Ombaomba, kwa mujibu wa fasili ya Kiswahili, ni mtu anayepata mahitaji yake kwa kuzurura mitaani na kuomba kutoka kwa wapita njia. 

Ombaomba ni mtu mwenye tabia ya kuitisha usaidizi kutoka kwa wengine kila mara. Kwa ujumla, ombaomba ni mtu aliyeamua kuendesha maisha yake kwa kuwategemea wengine, bila ya haki, na amefanya kuombaomba ndiyo kazi yake.

Uislamu umepiga vita sana tabia ya kuombaomba watu na ukaonyesha wale wanaostahili kusaidiwa ambao si hawa waliogeuza kuombaomba kuwa ndiyo nyezo ya kuwapatia mkate wao wa siku. Hawa hawastahili hata kupewa sadaka. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqarah), Aya ya 273 kuwa: “Na wapewe mafakiri waliozuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawang’ang’anii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayotoa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.”

Tunasoma pia katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Abu Hurayra (Allaah Amridhie) akisema: Amesema Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) : “Maskini si yule anayepitia watu kuwaomba wakamuondoa kwa tonge moja au mbili, au kwa kokwa moja au mbili za tende. Bali ni yule ambaye hana cha kumtosheleza, wala hatambuliki ili apewe sadaka, na wala hasimami kuomba watu.” (Hadithi hii inapatikana katika Kitabu cha Hadithi za Mtume kiitwacho Sahih Al-Bukhary).

Tunaona hapa kuwa maskini anayepaswa kuangaliwa na kusaidiwa ni yule ambaye jamii inamtambua kwa umaskini wake na yeye anachunga murua wake; katu hajidhalilishi kwa kuombaomba kwa hila mbalimbali.

Uislamu pia umeelekeza wale wanaostahili kuomba na kusaidiwa hata kutoka hazina ya umma au sadaka/zakah iliyokusanywa. Tunasoma katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Qabiiswa bin Al-Mukhaariq (Allaah Amridhie)  akisema:  “Nilijibebesha jukumu la kulipa fidia baada ya kupatanisha wenye kugombania jambo (lakini sikuwa na uwezo wa kutimiza). Basi nikamuendea Mtume ili anisaidie kutekeleza jukumu hilo. Akasema: “Subiri mpaka zitapofika mali za sadaka, tutakusaidia.” Kisha akasema: “Ewe Qabiiswa! Hawaruhusiwi kuomba isipokuwa watu watatu tu: Kwanza, mtu aliyechukua dhamana ya upatanishi wa mgogoro, akashindwa kuitekeleza, basi anaruhusiwa kuomba msaada. Akishaupata, hana budi kujizuia kuomba. Pili, mtu aliyepatwa na janga la kupoteza kila alichonacho, basi anaruhusiwa kuomba msaada mpaka pale atakapopata cha kumpa nguvu kidogo tu, au kuweza kuishi. Na tatu, mtu aliyekumbwa na njaa, mpaka ikafika hadi watu watatu, waadilifu, wanaomjua wakasema, wenyewe kwa wenyewe: “Ama kweli! Fulani amekumbwa na njaa.” Basi anaruhusiwa kuomba msaada mpaka pale atakapopata cha kumpa nguvu kidogo tu, au kuweza kuishi. “Yeyote mwingine anayeomba, zaidi ya hao watu watatu, Ewe Qabiiswa, anaomba kwa njia ya haramu, na anakula haramu.” (Hadithi hii inapatikana katika Kitabu cha Hadithi za Mtume kiitwacho Sahih Muslim) .

Tabia ya kuombaomba katika nchi yetu na hususan jijini Dar es Salaam imeshamiri na inaeneza maradhi ya kisaikolojia yanayoitafuna jamii na kuacha athari mbaya sana ya makuzi. Ombaomba wamewageuza watoto wadogo kivutio cha huruma ya wahisani wanaochangia kuendelea kuwepo kwa tatizo hili. Watoto wenye umri mdogo wanaostahili kuwepo shuleni wanahangaishwa mchana kutwa katika shughuli za kuombaomba.

Zipo taarifa kuwa mbali ya wale watoto wa familia moja wanaogawana mitaa ya kuomba asubuhi na jioni kufanya mahesabu na kurudi katika makazi yao wakiwa wameneemeka kwa mali haramu kwa mujibu wa Uislamu, baadhi ya ombaomba huwakodi watoto kutoka katika familia zao kwa ujira maalumu.

Raia wa aina gani tunayemtarajia kwa huyu mtoto aliyekoseshwa elimu na akaathiriwa kisaikolojia kwa kushiriki shughuli za kuombaomba mitaaani?

Mtume Muhammad katika hadithi mbalimbali amenukuliwa akimzungumzia ombaomba na ubaya wa kile anachokifanya.

Tunasoma katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ibnu Umar (Allaah Amridhie) akisema: Amesema Mtume : “Mtu hataacha kuwa anaomba watu hadi aje Siku ya Kiyama na hakuna kipande cha nyama usoni mwake.” (Hadithi hii inapatikana katika Vitabu vya Hadithi za Mtume, Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

Tunasoma pia katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Abdul-Rahmaani Bin Awfi (Allaah Amridhie) akisema: Amesema Mtume : “Mja haufungui mlango wa kuombaomba isipokuwa Mwenyezi Mungu humfungulia mlango wa ufukara.” (Hadithi hii inapatikana katika Kitabu cha Hadithi za Mtume, Musnad Ahmad).

Yaani, yule ambaye hana dharura yoyote ya kufanya kazi akiwa mzima wa viungo na afya ya kufanya kazi kisha akaamua kuufungua mlango wa yeye kuwa ombaomba, basi hatapata isipokuwa ufukara kumuandama.

Mtume Muhammad amekataza kumpa sadaka mtu ambaye ni mzima wa afya, mwenye uwezo wa kufanya kazi. Tunasoma katika Hadithi inayopatikana katika Kitabu cha Hadithi za Mtume kiitwacho Jaamii At-Tirmidhy kuwa: Amesema Mtume : “Si halali kumpa sadaka mtu mkwasi au mwenye nguvu ya mwili.”

Uislamu unatufundisha namna ya kuliondoa tatizo hili la ombaomba kwa njia ya kuwabadilisha fikra kutoka hali hii ya kuwa ombaomba na kuwa wazalishaji mali wanaokula kutokana na jasho lao na kutumia hata rasilimali yenye thamani ndogo anayoimiliki ombaomba ili iwe chanzo cha mabadiliko ya tabia na hali yake.

Mtume Muhammad anasisitiza watu wafanye kazi na watafute chumo halali ambalo litamzuia mtu kuwa ombaomba bila ya kujali ugumu wa kazi hiyo au uduni wake, madhali ni kazi halali. Amesema, kwa mfano, anayepata chumo lake kwa kazi ya kuuza kuni anazozibeba mgongoni mwake na akajizuia kuwa ombaomba, hilo ni bora kuliko kumuomba mtu ambaye aweza kukupa au kukunyima kwa sababu mkono wa juu (mkono wa kutoa) ni bora kuliko mkono wa chini (mkono wa kupokea).

Kuhusu tunachojifunza kutoka kwa Mtume Muhammad juu ya ombaomba wenye uwezo wa kufanya kazi ni Hadithi ifuatayo iliyopokewa kutoka kwa Anas Bin Malik (Allaah Amridhie) kuwa: Mtu mmoja miongoni mwa watu wa Madina (Al-Answaar) alimuendea Mtume kuomba sadaka. Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akamuuliza: “Kuna chochote nyumbani kwako?” Akasema: “Kipo; kitambaa kizito tunachokivaa sehemu yake na sehemu nyingine kutandika na gudulia la maji tunalonywea.” Mtume akasema: “Niletee.” Alivileta na Mtume akavichukua kwa mkono wake na kusema: “Nani atavinunua hivi?” Mtu mmoja akasema: “Nitavichukua kwa Dirham moja.” Mtume akasema: “Nani atazidisha juu ya Dirham moja?” Mtu mmoja akasema: “Mimi nitavichukua kwa Dirham mbili.” Mtume alichukua zile Dirham mbili na akampa yule mtu wa Madina na kusema: “Dirham moja kanunue chakula na kipeleke kwa familia yako na Dirham nyingine kanunue shoka na uniletee.” (Shoka lilipoletwa) Mtume alilitia mpini kwa mkono wake kisha akamwambia: “Nenda kachanje kuni na uziuze, na nisikuone kwa siku kumi na tano.”

Yule mtu alikwenda zake akawa anachanja kuni na kuziuza na akamjia Mtume hali ya kuwa amepata Dirham 15; akatumia sehemu yake kununua nguo na sehemu nyingine kununua chakula. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akasema: “Hili ni bora kwako kuliko kuomba kwako kuja kuwa baka (doa jeusi) usoni mwako Siku ya Kiyama…”

Nihitimishe makala hii kwa kuwajuza wasomaji wangu kuwa nchini Jordan kuombaomba ni kosa la jinai na ombaomba wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa kazi wanayoifanya ni haramu na kipato wanachopata pia ni haramu.

Tatizo la ombaomba limekuwa sugu na operesheni mbalimbali za mamlaka mbalimbali zimeshindwa. Ni vema ukafanywa utafiti wa kulishughulikia tatizo hili na athari zake hasi hususan kwa watoto ombaomba. 

Huenda kupitia utafiti huo zikapatikana fikra mpya na njia mpya za kulikabili tatizo hili au zikaimarishwa njia za awali za kuwadhibiti wazururaji kwa kuwapeleka Gezaulole, Kibugumo na Mwanadilatu; au kuwadhibiti wenye ulemavu kwa kuwaanzishia makazi yenye shughuli za uzalishaji mali na si eneo lisilo miundombinu ya kutatua tatizo kama ilivyokuwa Kipawa kwa maskini.

Kadhalika, ni vema serikali ikatafakari mustakabali wa watoto wa Kitanzania wanaonyimwa elimu na wanaingizwa katika ajira haramu ya ombaomba. Tukumbuke kuwa hawa watakapofikia umri mkubwa na hawana miundombinu ya kuyakabili maisha kwa kukosa elimu na malezi bora watakuwa mzigo kwa jamii na taifa na huenda wakaongeza idadi ya wahalifu sugu, kwani hawana cha kupoteza.

Mwito wangu kwa jamii ni kutoa ushirikiano kwa kuwapembua wale wenye kufaa kusaidiwa na wale waliogeuza kuombaomba ni sehemu ya maisha yao; na kwa wana dini tukumbuke kuwa tumekatazwa kuwapa sadaka ombaomba wenye uwezo wa kufanya kazi ambao ndio wengi hivi sasa.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri