Rais wangu pamoja na mimi kutangulia kuliona jua miaka mingi kabla yako, bado wote tumezaliwa Tanganyika na tumeanza kuifahamu dunia tukiwa Tanganyika.

Leo tuko hivi tulivyo, wewe ni Rais wangu na mimi ni mtumishi wako nisiyestahili, lakini tuko katika nchi yetu moja – Tanzania. Elewa, tuko hivi tulivyo kwa sababu wazazi wetu walituzaa vema na wakatulea katika njia ipasayo. Mila za makabila yetu yote zinasisitiza kuwaheshimu na kuwatunza wazazi wetu.

Hata maandiko yanasema waheshimu baba na mama yako upate miaka mingi na heri duniani. Wazazi wetu ni nani? Rais wangu hata Mwenyezi Mungu mwenyewe anajua kuwa Sh 50,000 wanazolipwa wazazi wetu wastaafu kama pensheni ni dhihaka. Muumba anajua ni utajiri kiasi gani aliwawekea waja wake katika nchi hii.

Ni utajiri gani ambao Mungu hakuuweka katika nchi hii? Wana wa shetani wamechukua vyote vilivyotolewa kwa ajili ya wote na kuvifanya kuwa vyao peke yao. Jua la Mwenyezi Mungu na liwahukumu katika siku zao hizi za mwisho ili wayajutie maisha ya anasa na ya kihuni waliyoishi.

Inachoma moyo kusikia wengine wakisema, wana bahati wale waliofiwa na baba zao kwa maana hawayaoni tena mahangaiko ya wazazi wao. Lakini ole wao ambao wazazi wao bado wangali hai na wako katika kundi la wanaoitwa wastaafu. 

Wanayashuhudia maisha ya mateso, dhiki na unyanyasaji mkubwa wanaofanyiwa wazazi wao na Serikali yao. Kosa lao kubwa ni kwamba katika utumishi wao waliitumikia nchi yao kwa uadilifu mkubwa kwa miaka yao yote.

Lakini ni uadilifu wao huo ambao leo umetufanya tuwe na vyeo hivi tulivyo navyo sasa. Manyang’au na walioipora nchi na watu wake bila huruma, wanapostaafu sasa wanachagua mahali pa kuishi. Wana makasri ya kutisha mijini na wana makasri ya kukufuru na ardhi kubwa waliyodhulumu masikini wanyonge vijijini kwao walikozaliwa. Utajiri mkubwa walionao huko duniani anajua Mungu mwenyewe.

Baba jinyenyekeshe mbele ya Muumba wako, ukijifikiria vizuri, utagundua kuwa pamoja na masahibu yote waliyonayo wazazi wetu wastaafu, nyongeza ya pensheni ya elfu hamsini ambayo Serikali pamoja na wewe ukiwamo, ilitangazwa bungeni kuwaongezea miezi tisa iliyopita bila mafanikio, hawakuwaomba.

Pengine ni kisebusebu chenu tu mlipoona mmepaliwa na joto la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mkaamua kuwarubuni kwa kuwaahidi kuwaongezea elfu hamsini juu ya hamsini wanazopata sasa ili wawape kura. Kura waliwapa lakini wao wametumika na kutupwa kama mipira ya kujamiiana inavyotupwa baada ya kutumika.

Leo unapowataka wastaafu hawa hawa wakuombee, watakuombea kwa Mungu yupi? Kwa sababu ni kwa Mungu huyu huyu ndiko walikompelekea maombi yao wakimtaka ailegeze mioyo yenu migumu na kuyang’oa maboriti yaliyomo ndani ya macho yenu  ili mpate kuyaona mateso yao ambayo yamesababishwa na ugumu wa mioyo yenu.

Baba, hebu fikiria; unadhani unahitaji shilingi ngapi kuwalipa hawa wastaafu wachache waliobaki hai, ile nyongeza ya shilingi elfu hamsini mliowaahidi bungeni? Ni matrilioni mangapi umeyakusanya mpaka sasa?

Kama fedha zinazopatikana kutokana na utumbuaji majipu haziwezi kuzuia au hata kupunguza vifo vya waja wa Mwenyezi Mungu, wastaafu wetu, ni Mungu yupi atakayeibariki kazi hiyo yenu mnayoifanya? Kinachokosekana hapa siyo fedha, fedha iko nyingi!

Ni dhamira na moyo wa huruma. Dhamira njema na moyo wa huruma vingekuwapo, ungekwishawalipa hata zaidi ya hapo. Pasopo hawa ni wazazi wetu.

Wanaumia sana moyoni kila mkikusanya matrilioni mnawajali kwanza wenye uwezo ambao hawana hitaji linalotishia uhai wao. Mnawapanulia barabara kama ile ya Bagamoyo ili magari yenu ya kifahari yasigusane mnapopishana. Tazama ughali wa magari yenu katika misafara yenu, maisha mnayoishi na hata bei ya nguo zenu mnazotoka nazo, halafu mnashindwa kuwalipa wazazi wenu elfu hamsini? Hizo baraka mnazoziomba zitatoka kwa Mungu yupi?

Rais wangu, tunatambua kuwa nyongeza ya elfu hamsini haiwezi kuzuia wazazi wetu wastaafu wasife, lakini ingewasaidia angalau kununua dawa ili badala ya kufa leo, wavute wafe kesho au keshokutwa au hata baadaye sana. Si mngewaacha waendelee na dhiki zao za hamsini kuliko kuwadanganya wazazi wenu kama watoto wadogo?

Rais wangu, wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki siku hizi hawasikiki tena. Hata mabarabarani ambako dunia ilizoea kuwaona wazee wale waliodhoofu wakimwagiwa maji ya kuwasha na wajukuu zao waliotumwa na wazazi wao kuwadhalilisha wazazi wa baba na mama zao nako hawaonekani. Koo zao zimekauka kama vigae baada ya sauti zao kuzimika huku machozi yao yakiwa yameenda na maji ya upupu ya polisi yaliyonunuliwa kwa kodi zao wenyewe na kodi za wana wao na wajukuu zao.

Wamezimishwa kama mshumaa. Nao wamemwachia Muumba wao, ili mapenzi yake yatimizwe!

Ni kweli wamechoka na kudhoofu sana. Wengi wametangulia mbele ya haki baada ya kunyimwa stahiki zao na viongozi wa Serikali yao! Siyo kazi yangu kumsemea Mwenyezi Mungu lakini kweli kweli nawaambieni viongozi hawa watakuwa na kitu cha kujibu siku yao ya mwisho!

Mwanzoni dunia ilidhani serikali inavuta muda ili wabaki wachache kwa maana vifo vinawachukua wengi. Lakini ukimya wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu suala hili unaleta ushawishi kama vile inangoja wajiishie wenyewe. Hakuna atakayebaki milele eti kuilinda dunia. Mwisho wetu ni au pepo au jehanam. Duniani ni mapito tu.

Rais wangu, siamini katika upuuzi wa chaguo la Mungu lakini namna ulivyofikia kuwa mgombea wa urais kupitia CCM wakati walikuwa na mteule wao tayari kunaashiria hisia za Kimungu. Lakini Watanzania wanapoambiwa juu ya vijana 46 wa kwenye mtandao ndipo hisia hiyo njema inapojipambanua na kujitofautisha na hila za kishetani. Mafundisho ya Mwenyezi Mungu yanasema, “Kilichoingia kwa hila kitaondoka kwa hila.”

Kwa uteuzi wa watu ambao tayari ni chukizo kwa wananchi wema, kwa ujinga wao wa kupandikiza chuki miongoni mwetu, naweza kuiona kesho yetu. Naiona kesho ambayo Watanzania katika ujumla wao watapata fahamu, nao wataziunganisha nguvu zao pamoja bila kujali tofauti za vyama vyao na kudai mabadiliko ya kweli kutoka kwa watesi wao, chini ya kaulimbiu moja tu,’NCHI YANGU KWANZA’.

 

Paschally Mayega 

078 3727 87

By Jamhuri