Wahitimu zaidi ya 3,000 wa mafunzo ya ujasiriamali katika taasisi ya The Fountain Justice Training College ya jijini Arusha, wameweza kujiajiri na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha hivi karibuni, mdau wa elimu kutoka taasisi hiyo, Wilson Kechegwa, amesema mafunzo ya ujasiriamali yana nafasi kubwa ya kuwezesha vijana wengi kujiajiri na kuajiri wengine.

 

Katika hatua nyingine, Kechegwa ametoa wito kwa Serikali kushirikiana na wananchi kutafuta ufumbuzi wa tatizo la anguko la elimu nchini.

 

“Taifa la kesho linategemea vijana katika kupiga hatua ya maendeleo,” amesema mdau huyo na kusisitiza kuwa jitihada za haraka zinahitajika kuwezesha wanafunzi walipata sifuri mwaka jana kurudia mtihani wa kitado cha nne.

 

Ameongeza kuwa masomo ya uongozi wa hoteli, ualimu na utalii nayo yana nafasi kubwa ya kuwezesha vijana wengi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi na serikalini.

 

Ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wazazi na walezi kukazania kuwaendeleza watoto wao kielimu, kuwajengea msingi wa kumudu maisha yao kuepuka utegemezi.

 

Kwa mujibu wa Kechegwa, jamii ina jukumu la kushirikiana na walimu, kufuatilia maendeleo ya wanafunzi katika masomo na kuchukua hatua madhubuti wanapoonekana kulegalega.

 

Hata hivyo, ameishauri Serikali kudhibiti siasa katika elimu kwani hali hiyo inaweza kusababisha kuzorota kwa taaluma ya wanafunzi.

 

Kechegwa amesisitiza pia suala la Serikali kuhakikisha inaboresha maslahi ya walimu na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika shuleni, ili kuwezesha ukuaji wa taaluma kwa wanafunzi.

 

By Jamhuri