Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imefanya upekuzi katika Hoteli ya Ramada iliyopo Mbezi Beach jijini na kuwakamata wafanyakazi watatu wa kigeni Julai 5.

Ukamataji huo umetokana na taarifa zilizoandikwa na gazeti hili la JAMHURI toleo lililopita lililoelezea uwepo wa wafanyakazi wa kigeni wasio na sifa za kufanya kazi nchini, huku wengine wakitumia vibali tofauti na kazi wanazozifanya.

Kutokana na taarifa hiyo, Idara ya Uhamiaji Mkoa iliwatuma maafisa wawili kutoka Kitengo cha Upelelezi kwenda kufuatilia wageni hao kisha kuwakamata na kuwafikisha katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, ambapo waliwekwa kizuizini kwa siku tatu na Ijumaa waliondolewa kituoni hapo.

JAMHURI ilifika Oysterbay na kuthibitishiwa kuwa Idara ya Uhamiaji iliwahifadhi raia watatu wa kigeni kituoni hapo, lakini walichukuliwa Ijumaa kupelekwa ofisini kwao.

Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa wafanyakazi hao wa Ramada wakiwa kituoni hapo, kiongozi wao alifanya kila mbinu kuwaondoa polisi kwa ushawishi wa fedha, lakini aligonga mwamba.

Julai 8, raia hao wa kigeni walipelekwa katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam ambako walihojiwa na maafisa wa Kitengo cha Upelelezi kisha kukutana na viongozi wa mkoa, lakini wakaachiwa huru.

Mpaka tunakwenda mitamboni, maafisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam hawakutoa ufafanuzi wowote kuhusiana na raia hao wa kigeni, huku baadhi ya maafisa wa Idara ya Uhamiaji wakibainisha kuwa suala hilo lina utata kutokana na ukaribu wa viongozi wao na mwekezaji huyo.

Hoteli ya kitalii ya Ramada iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam imeajiri wageni wasio na vibali vya kufanya kazi husika nchini.

Abdul Saleem Aboonhi Kollarathikkal, raia wa India mwenye hati ya kusafiria namba Z1873501, ameajiriwa katika Hoteli ya Ramada kama Mkurugenzi wa Fedha (Director of Finance), huku kibali chake kikionesha kitu kingine, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Abdul alipatiwa kibali cha miaka miwili na Wizara ya Kazi Na. WPQ/575/2015 kikibainisha kuwa ni Meneja Mfumo (System Manager) wa M/S. Beach Residence Ltd.

Kibali hicho kilichotolewa Januari 30, 2016 kitafikia ukomo Januari 29, 2018 na kimetiwa saini na Kamishna wa Kazi nchini.

Pamoja na mkurugenzi huyo, hoteli imeajiri raia kutoka nje ya nchi kwa kazi ambazo wazawa wanaweza kuzifanya na hazihitaji wataalamu kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya kazi walizoomba kufanya lakini hawazifanyi na badala yake wanafanya kazi zilizoko kwenye mabano, ambazo zingeweza kufanywa na wazawa, ni kama ifuatavyo:

1.  Executive Housekeeper – Karuna Karan (usafi)

2.  Business Analyst-Front Office – Ramesh Sundar (yupo yupo tu)

3.  IT Support – Information and Telecommunication – Ramakrishnan P.N. (Duty Manager & Night Manager).

4.  System Economic Analyst – Sumed Prasanna (Msaidizi wa Mkurugenzi wa Fedha, kuandaa malipo ya mishahara).

5.  Revenue Analyst – Finance – Dhammika Siriwardana (kazi yake ni kujumlisha mauzo yote ya siku).

6.  Cost Analyst-Finance – Satish Bindu (Mtunza stoo).

7. Chef de Cuisine-Kitchen – Adham Adel (mpishi/mchoma nyama).

8. Wine Tester-F & B – Deeoak N (Muonja mvinyo).

9. African Restaurant Manager – Rajesh Mondar (Meneja Huduma ya vyakula na vinywaji – chakula cha Kiafrika).

JAMHURI haikupata ushirikiano kutoka kwa uongozi wa juu wa Ramada, kutokana na kutoruhusiwa kuonana na wahusika kwa maelezo kuwa wako nje ya ofisi kwa zaidi ya miezi miwili.

1171 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!