoni mwayo!

Leo ni Januari 23. Siku nne za kuwapo kwangu mkoani Mara zimeshakwisha. Sasa ni wasaa wa kurejea Dar es Salaam. Wenyeji wangu hawataki nitoke mikono mitupu. Wameniandalia sato, dagaa na vyakula kadha wa kadha.

Nawasili katika Uwanja wa Ndege wa Musoma. Mizigo yangu imefungwa barabara kwa kujua haitafunguliwa hadi nitakapowasili nyumbani kwangu.

Hapa mlangoni kuna foleni ndefu. Nachungulia ndani, naona watu wakivuja jasho kweli kweli. Mizigo ya abiria imetapakaa chini. Nauliza kulikoni hali imekuwa hivi? Jibu nalipata: “Hakuna umeme”. Kwa ukosefu wa umeme, abiria tunakaguliwa kwa ‘kupapaswa’. Tunatakiwa tufungue mizigo yetu yote. Ukaguzi unafanywa kwa mzigo mmoja baada ya mwingine. Makasha na ndoo vilivyojazwa sato na dagaa vinafunguliwa vyote.

Hali hii inatufanya abiria kadhaa hapa tuhoji sababu zinazoufanya uwanja huu ukose japo ki-jenereta cha Sh milioni moja cha kuiendesha mashine hii ya ukaguzi. Inakuwaje jenereta kama hiyo isiwepo ili walau pangaboi lifanye kazi! Haya maswali tunabaki nayo mioyoni.

Zamu ya kupima mizigo yangu imeshawadia. Mzani unaonyesha uzito wa mizigo yangu ni kilo 24. Nimezidisha kilo moja! Natakiwa niilipie Sh 10,000. Naomba niachwe kwa hoja kwamba busara ya kawaida, hainishawishi kuamini kama hiyo kilo moja ni hatari kiasi cha kuhatarisha usalama wa ndege. Kijana anayehusika hapa kwenye tiketi na upimaji mizigo anakomaa. Kisha anauliza wenzake, ana mizingo mingine mingapi? Anajibiwa: “Anayo miwili ya mkononi”.

Kijana yule ananitazama, halafu anasema: “Unaruhusiwa kuwa na mzigo mmoja tu wa mkononi. Kwa maana hiyo huo mwingine uweke hapo upimwe pamoja na hiyo mingine. Baki na mmoja”.

Kauli hii inanifanya nifikiri kuwa kijana huyu na wenzake wanapenda utani! Kumbe mimi ndiye sielewi.

Nawaeleza kuwa hiki ki-mfuko kimoja ni nguo, viatu na vitu vyangu vidogo vidogo ikiwamo kamera ambavyo ni vitendea kazi. Huu mwingine nimetunza laptop.

Hawa wahudumu wanakomaa kweli kweli. Wanasema lazima niwe na mzigo mmoja. Najaribu kuwaeleza kwamba nimeshasafiri sana sehemu mbalimbali, lakini sijawahi kukumbana na sharti hili. Nasema kinachoangaliwa kwa mzigo wa mkononi ni kutokuwa na kemikali au vimiminika hatari, silaha; kuzingatia uzito uzizidi ule uliopangwa kwa mujibu wa taratibu za shirika la ndege, na mwisho lakini ni muhimu zaidi pia, ni ukubwa/upana wa mzigo huo wa mkononi. Upana ni muhimu ili mzigo uenea mahali pa kuwekea mizigo ndani ya ndege upande wa abiria.

Wahudumu hawa vijana wanakataa kata kata. Nawaambia kuwa juzi nilisafiri kwa ndege hii hii nikiwa na mizigo hii hii miwili na sikukumbana na haya wanayonieleza. Iweje leo mambo yawe tofauti?

Wananipuuza. Wanapima mzigo huu mmoja wakiujumuisha na mingine yenye sato na dagaa. Hapa naambiwa uzito ‘uliozidi’ ni kilo 8! Natakiwa Sh 10,000 kwa kila kilo moja ; kwa maana hiyo nilipe Sh 80,000.

Raha yote ya kununua sato imetoweka! Furaha yote ya safari imeyeyuka. Najaribu kuhoji huku nikitokwa jasho. Mmoja anaona kama naleta ‘ujuaji’. Anawaita polisi, na wao wanakaa mkao wa kuanza ‘kazi’. Kwa hoja nawamudu, lakini nakumbuka kuna polisi wetu wengine wanachojua ni maguvu tu. Naona ninyamaze kwa sababu watatumia kigezo hiki cha “abiria mkorofi” kunizuia nisisafiri. Wanalipwa hizo Sh 80,000 na wanatoa stakabadhi. Wananiomba namba yangu ya simu. Kwa hasira nakataa kuwapa. Wananipa stakabadhi iliyoandikwa kiasi hicho cha fedha.

Naingia sehemu ya kusubiria ndege. Namuona Mtangazaji wa ITV, Sam Mahela na abiria wengine. Sam ni mwana taaluma mwenzangu. Ana mizigo ya mkononi miwili. Nachungulia pembeni na kuwaona abiria wengine (samahani, ni wazungu) wakiwa na mizigo ya mkononi miwili, lakini mwingine akiwa nayo mitatu! Wameachwa wapite kwa sababu ni Wazungu? Hapana, mbona Sam, ni ‘mswahili’! Najua hapa kuna tatizo. Nakumbuka mwaka fulani nilivyokataa (japo ni kosa) kukaguliwa Uwanja wa Ndege Arusha baada ya kuona wakaguzi wakitukagua sisi wenye ngozi hizi na kuwaacha wazungu! Waliofanya hivyo baadaye wajiwajibishwa!

Kwa ushuhuda huu kwa abiria wenzangu, akili yangu inazidi kuchafuka. Naona nimeonewa. Narejea kwa wale wahudumu na kuwambia: “Njooni muone, mbona hawa wazungu wana mizigo ya mkononi miwili hadi mitatu? Wahudumu hawa wamejawa kiburi. Wananitazama bila kunijibu. Nami naapa kwa kuwambia: “Nawahakikishia hizi fedha zitarudi, na mtaniomba radhi.”

Kwa shingo upande naingia ndani ya ndege. Safari yetu tunapita Mwanza. Muda wa safari kutoka Musoma hadi Mwanza ni dakika 30. Muda huu nautumia kusoma jarida la Paa Tanzania linalochapishwa na Shirika la Ndege la Precision. Hili ni toleo la Novemba 2015-Januari 2016. Nafungua ukurasa wa 54. Hapa kuna maelezo mbalimbali kwa abiria. Miongoni mwayo, ni hili la Hand Luggage. Nasoma aya hii na kujiridhisha (kumbuka nilishajua) kuwa nimeonewa.

Tunatua Mwanza. Tunatakiwa abiria tushuke ili ndege ijazwe mafuta. Natumia fursa hii kumwomba mhudumu wa ndege anipe tafsiri ya aya hiyo. Naye ananiambia wana kiongozi wao anayeweza kufanya hivyo. Anaitwa Vanance. Namweleza, anapigwa butwaa! Anamwita Security Officer wao. Ananiomba nimpe habari ya tukio zima.

Venance na ofisa huyu wananihakikishia kuwa jawabu nitalipata nikishafika Dar es Salaam. Wanasema nitapokewa na Security Officer wao ili niweze kuwasilisha malalamiko yangu. Majibu na maelekezo ya Venance na mwenzake wanayatoa kwa staha. Nafarijika. Nawashukuru.

Safari yetu inaendelea. Kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam ni muda wa saa mbili. Hatimaye natua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Napokewa na Security Officer anayejitambulisha kwa jina la Charles Hizza. Ametambulishwa kwangu na Venance. Hizza ananipeleka moja kwa moja ofisini kwake. Nampa maelezo. Tunasubiri mzigo wangu uliosababisha nilipe Sh 80,000. Anauona na kujiridhisha kuwa ni kweli ulipakiwa sehemu ya mizigo mizito! Anaupima na kubaini una kilo 8. Anatazama vilivyomo, anakuta nguo, jozi moja ya viatu, kamera na vitendea kazi vingine.

Kabla hajasema mengi, anaanza kuniomba radhi. Anakiri tukio hilo si la kawaida. Ananipa namba ya simu ya Meneja wa Kituo wa Precision Air anayeitwa Michael Montana. Kwa kuwa leo ni Jumamosi, Hizza ananiomba niwasiliane naye kesho Jumapili.

Nami nafanya hivyo Jumapili. Napiga simu, najitambulisha. Kabla sijasema mengi, Montana anasema ana taarifa zote. Ananiomba radhi kwa usumbufu niliopata. Anasema kesho Jumatatu nitapigiwa simu mapema iwezekanavyo ili suala langu lipatiwe jawabu. Namshukuru kwa kupokea simu yangu na kuwa mnyenyekevu.

Leo ni Jumatatu. Ni mapema asubuhi. Najiandaa kwenda ofisini. Nasikia mlio kutoka katika simu yangu. Siifahamu namba hii. Sauti ya mwanamke inasikika. Anajitambulisha kwa jina la Kalunde Kasiga. Ni Meneja Uzoefu wa Wateja Precision Air. Ananieleza taarifa alizonazo ambazo zinanihusu. Nakubali kuwa yote aliyosema ni kweli, tena kweli tupu.

Ananiomba tuonane ili anieleze hatua zilizofikiwa. Namwambia kuwa kesho Jumanne narejea Musoma kwa dharura nyingine, kwa usafiri wa shirika lake hilo hilo. Anasema kama hivyo ndivyo, basi kabla ya kuondoka tuonane.

Nawasili Uwanja wa Julius Nyerere kwa ajili ya kuthibitisha kama nipo kwenye orodha ya wasafiri. Muda huo Kalunde ananipigia simu. Namweleza mahali nilipo. Ananifuata na kwa mara ya kwanza tunaonana ana kwa ana. Ananipokea kwa bashasha. Ananiomba radhi kwa yote yaliyonifika. Lakini anasema nimsubiri hapo kwa sababu uongozi wa Precision umeagiza niombwe radhi rasmi.

Baada ya dakika 10 hivi, anarejea hapa nilipo. Anakuja akiwa na mfanyakazi mwenzake. Ananikabidhi barua. Naisoma. Ni barua mahsusi kwangu ya kuombwa radhi kutoka uongozi wa Precision Air. Barua hii yenye kurasa mbili imesainiwa na Mtendaji Uhusiano kwa Wateja, Margareth Malifyuma.

Pamoja na barua hii, Kalunde anasema taratibu zinafanywa ili nirejeshewe fedha zangu Sh 80,000. Nami kwa msisitizo namwambia barua hii itakamilika tu endapo fedha hizo zitarejeshwa kwangu, ili nami nizipeleke hata zisaidie asasi inayojihusisha na utetezi wa haki za watu. Naam, tunapeana mikono na tunapiga picha kwa ukumbusho. Tunaagana nami nakwenda kupanda ndege kwenda Musoma nikiwa najiona kuthaminiwa.

Baada ya saa moja na dakika 50 tunatua Musoma. Wanaotupokea hapa ni watumishi vijana wale wale ‘wakorofi’. Lakini safari hii wamekuwa wapole, isipokuwa mmoja- mrefu. Nawaeleza, nao wanasema wamepata taarifa kutoka makao makuu, na kwamba uongozi ulipanga kuzuru Musoma kuona namna wateja wanavyohudumiwa, kichocheo kikiwa tukio lililonifika.

Najiandaa kuondoka hapa uwanjani, lakini ghafla mmoja wa wale wahudumu ananifuata akiwa na mwana mama. Naombwa niende ofisini kwake. Simjui. Anajitambulisha kwangu kuwa ndiye Meneja Uwanja wa Ndege Musoma. Anaitwa Bertha Bankwa. Ananikaribisha kwa unyenyekevu. Anasema amepata taarifa kuhusu tukio lililonifika. Anautumia muda huu kuniomba radhi kwa usumbufu nilioupata; na faraja aliyonayo baada ya uongozi wa Precision kunipa barua rasmi ya kuiomba radhi.

Anaona hiyo pekee haitoshi. Naye anaamua kuniomba radhi na kunishawishi niwasamehe wake wahudumu vijana. Nami namweleza kuwa alimradi nimeshaombwa radhi na kuahidiwa marejesho ya fedha nilizodhulumiwa, sina la ziada isipokuwa mhudumu mmoja jeuri ambaye hakuonekana kujutia kitendo alichoshiriki kunifanyia. Namweleza kuwa Mungu ametutaka tusamehe, lakini naye husamehe wanaotubu makosa yao!

Lakini pia yule asiyetubu, sina mamlaka ya kumhukumu. Kwa mhudumu yule hapa Musoma aitwaye Emmanuel, kitendo chake cha kujutia kosa alilonifanyia, nikaona Precision wanastahili kuwa na watumishi wa aina hiyo.

Nimeyasema haya kwa wasafiri wengine wanaotumia usafiri wa ndege au wa aina nyingine, kutambua kuwa wana haki ya kuushinda uonevu na dhuluma. Haki inapiganiwa! Kama walifanya hivyo kwangu, mambo yatakuwaje kwa vikongwe, ajuza na wengine wasio na ujuzi wa mambo haya? Kwa dhati kabisa nawapongeza Precision Air kwa kitendo cha kiungwana cha kuniomba radhi, na kwa sababu hiyo nawashawishi wananchi wengine wasisite kudai haki zao.

By Jamhuri