Ni Kitambo sasa, Watanzania wamo katika fikra na harakati za kumpata Rais mpya hapo mwakani, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya Rais wa sasa Profesa Jakaya Mrisho Kikwete kukamilisha muda wake wa uongozi na utawala wa miaka kumi.

Na kama hapana budi Rais huyo mpya ataendelea kuongoza tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.  Hii ina maana kwamba Rais ajaye awe na uwezo wa kuwaongoza Watanzania kwa kipindi cha miaka kumi: 2015 had 2025.

Wakati Watanzania wanagonganisha vichwa vyao kumpata Rais mpya, tayari baadhi ya Watanzania hao hao wamo waliojitokeza hadharani na kueleza kusudio la kuwania Urais na wengine wapo ingawa hawajatangaza rasmi nia hiyo.

Kwa vyovyote iwavyo lazima Rais mpya huyo atapatikana ndani ya chama cha siasa au  nje ya chama cha siasa.  Ninamaanisha kutoka chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) au chama cha upinzani ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), au mgombea binafsi ndani ya jamii ya Watanzania.

Hadi sasa watu wapatao 17 kutoka Chama Cha Mapinduzi wamejitokeza hadharani, na kila mtu anaeleza yeye anaweza kuwa Rais na kuongoza Watanzania wapatao milioni 45 wenye kupambana na maadui wakuu watatu ujinga, maradhi na umaskini.

Bado sijafahamu UKAWA na wagombea binafsi watakuwa wangapi, ambao wana nia kama ya hao waliojitokeza.  Watu wengi kujitokeza kutaka urais, sio hoja kwangu.   Wanaweza ujitokeza hata lukuki.  Hoja yangu ni tabia. Yukoje?

Hao waliojitokeza na hao watakaojitokeza ni watu tunaowafahamu kwa matandu na ukoko.  Tuwasikilize, tuwahoji na turidhike kweli kati yao yupo mwenye tabia na uwezo wa kuwanasua Watanzania kutoka hapa walipo.

Watanzania wengi wanatoa fikra na sifa za mtu anayefaa kuwa kiongozi. Kati ya sifa zinatotajwa ni kijana au mzee.  Baadhi wanataka Rais awe kijana na wengine wanataka Rais awe mtu wa makamo au mzee.

Binafsi nina machache kuzungumza na kuunga mkono kauli za wakubwa wangu wawili, Balozi Paul John Rupia, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Utumishi wa Umma na  Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Kada mkongwe wa  CCM.

Viongozi hao wastaafu wote walikaririwa na vyombo vya habari nchini wiki iliyopita, wakitoa mawazo na misimamo yao kwa mtu anayefaa kuwa Rais wa kuwaongoza Watanzania kwa kipindi cha miaka kumi ijayo  2015 – 2025.

Balozi Paul Rupia anasema “Awe mtu mwenye busara. Mtu ambaye anaelewa wito wa kazi ya urais.  Tunayemfahamu tabia yake, mwenendo wake na msimamo wake katika kusimamia mambo makuu ya nchi,  kutatua matatizo ya ujinga, maradhi na umaskini”

Mzee Kingunge anasema  “mtu anayetaka urais anapaswa kukubalika na jamii, hata suala la uzee sio sifa ya uongozi.  Sifa kubwa ya kuutaka urais ni kukubalika na wananchi”  ujana si kigezo cha kumuwezesha kuwa  Rais.

Kauli na misimamo hiyo inashtua mishipa yangu ya fahamu, jambo muhimu ni busara ambayo ndani yake unapata hekima na falsafa zinazokuwezesha kuwa na tabia njema na kukubalika na wananchi watakaokupa madaraka hayo ya urais.

Busara, hekima, falsafa na tabia yako ndivyo vitakavyojenga imani kwa wananchi kwamba fulani anaweza kuongoza watu.  Je, watu wanaojitokeza kutaka urais unawaangalia kupitia madirisha hayo au unawatazama kupitia madirisha hasi?

Kwa mtu atakaye urais amejitazama tabia na mwenendo wake?  Kauli za eti nimeoteshwa zinatoka wapi?  Huo ni ujanja tu.  Kila mtu anaota, pengine kuwa tajiri, bi. harusi au bwana harusi hata pengine mwizi,  je! unakuwa mwizi kweli?  Tajiri kweli? Tafakari!

Tatizo kubwa ambalo Watanzania tunalo ni mmomonyoko wa maadili; tabia.  Chimbuko la rushwa, ufisadi, ubakaji, uuaji na kadhalika yanatokana na maadili kumomonyolewa. Na hapa ndipo tunajenga taifa la hovyo na la watu wenye ubinafsi na kuathiri mifumo ya uchumi.

Suala la kujiamini na kujitegemea halipo. Suala la ombaomba kwa mataifa yaliyoendelea ndio mtaji.  Suala la kukosa ajira kwa vijana – nguvu kazi ni kilio, na suala la elimu duni na maradhi ndio shida pevu mbele yetu.

Kumbuka na tafakari “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alijitahidi kwa kiwango kikubwa kuwaelimisha na kuwaambia ukweli Watanzania kuhusu maisha yao na kuhusu nchi yao” je rais ajaye ataweza kuwaambia ukweli Watanzania?

Namalizia makala yangu kwa kumnukuu Balozi Paul Rupia “Tunataka rais ambaye akimaliza muda wake wa uongozi watu wamkumbuke na kusema huyu kafanya hiki na hiki, pamoja na kutumia utawala wake kusolve matatizo yanayowakabili watu wake”  mwisho wa kunukuu.

1302 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!