4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+KinanaMara baada ya kusoma makala hii, bila shaka utabaki kwenye akili ya mmoja wa wanafalsafa wa Uingereza aliyeitwa Francis Bacon (1561-1626). Alipata kunena kwamba “Anayeuliza mengi atajifunza mengi, na kubaki na mengi.”
  Hii maana yake ni kwamba hakuna mtu mjinga kuliko mwingine, na hakuna mtu mwerevu kuliko mwingine. Binadamu wote wana mwanga pia wana giza. Hivyo suala la kujiuliza maswali yaliyo na majibu na yasiyo na majibu baada ya kulimaliza kusoma mjadala huu ni kawaida.
  Ni matumaini yangu kwamba utabaki na mengi ila utasahau machache kwani tumeumbwa hivyo kiasili. Kila mlango na ufunguo wake, na kila tatizo na suluhisho lake. Kuna hatari kama una ufunguo mmoja tu kwa milango yote. Maana ya maneno ya hapo juu ni hii.


  Tanzania ni Taifa ambalo lina mfumo wa vyama vingi, na kila chama kinaamini kwamba kina uwezo wa kuishikilia dola na kuwaletea Watanzania maendeleo stahiki. Ukongwe wa Serikali ya CCM madarakani si kigezo cha kuwashawishi Watanzania na kuwaaminisha kwamba CCM ina ubora kuliko vyama vingine.
 Huo ni uongo, na mtazamo wa aina hiyo ni wa wana-CCM.   Ninaamini na nitaendelea kuamini kwamba Tanzania bila CCM inawezekana tena kwa asilimia 100.


  Naamini kwamba hata nje ya Serikali ya CCM kuna viongozi wenye weledi katika uongozi, nidhamu katika uongozi, upendo katika uongozi, uzalendo katika uongozi, na busara katika uongozi, na wanaoweza kuliongoza Taifa hili na likapata maendeleo kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani.
  Ninaendelea kuamini kwamba hata nje ya Serikali ya CCM kuna viongozi wenye hofu ya Mungu, wacheshi na wawajibikaji katika majukumu. Ninaamini kwamba ukomavu wa kiongozi hautokani na chama chake cha kisiasa tu, bali kwenye maarifa yake, busara zake, malezi yake, uadilifu wake na uzalendo wake.
  Hata mpigania uhuru wa Taifa hili alipata kusema, “CCM siyo mama yangu wala baba yangu naweza kutoka”. Huo ndiyo ukweli ingawa sikulazimishi kuubali. Ni kweli na itabaki kuwa kweli kwamba hakuna mahala popote pale iwe ni kwenye Biblia Takatifu ama Qur’an Tukufu palipoandikwa kwamba bila CCM, hakuna maendeleo katika Taifa la Tanzania.


 Baada ya tafakuri ya muda mrefu, na tafiti mbalimbali na uhalisia wa maisha ya Watanzania yalivyo, hatimaye nimeamini kwamba Tanzania inahitaji mabadiliko ya kiungozi.
 Imepita takribani miaka 54 tangu Taifa hili lilipopata uhuru, lakini cha ajabu ni kwamba bado linachechemea katika huduma za kimaendeleo. Hii ni aibu kwa Taifa kama la Tanzania, ambalo lina vitegauchumi lukuki na wasomi wa kutosha.
 Kwenye baadhi ya khanga za akinamama kuna maneno yanayosomeka hivi, “Kama huwezi kunihudumia niache wengine watanihudumia,” hivyo Serikali ya CCM imeshindwa kuwahudumia Watanzania, hivyo ikae pembeni wenye uwezo, wa kuihudumia Tanzania wawe ulingoni.
  Evangus Ponticus ni Mtawa wa Kikatoliki aliyeishi miaka kati ya 346 na 399, alipata kuandika hivi, “Ukitaka kumtambua Mungu, lazima ujitambue kwanza wewe mwenyewe.”


Nina mashaka kama viongozi wa Serikali ya CCM wanajitambua, maana uongozi wao unaonesha kwamba hawajitambui kabisa. Matendo yao yanaonesha kwamba hawajitambui kabisa. Kauli zao zinaonesha kwamba hawajitambu kabisa. Ahadi zao zinaonesha kwamba hawajitambui kabisa. Ninashawishika kusema yafuatayo juu ya chama tawala kwamba tumeona mbinu zake zisizo na dira wala ramani.


Tumeona jitihada zao za kuwalinda mafisadi na wawekezaji. Tumeona vipaumbele vyao vya kutaifisha rasilimali za Taifa hili. Tumeona uongozi wao wa kifisadi. Kama ni kujipima tumejipima sana. Kama ni kuona tumeona sana. Kama ni kutafakari tumetafakari sana. Kama ni kusikia tumesikia sana. Kama ni kuchekwa tumechekwa sana. Kama ni kuvumilia tumevumilia sana. Kama ni kupembua tumepembua sana. Kama ni ukimya sasa imetosha.
Watanzania si gogo ambalo linaweza kukaa miaka mingi kwenye maji lakini lisibadilike hata siku moja na kuwa mamba. Watanzania si magogo. Watanzania si mawe. Watanzania si kama nguo inayosubiri kuvaliwa ama kufuliwa. Watanzania ni watu wenye ufahamu kamili na utashi kamili. Watanzania tunaweza kubadilika, tunaweza kuwa mawakala wa mabadiliko.


Hali ya Taifa ni tete, nguvu za ziada zinahitajika ili kuirudisha Tanzania katika misingi iliyo thabiti na imara. Hali ya Taifa letu inahitaji uongozi mbadala. Hali ya Taifa inahitaji mawazo ya viongozi wenye itikadi na falsafa kama za Mwalimu Julius Nyerere.
Mwanafalsafa na Mchumi, Rosa Luxemburg [1871-1919] alipata kuandika hivi, “Wasiosogea hawatambui kuwa wana minyororo.” Watanzania wenzangu mnatambua kuwa tuna minyororo tuliyofungwa na Serikali ya CCM? Kama hamtambua ninaanza kukudokezeeni.
  Naomba unifutilie kwa usikivu na umakini. Rushwa ni minyororo, tusogee tuikate Oktoba, 2015. Ufisadi ni minyororo, tusogee tuikate Oktoba, 2015. Uongozi usio na maadili ni minyororo, tusogee tuikate Oktoba, 2015. Tanzania tuna viongozi mizigo, ambao hawashiriki mateso ya Watanzania wenzao, hiyo ni minyororo tusogee tuikate Oktoba, 2015.


  Tanzania tuna viongozi wasiofikiri vizuri, hiyo ni minyororo tusogee tuikate Oktoba, 2015. Tuna viongozi wanaoenda kuomba misaada isiyo ya lazima, hiyo ni minyororo tusogee tuikate Oktoba, 2015. Tuna viongozi ambao ni madalali wa rasilimali za Watanzania kwa mataifa ya nje, hiyo ni minyororo tusogee tuikate Oktoba, 2015.


Tuna viongozi wanaotamani kusafiri kila siku kwa ajili ya kujitangaza kwamba na wao ni viongozi wa taifa fulani, hiyo ni minyororo tusogee tuikate Oktoba, 2015. Ni aibu kwa Taifa kama la Tanzania kuitwa tegemezi. Aibu hii kaileta nani? Jibu ni Serikali ya CCM.
 Ubinafsi na uroho wa viongozi wetu ndiyo unaosababisha Taifa letu kutopiga hatua ya kimaendeleo. Ni uongozi dhaifu wa Serikali ya CCM ndiyo ulioawafanya Watanzania wengi kuishi maisha ambayo hawakutarajia kuyaishi. Hakuna mtu anayeweza kuishi kwa amani wakati jirani yake anateseka, lakini Serikali ya CCM inaweza.


  Ni Serikali ya CCM utakuta kiongozi anatembelea gari lenye thamani ya Sh milioni 800 huku wananchi wake hawana hata kituo cha afya. Ni Serikali ya CCM utakuta kiongozi anatembelea gari lenye thamani ya Sh milioni 800 na anakwenda kuwachangisha wananchi wake fedha za maabara.
  Ni Serikali ya CCM utakuta kiongozi anatembelea gari lenye thamani ya Sh milioni 800, lakini ukakuta jimboni kwake shule zina uhaba wa vyoo na madarasa. Serikali ya CCM ni kama mwanaume ambaye kwa nje anaonekana mtu mwema, lakini ndani anamtesa mke wake. Serikali ya CCM inafanana na mwanaume ambaye akienda baa anaagiza kwa kusema, “Lete kama tulivyo”, na wakati huo huo ameiacha familia yake ikiwa inataabiki mithili ya kufa.


  Mchungaji Dag Heward Mills Katika kitabu chake cha “Viongozi na Uaminifu” anasema yafuatayo: “Tatizo la Afrika ni uongozi. Afrika inatatizwa na viongozi wabaya, kuwa na viongozi wabaya ni sawa na kumkaribisha shetani kuwa rafiki yako. Nchi nyingi za Afrika zinapata viongozi ambao wanaiba rasilimali za mataifa yao. Viongozi wa nchi za Afrika wana utajiri binafsi kuliko wa nchi wanazoziongoza.”
Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, alipata kusema, “Uongozi ni fursa ya kuboresha maisha ya wengine. Siyo fursa ya kuridhisha uchoyo wa mtu.” Uongozi ni kuwatumikia waliokuchagua siyo kuwanyanyasa, siyo kuwaibia, siyo kuwafananisha kama katuni.
Katika Biblia Takatifu tunakutana na maneno haya, “Na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” Marko 10: 44-45.


Kiongozi ni mtetezi wa wanyonge. Mahatma Gandhi anathibitisha ukweli huu anaposema, “Siko tayari kukaa juu ya kiti mpaka Wahindi wakae juu ya viti ndiyo na mimi nikae,” Mungu tusaidie maana uongozi wa sasa ni wa kuhurumia, kwani viongozi wengi tunaowapata ni viongozi wanaojali matumbo yao na familia zao.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo viongozi wake wana utajiri mkubwa kuliko wa wananchi wanaowaongoza. Eti mmiliki halali wa rasilimali za Watanzania ni kiongozi na mwekezaji aliyetoka nje, wananchi ambao ni wazawa wa Taifa hili ni vibarua na wala hawana sauti juu ya rasilimali za Taifa lao. Wakihoji tu ni risasi kwa kwenda mbele.
Tanzania siasa ni biashara, siyo demokrasia tena. Ni ukweli ulio wazi kwamba wafanyabiashara wakubwa katika Taifa hili ni viongozi wa Serikali ya CCM. Miradi mikubwa inayoendeshwa hapa nchini iko chini ya viongozi wa Serikali ya CCM. Wamiliki wakubwa wa vitalu kwenye mbuga zetu za wanyama ni viongozi wa Serikali ya CCM.


Wamiliki wakubwa wa mashamba ni viongozi wa Serikali ya CCM. Wamiliki wakubwa wa majumba ya kifahari katika Taifa hili ni viongozi wa Serikali ya CCM. Wenye hisa kubwa katika migodi nchini ni viongozi wa Serikali ya CCM. Waliojenga majumba ya kifahari nje ya Taifa hili ni viongozi wa Serikali ya CCM.
Tukitafakari hapo uongozi bora uko wapi? Uaminifu na uzalendo wa viongozi uko wapi? Binafsi hapo ninaona ni majanga matupu. Binafsi hapo ninaona ni uroho wa mali. Binafsi hapo ninaona ni uongo uliotukuka. Binafsi hapo ninaona ni uonevu mkubwa wa watawala kwa wananchi wanaowaongoza.
Leo hii wananchi wakihoji ni kwa nini viongozi wa Serikali ndiyo wadau wakubwa na wafanyabiashara wakubwa katika Taifa hili, na wakati ni kinyume na maadili ya uongozi wanaambulia kung’olewa meno, ama kung’olewa kucha na kutupwa kwenye mapori.


Serikali ya CCM ni dhaifu, huo ni ukweli ulio wazi na usiohitaji hoja ya kuthibitisha. Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Bahati Bukuku, aliimba wimbo unaosema, “Dunia Haina Huruma”, leo mimi ninaimba “Serikali ya CCM haina huruma kwa taifa la Tanzania.”
Imekomba rasilimali za Watanzania mithili ya kuzimaliza.  Haya ndiyo majanga ya Serikali ya CCM. Ni Serikali ambayo inaongoza kwa ufisadi. Ni Serikali inayoongoza kwa kuwalinda wahujumu uchumi. Ni Serikali inayoongoza kwa maazimio butu.
Ni Serikali inayoongoza kwa kuwadanganya wananchi wake. Ni Serikali inayoongoza kwa kusaini mikataba hewa.  Ni Serikali inayoongoza kwa kutoa mishahara midogo kwa wafanyakazi wake. Ni Serikali inayoongoza kwa kutumia dola vibaya. Ni Serikali inayoongoza kwa miundombinu mibovu. Ni Serikali iliyo na kaulimbiu ya “Piga tu”. Ni Serikali inayoongoza kwa kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa kubagua. Ni Serikali inayoongoza kwa kutoa ahadi hewa.


Ni Serikali inayoongoza kwa uozo wa kimaadili katika uongozi. Ni serikali inayoongoza kwa kuwachekea wahujumu uchumi wa Taifa hili. Ni Serikali inayoongoza kwa kuwathamini wawekezaji kuliko wazawa wa Taifa hili. Ni Serikali ambayo ukimpiga kiongozi wa upinzani au mwandishi unapewa cheo.
  Sijui na mimi nimpige Steven Wasira nione kama nitapewa ukuu wa wilaya? Ni Serikali inayowatumia wananchi wake kama M-pesa ili kupitisha magendo yao. Ni Serikali inayowatumia wananchi wake kama Tigo pesa ili kupitisha magendo yao. Ni Serikali inayowatumia wananchi wake kama Airtel money ili kupitisha magendo yao.
Ipo methali inayosema mwezi hauwezi kuandama mpaka uliotangulia uwe umeondoka. Tanzania hii kupata maendeleo mpaka chama tawala kiondoke madarakani.


Kabila la Wasambaa waishio Tanzania wana msemo unaosema hivi, “Ukitaka kuepuka inzi tupa kibudu”’. Watanzania tukitaka kusonga mbele kimaendeleo lazima kwanza tuibwage chini Serikali ya CCM ili tuweze kuunda mfumo mpya chini ya chama kingine.
Mwanafalsafa Tolmons alipata kuandika hivi, “Katika maisha unayoishi unaweza kuonesha sura ya Mungu au sura ya shetani.” Kazini kwako unaweza kuonesha sura ya shetani au sura Mungu. Kwenye familia yako unaweza kuonesha sura  ya shetani au sura ya Mungu. Kwa majirani zako unaweza kuonesha sura ya shetani au sura ya Mungu.


Inategemea maisha yako unayoishi yanawakilishwa na matendo ya aina gani, kama ni matendo yasiyofaa kama ya Serikali ya CCM, basi hapo unaipeperusha bendera ya shetani, na kama ni matendo bora yenye uadilifu basi hapo unaipeperusha sura ya Mungu.
Serikali ya CCM inaonesha sura gani kati ya sura ya Mungu na sura ya shetani katika Taifa letu? Tupembue tuone. Ufisadi ni sura ya shetani. Rushwa ni sura ya shetani. Uchu wa madaraka ni sura ya shetani. Biashara haramu  kama ya dawa za kulevya ni sura ya shetani. Wizi wa pembe za ndovu ni sura ya shetani. Tanzania tunamtaka kiongozi atakayeonesha sura ya Mungu katika kuliongoza Taifa hili.


Sura ya Mungu ni sura ya uadilifu na uaminifu. Sura ya Mungu ni sura ya upendo. Sura ya Mungu ni sura ya amani. Sura ya Mungu ni sura ya mshikamano.  Sura ya Mungu ni sura ya unyenyekevu na huruma.
Mwalimu Nyerere alisema, “Watu safi hawakimbilii Ikulu”.  Inashangaza kuona Ikulu ya sasa hivi ikifuga mafisadi. Siku hizi hata fisadi aliyeiibia nchi mabilioni ya shilingi anaweza kula nyama na pombe kali kisha akalala na mke wake, asubuhi naye akasema nataka kuwa rais.
Akitumia uzoefu wake wa kukaa Ikulu kwa miaka 23, Mwalimu Nyerere alisema, “Mtu yeyote anayekimbilia Ikulu ikiwa ni pamoja na kuhonga fedha, basi huyo ni wa kumwogopa kama ukoma.” Mwalimu alifahamu ndani ya CCM nani mwizi, nani kibaka, nani jambazi.


Leo Mwalimu Nyerere akifufuka ataikimbia Tanzania, hataamini kinachoendelea katika Taifa letu. Atawakuta mafisadi ndiyo wenye meno. Atawakuta wawekezaji ndiyo wazawa na Watanzania ni watu wa kuja. Atakutana na mikataba ambayo tangu azaliwe hajawahi kuiona katika nchi yoyote ile duniani.
Hayo ndiyo mafanikio ya Serikali ya CCM.  Natamatisha mjadala wangu kwa maneno ya Mtawa wa Kikatoliki, Francis wa Asizi, kwa kusema:
 
“Ee Mungu unifanye kuwa chombo cha amani yako,
Mahali palipo na chuki, nilete mapendo,
Mahali palipo na ghadhabu, nilete msamaha,
Mahali palipo na utengano, nilete umoja,
Mahali palipo na wasiwasi, nilete matumaini,
Mahali palipo na uongo, nilete ukweli,
Mahali palipo na huzuni, nilete furaha,
Mahali palipo na giza, nilete mwanga.”
 
Mungu ibariki Tanzania.
 
0757 852377/0783 994403

2942 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!