Wana-JAMHURI, wiki iliyopita mtakumbuka kwamba nilieleza umuhimu wa vyombo vya habari na haja ya kulinda uhuru wake adimu. Nikagusia kiasi jinsi magazeti yanavyofungiwa, kutishiwa au kupewa adhabu nyingine.

Niliichambua hali hiyo, nikasema kwamba si sawa, si haki kwa maana wananchi wana haki ya kupata habari hizo, na kama kuna wanaoona zinawakwaza, kuna jinsi ya kulalamika. Nikagusia kisanga kilichompata Prince Harry, huyu mjukuu wa malkia wa Uingereza aliyekuwa Las Vegas nchini Marekani. Sasa  amesharejea jijini hapa.

 

Kule alikwenda hata na walinzi, akaishia kujirusha, kunywa pombe na washikaji zake hadi akasaula hadi nguo ya ndani akabaki mtupu. Kasri ya kifalme ya Buckingham ilitoa tamko, likiwa kama ombi kwa vyombo vya habari kutochapisha picha zile za utupu, maana zilikuwa zinadhalilisha si tu kijana huyo, bali ufalme na Uingereza kwa ujumla.

 

Yapo magazeti na mitandao iliyonyamaza kana kwamba hakuna kilichotokea, lakini baadhi, kama The Sun, walichapisha picha zile kitaaluma na kutoa sababu za kuchapisha – wateja wao ambao ni umma wanazihitaji. Basi, kwisha. Imekuja kutokezea kwamba Waingereza wanalalamika sana kwa maoni wakitumia na barua intaneti magazetini, wanasema Prince wao kawaaibisha.

 

Wanalia kuwa anatumia mapesa ya walipa kodi kusafiri, kustarehe na kulindwa huko, halafu anavua nguo zote na kubaki uchi wa mnyama akionesha viungo vyake nyeti. Kwa upande mwingine, serikali au kasri ya kifalme ikikwazwa na gazeti au chombo chochote cha habari, haiwezi hata siku moja kutamka eti inakifungia chombo hicho – hata kwa siku moja, hapana!

 

Inachoweza kufanya ni kutafuta wanasheria, mawakili au itumie wa kwake waliopo ofisi za sheria na kwenda tume iliyopewa kazi hiyo maalumu. Ngoja niitaje kwa ung’eng’e ilivyo. The Press Complaints Commission (PCC). Hii ni tume huru, haiagizwi na serikali wala kuburuzwa na matajiri wa vyombo vya habari au wafanyabiashara wanaotaka habari zao ziandikwe sana lakini vizuri tu au zisiandikwe kabisa.

 

Tume hii imewekwa kwa mujibu wa sheria za nchi na ina wataalamu ambao hupokea na kupitia malalamiko juu ya kilichomo kwenye magazeti, majarida na tovuti za nchini Uingereza. Ningesema hii inaweza kuwa kama Baraza la Habari Tanzania (MCT), lakini tatizo la Tanzania ni kuwa serikali yetu ikipigwa chini ya mkanda haiendi kwa refa, inatoa kadi yenyewe kwapani na kumwonyesha mchezaji mwenzake!

 

Kwa Uingereza, sawa na Marekani na mataifa mengine yanayojali uhuru wa vyombo vya habari si hivyo. Hata vyama vinavyotawala wala marais au mawaziri hawana nguvu ya kugandamiza chombo cha habari. Tume hii ya hapa Uingereza yenye ofisi zake Holborn House, Holborn, hapa hapa London, imeweka wazi namba zake za simu na anwani ya barua pepe au ukipenda unakwenda mwenyewe hadi pale kuwasilisha malalamiko yako dhidi ya chombo cha habari. Kinacholalamikiwa, kuchambuliwa na kuamuliwa ni habari, makala na picha na maudhui yake.

 

Tume pia hupokea na kutathmini malalamiko kuhusu vyombo vya habari kunyanyasa, kubagua au hata jinsi vinavyofanya kazi ya kuripoti masuala yaliyopo mahakamani au kwenye tume za uchunguzi, na huduma hiyo ni ya bure hulipi hata thumni, bali inalipiwa na walipa kodi, nikiwamo mimi.

 

Wahusika pale katika tume ni wahariri waliobobea wanaopokea malalamiko na kuyafanyia kazi na kutoa majibu ndani ya wiki moja, na ikiwa kazi haijakamilika mhusika huarifiwa kinachoendelea. Na walalamikaji wanaweza kuwa mfalme, malkia, mwana wa malkia, mjukuu, mfanyabiashara bilionea, mfagia barabara au mama muuza chakula gengeni, na wote hutendewa sawa bila kuangalia aina ya mlalamikaji.

 

PCC ina haki ya kukagua hadi barua za wasomaji na kuona maudhui yake, lakini pia inashughulikia tabia binafsi za waandishi wa habari. Hizo zinajumuisha kukithiri kwa baadhi yao kufuatilia mtu au watu walewale; kukataa wanapotakiwa kuacha kupiga picha au kufanya mahojiano; kutumia kamera zilizofichwa ili kupata picha.

 

Ni muhimu hapa kuwa makini na uwazi huu wa kamera za waandishi. Ni tabia na utamaduni wa Waingereza kuwa wazi. Hata unapochunguzwa kwa jambo, utaambiwa wazi moja kwa moja au kwa vibao barabarani au majengoni. Ni kawaida kukuta vibao vinavyosema kwamba kamera za CCTV zinawaka na kuchukua picha, hivyo uwe makini. Kwa mwendo kasi barabarani, pale kamera zilipowekwa kuna picha za wazi zinazoonyesha hivyo, na kila mtu anayejali kujua anafahamu vizuri zilipo.

 

Hakuna kufichaficha kama bangi, au rafiki zangu trafiki wa barabara ya Morogoro au Iringa wanavyojificha vichakani na magari yao au kuchomoka na kifaa cha kupima kasi ya gari. Hapa hata maeneo ya kuegesha hayo magari ya polisi yana vibao kabisa. Haya, tabia nyingine zinazoangaliwa na PCC ni kutokuwa makini wanaposhughulikia mambo yanayoweza kushitua au kuleta simanzi na hofu, kwa watu na kutopata ruhusa inayotakiwa kabla ya kuzungumza na watoto au watu walio hospitalini.

 

Hebu tujifunze kuwa kama hawa. Kama tuliamua kujifunza Kiingereza na kukifanya lugha rasmi shuleni na kuiga sheria zao, hili la uhuru wa habari linatushindaje?

leejoseph2@yahoo.com

 

 

1224 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!