Jipu la ujangili

Kazi ya kudhibiti ujangili katika mbuga na hifadhi za Taifa ni ngumu, kwani askari waliokabidhiwa kazi ya kulinda wanyama ndiyo wanaofanya ujangili, uchunguzi umebaini.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimesema ikiwa Rais Magufuli anataka kunusuru wanyama nchini, inamlazimu kusitisha ajira za askari karibu wote wanaolinda mbunga na hifadhi kisha kuajiri upya baada ya kuwachekecha vilivyo. 

Askari wa wanyamapori katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Iddi Mashaka, anayetuhumiwa kutoa amri ya kudunguliwa kwa helikopta ya doria katika Pori la Akiba Maswa wilayani Meatu, amethibitika kuwa sehemu ya mtandao wa askari ndani ya hifadhi unaosaidia majangili kuua wanyama na taarifa zinaonesha kuwa kabla ya kuajiriwa Ngorongoro alishawahi kufukuzwa kazi akiwa askari katika Jeshi la Polisi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Mashaka alifukuzwa mwaka 1997 baada ya kula njama na kufanikisha kutorosha malori mawili yenye shehena ya mahindi katika mpaka wa Tarakea mkoani Kilimanjaro. Mahidi hayo yaliingizwa nchini Kenya.

Baada ya kufukuzwa, aliajiriwa Ngorongoro, lakini baada ya kutokea mvutano mkali uliosababishwa na taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi ikieleza makosa yaliyofanya akafukuzwa kazi.

Mashaka alikamatwa kwenye msako mkali wa kuwakamata majangili waliodungua helikopta na kumuua rubani Roger Gower, raia wa Uingereza.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa jina la Mashaka kwenye duru za ujangili limekuwa likitajwatajwa na wakazi wa Meatu, hadi kufikia hatua ya kupanga mkakati wa kumkamata endapo vyombo vya dola vingeendelea kumfumbia macho.

“Wale watuhumiwa wa mwanzo walipobanwa walimtaja mwenzetu (Mashaka) kuwa ni mhusika mkuu. Ni mwenzetu ofisini. Walikiri mbele yake kwamba yeye ni mhusika mkuu na kwamba alikuwa anawatuma.

“Ni mtu ambaye tulikuwa tunamwamini mno kwa sababu alikuwa anakuja na information (taarifa) nyingi tu,” kilisema chanzo chetu.

 

Mambo yalivyokuwa

“Kuna bwana mmoja anaitwa Shija Mjika ambaye alikamatwa mwanzo kabisa. Huyu Shija ni mfanyakazi wa kempu moja ya Alex Walker inayofanya kazi zake Ngorongoro ndani.

“Mashaka alikwenda kumwomba bosi wake Shija (Walker) kwamba kuna kazi ya kufuatilia faru ambaye aliuawa na mwanae Serengeti. Kwa hiyo, alienda kumwomba Shija washirikiane kwenye hiyo operesheni.

“Alipoenda kumuomba, Walker akamruhusu kwamba mchukue mwende mkafanye hiyo operesheni kwa sababu Alex Walker naye ni mdau wa utalii, na angependa kuona wanyama wapo ili wageni wake wakija waone wanyama.

“Akaondoka huyo kijana kwenda kwenye shughuli za Mashaka (kufanya ujangili) mpaka siku alipokamatwa. Alipokamatwa kijana akasema moja kwa moja ‘hii kazi tumetumwa na Idi Mashaka na hata risasi za kutumia huku yeye ndiye ametupatia’.

“Bosi wake Shija (Walker), alipotafutwa, akiwa hajui kama Shija kakamatwa, akasema wazi Mashaka alikwenda kumuomba kwa maelezo kuwa ametumwa na Mhifadhi wa Ngorongoro amchukue huyu kijana wakafanye hiyo operesheni.

“Shija alipokamatwa alieza Iddi Mashaka ndiye mhusika mkuu. Alex Walker alipoulizwa ndipo akatoa hayo majibu kwamba alikuja kuombwa na huyo Mashaka kwenda kufanya operesheni na bado wako kwenye operesheni kwani alikuwa hajui kama Shija amekamatwa. Mpaka alipoambiwa amekamatwa, akashituka sana,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Bahati nzuri Walker alikuwa ameandika kwa maandishi tarehe ambayo Mashaka alikwenda kumuomba Shija. Kwa hiyo issue inaonekana inamgusa Iddi moja kwa moja.”

Uchunguzi wa JAMHURI  umebaini kuwa Mashaka, kama mlinzi ofisi ilimpa bunduki na risasi 30 kwa ajili ya ulinzi. Mashaka alipopekuliwa alikutwa akiwa na risasi 11 pekee kwenye bunduki yake.

“Anaulizwa risasi nyingine ziko wapi anasema alifukuzia wanyama wakali. Taratibu za risasi, ukitumia risasi unatakiwa ujaze kibali na waliokuwapo wawe mashuhuda, lakini pia unatakiwa ganda la risasi ulichukue ulipeleke kwa sababu ule ndiyo ushahidi zaidi. Hakufanya hivyo,”  kimesema chanzo chetu.

Mashaka ana wanawake wawili mmoja anaishi Makao na mwingine Karatu.

Wakati wa mahojiano, Njile Ngunga, aliyedungua helikopta alikiri kuwa na bunduki aina ya AK 47 na meno ya tembo.

“Meno alikuwa ameyaficha sehemu, akaenda akawaonesha askari na kweli hiyo bunduki ikapatikana.

Akasema alipata maelekezo kutoka kwa Iddi Mashaka kwamba kama hiyo helikopta inaleta shida, waidungue. Aliyasema hayo mbele ya Iddi,”  uchunguzi umebaini.

Mahakama ya Wilaya ya Bariadi iliwahukumu majangili wanne, mmoja kifungo cha miaka 20 jela na watatu miaka 15 kila mmoja kwa kudungua helikopta.

Akisoma hukumu hiyo wiki iliyopita, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Mary Mrio, alisema anawapa adhabu hiyo washitakiwa baada ya kukiri kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

Njile Gunga aliyedungua helikopta hiyo Januari 29, mwaka huu atatumikia kifungo cha miaka 20 jela, huku akisubiri kesi nyingine mbili za mauaji ya rubani na uhujumu uchumi ambazo zitatajwa katika Mahakama ya Mkoa wa Simiyu.

Shija Mjika, Dotto Pangani, Njile Ngunga na Moses Mandagu walikiri kukutwa na silaha.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi waliopo Ngorongoro wanasema kuna baadhi ya askari wenye rekodi za uhalifu wasiopungua watano waliokabidhiwa kazi ya kulinda wanyama.

Wanaomba ufanyike uchunguzi wa haraka juu ya historia za walinzi wote kwani wana uhakika miongoni mwao wapo waliokuwa wakishirikiana na Mashaka kufanya ujangili, hivyo bado wataendelea kufanya ujangili.

Katika hatua nyingine, mambo mapya yameibuka kuhusu kampuni ya Kimarekani ya Friedkin Conservation Fund (FCF) ambayo majangili walidungua helikopta yake mwezi uliopita na kusababisha kifo cha rubani raia wa Uingereza, Roger Gower.

FCF inamiliki kampuni tanzu za uwindaji wa kitalii za Mwiba Holdings Ltd, Tanzania Game Trackers Safaris (TGTS) Ltd na Wengert Windrose Safaris.

Wakati helikopta hiyo ikidunguliwa kwa kile kinachoelezwa kwamba ilikuwa kwenye doria dhidi ya majangili, kumbukumbu zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ni miongoni mwa watuhumiwa wa ujangili.

Kampuni hiyo ilikuwa mstari wa mbele, na hatimaye kufanikiwa kumshawishi Waziri wa Maliasili na Utalii aliyepita, Lazaro Nyalandu, kuongeza muda wa uwindaji kutoka miezi sita hadi tisa; kabla ya mpango huo kukwama katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hatua ya kuongeza muda wa uwindaji inatajwa kama mbinu ya kutoa mwanya zaidi kwa baadhi ya kampuni za uwindaji wa kitalii kuendesha vitendo vya ujangili na pia kuathiri mtiririko wa wanyama kuzaliana.

Uchunguzi unaonesha kumekuwapo matukio kadhaa ya wafanyakazi wa Mwiba kukamatwa wakiwa wameua wanyamapori na kukutwa na nyara za Serikali.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii vimesema mara zote kesi zinazoihusu kampuni hizo zimekwama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni urafiki wao wa karibu na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu.

Urafiki wa Nyalandu na wamiliki wa kampuni hizo ulikuwa mkubwa kiasi cha kumpatia moja ya helikopta zake aitumie kwenye mbio za kuwania urais, kabla ya kushindwa na kujielekeza kwenye ubunge. Helikopta iliyodunguliwa na majangili ndiyo aliyoitumia wakati wote wa kampeni zake za ubunge.

Saa chache baada ya kudunguliwa kwa ndege hiyo, haraka haraka, Nyalandu alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akielezea masikitiko yake juu ya tukio hilo na kifo cha rubani Gower.

Pamoja na ujangili, mwaka jana, gari la kampuni hiyo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba T695ARR lilikamatwa Longido mkoani Arusha, likivusha shehena kubwa ya bangi kwenda Kenya.

Gari hilo la kampuni ya Wengert Safaris lilikuwa likiendeshwa na dereva wa kampuni hiyo, Frank Faustine. Baadaye kampuni hiyo ilitoa taarifa ya kuikana shehena hiyo, ikisema haikuwa yake.

Katika tukio jingine, Nyalandu alimwamuru Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa wakati huo, Paul Sarakikya, kutoa Leseni ya Rais kwa familia ya Tom Friedkin (mmiliki wa kampuni hizi) kuwinda wanyamapori 700 katika vitalu vinane na eneo la wazi la Makao. Leseni hizo zilitolewa bure bila kulipiwa hata senti.

Miongoni mwa wanyamapori waliokuwa kwenye orodha ya kuuawa ni tembo walio katika hatari ya kutoweka.

Hata hivyo, masharti ya matumizi ya leseni yanasisitiza kuwa maslahi ya Taifa yazingatiwe na kwamba leseni hizo zisitumiwe kwa malengo binafsi na ya kibiashara.

Pia Nyalandu alikiuka sheria kwa kupuuza ukomo wa idadi ya vitalu vitano kwa kampuni moja. TGTS imemilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi; hali ambayo ni ukiukwaji wa kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori.

Kampuni hiyo pia ilipewa vitalu na Nyalandu kinyemela, ilhali sheria ikiagiza kuwa kitalu kinapobaki wazi sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi [Kanuni ya Uwindaji wa Kitalii 18(1).

Pamoja na kutoa Leseni ya Rais, Wamarekani hao walileta watoto wadogo, chini ya umri wa miaka 18 kuwinda; jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 43(3) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.

FCF na kampuni tanzu imekuwa ikiendesha shughuli za utalii kwenye eneo la Makao WMA tangu 2011 baada ya Mwiba Holdings Ltd kumilikishwa eneo jirani na WMA ya Makao kwa ajili ya shamba la mifugo na wanyama (Makao Ranch).

Jumuiya ya Jamii Iliyoidhinishwa (Authorized Association) (2009) ya Makao ni jumuiya iliyoanzishwa kisheria mwaka 2003 kwa ajili ya kusimamia shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Makao (Makao WMA).

Eneo la Maswa Makao linajumuisha Makao WMA iliyokuwa eneo la wazi la uwindaji (Maswa Makao Open Area).

JAMHURI  imeambiwa kuwa Robin Hurt Safaris Ltd ndiyo kampuni iliyokuwa imegawiwa kitalu kisheria katika eneo hilo.

Baada ya Makao WMA kuanzishwa mwaka 2003 taratibu zingine zilifuata ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji chini ya Jumuiya ya Jamii ya JUHIWAPOMA.

“JUHIWAPOMA iliingia mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya Mwiba Holdings Ltd kabla eneo hilo halijapata mwekezaji. Mkataba huo ulimalizika Machi 31, 2013. Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ya TGTS na chini ya Kampuni tanzu ya Friedkin Conservation, imekuwa ikijishughulisha na utalii wa picha. Utaratibu wa kumpata mwekezaji ulitangazwa tarehe 7 na 9 Mei 2012 na kurudiwa tena 17 Agosti 2012.

“Kampuni ya Fereck Safaris Ltd baada ya tathmini ilipata alama asilimia 94 na kuishinda kampuni ya Mwiba Holdings Ltd iliyopata asilimia 41. Kwa mantiki hiyo, Kamati ya Tathmini ilipendekeza Fereck Safaris Ltd ipewe zabuni ya kuwekeza katika eneo la Makao WMA.

“Kampuni ya Fereck Safaris Ltd na JUHIWAPOMA ziliwekeana saini ya makubaliano ya uwekezaji katika kitalu hicho Mei 8, 2013 baada ya kuridhiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori,” kimesema chanzo chetu.

 

Kiini cha matatizo

Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd chini ya TGTS Ltd ambazo zinamilikiwa na Friedkin Conservation Fund (FCF) imekuwa ikiendesha shughuli za utalii kwenye eneo la Makao WMA tangu 2011 baada ya Mwiba Holdings Ltd kumilikishwa eneo jirani na WMA ya Makoa kwa ajili ya shamba la mifugo na wanyama.

Hata baada ya kumalizika Mkataba wake na JUHIWAPOMA, kampuni ya Mwiba Holdings Ltd iling’ang’ania na kuendelea kukalia eneo la Makao WMA kwa mabavu na kinyume cha sheria.

Uchunguzi unaonesha kuwa Julai 12, 2013 Mkuu wa Wilaya (DC) wa Meatu wa wakati huo, Rosemary Kirigini, aliiandikia barua Fereck Safaris Ltd kusitisha shughuli za uwekezaji kwenye eneo la WMA Makao, baada ya maazimio ya Baraza la Madiwani ya Julai 9, mwaka huo kutaka mwekezaji huyo kusitisha uwekezaji wake. DC huyo alibainisha kwenye barua yake kuwa hatua hiyo inatokana na upungufu wa mchakato wa kumpata mwekezaji.

 

Mchakato ulivyokuwa

Mei 7 na 9, 2012 JUHIWAPOMA ilitangaza utaratibu wa kumpata mwekezaji kwenye kitalu cha Makao na kurudiwa Agosti 17 mwaka huo. Kampuni tatu ziliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwekeza ambazo ni Mwiba Holdings Ltd, Fereck Safaris Ltd na Tanzania Wildlife Corporation.

Wakati wa mchakato huo kampuni ya Fereck Safaris Ltd ilipata asilimia 94 na kuishinda kampuni ya Mwiba Holdings Ltd iliyopata asilimia 41.

Kampuni ya Fereck Safaris Ltd iliahidi kutoa Sh milioni 155 kwa mwaka na Mwiba Holdings Ltd ikiahidi kutoa Sh milioni 150. Kwa mantiki hiyo Kamati ya Tathmini ilipendekeza Fereck Safaris Ltd ipewe zabuni ya kuwekeza katika eneo la Makao WMA.

Chanzo cha habari kinasema wakati Kamati ya Tathmini ikiendelea na maandalizi ya mkataba, mwekezaji (Fereck Safaris Ltd) alifika wilayani Meatu kujadili na kuandaa mkataba na viongozi wa Jumuiya ya Makao. Katika majadiliano hayo walikubaliana ada ya kitalu kwa mwaka iwe Sh milioni 60 badala ya Sh milioni 155 ilizoahidi wakati wa maombi.

“Pamoja na kiasi hicho cha fedha, kampuni hiyo ingetoa mishahara Sh 33,600,000 kwa mwaka, kuchangia maendeleo ya jamii Sh milioni 21, kununua gari ya doria (Sh milioni 118) na kutunisha mfuko wa WMA Sh milioni 100. Jumla ya fedha ambayo JUHIWAPOMA ingelipwa kwa mwaka ni Sh milioni 158.2. Kutokana mabadiliko hayo rasimu ya Mkataba ilirekebishwa,”  kimesema chanzo chetu.  

 

Migogoro mingine inayoihusu FCF

Mgogoro uliopo Makao WMA kwa kampuni ya Mwiba Holdings Ltd/TGTS kukataa kuondoka Makao WMA, unafanana na ule unaofanywa na kampuni dada ya Wengert Windrose Safaris kwenye kitalu cha Lake Natron GCA (East) ambamo imeendelea kung’ang’ania eneo hata baada ya kupewa notisi ya kuondoka kwa kuwa si kitalu chake.

Katika kitalu hicho, WWS iliagiza watumishi wake kuchimba mashimo kwenye kiwanja cha ndege na kufunga barabara ili kampuni ya Green Miles Safaris Ltd iliyomilikishwa kitalu hicho ishindwe kufanya shughuli zake.

“Kimsingi vurugu zinazofanywa na kampuni hizo (Mwiba Holdings, TGTS na WWS) zinalenga kuvuruga tasnia ya uwindaji wa kitalii kwa kuhakikisha kuwa kampuni zinazogawiwa vitalu kihalali zinashindwa kufanya biashara na zinainyima Serikali mapato na kuiharibia sifa kimataifa kutokana na kujenga hisia ya kutokuwapo kwa hali ya usalama nchini,” imesema sehemu ya taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mgogoro huo ulisababisha JUHIWAPOMA na Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa za Maeneo ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (AA Consortium-AAC) kutoa tamko kwenye vyombo vya habari kukemea vitendo vinavyofanywa na Mwiba Holdings Ltd kwa JUHIWAPOMA na hatua ya DC wa Meatu kuhusu hujuma anazozifanya.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Fereck Safaris Ltd iliwasilisha malalamiko yake kuhusu utekelezaji wa mkataba wa uwekezaji wa uwindaji wa kitalii Makao WMA, ikitishia kuishtaki Serikali na Makao WMA kwa kushindwa kutekeleza na kuheshimu makubaliano yao.

 

Ujanjaujanja wa Mwiba Holdings Ltd

Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd inajishughulisha na utalii wa picha.  Hata hivyo, taarifa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa Julai 24, 2013 kampuni hiyo ilimwandikia Waziri wa Maliasili na Utalii barua ikimwomba atoe haki ya matumizi ya eneo la Mwiba Wildlife Ranch na kulazimisha kupewa kibali cha kuwinda kwa familia ya Friedkin.

Kampuni hiyo ilikataliwa maombi hayo ya kuwinda kwa maelezo kuwa ni kinyume cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009 na Kanuni zake  za Mwaka 2010.

 

Migogoro mingine ya Kampuni ya FCF

Wizara ya Maliasili na Utalii inakiri kuwapo vitendo vya ubabe vinavyofanywa na FCF na Mwiba Holdings Ltd/TGTS katika WMA ya Makao.

Vitendo kama hivyo pia vinadaiwa kufanana na mgogoro uliopo kati ya Wengert Windrose Safaris kwenye kitalu cha Lake Natron GCA (East). Kwenye kitalu hicho, WWS ambayo ni kampuni dada na TGTS imeendelea kung’ang’ania eneo hata baada ya kupewa notisi ya kuondoka kwa kuwa si kitalu chake.

Hata hivyo, Nyalandu kwa kuvunja Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, aliipa vitalu hivyo bila kushindanisha kampuni nyingine, lakini pia kwa kufanya hivyo akawa amevunja sheria ya ukomo wa vitalu vitano kwa kampuni.

“Fujo na vurugu zinazofanywa na kampuni hizo (Mwiba Holdings, TGTS na WWS) zina lengo la kuvuruga tasnia ya uwindaji wa kitalii kwa kuhakikisha kuwa kampuni zinazogawiwa vitalu kihalali zinashindwa kufanya biashara,” inakiri Wizara ya Maliasili na Utalii.

Msemaji wa TGTS, aliyetajwa kwa jina la Pratip, alipotafutwa, alikataa kuzungumza kwa maelezo kwamba alikuwa hana muda wa kufanya hivyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Herman Keraryo, alipoulizwa alikiri kuwapo kwa mvutano eneo la Makao, lakini akasema masuala mengine yako chini ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Meatu ambaye kwa sasa ni Erasto Sima.

Kwa upande wake, DC Sima, amesema uhusiano kati ya Mwiba na wananchi ni mzuri.

Kuhusu madai ya watu kuzuiwa kuingia katika eneo la kampuni hiyo, alisema pengine ni woga tu kwa vile mara kadhaa amewahimiza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuingia eneo hilo na kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wa ujangili, amesema uchunguzi unaendelea kufanywa na vyombo vya dola ili kubaini kama miongoni mwa watumishi wa kampuni hiyo wamo wanaowasaidia majangili.

“Uchunguzi unaendelea, tunaamini ukweli utajulikana. Yapo maneno yanasemwa, lakini nikiri kuwa hadi sasa hatujapata ushahidi wa moja kwa moja,” amesema DC Sima.