Uhuru wa Habari hatarini Kenya

Denis Galava alikuwa mhariri katika gazeti la Nation linalochapishwa kila siku jijini Nairobi. 

Hili ni gazeti linalomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG), pamoja na mengine  yaliyoko Uganda na Tanzania.

Mmiliki wake mkuu ni Aga Khan. Moja ya majukumu ya Galava ilikuwa ni kuandika tahariri. Mwishoni mwa 2015  ikaamuliwa kuwa aandike tahariri maalum kuukaribisha mwaka mpya wa 2016.

 Alitumia muda wa saa sita akifanya utafiti katika maktaba, akisoma habari kuhusu mwaka 2015. Akakuta habari kuhusu skandali, migomo ya wafanyakazi, mashambulizi ya kigaidi, kutetereka kwa uchumi na kadhalika.

 Mwishowe akaamua huo ulikuwa mwaka wa maumivu na mateso kwa wananchi wa Kenya.

Akaandika tahariri ikiwa katika mfumo wa barua kwa Rais Uhuru Kenyatta, ikisema: “Mheshimiwa Rais, jirekebishe katika mwaka huu wa 2016.”

 Akamkumbusha Rais kuwa anasahau ahadi alizotoa kabla ya kushika madaraka mwaka 2013. Akaendelea: “Mheshimiwa Rais, mwaka 2015 ulikuwa ni mbaya kwa Wakenya. Misingi ya taifa letu imetikisika na kuingia nyufa. Familia chache za matajiri zimekuwa zikizoa mabilioni kupitia  zabuni za ajabu kwa ushirikiano wa wanasiasa. Mwananchi anaachwa nyuma, mamilioni  wanakosa ajira na idadi yao inaongezeka.”

Galava akabuni neno la kimombo’ tenderpreneurs’ kwa maana ya ‘wajasiriazabuni’ badala ya ‘wajasiriamali’ kuelezea tabaka la mafisadi wanaochota mabilioni kupitia tenda/zabuni bandia za serikali.

Alimradi Galava hakumung’unya maneno. Alisema yale aliyokusudia Januari 2, 2016. Tahariri hiyo ikachapishwa katika gazeti la ‘Nation.’ Mara moja mitandao  ya jamii ikafurahia na kumpongeza Galava kwa kusema ukweli. Lakini si wote waliofurahi.  

Siku iliyofuata Mhariri Mtendaji wa NMG (wikiendi), Eric Obino alimwita na kumwambia  kuwa tahariri hiyo ilikuwa na maneno makali ingawa ni ya ukweli.

Baadaye Afisa Mwandamizi kutoka Ikulu ya Nairobi alipigia simu ofisi za NMG na kusema  Mheshimiwa Kenyatta alikuwa amekasirishwa na anakusudia kumueleza Aga Khan  ambaye ni mmiliki wa NMG. 

Mhariri Mkuu wa NMG, Tom Mshindi akawa na wakati  mgumu. Bila shaka mengi yalizungumzwa kati yake na Bodi ya Kampuni kwani siku tano baada ya tahariri kuchapishwa Galava akaitwa na bosi wake Tom Mshindi.  Akamtaarifu kuwa anasimamishwa kazi. Januari 20, akaambiwa anafukuzwa kazi.

 Galava aliambiwa kosa lake ni kutofuata utaratibu wa kushauriana na wakuu wake kabla ya  kuchapisha tahariri. Yeye akajibu kuwa amewahi kuandika tahariri zaidi ya 100 na hajawahi  kuelezwa kuhusu huo ‘utaratibu’. 

“Huo utaratibu haukuwepo, ulibuniwa wakati nikisimamishwa  na kufukuzwa,” akaongeza Galava. Anasema ukweli ni kuwa mabosi wake wamekuwa wakimkanya asiendelee kufichua  kashfa za NYS, Eurobond na kahawa.

Walimwambia kashfa hizo zinahusishwa na muungano wa vyama (Jubilee) unaoongozwa na Rais Kenyatta. Hicho ndicho chanzo cha kufukuzwa  kwake na wala si kutofuata taratibu.

Inakisiwa kuwa nchini Kenya asilimia 40 hadi 50 ya mapato ya vyombo vya habari yanatokana  na matangazo ya serikali na mashirika yake.  Hii inatumika kama njia ya kuwadhibiti wahariri.

Hata kampuni kubwa nazo zinatumia mbinu hiyo hiyo. Mwanaharakati wa Chama  cha Wahariri nchini Kenya amesema, kwa mfano, ni vigumu kuandika habari zikizikosoa kampuni za mawasiliano na benki.

Akaongeza kuwa wakati huo huo vyombo vya habari vinazidi kuhodhiwa na matajiri wachache. 

Hivyo, kampuni mbili za habari nchini zinamiliki magazeti 13, vituo vya redio vitatu,  na vituo  vya TV vitatu. Mara nyingi wanasiasa na watawala wanakuwa na hisa katika kampuni hizi.

Kwa maneno mengine, wamiliki wa magazeti na TV wakiwa wafanyabishara na wawekezaji,  basi ni muhali kwa vyombo hivyo vikahatarisha maslahi yao ya kibiashara na kisiasa. Katika hali kama hiyo ni vigumu kuzungumzia uhuru wa habari.

Galava sasa amewasilisha kesi mahakamani, akiishitaki NMG kwa kumfukuza kazi kinyume cha sheria.  Anadai fidia ya Sh milioni 400 za Kenya. Katika mashtaka yake anasema: “Naamini kuwa Mhariri Mkuu amekwepa weledi na wajibu wake kwa kunisimamisha kisha kuniachisha  kazi ili kujikomba kwa vigogo wa kibiashara na kisiasa.”

Hata hivyo, utawala wa NMG umekanusha kwa kusema kuwa Galava alikuwa amekiuka taratibu  na kanuni za kuchapisha tahariri. Galava anasema huo utaratibi haukuwepo na ulibuniwa baada  ya yeye kusimamishwa.

Katika kesi yake anadai kuwa Tom Mshindi aliwahi kumuonya kuwa aache kuandika habari za  skandali, hasa zile zinazohusu chama tawala cha Jubilee na Rais Kenyatta. 

Anasema alikataa  agizo hilo kwani lingewavunja moyo waandishi wanaofanya kazi chini yake. Galava anasema siku chache kabla ya Aga Khan kuwasili Kenya kama mgeni rasmi katika  sherehe ya Jamhuri Disemba, 2015, Tom Mshindi alimuita na kumwambia makala za kashfa zisimamishwe. 

“Akaniambia kuwa serikali inaweza kukasirishwa na hivyo kuikosesha NMG mapato,” akaongeza  Magazeti ya NMG yamekuwa yakisifika nchini kwa msimamo wake wa kutetea haki na  ukweli.

 Msimamo huu ulianza katika awamu ya Rais Daniel arap Moi, ambaye alitawala  kimabavu kwa muda wa miaka 24 chini ya chama chake cha KANU. Nation ilithubutu kusema ukweli na hata kumkosoa Moi.

 Gazeti likajenga umaarufu na likawa linaongoza katika sekta ya  habari. Moi alidai kuwa utawala wake ni “demokrasia ya chama kimoja”.  Wakati huo alikosolewa na  watu wengi, pamoja na viongozi wa dini waliofichua udikteta wake.

 Mwishowe wafadhili  walisimamisha misaada ya dola milioni 350.  Ndipo Moi akatii amri na kuanzisha uchaguzi wa vyama vingi. Hiyo ikawa ni fursa ya kumwondoa madarakani, licha ya jitihada zake za kuwagawa wananchi katika misingi ya kabila na dini. 

Pia, alifanya jitihada za kuchakachua matokeo ya uchaguzi, lakini akashindwa. Baada ya Moi akaja Mwai Kibaki kuanzia 2002 hadi 2013. Inasemekana chini ya utawala wake  vyombo vya habari vilipewa nafasi ya kupumua.

Lakini Kenyatta alipoingia Ikulu mwaka 2013  mambo yakaanza kuharibika na wengi sasa waamini kuwa Kenya inarudia mfumo wa zamani  Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 kwa kuminya uhuru wa habari.

Hata hivyo, tangu muungano wa  vyama vya Jubilee (sawa na Ukawa ya hapa petu) kuchaguliwa mwaka 2013, Rais Kenyatta  amepitisha sheria zinazominya uhuru huo.

Kwa mfano iwapo mwandishi anaandika habari ambayo inakisiwa kuwa inadhoofisha jitihada za kupambana na ugaidi, basi anaweza kuwekwa gerezani miaka mitatu na kutozwa faini ya shilingi za Kenya milioni 5.

Asasi za wanahabari zikapinga sheria hizo mahakamani na kesi inaendelea. Wakati huo huo, wanaharakati wanasema waandishi wanaendelea kudhalilishwa. Asasi ya Freedom House (Kituo cha Uhuru) mwaka 2014 imeripoti kuwa waandishi wasiopungua 19  walishambuliwa.

 Mmoja kati yao ni John Kituyi ambaye alipigwa hadi kufa mjini Eldoret, Aprili mwaka  jana. Wauaji waliondoka na simu yake wakaacha fedha na saa ya mkononi.

Leo Kenya inashika nafasi ya 100 kati ya nchi 180 katika uhuru wa habari. Mwaka 2002 ilikuwa ya 75, yaani kiwango chake kimeporomoka.

 Pia mwaka 2013 wanahabari takriban 300 walihojiwa kote nchini. Zaidi ya asilimia 90 walisema  wamewahi kutishwa kutokana na kazi zao. Wengi wao walisema kutokana na mazingira  hayo waaandishi wameamua kujizuia kuandika habari za kashfa. 

Tukiachia kufukuzwa kwa Galava, mwingine aliyeachishwa kazi hapo Nation ni mchoraji  maarufu wa vibonzo anayejulikana kama Gado. Huyu ni Mtanzania aitwae Godfrey  Mwampembwa ambaye amekuwa na NMG tangu 1992. 

Mwishoni mwa mwaka jana aliitwa na Tom Mshindi na kuambiwa kuwa mkataba wake  umemalizika. Alipouliza sababu aliambiwa “wao wameamua” Alipouliza ni nani hao hakupata  jibu.

Mara kadha Gado amewahi kuchora vibonzo vilivyowakwaza watawala wa nchi za Afrika Mashariki – kuanzia Kenyatta na Museveni hadi Kikwete.  

Kufukuzwa kwa Gado kumelaaniwa na Asasi ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Wanahabari (PEN) na matawi yake nchini Kenya na Afrika Kusini.

 Mchoraji maarufu wa vibonzo nchini, Afrika Kusini aitwae Zapiro naye amelaani kufukuzwa kwa Gado.